Monday, December 7, 2020

TANZANIA YAUNGA MKONO AZIMIO LA AU KUONGEZA MIAKA 10 YA KUONDOA NA KUTOKOMEZA SILAHA HARAMU

Umoja wa Afrika (AU) umezitaka nchi wanachama wa umoja huo kutilia mkazo azimio la kuondoa na kutokomeza silaha haramu ili kuliondoka na migogoro inayolifanya bara hilo kushindwa kusonga mbele kiuchumi.

Akifungua Mkutano wa 14 wa dharura wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia ya mtandao (virtual Conference) Mwenyekiti wa Umoja huo ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa amesema ni vigumu Bara la Afrika kupiga hatua za kimaendeleo kiuchumi endapo suala la usalama halitapewa kipaumbele na kuruhusu migogoro kuendelea.

Rais, Ramaphosa ameongeza kuwa wakati umefika kwa nchi za afrika hususani zilizopo katika migogoro na vita kuhakikisha kuwa zinatatua vyanzo vya machafuko hayo na kuboresha hali ya kiuchumi kwa wananchi, utawala wa sheria, na kuzingatia misingi ya haki na utawala bora.

Akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Meh. John Pombe Joseph Magufuli katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi amesema mkutano huo ulikuwa unajadili mpango na mkakati wa miaka 10 iliyopita wa kuondoa na kutokomeza silaha haramu na kujenga amani katika bara la Afrika.

"Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeunga mkono azimio la nchi za AU kuongeza miaka mingine 10 ya kutokomeza silaha haramu na kusisitiza tena ushiriki wake kikamilifu katika kuhakikisha kuwa Afrika inatatua migogoro yake yote yenyewe bila kuingiliwa na nchi za nje, lakini pia kuzitaka nchi za Afrika kuzuia mitafaruku na migogoro yote ambayo kwa miaka mingi imeigharimu sana bara la Afrika," Amesema Prof. Kabudi

Prof. Kabudi ameongeza kuwa, toka hatua ya kuondoa na kutokomeza silaha haramu ilipoanza mwaka 2017 hadi 2019, silaha zaidi ya 1,233 zimerejeshwa na Serikali itaendelea na jitihada ya kuhakikisha kuwa inazitambua silaha zote.

Aidha, Prof. Kabudi ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi zote ili kuwa na amani endelevu na utulivu endelevu katika eneo lote la Maziwa Makuu, pia Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa mchango wake katika nchi mbalimbali zenye mapigano ikiwemo DRC halikadhalika katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na sehemu nyingine ambapo vikosi vyake vya kijeshi vitatumwa kulinda amani.     

Nae Rais wa Ghana, Mhe. Nana Akufo-Addo amesema kuwa Ghana inaungana na Umoja wa Afrika (AU) na itaendelea kuhakikisha inaondoa na kutokomeza silaha haramu kwa lengo la kuimarisha masuala ya Amani, umoja na ushirikiano wa nchi za AU.

"Ghana tangu mwaka 2014 tulishaanza mkakati wa kuzuia na kutokomeza matumizi holela silaha haramu kwa kuzihakiki na kuandikisha wamiliki wote wanaomiliki silaha,….….pia mwaka jana 2019 kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) tumeweza kuendelea kudhibiti silaha matumizi ya silaha holela," Amesema Rais Akufo-Addo

Nae Rais wa Somalia, Mhe. Mohamed Farmajo amesema kuwa suala la Amani na usalama ni suala muhimu sana kwenye jamii hivyo Somalia inaungana na Umoja wa Afrika katika kuhakikisha kuwa wanaondoa na kutokomeza silaha haramu na kujenga amani katika bara la Afrika.

Rais Mohammed ameongeza kuwa amani na usalama vitakumbukwa kuwa ni msingi wa maendeleo kwenye katika jamii. Aidha, Rais huyo ameuomba umoja wa Afrika kushirikiana kwa karibu na Somalia katika kuhakikisha kuwa wanatokomeza vikundi vya kigaidi (Alshabab) kwa maendeleo ya ukanda wa Afrika.

Pamoja na mambo mengine, Umoja wa Afrika umekubaliana kuongeza muda wa kuondoa na kutokomeza silaha haramu na kujenga amani katika bara la Afrika kwa kipindi cha miaka 10 ijayo kuanzia mwaka 2021 hadi 2030.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akichangia moja ya agenda katika mkutano wa 14 wa dharua Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandao (virtual Conference) jijini Dar es Salaam 



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akiwa pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe pamoja na washiriki wengine wakifuatilia mkutano wa 14 wa dharua Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandao (virtual Conference) 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.