Sunday, June 14, 2020

WACHEZAJI WA MASHINDANO YA DIPLOMATIC GOLF' WAMUAGA MKURUGENZI MKAAZI WA WFP


Wachezaji wa Mashindano ya Diplomatic Golf mchezo ambao  unaoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wamemuaga mchezaji mwenzao ambae pia ni Mkurugenzi mkaazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bw. Michael Dunford.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro, amebainisha hayo wakati walipokuwa wakifanya mazoezi pamoja na wachezaji wengine akiwemo, Mkurugenzi mkaazi wa (WFP) Bw. Michael Dunford leo katika viwanja vya gymkhana jijini Dar es Salaam. 

Tumekutana Jijini Dar es Salaam, kumuaga mcheza mwenzetu Michael Danford gofl ambaye anakwenda Nairobi kikazi……. limekuwa pambano kali lakini tumemaliza salama.

Pia tutakuwa na fursa ya kumpa zawadi zilizoandaliwa na wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na washindi wengine.

Mchezo wa leo ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kumuaga Bw. Michael Dunford ambaye amemaliza muda wake wa kufanya kazi hapa nchini ambapo kwa sasa amepangwa kikazi katika nchi jirani ya Kenya.

"Diplomatic Golf, ni fursa mahsusi kwa mawaziri, wabunge, wanasiasa, wanadiplomasia na wananchi wote wa kawaida kukutana na kubadilishana uzoefu wa mchezo huo na kutengeneza njia mbadala ya kuikuza tasnia hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wapenda golf," Amesema Dkt. Ndumbaro.

Kwa upande wake, Mkurugenzi mkaazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bw. Michael Dunford amesema kuwa mchezo ulikuwa mzuri na wakufurahisha.

"Mchezo wetu wa leo ulikuwa mzuri sana na wakufuraisha…..mimi pamoja na Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro tumepata alama sawa," Amesema Bw. Dunford 

Mwaka 2019, Mashindano ya Diplomatic Golf yalifanyika visiwani Zanzibar katika Viwanja vya Zanzibar Golf Course Sea Cliff, ambapo mwaka huu yanatarajiwa kuwa tofauti huku vitu vingi vikiwa vimeboreshwa zaidi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro akicheza golf katika viwanja vya gymkhana leo jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi mkaazi wa (WFP) Bw. Michael Dunford akicheza golf katika viwanja vya gymkhana leo jijini Dar es Salaam


Wachezaji wa Mashindano ya Diplomatic Golf wakiwa katika picha ya pamoja katika viwanja vya gymkhana leo jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ndumbaro akimkabidhi Mkurugenzi mkaazi wa (WFP) Bw. Michael Dunford moja kati ya zawadi zilizoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje


Mkurugenzi mkaazi wa (WFP) Bw. Michael Dunford akipokea moja kati ya zawadi zilizoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje kutoka kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ndumbaro 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ndumbaro akiagana na Mkurugenzi mkaazi wa (WFP) Bw. Michael Dunford 


DKT. NDUMBARO ASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO CHA RAIS NKURUNZIZA


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amesaini kitabu cha maombolezo katika ubalozi wa Burundi nchini kufuatia kifo cha Rais wa Taifa hilo Pierre Nkurunziza aliyefariki Juni 08, 2020.

Akizungumza mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo katika ubalozi ubalozi wa Burundi nchini, Jijini Dar es Salaam Dkt. Ndumbaro ametoa pole kwa wananchi wote wa Burundi na kuwasihi kuendelea kuwa watulivu na wastahimilivu wakati huu wa msiba.

"Kusaini kitabu cha maombolezo ni ishara ya ushirikiano wetu, umoja wetu na undugu wetu na ndugu zetu wa Burundi. Kifo cha Rais Nkurunzinza kinawahusu pia watanzania kwa sababu Rais Nkurunzinza ni Rais aliyekuwa karibu sana na Tanzania kuliko nchi nyingine yeyote ile, lakini pia Burundi ipo karibu sana na Tanzania, Amesema Dkt. Ndumbaro.

Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa, Pengo la Rais Nkurunzinza ni pengo kubwa sana kwa watanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Afrika kwa ujumla.

Nae Balozi wa Burundi nchini, Mhe. Gervais Abayeho, amemshukuru Naibu Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro kwa kufika kwake kuhani msiba huo na kuongeza kuwa hali hiyo inaonesha upendo ambao unaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya mataifa hayo mawili.

