Wednesday, October 13, 2021

Balozi Bana awapokea Wanajeshi watakao shiriki Michezo ya Amani na Mshikamano ya Kijeshi, nchini Nigeria.


Balozi wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana amewapokea Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliowasili nchini humo kujumuika na wanamichezo wengine kutoka nchi mbalimbali za Barani Afrika kushiriki michezo ya Amani na Mshikamano ya Kijeshi ya Sahel Barani Afrika iliyoandaliwa na Taasisi ya Michezo ya Kijeshi Afrika (Organization of Military Sports in Africa - OSMA) Sahel Countries Military Games for Peace and Solidarity.

Sambamba na kuwajengea utimamu wa mwili na akili washiriki Wanajeshi wanaoshiriki michezo hii, michezo hiyo pia inalenga kujenga umoja, ushirikiano na udugu miongoni mwao hasa katika kupambana na vitendo vya uhalifu katika eneo la Sahel na kuleta amani katika eneo hilo ambalo limekuwa na matatizo ya uasi na changamoto nyingine za kiusalama. 

Akizungumza wakati wa mapokezi ya Wanajeshi hao Balozi Bana ameongeza kusema ushiriki wa Tanzania katika michezo hiyo kutasaidia kuimarisha na kuongeza ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwemo kubadilishana taarifa katika eneo la ulinzi na usalama na nchi zingine za Afrika

“Wakati huu dunia inapokabiliana na changamoto mbalimbali za kiusalama ni muhimu pia kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuendelea kuimarisha mahusiano na vyombo vingine vya nje ya nchi ili kwa pamoja kuweza kushirikiana katika kukabiliana na changamoto hizo.” Balozi Bana. 

Michezo hiyo ilifunguliwa Oktoba 11, 2021 jijini Abuja, na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu Mhe. Dkt. Ogbonanya Onu wa Serikali ya Shirikisho la Nigeria. Katika ufunguzi Dkt. Onu alibainisha kuwa michezo hiyo ni muhimu kwa sasa kwa kuzingatia hali ya usalama ya sasa inayokabili taifa hilo.

Michezo hiyo inatarajiwa kuudhuliwa na washiriki takribani 327 kutoka nchi 14 zikiwemo Nigeria, Burkina Faso, Cameroon, Congo Brazzaville, Guinea Conakry, Kenya, Mali, Tanzania na Chad. Michezo mingine itakayofanyika ni mpira wa miguu na gofu.
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wanariadha wa JWTZ wanaoshiriki michezo ya Amani na Mshikamano ya Kijeshi ya Sahel Barani Afrika



Chuo Kikuu cha Port Harcourt cha nchini Nigeria chaonesha nia ya kufundisha Lugha ya Kiswahili
Balozi wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana ameeleza kuwa Chuo Kikuu cha Port Harcourt kimeonesha utayari wa kuanza kufundisha tena somo la lugha ya Kiswahili kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Slaam kama ilivyokuwa halo awali. 

Balozi Bana amebainisha hayo baada ya kutembelea na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Chuo cha Port Harcourt Prof. Owunari Abraham Georgewill, ambapo pamoja na masuala mengine walijadili kuhusu uwezekano na namna ya kuanza kufundisha somo la Kiswahili katika Chuo hicho.

“Taratibu zimeanza kufanyika ili kukamilisha makubaliano ambayo yatapelekea somo la Kiswahili kufundishwa chuoni hapo, hii itatoa fursa kwa Walimu wa Kiswahili wa Tanzania kufundisha somo hilo katika chuo hicho, pia ni fusa muhimu katika kukuza lugha ya Kiswahili ambayo ni sehemu ya Utamaduni wa Mtanzania” Amesema Balozi Bana.

Miongo minne iliyopita Chuo kikuu cha Port Harcourt kilikuwa kikifundisha somo la Lugha ya Kiswahili. Hata hivyo kutokana na sababu ambazo hazikuwekwa wazi, Chuo hicho hakikuendelea kufundisha somo hilo. 

