Saturday, March 20, 2021

MARAIS WASTAAFU, VIONGOZI WAANDAMIZI WA SERIKALI NA MABALOZI WAMLILIA MAGUFULI

Na mwandishi wetu

Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi waandamizi wa Serikali na mabalozi waonaziwakilisha nchi zao hapa Nchini wamewataka watanzania kuendelea kudumisha uzalendo, fikra na maono aliyokuwa nayo Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ili kuiwezesha Tanzania kukua kimaendeleo

Akizungumza mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee, Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Kikwete amesema kifo cha Hayati Magufuli hakikutarajiwa hasa wakati huu ambapo taifa lilimuhitaji na kuwasihi watanzania kudumisha mema aliyoyaasisi kwa maslahi ya taifa.

“Kwa kweli kifo chake hakikutarajiwa, tulitegemea kwa kweli aendelee kuliongoza taifa kwani katika mhula wake wa kwanza aliliongoza taifa vizuri sana…….naamini kuwa yale ambayo hayakukamilika, Rais wa Jamhuri ya Tanzania mhe. Samia Suluhu Hassan atayaendeleza kikamilifu,” Amesema Dkt. Kikwete na kuwasihi watanzania kuendelea kudumisha uzalendo, fikra na maono aliyokuwa nayo Hayati Dkt. Magufuli.

Rais wa Awamu ya Pili, Mhe. Alhaji Ali Hassan Mwinyi nae amefika katika viwanja vya Karimjee na kusaini kitabu cha maombolezo akifuatiwa na Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mohamed Gahib Bilali, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma na pamoja na Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai nae pia amefika na kusaini kitabu hicho akifuatiwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mhe. Zubeir Ali Maulid ambaye amesema kuwa Hayati Magufuli katika kipindi kifupi cha uongozi wake amefanya mambo mengi yatakayosalia kuwa historia katika taifa la Tanzania.

“Msiba huu ni wetu sote watanzania na umetugusa sana kwani  hayati Magufuli ameyafanya mengi katika mhula wake wa kwanza ambapo mengi hayo tumekuwa tukinufaika nayo sisi watanzania…..kwa sasa tushikamane kudumisha umoja wetu ili kuweza kusonga mbele kimaendeleo,” Amesema Mhe. Maulid

Aidha, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini nao wameungana na watanzania kuomboleza kifo cha Hayati Dkt. Magufuli kwa kusaini kitabu cha maombolezo ambapo baadhi yao wamemuelezea kuwa katika uhai wake Hayati Magufuli alitamani kuiona Tanzania inayojitegemea kiuchumi na watu wake kuondokana na umasikini.

Naibu Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Mhe. Prefere Ndayishimiye amesema kuwa msiba wa Hayati Magufuli umewagusa sana kwani alikuwa kiongozi aliyependwa na kujulikana na bara lote la Afrika.

“Amefanya maendeleo makubwa ambapo naamini kuwa vizazi vijavyo vitayaona na kuendeleza pale alipoishia Dkt. Magufuli,” Amesema Naibu Balozi

Kadhalika, mbali na viongozi wastaafu pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali wananchi wa kada mbalimbali wamejitokeza kwa wingi kusaini kitabu cha maombolezo na kumuelezea hayati Magufuli kuwa alikuwa kiongozi aliyeweka maslahi ya nchi mbele kwa manufaa ya watanzania.

Rais wa Mstaafu wa awamu ya pili Mhe. Alhaj Ali Hassan Mwinyi akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi 2021  


Rais wa Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Jakaya Kikwete akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi 2021 


Makamu wa Rais, Mstaafu Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli 


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli 


Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Pombe Joseph Magufuli  


Spika wa Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mhe. Zubeir Ali Maulid akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli   


Balozi wa Oman nchini Tanzania, Mhe. Ali Abdulla – Al Mahrouq akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  


Balozi wa Somalia nchini Tanzania, Mhe. Mohamed Hassan Abdi akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  


Balozi wa Misri nchini Tanzania, Mhe. Mohamed Gaber Abulwafa akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  


Balozi wa Sudan nchini Tanzania, Mhe. Jaafer Nasir Abdalla akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli   


Naibu Balozi wa Italia nchini, Mhe. Roberte Cocconi akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli



Friday, March 19, 2021

RAIS SAMIA AONGOZA VIONGOZI, MABALOZI MBALIMBALI KUASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewaongoza viongozi waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar akiwemo Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli huku baadhi ya mabalozi wakibubujikwa na machozi.

