Friday, March 12, 2021

TANZANIA YAJIVUNIA MIAKA 40 YA MAFANIKO SADC

 Na Mwandishi wetu,

Tanzania imejivunia mafanikio iliyoyapata katika kipindi cha  miaka 40 ya uanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) ameyataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na miaka 40 ya uanachama wa SADC tangu 1979, lugha ya kiswahili kutumika katika mikutano yote ya kisekta ya SADC pamoja na kutengenzwa sanamu maalumu ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.  

“Pamoja na mambo mengine, mkutano wetu wa leo wa Baraza la Mawaziri wa SADC tunategemea kujadili masuala mbalimbali anayohusu jumuiya hiyo likiwemo suala la matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mikutano yote ya kisekta,” Amesema Prof. Kabudi.

Mambo mengine yatakayojadiliwa ni pamoja na suala la kutengeneza sanamu maalumu ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambapo sanamu hiyo itawekwa katika jengo la Amani Addis Ababa nchini Ethiopia, pamoja na maadhimisho ya miaka 40 ya SADC.

“Hivyo kupitia mkutano huu tutakamilisha mchakato wa kumpata mtu atakae ifua sanamu hiyo ya Mwl. Nyerere ambapo itawekwa katika jingo la Amani Ethiopia,” Amesema Prof. Kabudi

Prof. Kabudi ameendelea kueleza kuwa katika mkutano huo suala la maadhimisho ya miaka 40 ya SADC pia limejadiliwa ikiashiria umoja wa SADC kudumu kwa miaka 40.

“Miaka 40 ya SADC ina umuhimu mkubwa sana kwa Tanzania kwa sababu miongoni mwa viongozi nane walioasisi sadc ni Mwl. Julius Nyerere katika mkutano uliofanyika mwaka 1979 mkoani Arusha ambapo Tanzania iliamua kuingia rasmi katika jumuiya hiyo,” Ameongeza Prof. Kabudi 

Tanzania itakuwa inasherekea miaka 40 ya SADC ikiwa tayari Kiswahili ni moja ya lugha rasmi za jumuiya hiyo, lakini pia ikiwa na sanamu maalumu ya kumuenzi na kumheshimu baba wa Taifa na Muasisi wa SADC Mwl. Julius Nyerere.

Hivyo Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), Waziri wa Afya wa Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, Waziri wa Fedha na Mipango – Zanzibar Mhe. Jamal Kassim Ali, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe. Omar Said Shaaba, Naibu Waziri Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Godwin Mollel, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaban.

Februari 27, 2021 katika mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulifanyika kwa njia ya Mtandao, wakuu wan chi waliridhia lugha ya Kiswahili iwe lugha ya tatu katika shughuli za jumuiya hiyo sambamba na lugha ya kifaransa kuwa lugha ya nne.

Kadhalika, Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC katika mkutano wao wa 39 uliofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Augusti, 2019 waliridhia na kuipitisha kiswahili nne ya mawasiliano, ikiungana na lugha za Kifaransa, Kiingereza na Kireno zinazotumika katika jumuiya hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akifuatilia Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), katikati pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Agnes Kayola wakifuatilia mkutano


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (anaesoma taarifa) na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (kulia) pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge (kushoto) wakifuatilia mkutano  


Ujumbe wa Tanzania ukiendelea kufuatilia mkutano wa Baraza la Mawaziri SADC


Ujumbe wa Tanzania ukiendelea kufuatilia mkutano wa Baraza la Mawaziri SADC

Mkutano ukiendelea  


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.