Aidha, Serikali ya Burundi kupitia ubalozi wake hapa nchini, imetoa mualiko kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wa kushiriki mazishi ya Rais Nkurunzinza yanayotarajiwa kufanyika Alhamisi tarehe 18 Juni 2020 nchini Burundi.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akisaini kitabu cha maombolezo katika ubalozi wa Burundi nchini leo Jijini Dar es Salaam



Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ndumbaro akisaini kitabu cha maombolezo katika ubalozi wa Burundi nchini leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Balozi wa Burundi nchini, Mhe. Gervais Abayeho.  



Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ndumbaro akisaini kitabu cha maombolezo katika ubalozi wa Burundi nchini leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Balozi wa Burundi nchini, Mhe. Gervais Abayeho.  



Friday, June 12, 2020

KATIBU MKUU BALOZI BRIGADIA JENERALI IBUGE AMEKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA UJUMBE KUTOKA NMB

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigadia Jenerali Wilbert A.Ibuge akiwa na Ujumbe kutoka National Microfinance Bank (NMB) punde baada ya kuwasili katika Ofisi za Wizara Mtumba, Dodoma.

Ujumbe kutoka NMB ukiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Huduma na Mahusiano ya Serikali,  Bi. Vicky Bishumbo ulitembelea Wizara kwa lengo la kuwasilisha mkakati wao wa namna walivyo jiandaa kuzifika fursa zinazopatikana kwenye soko la fedha la nje (kimataifa) katika kutoa huduma na kujitengenezea faida. Sambamba na hilo walionyesha namna wanavyoshiriki katika kuhudumia Wawekezaji wa nje kupitia sekta ya fedha. 

Katibu Mkuu Balozi Brigadia Jenerali Ibuge kwa upande wake amewapongeza na kuwashukuru NMB kwa namna wanavyoshirikiana na Serikali katika kujenga uchumi wa nchi na namna wanavyoshiriki katika shughuli nyingi za kuisaidia jamii, ikiwemo kutoa misaada wakati wa majanga na udhamini wao katika shughuli mbalimbali za Serikali. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigadia Jenerali Wilbert A.Ibuge akisimsikiliza Bw. Jeremiah Lymo kutoka NMB wakati akiwasilisha mada. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigadia Jenerali Wilbert A. Ibuge akichangia jambo wakati wa mazungumzo  na ujumbe kutoka NMB 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigadia Jenerali Wilbert A. Ibuge akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa NMB na baadhi ya Watumishi wa Wizara

TAARIFA KWA UMMA FURSA YA KAZI YA MCHAMBUZI WA MASUALA YA BIASHARA SEKRETARIETI YA JUMUIYA YA MADOLA, LONDON


Thursday, June 11, 2020

TAARIFA KWA UMMA WATANZANIA 146 WALIOKWAMA NCHINI SAUDI ARABIA KUTOKANA NA MLIPUKO WA UGONJWA WA COVID-19 WAREJEA NCHINI


MKURUGENZI MKAZI WA WFP APONGEZA UAMUZI WA RAIS DKT.JOHN POMBE MAGUFULI WA KUTOWEKA ZUIO LA KUTOKA NJE (LOCKDOWN) KATIKA KIPINDI CHA MAPAMBANO YA UGONJWA WA COVID 19.




 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brig. Jen. Wilbert A. Ibuge na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bw. Michael Dunford wakisalimia walipokuna kwa mazungumzo jijini Dodoma
  Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bw. Michael Dunford  ametembelea vikundi vya wakulima vinavyofadhiliwa na miradi ya Shirika hilo Kibaigwa mkoani Dodoma. Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kupata mrejesho wa maendeleo ya mradi kutoka kwa wanakikundi, na kupokea mapendekezo ya kuboresha maradi huo. 
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bw. Michael Dunford, akimsikiliza mmoja wa  wanufaika wa ufadhili wa WFP alipowatembelea wanufaika hao Kibaigwa, Dodoma.

Wanakikundi wakiwa katika majadala na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bw. Michael Dunford .



Monday, June 8, 2020

SERIKALI YAAGIZA CHUO CHA DIPLOMASIA KUONGEZA TAFITI, MACHAPISHO


Serikali imekiagiza Chuo cha Diplomasia kujikita kuongeza tafiti pamoja na machapisho mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha wahitimu wa chuo hicho kutoa mchango wao katika Taifa hususani wakati huu wa utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi.

Maagizo hayo yametolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakati alipotembelea chuo hicho na kuongea na wahadhiri, wafanyakazi pamoja na wanafunzi.

Dkt. Ndumbaro amesema ili chuo cha diplomasia kiendelee kuheshimika zaidi duniani lazima kihakikishe kuwa kinazalisha tafiti na machapisho ya kutosha.