Rais Samia Suluhu Hassan amesaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Kamrijee Dar es Salaam mchana wa leo na kufuatiiwa na baadhi ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena kwa maradhi ya moyo.

Pia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Hussein Ally Mwinyi nae pia amesaini kitabu cha maombolezo akifuatiwa na Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe Othaman Masoud

Baadhi ya Mabalozi wanaoziwakilisha Nchi zao hapa Nchini walishindwa kujizuia na kutokwa na machozi kumlilia Hayati Dkt. Magufuli na kumuelezea kuwa alikuwa kiongozi jasiri na mzalendo si kwa manufaa ya Tanzania pekee bali Afrika kwa ujumla ambapo Balozi wa Jamaica hapa nchini Mhe. Velisa Delfosse amemuelezea Hayati Dkt Magufuli kama mwanampinduzi na mzalendo halisi wa Afrika wa wakati huu

“Rais Magufuli alikuwa mwanampinduzi na mzalendo halisi wa Afrika wa wakati huu, kwa kweli tumeguswa sana na msiba wake hakika pengo lake halitazibika, tunamuombea kwa Mungu apumzike salama,” Amesema Balozi Delfosse

Nae Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo amemuelezea Hayati Magufuli kama kiongozi mwenye maono na mzalendo mwaminifu kwa Afrika,na kwamba atakumbukwa na Watanzania kwa jitihada zake kubwa za kuleta mabadiliko chanya  ili kuinua hali ya maisha hususani wale wa kipato cha chini.

Kwa upande wake Balozi wa Sudani ya Kusini Mhe. William Ruben amewasihi viongozi wa Afrika na Watanzania kwa ujumla kufuata nyayo za Hayati Dkt Magufuli kwa kuwa alikuwa alama halisi ya Afrika na alitufundisha wengi wetu kuamini kuwa Afrika imebarikiwa na ni tajiri kinyume na tulivyoamini kuwa tunahitaji msaada kutoka kwa mataifa ya nje ya bara la Afrika 

“Naomba kuwasihi viongozi wa Afrika na Watanzania kwa ujumla kufuata nyayo za Hayati Dkt Magufuli kwa kuwa alikuwa alama halisi ya Afrika na alitufundisha wengi wetu kuamini kuwa Afrika imebarikiwa na ni tajiri kinyume na tulivyoamini kuwa tunahitaji msaada kutoka kwa mataifa ya nje ya bara la Afrika,” Amesema Balozi Ruben

Mabalozi wengine waliofika katika viwanja vya Karimjee na kusaini kitabu cha maombolezo ni pamoja na Balozi wa Morocco Mhe. Abdililah Benryane, Balozi wa Ethiopia Mhe Yonas Sanbe, Balozi wa Qatar Mhe Abdulla Jassim Al Madadadi, Balozi wa Japan Mhe Shinichi Goto Balozi wa Palestina Mhe Derar Ghannan, Balozi wa Cuba Mhe Lucas Damingo, Balozi wa Pakistan Mhe Mohammed Salem, Balozi wa Uswis Mhe Didier Chassot, Balozi wa Ireland Mhe Mary Oneill.

Wengine ni Balozi wa Rwanda Meja Jeneral Charles Karamba, Balozi wa Syria Dr Sawsan Alani, Balozi wa Korea Mhe Kim Yong Su, Balozi wa Iran Mhe Hussein Alvandi Behined, Balozi Hispania Mhe Fransisca Pedros, Balozi wa Zambia nchini Mhe. Benson Chali na Balozi Vietnam Mhe Nguyen Namtien.

Baadhi ya Wakuu wa mashirika na Taasisi za Kimataifa waliofika kusaini kitabu cha maombolezo ni pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Mhe. Zlatan Milisic, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF, Mhe. Shahini Bahuguna,Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu,sayansi na utamaduni Mhe Tirso Do Santos,Shirika la Kazi duniani Wellingtone Chibebe,Shirika la Maendeleo la Umoja wa mataifa Mhe Christine Musisi na Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa Mhe Antonio Jose Canandula.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee  kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi 2021 jijini Dar es Salaam 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akitoa heshima mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi 2021 jijini Dar es Salaam 


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi 2021 jijini Dar es Salaam 


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Othman Masoud akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  


Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Shinichi Goto akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  


Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Mhe. Benson Chali akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  


Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Mary O’neill kisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  


Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) Zlatan Milisic akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  


Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bi. Christine Musisi akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  


Balozi Hispania Mhe Fransisca Pedros akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli


Balozi wa Rwanda Meja Jeneral Charles Karamba akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli



Wednesday, March 17, 2021

TANZANIA–CHINA KUENDELEA KUDUMISHA USHIRIKIANO


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge mapema leo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke katika ofisi za Wizara jijini Dodoma. 

