Thursday, July 6, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Taarifa ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Kenya kuhusu utekelezaji wa maamuzi ya Wakuu wa Nchi Mhe. Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania na Mhe. Rais Uhuru Kenyatta wa Jamhuri Kenya
  
Itakumbukwa kuwa tarehe 28 Juni, 2017 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa taarifa kwa umma kuhusu vikwazo vya kibiashara ambavyo nchi ya Kenya iliweka katika baadhi ya bidhaa kwa kipindi cha hivi karibuni. Katika taarifa ile, Serikali ya Tanzania ilibainisha dhamira yake ya kufanya mazungumzo na Serikali ya Kenya kwa lengo la kumaliza tofauti hizo za kibiashara baina ya nchi hizi mbili kwa kuzingatia taratibu za kibiashara tulizokubaliana katika Jumuiya yetu ya Afrika ya Mashariki.
Bidhaa za Tanzania ambazo ziliwekewa vikwazo na nchi ya Kenya ni unga wa ngano pamoja na gesi ya kupikia (LPG). Aidha, juhudi za awali za Serikali ya Tanzania kuona vikwazo hivyo vinaondelewa na Serikali ya Kenya kwa wakati hazikuzaa matunda. Hali hiyo ilipelekea Serikali ya Tanzania nayo kuchukua hatua.
Kwa kuzingatia mahusiano mazuri ya kindugu yaliyopo kati ya nchi zetu mbili na kwa kujali manufaa mapana ya Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, Viongozi Wakuu wa nchi hizi mbili Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya walizungumza na kukubaliana kuondoleana vikwazo hivyo maramoja, Vikwazo hivyo ni;

1.     Serikali ya Kenya kuondoa vikwazo kwa bidhaa za unga wa ngano na gesi ya kupikia (LPG) kutoka Tanzania.

2.     Serikali ya Tanzania kuondoa vikwazo kwa bidhaa za maziwa zinazozalishwa nchini Kenya.

3.     Serikali za Kenya na Tanzania kuondeleana vikwazo vyovyote vile ambavyo vinaweza kuathiri biashara ya bidhaa na huduma kati ya nchi zetu mbili.

4.     Sigara ni kati ya mambo yaliyojadiliwa. Hata hiyo utekelezaji wake utafuata taratibu za ndani

Hivyo, Viongozi Wakuu wa nchi zetu mbili waliwaelekeza Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi wa Tanzania na Kenya, Mhe. Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb) na Dkt. Amina Mohammed, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Kenya kuutarifu umma kwamba pande zote mbili zimekubaliana kumaliza tofauti hizo za kibiashara zilizojitokeza hapo awali.
Katika kutekeleza hilo, Mhe. Waziri Dkt. Amina Mohamed alimwalika Mhe.Waziri Dkt. Mahiga nchini Kenya tarehe 23 Julai, 2017 ambapo walifanya Mkutano wa Pamoja na waandishi wa habari kuutangaza uamuzi wa Viongozi Wakuu wa Kenya na Tanzania kuondoleana vikwazo hivyo maramoja.

Kufuatia makubaliano haya ya pamoja kati ya nchi hizi majirani ambazo ni waasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pia, tunapenda kutaarifu kwamba Mataifa haya mawili yamekubaliana kuunda Tume ya Pamoja ambayo itakuwa na jukumu la kuepusha tofauti za kibiashara kati ya Tanzania na Kenya pamoja na kutolea ufumbuzi changamoto za kibiashara kati ya nchi hizi mbili pindi zinapojitokeza. Tume hii itaongozwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Kenya na kujumuisha Mawaziri wanaohusika na masuala yaJumuiya ya Afrika Mashariki, Biashara, Fedha, Mambo ya Ndani ya Nchi, Kilimo, Uchukuzi na Utalii wa nchi zote mbili.
Vilevile, Mawaziri hawa wataunda mfumo wa kupeana taarifa mara kwa mara kuhusu masuala yenye changamoto za kibiashara kwa lengo la kuepusha kujirudia kwa tofauti kama hizi. Ni matarajio yetu kuwa uamuzi huu wa pamoja utakuza zaidi mahusiano ya kibiashara baina ya nchi hizi mbili. Aidha, tunapenda kuwashukuru wafanyabiashara wa nchi zetu mbili kwa uvumulivu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 24 Julai, 2017



