Monday, March 15, 2021

WATUMISHI WA WIZARA WAHIMIZWA KUFANYA KAZI KWA UWELEDI NA NIDHAMU.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewahimiza Watumishi wa Wizara kufanya kazi kwa kujituma, weledi na nidhamu. Amesema haya alipokuwa akifungua mafunzo maalumu ya siku tano kwa Watumishi wa Wizara yanayoendelea jijini Dodoma.

Katibu Mkuu amewakumbusha na kusisitiza kuwa, Watumishi wa Wizara wakati wote wakiwa katika utekelezaji wa majumu yao iwe ndani au nje ya mipaka ya nchi, wanapaswa kuielewa na kuzingatia miongozo mbalimbali inayotumiwa na Wizara. Ameitaja baadhi ya miongozo hiyo kuwa ni pamoja na Sera ya Mambo ya Nje, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Ilani ya CCM ya Mwaka 2020-2025, Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati anafungua Bunge la 12, Mpango Mkakati wa Wizara ambao huhuishwa kila mwaka wa fedha, na sheria na kanuni zinazoongoza utumishi nje. Aliongeza kuwa Mkataba wa Vienna (Vienna Convention) wa Mwaka 1961 na ule wa mwaka 1963 unaohusu mahusiano ya kidiplomasia na mahusiano ya kikonseli mtawalia pamoja na Kanuni za Utumishi Nje za Mwaka 2016 pia ni muhimu zizingatiwe. 

“Natambua ni ndoto ya kila Afisa Mambo ya Nje (Foreign Service Officer) ni kwenda posting siku moja, kwa mtakaobahatika kupata fursa ya kwenda kwenye Balozi zetu, mjue kwamba mna deni kubwa kwa nchi yenu. Mnawiwa kutekeleza majukumu yenu kwa kujituma, uzalendo, na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maslahi ya nchi yetu.” Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge. 

Licha ya mafunzo hayo kulenga kuwasaidia watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuelewa misingi bora ya maadili ndani ya Utumishi wa Umma, Balozi Brigedia Jenerali Ibuge ameeleza mataumani yake kuwa mafunzo hayo yatawasaidia watumishi kupata uelewa wa jumla kuhusu Maslahi ya Taifa, Diplomasia ya Uchumi, Itifaki, Usalama wa kimtandao na utendaji wa kazi katika mazingira ya kimataifa. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akizungumza na Watumishi wa Wizara (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalumu kwa watumishi hao yatakayofanyika katika ukumbi wa Veta, jijini Dodoma.

Sehemu ya Watumishi wa Wizara wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge kwenye ufunguzi wa mafunzo maalumu kwa watumishi wa Wizara yanayofanyika katika ukumbi wa Veta, jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge (katikati walioketi), Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu Bw. Alex Mfungo (kulia walioketi) na Mhe. Balozi Abdulrahman Kaniki wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo.

Shemu nyingine ya Watumishi wa Wizara wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo

Shemu nyingine ya Watumishi wa Wizara wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.