Wawili hao wamejadili masuala mbalimbali yanayolenga kudumisha zaidi ushirikiano na uhusiano wa kidiplomasia na biashara. Vilevile wamejadili kuhusu ufuatiliaji wa maendeleo ya miradi na programu mbalimbali zinazotekelezwa kwa ushirikiano wa Tanzania na China ili kuhakikisha zinaleta tija kwa manufaa ya pande zote mbili.

Balozi Ibuge kwa upande wake ameeleza kuwa kuwepo kwa uhusiano mzuri wa Kidiplomasia baina ya Tanzania na China kumechagiza kwa kiasi kikubwa kukuwa kwa biashara, utali na uwekezaji baina ya nchi hizi mbilia hivyo urafiki na undugu kati ya Mataifa haya mawili unapaswa kulindwa, kudumisha na kuendelezwa siku zote na katika hali yoyote. “China kwa muda mrefu imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya Taifa letu kupitia sekta mbalimbali kama vile ujenzi wa mundombinu ya usafirishaji na mawasiliano kama vile reli na barabara, hivyo Wizara na Serikali kwa ujumla inadhamini na kulinda undugu huu wa kihistoria” Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge

Mheshimiwa Balozi Wang Ke kwa upande wake ameshukuru kwa ushirikiano ambao amekuwa akiendelea kuupata kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Serikali kwa ujumla katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. Ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha serikali za nchi hizi mbili na watu wake wananufaika kotokana na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge afafanua jambo kwa Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akimsikiliza Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

  Mazungumzo yakiendelea



Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akisisitiza jambo kwa Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke wakiwa katika picha ya pamoja  mara baada ya kuhitimisha mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dodoma

Monday, March 15, 2021

TANZANIA, VATICAN KUHIMIZA AMANI

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Tanzania na Vatican zimeahidi kuendelea kuhimiza amani na utulivu katika masuala yenye changamoto mbalimbali ili kuwezesha uwepo wa amani na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Baba Mtakatifu katika kuhimiza amani, utulivu na usalama duniani.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi, (Mb) wakati alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa Vatican nchini Mhe. Askofu Mkuu Marek Solczynski leo jijini Dar es Salaam.

Prof. kabudi amesema kuwa Tanzania na Vatican kwa kutambua umuhimu wa amani, zimeahidi kuendelea kushirikiana katika mikutano ya Umoja wa Mataifa kuhimiza amani, utulivu na mshikamano katika masuala mbalimbali yenye changamoto kwa binadamu duniani.

 “Tumeongelea umuhimu wa kulinda amani, utulivu na usalama duniani kote hasa katika maeneo yanayokumbwa na matatizo ya vita…….. katika hilo pia tuliongela suala la amani na usalama katika ukanda wa nchi za maziwa makuu, Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika tukijua kuwa kuna maeneo yanayohitaji amani ikiwemo eneo la kaskazini mwa Masumbiji, na mashariki ya Demokrasia ya Kongo,” Amesema Pro. Kabudi

Prof. Kabudi ameongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni na hata sasa dunia inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinahitaji mshikamano wa mataifa yote duniani ili kuweza kuyakabili hii ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusu amani, utulivu, majanga, na magonjwa ya mlipuko kama vile Covid 19, na yale yanayohusu umasikini na hali yamaisha ya watu kubaguliwa na kuonewa.

“Mfano katika mapambano dhidi ya Uviko 19, Vatican na Baba Mtakatifu wanayo nafasi kubwa ya kutoa mchango wao katika eneo hilo katika kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya Covid 19 hayageuzwi kuwa katika masuala ya kibiashara na kisiasa na badala yake mapambano hayo yazingatie utu, undugu na imani, Ameongeza Pro. Kabudi

Kwa upande wake Balozi wa Vatican hapa Nchini Mhe. Askofu Mkuu Marek Solczynski amesema kuwa Vatican itaendelea kuimarisha mahusiano yake ya kidiplomasia na Tanzania kwa masuala yenye maslahi ya haki, utu, amani na utulivu.