"Utafiti na machapisho siyo suala la wahadhiri peke yao…..siyo suala la wanafunzi peke yao ni suala la wanachuo…… mawazo yenu lazima yafanyiwe utafiti kwa kushirikiana na wahadiri wenu na ni lazima tuwe na machapisho zaidi," Amesema DKt. Ndumbaro

Naibu Waziri ameongeza kuwa moja kati ya changamoto inayoikumba diplomasia hivi sasa ni mabadiliko ya mifumo mbalimbali duniani ambapo wanadiplomasia wanapaswa kujua kuwa dunia ipo katika mlengo upi, hivyo vyema mkajikita katika tafiti zenu ili kuweza kusaidia kufafanua masuala ya kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa yanayotokea duniani.

"Lakini pia niliagiza muongeze lugha zaidi kwa sababu pia diplomasia pia ni mawasiliano na unawasiliana na watu wa lugha tofauti tofauti, kwa hiyo tuongeze lugha mbalimbali ili diplomasia iweze kufanya kazi yake," Amesema DKt. Ndumbaro.

Aida, Naibu Waziri ameagiza pia chuo hicho kuanzisha semina za kila mwezi ambapo zitajumuisha Wahadiri na wanafunzi pamoja na mabalozi wastaafu kwa lengo la kujadili mambo yanayohusu diplomasia na kuwapa uzoefu wa masuala ya kidiplomasia.

Wanafunzi kwa upande wao wamepata fursa ya kumuelezea Naibu Waziri changamoto mbalimbali zinazo wakabili zikiwemo za kupata asilimia ndogo za mkopo wa elimu ya juu, ukosefu wa mafunzo kwa vitendo, ukosefu wa mabweni pamoja na mazingira ambayo siyo wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

"Mkopo tunaopewa ni mdogo sana na hautoshi hivyo tunaomba serikali itusaidie kutuongezea fedha za mkopo ili tuweze kukidhi mahitaji yetu wakati tunapokuwa chuoni,"Amesema Isack Sadock  

Pia, Dkt. Ndumbaro baada ya kusikiliza changamoto zinazowakabili wanafunzi chuoni hapo, ameuagiza uongozi wa chuo kuandaa na kuratibu mafunzo kwa vitendo badala ya kufuatiliwa na wanafunzi, kutoa huduma stahiki kwa wanafunzi wenye ulemavu/maitaji maalumu ili waweze kusoma katika mazingira mazuri.

Nae Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Jeremia Ponera amemhakikishia Naibu Waziri kuwa chuo kitayafanyia kazi na kuyatekeleza maagizo yote aliyoyatoa.

"Mhe. Naibu Waziri naomba nikuhakikishie kuwa maagizo yako tumeyapokea……….mimi kwa kushirikiana na menejimenti, wahadhiri na wafanyakazi tayafanyia kazi kwa wakati," Amesema Dkt. Ponera  
Aidha, Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro amekagua mradi wa ujenzi wa jengo jipya la chuo cha Diplomasia.

Katika hatua nyingine, ametoa msimamo wa Serikali kuhusu changamoto zinazojitokeza mipakani hasa katika mpaka wa Tanzania na Kenya na kusema kuwa Serikali ipo kwenye mazungumzo na Kenya ili kuweza kubaini tatizo ni kitu gani.

"Kwa sasa tupo kwenye majadiliano na wenzetu wa Kenya na kuona tatizo ni kitu gani je ni corona tu au ni zaidi ya corona? Msimamo wa serikali yetu ni kuwa kila nchi ipime watu wake…..na tunaamini huo ndiyo msimamo sahihi wa diplomasia ya uchumi," Amesema Dkt. Ndumbaro.

Chuo cha Diplomasia kilianzishwa rasmi tarehe 13 Januari 1978 kwa kusainiwa Makubaliano yaliyofanywa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wa wakati huo, Mhe. Benjamini William Mkapa wa Tanzania na Mhe. Joaquim Chissano wa Msumbiji.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Jeremia Ponera (aliyesimama ktk meza kuu) akimkaribisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakati alipotembelea chuo hicho leo na kuongea na wahadhiri, wafanyakazi pamoja na wanafunzi 

Baadhi ya wanafunzi wakimsikiliza Mhe. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (hayupo pichani)

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro akiongea na wanafunzi (hawapo pichani)

Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro akioneshwa mchoro wa jengo jipya la chuo cha Diplomasia na meneja mradi Abdalla Khama 

Meneja mradi wa jengo jipya Abdalla Khama akimuelezea jambo Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro wakati alipotembelea eneo la mradi

