JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Afrika na Korea zajadili maendeleo jijini Addis Ababa
Mkutano wa nne wa siku mbili wa Ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Jamhuri ya Korea kwa ngazi ya Mawaziri ambao kwa mara ya kwanza unafanyika barani Afrika umeanza leo jijini Addis Ababa, Ethiopia kwa kikao cha Maafisa Waandamizi. Katika kikao hicho ambapo Tanzania inawakilishwa na Balozi wake nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz ni kwa ajili ya kuandaa mkutano wa Mawaziri utakaofanyika kesho tarehe 07 Desemba 2016, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga tayari alishawasili Ethiopia kuiwakilisha Tanzania.
Maafisa Waandamizi pamoja na mambo mengine, walipata fursa ya kupokea taarifa mbalimbali ikiwemo kupitia Azimio la Addis Ababa litakaloidhinishwa na Mkutano wa Mawaziri pamoja na utekelezaji wa mpango kazi (Kati Ya mwaka 2013-2015) katika maeneo yaliyoafikiwa katika Mkutano wa tatu wa Korea-Afrika uliofanyika mwaka 2012, Seoul, Jamhuri ya Korea. Mkutano wa kwanza na wa pili ilifanyika mwaka 2006 Na 2009, Seoul, Korea.
Maeneo ambayo Nchi za Afrika zilikubaliana kushirikiana na Korea ni pamoja na maendeleo endelevu, elimu, afya, kilimo, mabadiliko ya tabianchi, biashara, uwekezaji na uchumi, amanina usalama na masuala ya mtambuka kama vile masuala ya jinsia, wanawake na watoto, masuala Ya TEHAMA n.k.
Wajumbe walielezwa kuwa katika maeneo yote hayo Korea ilitekeleza wajibu wake ipasavyo kwa kuongeza fedha takriban katika kila eneo kuanzia mwaka 2012 hadi 2015.
Kwa upande wa kilimo Korea imekuwa ikishirikiana na nchi za Afrika kwenye ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji na masuala mengine ya kiufundi ambapo kiasi cha msaada katika eneo hilo kimeongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 16 mwaka 2012 na kufikia Dola bilioni 40 mwaka 2015. Kwa upande wa Tanzania; Zanzibar imefaidika na fedha hizo ambapo imepokea Dola milioni 50 kwa ajili ya uendelezaji wa kilimo cha mwani.
Eneo lingine ambalo Korea iliwekeza fedha za kutosha ni lile la afya ambapo kiasi kilichotolewa kimefikia Dola milioni 27 mwaka 2015 ukilinganisha na kiasi cha Dola milioni 16 kilichotolewa mwaka 2012. Jiji la Dar es Salaam limefaidika na fedha hizo kwa kujengewa hospitali ya uchunguzi ya afya ya mama kwenye eneo la Chanika wilayani Ilala ambayo inatarajiwa kukamilika mwaka 2017.
Aidha, kwa kutambua umuhimu wa amani na usalama katika maendeleo ya Bara la Afrika, Korea imekuwa ikifadhili programu mbalimbali ndani ya Umoja wa Afrika zinazolenga kutatua migogoro na kuleta amani ya kudumu barani humo.
Katika kikao hicho wajumbe walisisitiza umuhimu wa kufikia malengo yaliyowekwa na ushirikiano huo kwa kutekeleza kikamilifu miradi ya maendeleo iliyoainishwa na Umoja wa Afrika ili kuweza kupiga hatua za kiuchumi kwa faida ya Afrika kwa ujumla.
Mkutano huo unatarajiwa kukamilika kwa kutolewa Tamko ambalo pamoja na mambo mengine litainisha maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Korea na nchi za Afrika kwa kipindi cha miaka mitano ijayo 2017 - 2021.
Imetolewa na: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI.
06 DESEMBA, 2016