Monday, December 14, 2020

UBALOZI WA TANZANIA NCHINI QATAR WAANZISHA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO WATANZANIA WANAOAJIRIWA NCHINI HUMO

Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar umeanzisha rasmi programu ya  mafunzo  kwa waajiriwa wapya kutoka Tanzania wanaokwenda kufanya kazi nchini humo.

Mafunzo hayo yameanzishwa kwa makubaliano kati ya Ubalozi na  Kampuni zote zinazoajiri wafanyakazi kutoka Tanzania ambao  Ubalozi huwapatia barua kwa ajili ya kuthibitisha uhalali wao ili kupata kibali cha kuingia nchini humo. Mafunzo hayo ambayo hutolewa mara tu wanapowasili nchini humo, yanalenga kuwajengea uwezo wa kazi pamoja na kuwaelewesha sheria na taratibu za ajira za Qatar pamoja na haki zao za msingi.

Kadhalika, mafunzo hayo  yameanzishwa ili kuwajulisha maadili, mila na utamaduni za Qatar pamoja na kuwahimiza kujua wajibu wao ili kudumisha heshima ya Tanzania kimataifa na kuitangaza vyema nchi. 

Mafunzo ya awali yametolewa tarehe 12 Desemba, 2020 kwa Mabinti 9 kutoka Tanzania ambao wameajiriwa na Kampuni ya Qatar Manpower Solutions (WISA) inayomilikiwa na Serikali kwa ajili kufanya usafi na huduma za ndani. 

Mafunzo hayo ambayo yamesimamiwa na Bw. Volka Gowele, Afisa wa Ubalozi yameendeshwa na Bw. Sahim Ayoub Khatib, Diaspora wa Tanzania na Mwajiriwa kwenye Kampuni ya HBK ya Qatar kwenye Kitengo cha Utawala na Rasilimali Watu. Bw. Khatib amejitolea kusaidia kuendesha mafunzo hayo kwa Watanzania.

Bw. Sahim Ayoub Khatib (mwenye karatasi), Diaspora wa Tanzania nchini Qatar ambaye pia ni Mwajiriwa wa Kampuni ya HBK ya nchini humo akitoa mafunzo kwa Mabinti 9 kutoka Tanzania ambao wameaajiriwa na Kampuni ya Manpower Solutions (WISA) inayomilikiwa na Serikali kwa ajili ya kufanya kazi za usafi na huduma za ndani. Mafunzo hayo ambayo yanalenga kuwajengea uwezo  pamoja na kuwaelewesha sheria na taratibu za ajira za Qatar, yameandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini humo. Mafunzo hayo yalifanyika kwenye Ofisi za Ubalozi hivi karibuni na kusimamiwa na Bw. Volka Gowele (mwenye barakoa), Afisa wa Ubalozi.


Mafunzo yakiendelea kwa Mabinti hao
Mabinti tisa kutoka Tanzania walioshirki mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar


Picha ya pamoja kati ya Bw. Khatib (kushoto), Bw. Gowele (wa pili kushoto) pamoja na Mabinti tisa kutoka Tanzania walioshiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar.

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.