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Jeremia Ponera (aliyesimama) akimkaribisha Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro (aliyekaa wa kwanza kushoto) kwenye kikao cha menejimenti ya chuo  




Saturday, June 6, 2020

UNFORGETTABLE EXPERIENCE


NCHI ZA NORDIC ZAAHIDI KUENDELEZA, KUIMARISHA UHUSIANO WAKE NA TANZANIA


Nchi za NORDIC ambazo ni Norway, Sweden, Finland na Dernmark zimeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania na kuhakikisha kuwa Tanzania inasonga mbele katika maendeleo yake kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Akiongea wakati wa maadhimisho ya wiki ya Nordic jijini Dar es Salaam, Balozi wa Norway nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen amesema kuwa nchi za Nordic zimeadhimisha wiki ya Nordic nchini Tanzania na zimejadili masuala ya malengo ya maendeleo endelevu ambapo pamoja na mambo mengine, wametumia wiki ya Nordic kuendeleza uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Nordic na Tanzania.

"Wiki ya Nordic inatoa fursa ya kushirikiana na kujifunza mambo mbalimbali yakiwemo ya kijamii, kisiasa na kichumi pamoja na kupata uzoefu wa maendeleo kutoka kwa kila mmoja wetu," Amesema Balozi Jacobsen.

Ameongeza kuwa, nchi za Nordic zimejidhatiti kufanya kazi kwa karibu na Tanzania ili kuhakikisha kuwa Tanzania inasonga mbele katika maendeleo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiongea mara baada ya kukabidiwa mpira ulioandikwa malengo 17 ya maendeleo endelevu ikiwa ni ishara ya kuhamasisha maendeleo ya Tanzania, amesema kuwa mpira huo ni ishara ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi za Nordic.

"Ushirikiano wetu (Tanzania) na nchi za Nordic ni wa muda mrefu kabla ya uhuru na hata baada ya uhuru. Tumekuwa tukifurahia ushirikiano wetu na nchi za Nordic na umekuwa ukimarika kila wakati, ni matumaini yetu sisi kama serikali kuwa uhusiano utaendelea kuimarika zaidi," amesema Dkt. Ndumbaro     

Mwezi Novemba 2019, ulifanyika Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya nje wa Afrika na Nordic, ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo uzikutanisha nchi za Afrika na Nordic na kutoa fursa ya kujadili masuala mbalimbali yakiwemo, elimu, kilimo biashara na uwekezaji.

Balozi wa Norway nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen akimkabidhi mpira ulioandikwa malengo 17 ya maendeleo endelevu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.  Damas Ndumbaro (Mb) jijini Dar es Salaam 

Kaimu Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Mette Pilgaard (wa pili kushoto) akiwaelezea jambo Mabalozi wa Sweden, Mhe. Anders Sjöberg, (wa kwanza kushoto), Norway Mhe. Elisabeth Jacobsen na Finland Mhe. Riitta Swan pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.   Damas Ndumbaro (Mb) akiwaelezea jambo Mabalozi wa nchini za Nordic

Balozi wa Sweden nchini, Mhe. Anders Sjöberg (wa kwanza kushoto) akiongea na mabalozi wenzake wa nchini za Nordic pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.  Damas Ndumbaro (Mb)         

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.   Damas Ndumbaro (Mb) akiwa ameshikilia mpira ulioandikwa malengo 17 ya maendeleo endelevu katika picha ya pamoja na mabalozi wa nchini za Nordic   

Mabalozi wa nchini za Nordic pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakipiga makofi mara baada ya naibu waziri kukabidiwa mpira ulioandikwa malengo 17 ya maendeleo endelevu

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.   Damas Ndumbaro (Mb) pamoja na mabalozi wa nchini za Nordic wakiwa wameshikilia mpira ulioandikwa malengo 17 ya maendeleo endelevu


Monday, June 1, 2020

KATIBU MKUU BALOZI KANALI IBUGE AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA TAIFA LA ISRAEL KWA TANZANIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Taifa la Israel  kwa Tanzania Mhe. Oded Joseph ambaye analiwakilisha Taifa hilo kutokea Nairobi, Kenya.

Kanali Balozi Ibuge katika mazungumzo hayo amweleza Balozi Oded, kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kukakabiliana  na kusambaa kwa COVID-19 
na madhara sambamba na madhara cake.
Aidha, pamoja na mambo mengine Wawili hao katika mazungumzo yao wamejadili masuala mbalimbali ikiwemo ya kuendelea kukuza na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na biashara baina ya Tanzania na Israel. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge akifafanua jambo kwa Balozi wa Taifa la Israel nchini Mhe.Balozi Oded wakati wa mazungumzo. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge akiagana na Balozi wa Taifa la Israel nchini Mhe.Balozi Oded  mara baada ya kuhitimisha mazungumzo yao.