MASWALI NA MAJIBU BAADA YA TAARIFA YA MSINGI
SWALI:  Je ni kwa nini Kenya waliweka vikwazo hivyo hapo awali?
JIBU: Sababu za awali zilizotolewa na Serikali ya Kenya zilidai kwamba bidhaa hizo hazikidhi viwango vya ubora wa kimataifa. Hata hivyo, Wataalamu wa Tanzania wameihakikishia Kenya kuwa bidhaa za unga wa ngano kutoka Tanzania zina ubora  unaokubalika Kimataifa na huuzwa nchi nyingine za Jumuiya ya afrika Mashariki na Afrika ya Kati. Halikadhalika bidhaa ya gesi ya kupikia (LPG) inakidhi viwango vya ubora vya Kimataifa
.
SWALI: Nini msimamo wa Serikali ya Tanzania kuhusu tuhuma za baadhi ya wanasiasa wa Kenya na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu Tanzania kuingilia uchaguzi wa Kenya.
JIBU: Tuhuma hizi hazina ukweli wowote, na hata nilipokuwa  nchini Kenya juzi niliona zimeripotiwa tena na vyombo vya habari vya Kenya. Naomba nikanushe tena kwa mara nyingine, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haijawahi, na wala haifikirii kuingilia maswala ya ndani ya nchi nyingine tunazoshirikiana nazo ikiwemo maswala ya uchaguzi. Hatujawahi kuingilia uchanguzi wa Kenya na hututegemei kufanya hivyo kwenye uchaguzi huu na chaguzi nyingine zozote. Naomba waandishi wa habari, kabla ya kuandika taarifa hizi, wazihakiki mara mbili, na watutafute kutoa ufafanuzi kabla ya kuwapelekea wananchi taarifa hizi za kupotosha. Natoa rai, tuwe waangalifu na walaghai wa nje  wanaotaka kutugombanisha. Nichukue pia fursa hii kuwatakia wananchi wa Kenya uchaguzi mwema wa amani na huru.


SWALI:  Je ni kwanini Tanzania inaonekana kuweka vizingiti vingi vya kibiashara ikilinganishwa na nchi nyingine kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika ya kati kwenye siku za hivi karibuni? Je hii haitakwaza ukuaji wetu wa uchumi kama nchi?
JIBU: Hapana, hata kidogo. Serikali ya Tanzania inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara ili kuwezesha uchumi wa nchi kukua na kuendelea, kutokana na biashara ndani ya bara la Afrika na hususan ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati. Tanzania kwa siku za hivi karibuni chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Tano, Mhe. John Joseph Pombe Magufuli, imefanya mageuzi makubwa kwenye taasisi zetu za bandari na ushuru yaani TRA. Hatua hizi zinalenga kwenye kuziba mianya iliyokuwepo huko nyuma ambayo ilisababisha ukusanywaji hafifu wa mapato. Ni wazi sasa mambo yanaenda kwa uwazi zaidi na ushuru unatozwa na kukusanywa kwa wakati. Tuna hakika sasa changamoto hizi zimepungua na nchi jirani zitaendelea kufanya biashara na sisi bila vikwazo.

SWALI: Kabla ya kuunda hii kamati ya kutatua changamoto zilizojitokeza hivi karibuni, Jumuiya ya Afrika Mashariki imekua ikitatua vipi changamoto kama hizi za kibiashara hususan kwenye nchi zenye ushindani mkubwa kama Kenya na Tanzania?
JIBU: Jumuiya ya Afrika Mashariki imejiwekea misingi imara na muhimu ya kutatua changamoto pindi zinapojitokeza. Hivyo ukiacha jopo la wataalam wa Serikalini kuna Baraza la Mawaziri wa Biashara wa Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki  ambao pia huweza kupendekeza ufumbuzi wa changamoto mbalimbali kwa wakuu wa nchi ili kutatua changamoto hizi. Lakini kutokana na ukaribu uliopo baina ya Tanzania na Kenya, hili la sasa tumelitatua kwa haraka na kwenda mbele zaidi kuunda tume ya mawaziri wa nchi zetu mbili ili huko baadae tuweze kutatua masuala kama haya mapema sana kabla ya kuathiri biashara kati ya nchi zetu mbili.

Ni dhahiri kwamba nchi zetu mbili ni jirani na tunalindwa na Itifaki za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, lakini pia tuna ushindani kati yetu. Na ili tupate maendeleo ni lazima kuweka ushindani wenye tija kwa manufaa ya ukanda wetu na wananchi wetu. Japo kuwa Kenya ipo kwenye kundi la nchi zenye kipato cha kati, uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi kubwa na ni hali ya kawaida kwa changamoto kama hizi kujitokeza pindi nchi zinapokuwa katika ushindani wa kiuchumi.Kwa namna ya pekee naomba kusifu tena hekima za Viongozi wetu wa Juu kwa kutatua changamoto hizi kwa wakati.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.