Thursday, July 13, 2017

Ziara ya Mhe. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco nchini 12 -13 Julai, 2017


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ziara ya Mhe. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco nchini 12 -13 Julai, 2017

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Serikali ya Ufalme wa Morocco Mhe.Mounia Boucetta na ujumbe wake wametembelea Wizara leo tarehe 13 Julai, 2017 na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Suzan Kolimba katika ukumbi wa Wizara, Dar es Salaam. Mhe. Mounia Boucetta yupo nchini kwa ziara ya kikazi tangu tarehe 12 Julai, 2017.

Lengo la ziara hiyo ni kufuatilia utekelezaji wa Maazimio na makubaliano ya Ushirikiano kati ya taasisi za Tanzania na Morocco katika sekta mbalimbali, yaliyosainiwa wakati wa ziara ya Mfalme Mohammed VI wa Morocco nchini Tanzania tarehe 23 – 25 Octoba, 2016. 

Itakumbukwa katika ziara hii jumla ya mikataba 21 ya Ushirikiano katika maeneo mbalimbali ilisainiwa. Mikataba hiyo ni katika masuala yafuatayo; Masuala ya Usafiri wa Anga, Kilimo na Uvuvi, Nishati, Utalii, Viwanda Usafiri wa Reli, Biashara, Masuala ya Bima, Masuala ya Afya, Masuala ya Gesi, Masuala ya Siasa, Uchumi, Sayansi na Utamaduni. 

Aidha Mheshimiwa Mfalme Mohamed VI aliahidi mambo makuu matatu
·        Ujenzi wa msikiti mkubwa wa kisasa jijini Dar es salaam
·        Ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira mjini Dodoma
·        Kuanzisha programu ya mafunzo kwa maafisa wa majeshi yetu ya ulinzi na usalama

Tangu ziara hiyo ifanyike Serikali ya Ufalme wa Morocco, katika kuimarisha urafiki na ushirikiano ilifungua Ubalozi wake jijini Dar es salaam, na Mwezi Februari, 2017 Mheshimiwa Balozi Abdelillah Benryane aliwasilisha hati zake za utambulisho Nchini.

Wizara inawataarifu kuwa Ubalozi umeanza kufanya kazi nzuri, kazi mojawapo kubwa ni kufuatilia utekelezaji wa mikataba hiyo iliyosainiwa wakati wa ziara ya Mheshimiwa Mfalme.

Hivyo ujio wa Mheshimiwa Naibu Waziri Mounia Boucetta ni sehemu ya ufuatiliaji wa hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mikataba hiyo iliyosainiwa.

Wizara ilifanya kikao na Mheshimwa Mounia Boucetta  na kupitia taarifa ya utekelezaji wa mikataba hiyo kwa sekta ya umma na sekta binafsi, na kwa kweli tunaridhishwa na kasi ya utekelezaji.

Pamoja na kasi nzuri hiyo ya utekelezaji Wizara imezielekeza taasisi husika kuongeza kasi zaidi ili tukamilishe utekelezaji wa maeneo hayo tuliokubaliana na kuwawezesha Watanzania wafanyabiashara, wakulima, wazalishaji na wasomi kunufaika na fursa mbalimbali.

Aidha, akizungumza katika majadiliano hayo Naibu Waziri Mhe. Dr. Suzan Kolimba (Mb) amesema wamekubaliana kuundwa Kamati ya Ufuatiliaji ya utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa kati ya Tanzania na Morocco. 

Mhe. Mounia Boucetta pamoja na ujumbe wake leo saa 4:00 asubuhi watakutana na ujumbe wa wadau wa biashara na uwekezaji kutoka Wizara na taasisi za Serikali pamoja na taasisi binafsi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 13 Julai, 2017
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima akitoa neno la ukaribisho kwa ujumbe wa Morocco kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt Suzan Kolimba (Mb) kusoma hotuba ya ufunguzi wa kikao kazi cha kufuatilia utekelezaji wa maazimio na Makubaliano mbalimbali baina ya sekta za Tanzania na Morocco yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Mfalme VI wa Morocco nchini Tanzania.

Naibu Waziri Suzan Kolimba akisoma hotuba yake katika kikao hicho
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Ufalme wa Morocco, Mhe. Mounia Boucetta akisoma hotuba katika kikao kazi cha kufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya Tanzania na Morocco

Ujumbe wa Tanzania ukiwajumuisha Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi mbalimbali wanaounda kikosi kazi cha kufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya Morocco na Tanzania
Ujumbe wa Morocco katika kikao hicho
Washiriki wa kikao kazi cha kufuatilia utekelezaji wa makubaliano kati ya Tanzania na Morocco wakiwa katika kikao cha tathmini ya utekelezaji kilichofanyika Serena Hoteli

Mhe. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.Suzan Kolimba (kulia) akiwa katika mazungumzo na Mhe. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kutoka  Ufalme wa Morocco Mhe.Mounia Boucetta katika ukumbi wa Wizara- Dar es Salaam, tarehe 13 Julai,2017.
 
