TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola nchini
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mheshimiwa Patricia Scotland anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi
ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 10 hadi 12 Agosti, 2017.
Lengo la ziara hiyo ni kueleza Viongozi wa Ngazi za
Juu wa Taifa kuhusu mageuzi yanayofanywa
na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola na vipaumbele vya Jumuiya hiyo kwa sasa; Hatua
zinazochukuliwa ili kuimarisha kazi za Jumuiya hiyo na kutoa taarifa kuhusu
Mkutano wa Wakuu Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaotarajiwa kufanyika
London, Uingereza mwezi Aprili, 2018.
Mageuzi hayo yanajumuisha kuondoa vyeo vya Naibu
Makatibu Wakuu watatu na kupunguza idadi ya Wakurugenzi kutoka 12 hadi 6.
Mageuzi haya yataiwezesha Jumuiya kuokoa kiasi cha Pauni milioni 3 kwa mwaka. Mageuzi
mengine ni ya kuanzisha nafasi tano za Maafisa Waandamizi kutoka maeneo ya
kijiografia ya Jumuiya ya Madola kwa maana ya Afrika, Ulaya na Amerika,
Karibeani, Asia na Pacific Kusini. Nafasi hizi zitaziba zile za Naibu Makatibu
Wakuu.
Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Scotland atakutana na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo
tarehe 11 Agosti, 2017, Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha, Mhe. Scotland ataonana na
Mawaziri mbalimbali kwa nyakati tofauti ikiwa ni pamoja na Mhe. Prof. Joyce
Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. January Makamba,
Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Mhe. Scotland na ujumbe wake wataondoka
nchini tarehe 12 Agosti, 2017 kuelekea Msumbiji.
Historia
fupi kuhusu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola,
Mhe. Patricia Scotland alichaguliwa kwenye nafasi hiyo mwezi Novemba, 2015
wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali (CHOGM) uliofanyika nchini
Malta. Kabla ya kuchaguliwa kwake Jumuiya hiyo iliongozwa na Bw. Kamalesh
Sharma ambaye alishikilia nafasi hiyo kuanzia mwaka 2008 hadi 2016.
Jumuiya
ya Madola
Jumuiya ya Madola ni Umoja
ulioanzishwa mwanzoni mwa karne ya 20. Jumuiya hiyo inajumuisha Uingereza
pamoja na nchi ambazo zilikuwa koloni la Uingereza. Uanachama wa Jumuiya hiyo
kwa sasa hauzingatii kigezo cha koloni hivyo nchi yoyyote inaweza kujiunga na
Jumuiya ya Madola kama itapenda. Malkia ndiye Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya
Madola.
Jukumu kubwa la Jumuiya ya Madola
ni kuhakikisha nchi wanachama zinajikwamua kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa
kutumia jukwaa la majadiliano, makubaliano na utekelezaji.
Ushiriki wa Tanzania katika Jumuiya ya Madola
Jumuiya ya Madola inajumuisha nchi
52 Tanzania ikiwa ni mwanachama wa Jumuiya hiyo tangu mwaka 1961. Tangu
kujiunga kwake, Tanzania imewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya
Jumuiya hiyo. Miongoni mwa nafasi hizo ni ile ya Uenyekiti wa Kundi la Mawaziri
la Utekelezaji la Jumuiya ya Madola (Commonwealth Ministrial Action Group
(CMAG). Kundi hili lilijumuisha Mawaziri tisa ambao walipewa jukumu la
kusimamia misingi mikuu ya Jumuiya ya Madola. Tanzania ilishikilia nafasi hii
kuanzia mwaka 2013 hadi 2015.
Pia Tanzania ni mjumbe kwenye Bunge
la Jumuiya ya Madola (CPA). Kutokana na mchango mkubwa wa Tanzania kwenye
Jumuiya ya Madola, kuanzia mwaka 2007 hadi 2014 Marehemu Dkt. William F. Shija
aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Bunge hilo. Aidha, mwaka 2009 Tanzania ilikuwa
mwenyeji wa Mkutano wa 55 wa Bunge la Jumuiya ya Madola uliofanyika Jijini
Arusha.
Aidha, miongoni mwa faida ambazo
Tanzania imepata kutokana na kujiunga na Jumuiya hii ni pamoja na kukuza
biashara na uwekezaji na nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola zikiwemo
Uingereza, India, Kenya na Afrika Kusini. Nchi hizi ni miongoni mwa nchi
zilizowekeza zaidi kwa biashara nchini Tanzania.
Tanzania imenufaika kwenye masuala
ya Teknolojia kupitia Taasisi ya
Commonwealth of Learning (COL) ambayo inahamasisha mafunzo ya wazi na ya mbali
miongoni mwa nchi wanachama. Pia Jumuiya ya Madola ina mchango mkubwa kwenye mageuzi katika Sekta ya Umma na utoaji mafunzo, kozi na
misaada mbalimbali ya kiufundi kupitia Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola na
Mfuko wa ushirikiano wa Kiufundi wa
Jumuiya ya Madola (CFTC).
Tanzania imekuwa mshiriki mzuri wa
michezo maarufu ya Jumuiya ya Madola ambayo inalenga kuhamasisha ushirikiano na
urafiki miongoni mwa nchi wanachama. Itakumbukwa kuwa mwaka 1974 Bw. Filbert Bayi
alivunja rekodi kwa kukimbia mita 1,500
mashindano yaliyofanyika huko Christchurch, New Zealand.
Michezo ya Madola hufanyika kila
baada ya miaka minne. Tanzania inajiandaa kushiriki kwenye michezo ya Madola itakayofanyika mwezi Aprili, 2018
huko Gold Coast, Australia.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Dar es Salaam
09 Agosti, 2017
|