Sunday, May 31, 2020

Awamu ya Pili ya Watanzania warejea nchini kutoka India kutokana na ugonjwa wa COVID-19

Baadhi ya watanzania waliokuwa wamekwama India kutokana na ugonjwa wa COVID-19 wakiwa ndani ya ndege maalum ya Air Tanzania wakisubiri kuondoka kurejea Tanzania katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chhatrapati Shivaji Jijini Mumbai tarehe 30 Mei 2020. Serikali ya India ilisitisha huduma ya kuingia na kutoka kwa ndege za kimataifa ikiwa ni moja ya mkakati wa kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19.
Sehemu nyingine ya watanzania waliokuwa wamekwama nchini India wakiwa ndani ya ndege maalum ya Air Tanzania wakisubiri kuondoka kurejea Tanzania katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chhatrapati Shivaji Jijini Mumbai tarehe 30 Mei 2020.

Baadhi ya watanzania waliokuwa wamekwama India wakisubiri kuingia katika ndege maalum ya Air Tanzania katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chhatrapati Shivaji Jijini Mumbai tarehe 30 Mei 2020.

Ndege  aina ya Boeng 787-8 ya Dreamliner ya Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) ikipakia watanzania 119 waliokuwa wamekwama nchini India katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chhatrapati Shivaji Jijini Mumbai tarehe 30 Mei 2020.
================================================
Serikali yarejesha kwa awamu ya pili Watanzania 192 waliokuwa wamekwama nchini India kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19
Ubalozi wa Tanzania nchini India kwa kushirikiana na Shirika la Ndege la Tanzania [ATCL] pamoja na Diaspora wa Tanzania nchini India kwa mara nyingine wamefanikisha safari ya pili ya kuwarejesha nchini Watanzania 192 waliokuwa wamekwama katika miji mbalimbali nchini India. Watanzania hao walikwama kutokana na zuio la kuingia na kutoka kwa ndege za Kimataifa lililowekwa na Serikali ya India kama hatua mojawapo ya kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
Ndege maalum ya aina ya Boeng 787-8 ya Dreamliner ya Shirika la Ndege la Tanzania ilitumwa tena na Serikali Jijini Mumbai kuja kuwachukua Watanzania hao waliokwama nchini India tangu tarehe 22 Machi 2020 lilipowekwa zuio hilo na Serikali ya India. Ndege hiyo iliondoka tarehe 30 Mei 2020 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chhatrapati Shivaji,  Mumbai ikiwa imebeba jumla ya raia wa Tanzania 192, miongoni mwao ni waliokuwa wamekwenda India kwa ajili ya matibabu; wahitimu kutoka vyuo mbali mbali na wanafunzi ambao wanalazimika kurudi nyumbani kwa kuwa vyuo vimefungwa hadi mwezi Agosti/Septemba 2020.
Tofauti na awamu ya kwanza, safari hii pia ilihusisha kuwarejesha nchini India raia wa nchi hiyo wapatao 202 ambao walikuwa wamekwama nchini Tanzania. Hatua hii ya Serikali ya Tanzania itasaidia sana katika kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya India na Tanzania.
Mpaka sasa jumla ya Watanzania 438 wamerejeshwa Tanzania kutoka India kwa utaratibu huu maalum. 

Friday, May 29, 2020

PROF. KABUDI AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA ITALIA NCHINI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge, ambapo walijadili masuala mbalimbali yanayohusu mahusiano baina ya Tanzania na Italia.

Aidha, walitumia mazungumzo hayo kujadili hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania pamoja na Serikali ya Italia katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19. Mhe. Waziri alifahamisha kuwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania kwenye mapambano ya ugonjwa huo zimezingatia mazingiria na hali halisi ya Tanzania pamoja na nchi jirani zinazozunguka Tanzania.

Kwa upande wake Balozi Mengoni alipongeza juhudi hizo za Serikali ambapo alifahamisha kuwa Serikali yake ya Italia inaziunga mkono na kwamba ipo tayari kutoa ushirikiano pale itakapohitajika kufanya hivyo.

Viongozi hao walikubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria baina ya Mataifa hayo mawili ambao umejikita katika sekta za elimu, afya, utalii pamoja na biashara na uwekezaji.


Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akimuelezea jambo Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akimuelezea jambo Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge