Monday, March 1, 2021

PROF. KABUDI APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO ZA MABALOZI WATEULE

 

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kupokea nakala za hati za utambulisho za mabalozi wateule hapa nchini pamoja na hati ya utambulisho ya Konseli Mkuu wa China Zanzibar.

Mabalozi waliowasilisha nakala za hati za utambulisho kwa Prof. Kaabudi katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ni Balozi mteule wa Namibia, Mhe. Lebbius Tangeni Tobias na Balozi mteule wa Ireland mhe. Mary O’Neil, pamoja na Konseli Mkuu wa China Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng.

Awali akiongea mara baada ya kupokea nakala ya hati ya utambulisho wa Balozi mteule wa Namibia, Prof. Kabudi amesema kuwa Tanzania na Namibia zimekubaliana kuendeleza kuimarisha sekta ya biashara na uwekezaji, mifugo na uvuvi katika bahari kuu pamoja madini kwa maslahi ya mataifa yote mawili.

“Tanzania na Namibia tuna historia inayofanana iliyoanza tangu vita vya ukombozi wa uhuru wa Namibia….wote tulikuwa makoloni ya Wajerumani, hivyo tumekubaliana kuimarisha sekta za biashara na uwekezaji, na katika maeneo ya mazao ya mifugo, uvuvi, kilimo, na madini, ambapo katika maeneo hayo Tanzania tunayo mengi ya kujifunza kutoka Namibia hasa katika sekta ya mifugo na uvuvi katika bahari kuu,hivyo tukiimarisha maeneo hayo uchumi wan chi zetu mbili utazidi kukua na kuimarika” Amesema Prof. Kabudi

Kwa upande wake Balozi Mteule wa Namibia hapa nchini, Mhe. Lebbius Tangeni Tobias ameahidi kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Namibia.

“Mimi kama mwakilishi wa Serikali ya Namibia nitajitahidi wakati wa utumishi wangu hapa Tanzania kuhakikisha kuwa uhusiano wetu sisi Namibia na Tanzania unazidi kuimarika kwa maslahi mapana ya wananchi wetu wote,” Amesema Mhe. Tobias     

Kadhalika, Prof. Kabudi amepokea nakala ya hati za utambulisho wa Balozi mteule wa Ireland hapa nchini, Mhe. Mary O’Neil ambapo mara baada ya kukabidhi hati za utambulisho Balozi Mteule ameahidi kuendeleza uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Ireland.

“Ni furaha kwangu kuwepo hapa leo na kukabidhi nakala ya hati ya utambulisho wangu hapa nchini Tanzania, napenda kuahidi kwa kipindi nitakachokuwa hapa nitahakikisha kuwa uhusiano wetu wa kidiplomasia unakuwa na kuimarika kwa maslahi ya mataifa yetu,” Amesema Balozi O’Neil

Kwa upande wake Prof. Kabudi amesema kuwa mahusiano ya kibalozi kati ya Tanzania na Ireland yalianza tangu mwaka 1979 ambapo Ireland ilianzisha utaratibu wa kutoa ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu vya Ireland kwa watanzania katika taaluma mbalimbali.

“Mbali na kutoe ufadhili wa elimu kwa Watanzania, tumeongelea masuala ya kuimarisha ufadhili wa masomo, biashara na uwekezaji hasa kwa kutumia teknolojia ya habari pamoja na kuimarisha uvuvi wa bahari kuu na katika kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini tutaangalia maeneo mapya ya ushirikiano ili tuweze kuendele kuimarisha ushirikiano baina yetu na Ireland,” Amesema Prof. Kabudi.

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kupokea hati ya utambulisho wa Konseli Mkuu wa China Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng.

Prof. Kabudi amesema kuwa China imekuwa ikiisaidia sana Zanzibar tangu mapinduzi ya mwaka 1964, katika maeneo mbalimbali kama vile ujenzi wa barabara, ujenzi wa shule, ukarabati wa uwanja wa ndege, hospitali ya Mnazi mmoja pamoja na Abdallah Mzee………na “tumekubaliana kuwa tutaendelea kuimarisha mahusiano kati ya China na Tanzania – Zanzibar ikiwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” Amesema Prof. Kabudi   

Nae Konseli Mkuu wa China Zanzibar amesema kuwa China kama taifa lililoendelea wataendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha mahusiano ya China na Tanzania yanaimarika kijamii, kisiasa na kiuchumi.

“China inaunga mkono umoja, amani na mshikamano wa Tanzania, sisi tumekuwa marafiki wa muda mrefu na tutaendelea kusaidiana ili kuhakikisha kuwa mahusiano kati ya China na Tanzania yanazidi kuimarika hasa katika kipindi hiki cha uongozi wa Rais Magufuli na Rais Mwinyi,” Amesema Mhe. Zhisheng 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mteule  wa Namibia, Mhe. Lebbius Tangeni Tobias leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Balozi mteule wa Ireland mhe. Mary O’Neil akimkabidhi nakala ya hati za utambulisho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipokea hati za utambulisho kutoka Konseli Mkuu wa China Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng 

Friday, February 26, 2021

WAKUU WA NCHI WA AFRIKA MASHARIKI KUFANYAUTEUZI WA VIONGOZI WA JUMUIYA

Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanatarajiwa kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa Jamuiya katika Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi hao unaotarajiwa kufanyika Jumamosi tarehe 27 Februari, 2021. Viongozi waonatarajiwa kuteuliwa ni wale wa ngazi za maaumuzi katika Jumuiya ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya na Katibu Mkuu wa Jumuiya.

Haya yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) muda mfupi baada ya hitimisha Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki. Mkutano huu uliofanyika kwa njia ya ana kwa ana na video umefanyika katika ngazi tatu, ambazo ni; ngazi ya Wataalam (tarehe 22-23 Februari), ngazi ya Makatibu Wakuu (tarehe 24 Februari) na hatimaye ngazi ya Mawaziri tarehe 25 Februari 2021. 

Waziri Kabudi aliendelea kueleza kuwa Mkutano wa Baraza la Mawaziri limepitia nyaraka mbalimbali zinazohusu maendeleo na utendaji wa Taasisi mbalimbali za Jumuiya ambapo wamebaini kuwa, licha ya kuwepo kwa changamoto za Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID-19) Jumuiya pamoja na Taasisi zake zimeendelea kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Kila mwaka, Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki hukutana mara mbili, mkutano mmoja hufanyika mara moja kabla ya mkutano wa Wakuu wa Wakuu wa Nchi. Mikutano ya baraza husaidia kudumisha uhusiano kati ya maamuzi ya kisiasa yaliyochukuliwa kwenye Mkutano na utendaji wa kila siku wa Jumuiya. Kanuni, maagizo na maamuzi yaliyochukuliwa au kutolewa na Baraza yanatekelezwa na Nchi Wanachama na Taasisi zingine zote za Jumuiya isipokuwa Wakuu wa Nchi, Mahakama na Bunge.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akichangia jambo kwenye Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) akichangia jambo kwenye Mkutano wa Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Ole Nasha (Mb) akichangia jambo kwenye Mkutano wa Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki.
Washiriki kutoka Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea
Kutoka kushoto; Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiwa unapigwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akisaini ripoti ya Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki
Mkutano ukiendelea

Wednesday, February 24, 2021

MKUTANO WA 21 WA WAKUU NCHI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KUFANYIKA FEBRUARI 27

 Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam   

Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepangwa kufanyika Jumamosi, 27 Februari, 2021 kwa njia ya mtandao (video conference).

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amewaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa mkutano huo ni muhimu kwa sababu ya maamuzi ya msingi ya kuiwezesha jumuiya hiyo iweze kuendelea kufanya kazi zake.

 

“………Jambo la kwanza ni uteuzi wa Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Afrika mashariki, kwa hiyo Wakuu wa nchi watamchagua Katibu Mkuu mpya siku hiyo,” Amesema Prof. Kabudi na kuongeza kuwa mkutano huo pia utafanya uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (The East African Court of Justice) kutokana na baadhi ya majaji kufikia umri wa kustaafu wa miaka 70, ambapo Tanzania imempendekeza jaji Yohane Masara kuwa jaji wa jopo la kwanza la mahakama ya Afrika Mashariki.

 

“Pamoja na kuteuliwa kwa majaji hao, pia Wakuu wa nchi watamteua Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (Judge President) pamoja na kumchagua Makamu wa Rais (Vice President) kwa ngazi ya Rufaa ya Mahakama hiyo, lakini katika ngazi ya awali Mkutano huo utamchagua Principla Judge wa Mahakama hiyo, kwa hiyo mtaona hizo ni baadhi ya shughuli zilizopelekea Wakuu wa nchi wakutane ili kuweza kufanya teuzi hizo muhimu ili shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki ziweze kuendelea”  Ameongeza Prof. Kabudi

 

Prof. Kabudi ameongeza kuwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pia utajadili Muswaada ulipitishwa na Bunge la Afrika Mashariki kwa ajili ya kupata bajeti.

 

Mkutano huo utatanguliwa na mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki utakaofanyika Alhamisi tarehe 25 Februari 2021 kwa ajili ya kuandaa mkutano wa wakuu wa nchi. Aidha, mkutano wa Baraza la Mawaziri umetanguliwa na mkutano Wataalam ulifanyika tarehe 22-23 Februari na mkutano wa Makatibu Wakuu ulifanyika tarehe 24 Februari.

 

Tarehe 1 Januari 2019, Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame alikabidhiwa Uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Mkutano wa wakuu wa jumuiya hiyo jijini Arusha Tanzania.

 

Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi ameelezea kuhusu ziara ya kikazi aliyoifanya nchini Ufaransa kuanzia tarehe 16 mpaka 21 Februari 2021, kufuatia mwaliko wa Mhe. Jean-Yves Le Drian, Waziri anayeshughulikia Masuala ya Ulaya na Mambo ya Nje wa Ufaransa na kuelezea mafanikio makubwa ya ziara hiyo.

 

“Pamoja na mambo mengine niliweza kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali ya Ufaransa, Umoja wa Wafanyabiashara wa Ufaransa (MEDEF), Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Uongozi wa Kampuni ya Total, Kundi la Maseneta wa Bunge la Ufaransa ambao ni Marafiki wa Tanzania, Uongozi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Wadau wa Utalii pamoja na kuzungumza na Watanzania wanaoishi nchini Ufaransa,” Amesema Prof. Kabudi.


Aidha, kupitia ziara hiyo, Ufaransa imeeleza kuwa itaendelea kuhamasisha Makampuni yake kuja kuwekeza Tanzania pamoja na kuhamasisha watalii kuja kuwekeza Tanzania, kuiunga mkono Tanzania katika masuala mbalimbali kwenye ngazi ya Umoja wa Mataifa.

Mengine ni kuwa Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo la AFD itaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleao hapa nchini hususan kwenye sekta ya maji, elimu, nishati, miundombinu, utalii, ulinzi na usalama;na Ufaransa kuwa tayari kushirikiana na Tanzania kwenye masuala mbalimbali yanayohusu ulinzi na Usalama.

Mafanikio mengine ni pamoja na kukubaliana kuanza mara moja mchakato wa kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi zinazotumika kwenye Umoja wa Mataifa. Nilimweleza mafanikio yaliyopatikana kwenye lugha ya Kiswahili ikiwa ni pamoja na kuwa miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa zaidi barani Afrika pamoja na kutumika kama lugha rasmi kwenye Umoja wa Afrika (AU) na SADC;

“Tulikubaliana kuanza mchakato ili kuwa na siku rasmi ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili duniani kila mwaka. Nilipendekeza tarehe 7 Julai kila mwaka kwa kuzingatia kuwa tarehe hiyo ndio kilizaliwa Chama cha TANU. TANU ilikifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kupigania uhuru wa Tanganyika wakati huo. Tumeona ni jambo jema kuienzi tarehe hiyo muhimu kwenye historia ya nchi yetu,” Amesema Prof. Kabudi

Kupitia ziara hiyo, Prof. Kabudi aliweza kuyakaribisha Makampuni ya Ufaransa kuja kuwekeza nchini hususan kwenye sekta ya viwanda, kilimo, nishati, maji, elimu, miundombinu, uvuvi na utalii. Makampuni hayo yalionesha kuridhika na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi wa Tanzania.

“Baadhi ya Makampuni makubwa yaliyoshiriki majadiliano hayo ni pamoja na Bureau Veritas; Mitsubishi II; Biolore Transport and Logistics; Eutelsat Company; Artelia Company; Catering International Services-CIS; Systra Company;  Transder Group; Credit Agricole Corporate and Investment Bank; Air Bus; na Bouyegues Construction. Mengi ya makampuni haya tayari yamefanya uwekezaji mkubwa nchini katika maeneo mbalimbali,” Amesema Prof. Kabudi.

Aidha, makampuni hayo yameonesha utayari wa kutekeleza miradi hapa nchini kwa kutumia fedha kutoka Serikali ya Ufaransa zitakazotolewa kama mkopo wenye masharti nafuu. Tumeyakaribisha Makampuni hayo kuja nchini ili kukutana na wataalam wetu kwa ajili ya majadiliano.

Prof. Kabudi ameelea kuwa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha majadiliano ya miradi ya kimkakati kwa Tanzania katika sekta ya maji safi na usafi wa mazingira, nishati na miundombinu ambapo tayari jumla ya fedha Euro milioni 791.70 tayari zimeshatengwa kwa ajili ya miradi hiyo. Fedha hizo zitaelekezwa katika baadhi ya miradi ambayo ni mradi wa ujenzi wa awamu ya tano ya mwendokasi BRT Phase 5 (Euro milioni 150), mradi wa Maji safi na Usafi wa Mazingira mkoani Shinyanga (Euro milioni 70), ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Kakono (Euro milioni 100), mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia jua chini ya TANESCO (Euro milioni 130) na mradi wa kuunganisha umeme Tanzania na Uganda (Euro milioni 100).

Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amewasihi watanzania kuheshimu katiba na kuacha mara moja tabia ya kusambaza taarifa za uongo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwasomea waandishi wa habari (hawapo pichani) moja ya kifungu cha katiba kuhusu mipaka ya haki na Uhuru na hifadhi kwa haki na wajibu jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) aina za cocoa zinazozalishwa Tanzania na kuuzwa nchini Ufaransa jijini Dar es Salaam



Tuesday, February 23, 2021

MKUTANO WA 40 WA KAWAIDA WA BARAZA LA MAWAZIRI WA AFRIKA MASHARIKI WAENDELEA KUFANYIKA JIJINI ARUSHA

 Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki umeendelea kufanyika kwa siku ya pili leo jijini Arusha. Mkutano huo utakaofanyika kwa kipindi cha siku nne (4) (tarehe 22 hadi 25 Februari 2021) utafanyika katika ngazi tatu, ambazo ni; ngazi ya Wataalam (tarehe 22-23 Februari), ngazi ya Makatibu Wakuu (tarehe 24 Februari) na ngazi ya Mawaziri (tarehe 25 Februari). Mkutano huu unafanyika kwa njia ya ana kwa ana na video


Miongoni mwa masuala yaliyopo kwenye agenda ni pamoja uwasilishwaji wa ripoti mbalimbali ikiwemo ripoti za utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya Baraza la Mawaziri, Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya, Mipango na Miundombinu na Sekta ya Uzalishaji na Huduma za Jamii.

Sambamba na hayo masuala mengine yatakayo jadiliwa ni kuhusu; Siasa, Forodha na Biashara; Masuala ya Fedha na Utawala; na Ripoti ya Taasisi zingine zilizopo chini ya Jumuiya zikiwemo Bunge la Afrika Mashariki na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.

Baraza pia linatarajiwa kujadili na kupitisha agenda na ratiba iliyopendekezwa ya Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliopangwa kufanyika Jumamosi, 27 Februari, 2021. 

Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki ni Chombo kinachounda Sera za Jumuiya. Baraza hili linaundwa na Mawaziri wanaosimamia Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na/au Ushirikiano wa Kikanda kutoka Nchi Wanachama. 

Mjukumu mengine ya Baraza hili ni ufuatiliaji, uangalizi na usimamizi wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Jumuiya na kuhakikisha utendaji mzuri wenye tija wa Taasisi zingine za Jumuiya.

Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huu katika ngazi ya wataalamu unaongoza na Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi.
Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania Balozi Stephen P. Mbundi akichangia jambo kwenye Mkutano wa 40 Wakawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki unaofanyika jijini Arusha, Tanzania. 
Sehemu ya washikiri kutoka Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki unaondelea jijini Arusha
Mkutano ukiendelea

Meza kuu kutokea kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala uzalishaji na sekta ya kijamii Christophe Bazivamo na Mshauri wa Masuala ya Jumuiya Dkt. Antony L. Kafumbe wakifuatilia mkutano.
Sehemu nyingine ya washiriki wa mkutano wakifuatilia majadala uliokuwa ukiendelea



Friday, February 19, 2021

WAZIRI PROF. KABUDI AWASILI NCHINI UFARANSA KWA ZIARA YA KIKAZI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akisalimiana na Waziri wa Ulaya na Mambo ya Nje wa Ufaransa Mhe. Jean Yves Le Drian mara baada ya kuwasili katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Ufaransa
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiteta jambo na Waziri wa Ulaya na Mambo ya Nje wa Ufaransa Mhe. Jean Yves Le Drian wakiwa wanaelekea sehemu ya mazungumzo rasmi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiteta jambo na Waziri wa Ulaya na Mambo ya Nje wa Ufaransa Mhe. Jean Yves Le Drian wakiwa wanaelekea sehemu ya mazungumzo rasmi

Thursday, February 18, 2021

MABALOZI ‘WAMLILIA’ MAALIM SIEF SHARIF HAMAD

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, ‘wamemlilia’ Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad na kumuelezea kwa mema aliyoyafanya enzi za uhai wake hapa duniani.

Mabalozi hao wamewasili katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti kwa ajili ya kusaini kitabu cha maombolezo ambapo mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo baadhi yao wakaelezea walivyoguswa na msiba wa Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad.

Balozi wa Ufaransa chini Tanzania, Mhe. Frederic Clavier amesema kuwa ni pengo kubwa kwa Zanziba na kwa Tanzania pia kwani Mhe. Maalim Seif alikuwa kiongozi mahiri kwa taifa na aliyekuwa na uhamasisho kwa bara la Afrika.

“Alikuwa mtetezi wa masuala mbalimbali ikiwemo demokrasia na haki, pia katika enzi za uhai wake alikubali kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa Serikali ya Zanzibar ni jambo la kuigwa kwa taifa la Zanzibar na Taifa la Tanzania kwa Ujumla,” Amesema Mhe. Clavier

Mhe. Clavier ameongeza kuwa “Maalimu Seif alikuwa kiongozi aliyependa amani, na aliyekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya nchi yake……lakini pia alikuwa mpenda amani na alikuwa mwanasiasa makini ……..kwa kweli tutamkumbuka daimia, tunamuombea kwa Mungu apumzike kwa amani,”.

Kwa upande wake Balozi wa Finland hapa nchini Mhe. Riitta Swan amesema kuwa Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa kiongozi makini aliyependa amani na mshikamano wakati wa uhai wake.

“Kwa muda mfupi niliomfahamu kwa kweli alikuwa kiongozi mahiri aliyependa amani na umoja hakika pengo lake halitazibika kwa urahisi, Mungu ampumzishe kwa amani,” Amesema Mhe. Swan

Nae Balozi wa Zimbabwe hapa nchini, Mhe. Luteni Jenerali Mstaafu, Anselem Sanyatwe amesema kuwa Mhe. Maalim Seif alikuwa ni kiongozi mchapakazi na mzalendo kwa taifa la Zanzibar na Tanzania. “Kwa kweli Jamhuri ya MUungano imepoteza kiongozi mzalendo, kwa niaba ya Jamhuri ya Zimbabwe natoa pole kwa Tanzania kwa kuondokewa na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar…..poleni sana watanzania kwa msiba huu mzito,” Amesema Mhe.

Kwa upande wake Balozi wa Kuwait nchini, Mhe. Balozi Mubarak Mohammed Alsehaijan amesema kuwa Mhe. Maalim Sief kiongozi mpenda amani na atakumbukwa daima kwa mema aliyoyafanya kwa Wazanzibari na watanzania kwa ujumla.

Baadhi ya mabalozi waliofika na kusaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam ni pamoja na Balozi wa Zambia nchini mhe. Benson Keith Chali, Balozi wa Finland chini Tanzania, Mhe. Riitta Swan na Balozi wa Kuwait nchini, Mhe. Balozi Mubarak Mohammed Alsehaijan.

Wengine ni Balozi wa Pakistani hapa nchini, Mhe. Mohammad Saleem, Balozi wa Ufaransa hapa chini, Mhe. Frederic Clavier, Balozi wa Zimbabwe hapa nchini, Mhe. Luteni Jenerali Mstaafu, Anselem Sanyatwe pamoja na Mwakilishi wa Balozi wa Irani hapa nchini. Bwn. Mohammad Rezaee.  

Balozi wa Ufaransa chini Tanzania, Mhe. Frederic Clavier akisaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad jijini Dar es Salaam


Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Riitta Swan akisaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad jijini Dar es Salaam


Balozi wa Kuwait hapa nchini, Mhe. Balozi Mubarak Mohammed Alsehaijan akisaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad jijini Dar es Salaam


Balozi wa Zimbabwe hapa nchini, Mhe. Luteni Jenerali Mstaafu, Anselem Sanyatwe akisaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad jijini Dar es Salaam


Balozi wa Pakistani hapa nchini, Mhe. Mohammad Saleem akisaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad jijini Dar es Salaam


Mwakilishi wa Balozi wa Irani hapa nchini. Bwn. Mohammad Rezaee kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad jijini Dar es Salaam