Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa China mhe. Wangi Yi atawasili nchini Tanzania kesho kwa ziara ya kikazi ya siku mbili tarehe 7 na 8 Januari 2021.
Prof. Kabudi ametoa kauli hiyo wakati anaongea na waandishi wa Habari leo Wilayani Chato mkoani Geita, ambapo amesema kuwa Waziri Yi atakapokuwa nchini atafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuzindua Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) katika wilaya ya Chato mkoani Geita.
“Hapo kesho mara baada ya Mhe. Yi kuwasili hapa Chato, atazindua Chuo cha VETA cha wilaya ya Chato ambacho kimejengwa kwa fedha za watanzania,” alisema Prof. Kabudi.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa “sababu ya kumuomba afungue chuo hicho ni utamaduni wetu wa kumpa heshima mgeni anapokuja hapa nchini kwetu, sambamba na kutambua elimu ya mafunzo na ufundi stadi ilivyopiga hatua huko nchini China.”
Pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi amesema kuwa Serikali ya China itajenga Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) mkoani Kagera ikiwa ni namna ya kufikia lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga VETA kila Wilaya hapa nchini.
Waziri Kabudi ameongeza kuwa shughuli nyingine zitakazofanywa na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, kuwa ni mazungumzo na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, pamoja na kufanya mazungumzo rasmi kati yake na ujumbe wake kutoka nchini China.
Aidha, shughuli nyingine atakazofanya Waziri Yi ni pamoja na kutembelea mwalo wa Chato ili kuona shughuli za uvuvi, ikizingatiwa kuwa ziwa Viktoria ni ziwa la pili kwa ukubwa dunia Pamoja na kusaini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha tano kutoka Mwanza hadi Isaka chenye urefu wa km 341 ambapo kitagharimu kiasi cha Shilingi trilioni 3.0617
Waziri Kabudi ameogeza kuwa, Februari mwaka huu Serikali ya Tanzania inatarajia kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Guanzhou nchini China ili kukuza sekta ya utalii.
Historia ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya watu wa China ulianza mwaka 1965.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi (Mb) akiwaelezea waandishi wa Habari Chato mkoani Geita (Hawapo pichani)
juu ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi ambaye anatarajiwa
kuwasili nchini Tarehe 7 Januari, 2021.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi (Mb) akiongea na waandishi wa Habari Chato mkoani Geita (Hawapo pichani)
juu ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi. Kulia mwa Prof.
Kabudi ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge, na kushoto mwa Waziri ni
Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Mbelwa Kairuki.
Mkutano
ukiendelea