 Mhe. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt.Suzan Kolimba akipokea zawadi kutoka kwa, Mhe. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Ufalme wa Morocco baada ya mazungumzo.

Mhe. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.Suzan Kolimba, Mhe. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Ufalme wa Morocco na ujumbe wake, wengine ni wataalam kutoka Wizarani wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mazungumzo 





Wednesday, July 12, 2017

Kuwaiti Ambassador visit Ministry of Foreign Affairs

Ambassador of Kuwait to Tanzania H.E Jasem Al-Najem (L) gets greetings with the Permanent Secretary for the Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation, Dr. Aziz Mlima, when the two met today at the Ministry's office to discuss various issues relating to the bilateral relations between the two countries.

Dr. Mlima and Ambassador of Kuwait proceed with their conversations in which among other things, Dr. Mlima promised that the Government will work on to see the possibility of hosting the First Joint Permanent Commission meeting with Kuwait where its agreement was signed since 2013.


Conversation are in progress. Another in the photo is the Kuwait Desk Officer, Mr. Hangi Mgaka.

Group photo

Monday, July 10, 2017

Balozi wa Italia atembelea Wizara ya mambo ya Nje

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba (Mb), akimkaribisha ofisini kwake Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Roberto Mengoni na ujumbe wake kwa ajili ya kufanya mazungumzo.

Dtk. Kolimba akisisitiza jambo kwenye mazungumzo na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Roberto Mengoni.   Katika mazungumzo hayo alikuwepo pia Makamu wa Rais wa Shirika la Taifa la Reli la Italia, Bw. Giovanni Roca ambaye amekuja nchini kuangalia fursa za uwekezaji katika sekta ya reli baada ya kuhamasishwa na Mhe. Naibu Waziri alipotembelea Italia hivi karibuni.


Ujumbe wa Italia uliofuatana na Mhe. Balozi ukifuatilia mazungumzo.

Bw. Charles Faini (kulia), Katibu wa Naibu Waziri na Bw. Salvatory Mbilinyi wa Wizara ya Mambo ya Nje wakinukuu taarifa muhimu
Picha ya pamoja


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India atembelea Wizara ya Mambo ya Nje

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima akiwa katika mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa India anayeshughulikia Masuala ya nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Neena Malhotra.  Wawili hao walizungumzia namna nchi zao zinatakavyoweza kuendeleza ushirikiano katika sekta mbalimbali kama za uwekezaji, miundombinu, afya, elimu, TEHAMA, biashara na kilimo. Aidha, Balozi Mlima alimuomba asaidie kuhamasisha wawekezaji kutoka India kuja kuwekeza nchini katika viwanda ili kuunga mkono agenda ya Serikali ya awamu ya tano inayoweka mkazo kwenye viwanda. 
Ujumbe wa Tanzania (kulia) na ule wa India ukiongozwa na Makatibu Wakuu wao ukiwa katika majadiliano ya namna ya kuboresha zaidi mahusiano kati ya Tanzania na India ambayo yemedumu kwa miaka mingi sasa

Balozi Mlina akikabidhi zawadi kwa Katibu Mkuu wa India

picha ya pamoja



Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Korea-Afrika atembelea Wizara ya Mambo ya Nje

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ,Balozi Dkt. Aziz Mlima (kulia) akibadilishana kadi za mawasiliano na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Korea-Afrika (Korea-Africa centre) cha Jamhuri ya Korea, Balozi KIM IL Soo kabla ya kufanya mazungumzo.

Balozi Mlima akiwa katika mazungumzo na Balozi KIM ambapo walijadiliana namna ya Tanzania na Korea zitakavyoboresha mahusiano ya kidiplomasia na kusisitiza umuhimu wa Chuo cha Diplomasia na Kituo cha Korea-Afrika kuwa na ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo kubadilishana walimu na wanafunzi.

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mazungumzo. kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Bi. Justa Nyange

Ujumbe wa Jamhuri ya Korea ukifuatilia mazungumzo

Mazungumzo yakiendelea

Balozi Mlima akimkabidhi Balozi KIM kifurushi cha zawadi ya kahawa na chai ya Tanzania

Picha ya Pamoja

Thursday, July 6, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Taarifa ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Kenya kuhusu utekelezaji wa maamuzi ya Wakuu wa Nchi Mhe. Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania na Mhe. Rais Uhuru Kenyatta wa Jamhuri Kenya
  
Itakumbukwa kuwa tarehe 28 Juni, 2017 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa taarifa kwa umma kuhusu vikwazo vya kibiashara ambavyo nchi ya Kenya iliweka katika baadhi ya bidhaa kwa kipindi cha hivi karibuni. Katika taarifa ile, Serikali ya Tanzania ilibainisha dhamira yake ya kufanya mazungumzo na Serikali ya Kenya kwa lengo la kumaliza tofauti hizo za kibiashara baina ya nchi hizi mbili kwa kuzingatia taratibu za kibiashara tulizokubaliana katika Jumuiya yetu ya Afrika ya Mashariki.
Bidhaa za Tanzania ambazo ziliwekewa vikwazo na nchi ya Kenya ni unga wa ngano pamoja na gesi ya kupikia (LPG). Aidha, juhudi za awali za Serikali ya Tanzania kuona vikwazo hivyo vinaondelewa na Serikali ya Kenya kwa wakati hazikuzaa matunda. Hali hiyo ilipelekea Serikali ya Tanzania nayo kuchukua hatua.
Kwa kuzingatia mahusiano mazuri ya kindugu yaliyopo kati ya nchi zetu mbili na kwa kujali manufaa mapana ya Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, Viongozi Wakuu wa nchi hizi mbili Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya walizungumza na kukubaliana kuondoleana vikwazo hivyo maramoja, Vikwazo hivyo ni;

1.     Serikali ya Kenya kuondoa vikwazo kwa bidhaa za unga wa ngano na gesi ya kupikia (LPG) kutoka Tanzania.

2.     Serikali ya Tanzania kuondoa vikwazo kwa bidhaa za maziwa zinazozalishwa nchini Kenya.

3.     Serikali za Kenya na Tanzania kuondeleana vikwazo vyovyote vile ambavyo vinaweza kuathiri biashara ya bidhaa na huduma kati ya nchi zetu mbili.

4.     Sigara ni kati ya mambo yaliyojadiliwa. Hata hiyo utekelezaji wake utafuata taratibu za ndani

Hivyo, Viongozi Wakuu wa nchi zetu mbili waliwaelekeza Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi wa Tanzania na Kenya, Mhe. Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb) na Dkt. Amina Mohammed, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Kenya kuutarifu umma kwamba pande zote mbili zimekubaliana kumaliza tofauti hizo za kibiashara zilizojitokeza hapo awali.
Katika kutekeleza hilo, Mhe. Waziri Dkt. Amina Mohamed alimwalika Mhe.Waziri Dkt. Mahiga nchini Kenya tarehe 23 Julai, 2017 ambapo walifanya Mkutano wa Pamoja na waandishi wa habari kuutangaza uamuzi wa Viongozi Wakuu wa Kenya na Tanzania kuondoleana vikwazo hivyo maramoja.

Kufuatia makubaliano haya ya pamoja kati ya nchi hizi majirani ambazo ni waasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pia, tunapenda kutaarifu kwamba Mataifa haya mawili yamekubaliana kuunda Tume ya Pamoja ambayo itakuwa na jukumu la kuepusha tofauti za kibiashara kati ya Tanzania na Kenya pamoja na kutolea ufumbuzi changamoto za kibiashara kati ya nchi hizi mbili pindi zinapojitokeza. Tume hii itaongozwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Kenya na kujumuisha Mawaziri wanaohusika na masuala yaJumuiya ya Afrika Mashariki, Biashara, Fedha, Mambo ya Ndani ya Nchi, Kilimo, Uchukuzi na Utalii wa nchi zote mbili.
Vilevile, Mawaziri hawa wataunda mfumo wa kupeana taarifa mara kwa mara kuhusu masuala yenye changamoto za kibiashara kwa lengo la kuepusha kujirudia kwa tofauti kama hizi. Ni matarajio yetu kuwa uamuzi huu wa pamoja utakuza zaidi mahusiano ya kibiashara baina ya nchi hizi mbili. Aidha, tunapenda kuwashukuru wafanyabiashara wa nchi zetu mbili kwa uvumulivu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 24 Julai, 2017



MASWALI NA MAJIBU BAADA YA TAARIFA YA MSINGI
SWALI:  Je ni kwa nini Kenya waliweka vikwazo hivyo hapo awali?
JIBU: Sababu za awali zilizotolewa na Serikali ya Kenya zilidai kwamba bidhaa hizo hazikidhi viwango vya ubora wa kimataifa. Hata hivyo, Wataalamu wa Tanzania wameihakikishia Kenya kuwa bidhaa za unga wa ngano kutoka Tanzania zina ubora  unaokubalika Kimataifa na huuzwa nchi nyingine za Jumuiya ya afrika Mashariki na Afrika ya Kati. Halikadhalika bidhaa ya gesi ya kupikia (LPG) inakidhi viwango vya ubora vya Kimataifa
.
SWALI: Nini msimamo wa Serikali ya Tanzania kuhusu tuhuma za baadhi ya wanasiasa wa Kenya na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu Tanzania kuingilia uchaguzi wa Kenya.
JIBU: Tuhuma hizi hazina ukweli wowote, na hata nilipokuwa  nchini Kenya juzi niliona zimeripotiwa tena na vyombo vya habari vya Kenya. Naomba nikanushe tena kwa mara nyingine, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haijawahi, na wala haifikirii kuingilia maswala ya ndani ya nchi nyingine tunazoshirikiana nazo ikiwemo maswala ya uchaguzi. Hatujawahi kuingilia uchanguzi wa Kenya na hututegemei kufanya hivyo kwenye uchaguzi huu na chaguzi nyingine zozote. Naomba waandishi wa habari, kabla ya kuandika taarifa hizi, wazihakiki mara mbili, na watutafute kutoa ufafanuzi kabla ya kuwapelekea wananchi taarifa hizi za kupotosha. Natoa rai, tuwe waangalifu na walaghai wa nje  wanaotaka kutugombanisha. Nichukue pia fursa hii kuwatakia wananchi wa Kenya uchaguzi mwema wa amani na huru.


SWALI:  Je ni kwanini Tanzania inaonekana kuweka vizingiti vingi vya kibiashara ikilinganishwa na nchi nyingine kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika ya kati kwenye siku za hivi karibuni? Je hii haitakwaza ukuaji wetu wa uchumi kama nchi?
JIBU: Hapana, hata kidogo. Serikali ya Tanzania inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara ili kuwezesha uchumi wa nchi kukua na kuendelea, kutokana na biashara ndani ya bara la Afrika na hususan ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati. Tanzania kwa siku za hivi karibuni chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Tano, Mhe. John Joseph Pombe Magufuli, imefanya mageuzi makubwa kwenye taasisi zetu za bandari na ushuru yaani TRA. Hatua hizi zinalenga kwenye kuziba mianya iliyokuwepo huko nyuma ambayo ilisababisha ukusanywaji hafifu wa mapato. Ni wazi sasa mambo yanaenda kwa uwazi zaidi na ushuru unatozwa na kukusanywa kwa wakati. Tuna hakika sasa changamoto hizi zimepungua na nchi jirani zitaendelea kufanya biashara na sisi bila vikwazo.

SWALI: Kabla ya kuunda hii kamati ya kutatua changamoto zilizojitokeza hivi karibuni, Jumuiya ya Afrika Mashariki imekua ikitatua vipi changamoto kama hizi za kibiashara hususan kwenye nchi zenye ushindani mkubwa kama Kenya na Tanzania?
JIBU: Jumuiya ya Afrika Mashariki imejiwekea misingi imara na muhimu ya kutatua changamoto pindi zinapojitokeza. Hivyo ukiacha jopo la wataalam wa Serikalini kuna Baraza la Mawaziri wa Biashara wa Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki  ambao pia huweza kupendekeza ufumbuzi wa changamoto mbalimbali kwa wakuu wa nchi ili kutatua changamoto hizi. Lakini kutokana na ukaribu uliopo baina ya Tanzania na Kenya, hili la sasa tumelitatua kwa haraka na kwenda mbele zaidi kuunda tume ya mawaziri wa nchi zetu mbili ili huko baadae tuweze kutatua masuala kama haya mapema sana kabla ya kuathiri biashara kati ya nchi zetu mbili.

Ni dhahiri kwamba nchi zetu mbili ni jirani na tunalindwa na Itifaki za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, lakini pia tuna ushindani kati yetu. Na ili tupate maendeleo ni lazima kuweka ushindani wenye tija kwa manufaa ya ukanda wetu na wananchi wetu. Japo kuwa Kenya ipo kwenye kundi la nchi zenye kipato cha kati, uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi kubwa na ni hali ya kawaida kwa changamoto kama hizi kujitokeza pindi nchi zinapokuwa katika ushindani wa kiuchumi.Kwa namna ya pekee naomba kusifu tena hekima za Viongozi wetu wa Juu kwa kutatua changamoto hizi kwa wakati.