“Maongezi yangu na Mhe. Waziri yalikuwa mazuri kwani tuliongelea masuala mbalimbali yenye maslahi kwa binadamu yakiwemo masuala ya kukuza diplomasia yetu pamoja na masuala ya amani na usalama duniani,” Amesema Askofu Mkuu Solczynski.

Baba Mtakatifu Papa Francisko alimteua, Askofu Mkuu Marek Solczyński kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Tanzania mwezi Aprili, 2017. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Solczyński alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Georgia, Armenia na Azerbaijan.

Katika tukio jingine, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Tate Olenasha amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Algeria hapa nchini Mhe. Ahmed Djellal ambapo pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu kuimarisha diplomasia baina ya Tanzania na Algeria.  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi, (Mb) akisalimiana na Balozi wa Vatican nchini Mhe. Askofu Mkuu Marek Solczynski wakati walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi, (Mb) akiongea na Balozi wa Vatican nchini Mhe. Askofu Mkuu Marek Solczynski wakati walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam 




Balozi wa Vatican nchini Mhe. Askofu Mkuu Marek Solczynski akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi, (Mb) wakati walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam 


Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika MAshariki, Mhe. William Tate Ole Nasha akiongea na Balozi wa Algeria nchini Mhe. Ahmed Djellal wakati walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam 


Balozi wa Algeria nchini Mhe. Ahmed Djellal akiongea na Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika MAshariki, Mhe. William Tate Ole Nasha wakati walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam 



WATUMISHI WA WIZARA WAHIMIZWA KUFANYA KAZI KWA UWELEDI NA NIDHAMU.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewahimiza Watumishi wa Wizara kufanya kazi kwa kujituma, weledi na nidhamu. Amesema haya alipokuwa akifungua mafunzo maalumu ya siku tano kwa Watumishi wa Wizara yanayoendelea jijini Dodoma.

Katibu Mkuu amewakumbusha na kusisitiza kuwa, Watumishi wa Wizara wakati wote wakiwa katika utekelezaji wa majumu yao iwe ndani au nje ya mipaka ya nchi, wanapaswa kuielewa na kuzingatia miongozo mbalimbali inayotumiwa na Wizara. Ameitaja baadhi ya miongozo hiyo kuwa ni pamoja na Sera ya Mambo ya Nje, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Ilani ya CCM ya Mwaka 2020-2025, Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati anafungua Bunge la 12, Mpango Mkakati wa Wizara ambao huhuishwa kila mwaka wa fedha, na sheria na kanuni zinazoongoza utumishi nje. Aliongeza kuwa Mkataba wa Vienna (Vienna Convention) wa Mwaka 1961 na ule wa mwaka 1963 unaohusu mahusiano ya kidiplomasia na mahusiano ya kikonseli mtawalia pamoja na Kanuni za Utumishi Nje za Mwaka 2016 pia ni muhimu zizingatiwe. 

“Natambua ni ndoto ya kila Afisa Mambo ya Nje (Foreign Service Officer) ni kwenda posting siku moja, kwa mtakaobahatika kupata fursa ya kwenda kwenye Balozi zetu, mjue kwamba mna deni kubwa kwa nchi yenu. Mnawiwa kutekeleza majukumu yenu kwa kujituma, uzalendo, na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maslahi ya nchi yetu.” Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge. 

Licha ya mafunzo hayo kulenga kuwasaidia watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuelewa misingi bora ya maadili ndani ya Utumishi wa Umma, Balozi Brigedia Jenerali Ibuge ameeleza mataumani yake kuwa mafunzo hayo yatawasaidia watumishi kupata uelewa wa jumla kuhusu Maslahi ya Taifa, Diplomasia ya Uchumi, Itifaki, Usalama wa kimtandao na utendaji wa kazi katika mazingira ya kimataifa. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akizungumza na Watumishi wa Wizara (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalumu kwa watumishi hao yatakayofanyika katika ukumbi wa Veta, jijini Dodoma.

Sehemu ya Watumishi wa Wizara wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge kwenye ufunguzi wa mafunzo maalumu kwa watumishi wa Wizara yanayofanyika katika ukumbi wa Veta, jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge (katikati walioketi), Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu Bw. Alex Mfungo (kulia walioketi) na Mhe. Balozi Abdulrahman Kaniki wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo.

Shemu nyingine ya Watumishi wa Wizara wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo

Shemu nyingine ya Watumishi wa Wizara wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo