Sunday, March 21, 2021

DODOMA WAENDELEA KUMLILIA MHE. DKT. MAGUFULI


Viongozi wa Serikali, Kitaifa na Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya jijini Dodoma wameendelea kumlilia aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyefariki dunia tarehe 17 Machi, 2021 jijini Dar es Salaam. 

Wananchi hao wamejitokeza kwa wingi katika viwanja vya Nyerere Square jijini humo kusaini kitabu cha maombolezo. Wananchi hao pia wameelezea hisia zao jinsi walivyokea msiba huo na walivyomfahamu Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 

Akiandika katika kitabu cha Maombolezo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge ameelezea jinsi alivyoguswa na msiba huo na kusema kuwa atamkumbuka daima Hayati Magufuli kwa jinsi alivyojitoa kuwatumikia wananchi wa Tanzania. " Kwa uchungu na masikitiko makubwa sana sababu Watanzania tumempoteza kiongozi na mpenda maendeleo aliyejipanga kuwaletea maendeleo ya kweli Watanzania," ameandika .

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira na Mbunge wa Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi ameelezea hisia zake kwa kuandika "Tunakushukuru na kumshukuru kwa zawadi ya uhai wako uliyoitoa kwa Watanzania kizalendo kuwapigania, Mungu kazi sake haina makosa. Taifa limetikisika tutakuenzi kwa mema mengi, uongozi bora, uzalendo, maendeleo, upendo, amani na taifa".

 
Kwa upande wake Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia alijitokeza katika viwanja vya Nyerere Square kusaini kitabu cha maombolezo ameelezea hisia zake akisema “Hayati Dkt. Magufuli ametutoka katika kipindi ambacho tulikuhitaji sana. Watanzania tunakupenda na tutaendelea kukuoenda kwa matendo na mambo mema uliyotufanyia na kutuachia kama Taifa”. Aliendelea kueleza kuwa Afrika imepoteza shujaa na mtetezi wa Bara.

Wakati huo huo Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Mhe. Dormohamed Issa Rahmat amesema “Kwa majonzi, masikitiko na maumivu makubwa tuliyonayo Watanzania kwa kuondokewa na mzalendo namba moja, Jemedari wa Maendeleo na shujaa wa kupambania maskini na wanyonge. Sina cha kusema zaidi ya kumshukuru Mungu na kumuomba ialaze Roho ya Marehemu Mahala pema Peponi”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Bw. Mohamed Ramadhani ameeleza “Mheshimiwa Rais ulikuwa kiigizo chema kwetu, umeweza kutufumbua Watanzania kuwa hakuna kinachoshindikana panapo dhamira ya dhati tukiamua kufanya masuala ya msingi katika kutatua changamoto zinazoikabili nchi yetu, tutakuenzi kwa kuendeleza yale uliyoyanzisha huku tukitambua na kuzingatia kauli yako ya vita ya kiuchumi hakuna Mataifa yasiyo na nia njema yatakayo tupenda. Pumzika kwa amani Jemadari Wetu Mungu akujalie Pepo”. 

Mwili Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli umewasili jijini Dodoma majira ya saa 10 jioni kutokea Dar es Salaam na kupokelewa na Wananchi wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Dkt, Benelith Mahenge na Viongozi weinigen wa Serikali.

Mwili wa Hayati Dkt. Magufuli umepitishwa katika Mitaa mbalimbali ya Jiji la Dodoma na kuelekea Ikulu Chamwino. Tarehe 22 Machi, 2021 ataagwa rasmi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadaye kueleekea katika uwanja wa Jamhuri. Miongoni mwa shughuli zitakazofanyika Uwanjani hapo ni pamoja na gwaride la mazishi kutoka Jeshi la Wananchi la Tanzania, dua na sala, salamu za maombolezo na kutoa heshima za mwisho.

Jumanne Machi 23, 2021 saa 12 asubuhi mwili wa Hayati Dkt. Magufuli utatolewa katika hospitali ya Banjamin Mkapa na kusafirishwa kuelekea Zanzibar.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea jijini Dar es Salaam tarehe 17, Machi 2021.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana Mhe. Patrobas Katambi akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea jijini Dar es Salaam tarehe 17, Machi 2021.

Mke wa Rais wa Awamu ya Nne na Mbunge wa Jimbo la Mchinga mkoani Lindi Mhe. Salma Kikwete akitia saini katika kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea jijini Dar es Salaam tarehe 17, Machi 2021.

Sheikh wa Mkoa wa Dodoma Mustafa Rajabu akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea jijini Dar es Salaam tarehe 17, Machi 2021.

Wakazi wa jijini Dodoma wakiwa katika Viwanja vya Nyerere Square jijini humo kwa ajili ya kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea jijini Dar es Salaam tarehe 17, Machi 2021.

Mtoto huyu alikuwa miongoni mwa wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kwa ajili ya kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea jijini Dar es Salaam tarehe 17, Machi 2021.

Mwanahabari kutoka Television ya Serbia akisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea jijini Dar es Salaam tarehe 17, Machi 2021.

























No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.