Tuesday, October 12, 2021

EALA WAKUTANA MKUTANO WA KWANZA JIJINI ARUSHA

Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala) limeanza leo mkutano wake wa kwanza, kikao cha tano, bunge la nne ambapo pamoja na mambo mengine, Bunge hilo limejadili masuala mbalimbali ya kamati ya sheria na maendeleo yake ndani ya Jumuiya hiyo.

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) Mhe. Martin Ngoga akifungua Mkutano wa Kwanza, Kikao cha tano, Bunge la nne ulioanza leo Jijini Arusha


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) pamoja na wabunge wengine wa Bunge hilo wakifuatilia Mkutano kwanza wa (Eala), leo Jijini Arusha


Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Mhe. Wanjiku Muhya kutoka Kenya akichangia hoja kuhusu Kamati ya Sheria katika Mkutano Kwanza leo Jijini Arusha


Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Mhe. Gasinzigwa Oda kutoka Rwanda akichangia hoja kuhusu Kamati ya Sheria katika Mkutano Kwanza leo Jijini Arusha


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akinukuu jambo wakati wa Mkutano Kwanza wa (Eala), ukiendelea leo Jijini Arusha


Mbunge wa Eala kutoka Sudan Kusini Mhe. Mukulia Kennedy Ayason  akichangia hoja kuhusu Kamati ya Sheria katika Mkutano Kwanza leo Jijini Arusha


Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kanda wa Kenya, Adan Mohamed (kulia) akijadili jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) nje ya Ukumbi wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala), mara baada ya kuahirishwa kwa Mkutano wa Kwanza, Kikao cha tano, Bunge la nne, ulioanza leo Jijini Arusha



Monday, October 11, 2021

TANZANIA YAPONGEZWA KUFANIKISHA MAONESHO YA UTALII UKANDA WA AFRIKA MASHARIKI

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongezwa kwa kufanikisha maonsho ya kwanza ya kitaifa ya kikanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Jijini Arusha kuanzia tarehe 9 – 11 yaliyolenga kutangaza vivutio na fursa mbalimbali za utalii ndani ya Jumuiya hiyo.

Pongezi hizo zimetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na baadhi ya Mawaziri wa Utalii wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa kufunga maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo jijini Arusha.

“Nawapongeza kwa kufanikisha maonesho haya ni imani yangu kuwa kupitia maonesho haya nchi zetu za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimepata fursa ya kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii pamoja na kujadili njia mbalimbali za kukabiliana changamoto zinazoikabili sekta ya Utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki,” Amesema Dkt. Mwinyi

“Natoa wito kupitia maonesho haya ambayo yatakuwa yanafanyika kila mwaka kwa mzunguko kwa kila nchi mwanachama……..jitihada zaidi zinahitajika katika kutangaza vivutio vya utalii katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kuboresha sera zetu za utalii,” ameongeza Dkt. Mwinyi

Dkt. Mwinyi pia ameitaka Kamati Maalumu ya Kikanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya ziara Zanzibar na kujionea fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya utalii pamoja na zile za biashara na uwekezaji.

Awali Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema kupitia maonesho haya ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki yamekuwa na mafanikio makubwa ambapo zaidi ya waoneshaji 100 kutoka mataifa mbalimbali duniani wameshiriki, kati yao 41 wakitoka mataifa mbalimbali na nchi 25 zikishiriki ikiwa ni pamoja na sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Nae Waziri wa Uhifadhi wa Wanyamapori na Utalii kutoka Sudan ya Kusini Mhe. Luteni Jenerali Rizik Zakaria Hassan ameipongeza Tanzania kwa kufanikisha maonesho ambayo yemeweza kuvitangaza vivutio mbalimbali vya utalii ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki ambayo pia yametoa fursa ya kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya utalii.

“Maonesho haya yemekuwa na manufaa makubwa sana kwa kutuweka sekta ya utalii ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki ……….binafsi nawapongeza sana Tanzania kwa kulifanikisha jambo hili muhimu kwetu, naamini kupitia maonesho haya tutazidi kuimarika ziadi kama jumuiya kwa maendeleo yetu sote,” Amesema Luteni Jenerali Hassan.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Forodha na Biashara Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bwn. Keneth Bagamuhunda ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Peter Mathuki, amesema maonesho yalilenga kutoa fursa kwa kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii ili kuifahamisha Afrika na Dunia kuwa ndani ya Afrika Mashariki kuna vivutio vya utalii.

“Tutaendelea na maonesho haya kwa kila mwaka lengo likiwa ni kutangaza utalii na kuhakikisha soko la utalii ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki linakuwa kila mwaka,” Amesema Bwn. Bagamuhanda.

Kwa upande wake, Waziri wa Utalii na Malikale wa Zanzibar, Mhe. Leila Mohamed Mussa (Mb) amesema Afrika kwa sasa inatakiwa fursa za utalii na biashara ili kuweza kuziongezea Serikali zetu mapato.

“Afrika Mashariki inayo mambo mengi ya kutoa katika bara la Afrika na Duniani kwa ujumla hasa katika sekta ya utalii kwa kuwa tumejaliwa vivutio mbalimbali vya utalii,” amesema Bibi Leila Mohamed Mussa.

Oktoba 09, 2021 maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki yalizinduliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki jijini Arusha.

Kufanyika kwa maonesho hayo kunatokana na kuzinduliwa hivi karibuni mpango wa pamoja kutangaza utalii katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki uliozinduliwa rasmi na Mawaziri wa Maliasili na Utalii wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Maonesho hayo yalihudhuriwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania (Mwenyeji), Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akihutubia washiriki wa maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki, leo Jijini Arusha


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akipata maelezo wakati alipotembelea banda la Rwanda katika maonesho ya kwanza ya Kikanda ya Utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo Jijini Arusha


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akikaribishwa na Balozi wa Kenya nchini Tanzania katika banda la Kenya wakati alipokuwa akitembelea mabanda mbalimbali katika maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki, leo Jijini Arusha


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Mkewe Mhe. Mama Mariam Mwinyi na viongozi mbalimbali katika banda la Zanzibar leo Jijini Arusha

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro wakifungua na kuweka jiwe la msingi la kwanza la maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki, leo Jijini Arusha


Kikundi cha ngoma kutoka Makumira Arusha kikitumbuiza wakati wa maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo Jijini Arusha


Kikundi cha ngoma kutoka Sudan Kusini kikitumbuiza wakati wa maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo Jijini Arusha


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali mara baada ya kufunga maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo Jijini Arusha


Sekta zaidi nchini kunufaika na mikopo nafuu ya Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas A. Nyamanga akiwa katika mazungumzo na Mkuu wa ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wa Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya. 
Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas A. Nyamanga wakikabidhiana zawadi baada ya kufanya mazungumzo na Mkuu wa ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wa Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya. 

-------------------------------------------

Sekta zaidi nchini kunufaika na mikopo nafuu ya Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya

Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (European Investment Bank-EIB) imekubali kuongeza kasi na wigo wa maeneo ya ushirikiano baina ya Tanzania na Benki hiyo. Hayo yameelezwa wakati wa mazungumzo baina ya Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Luxembourg na kwenye Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas A. Nyamanga na Mkuu wa ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wa benki hiyo, Bw. Diederick Zambon yaliyofanyika hivi karibuni kwenye Ubalozi wa Tanzania, Brussels. 

Katika mazungumzo hayo, wawili hao walijadili kwa kina juu ya miradi mbalimbali na fursa nyingine zinazoweza kunufaisha Tanzania kupitia mikopo nafuu inayotolewa na Benki hiyo. Miongoni mwa miradi iliyojadiliwa ni pamoja na ujenzi wa awamu ya pili ya mradi wa kuboresha msongo mkubwa wa umeme katika vituo vya Iringa na Shinyanga (Tanzania Electricity Backboneinterconnector project-TBIP II. EIB ilikuwa ni moja ya taasisi za fedha zilizotoa mkopo nafuu kwa ajili ya mradi huu kwa awamu ya kwanza (TBIP I). Katika mazungumzo hayo, Bw. Zambon ameonesha utayari wa kuendeleza mazungumzo zaidi na Serikali ya Tanzania kuhusu mradi huu na miradi mingine ikiwemo miradi ya maji.

Wawili hao pia wamesisitiza umuhimu wa kuongeza kasi kwenye utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa viwanja vya ndege vya Tabora, Shinyanga na Kigoma pamoja na ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa Sumbawanga. Mradi huu pia unafadhiliwa na Benki ya EIB kwa mkopo nafuu wa Euro milioni 50.

Benki hiyo yenye makao yake makuu nchini Luxembourg pia imekubali kuanza majadiliano na Serikali ya Tanzania pamoja na sekta binafsi ili kukubaliana juu ya mazingira yatakayoiwezesha Benki hiyo kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa sekta binafsi ili kuchochea zaidi maendeleo ya Watanzania. Mikopo hiyo italenga zaidi wajasiriamali wadogo na wakati; wakulima na watanzania wenye viwanda vinavyoongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo; taasisi mbalimbali za fedha na wafanyabiashara kwa ujumla.

Ujumbe wa Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya ukiongozwa na Bw. Zambon unatarajiwa kufanya ziara nchini Tanzania mwezi huu wa Oktoba au mwanzoni mwa Mwezi Novemba mwaka huu kwa ajili ya kuendeleza majadiliano na Serikali pamoja na sekta binafsi kwenye masuala haya muhimu kwa uchumi wa Tanzania.

EIB ni miongoni mwa wadau wakubwa wa maendeleo wa Tanzania na imekuwa ikishirikiana na Serikali na sekta binafsi katika utoaji wa mikopo nafuu kwa miradi mbalimbali nchini.



Friday, October 8, 2021

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI BALOZI LIBERATA MULAMULA KATIKA MKUTANO WA KIMATAIFA WA AMANI - ROMA,ITALIA

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis (aliyevaa kanzu nyeupe) akiwa pamoja na viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali duniani wakati wa kufunga Mkutano wa Kimataifa kuhusu Amani. Mkutano huo umefanyika Roma,Italia.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa  ameshika ujumbe wa Amani aliokabidhiwa katika hafla ya kufunga Mkutano wa Kimataifa wa Amani ambar umehudhuriwa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis. Mkutano huo umefanyika Roma,Italia

 

TANZANIA, CZECH ZAAHIDI KUIMARISHA BIASHARA NA UWEKEZAJI

 Na Mwandishi wetu, Dar

 

Katika jitihada za kukuza na kuendeleza diplomasia ya uchumi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Czech zimeahidi kukuza na kuimarisha sekta ya biashara na uwekezaji.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek wakati alipokutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk leo katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam. 

Mhe. Staŝek amesema kuwa wamejadili masuala mbalimbali ya kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Czech hasa katika sekta ya biashara na uwekezaji wa viwanda hapa nchini………..”na leo nimeambatana na wafanyabiashara mbalimbali kutoka Czech ambao wamekuja kuangalia fursa za biashara zinazopatikana hapa Tanzania” amesema Mhe. Staŝek.

“Pia tunajitahidi kuleta teknolojia mpya hapa Tanzania kuinua uchumi, ambapo tunaamini itasaidia kutangaza fursa mbalimbali katika sekta ya biashara na uwekezaji,” Ameongeza Mhe. Staŝek

Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amesema katika mazungumzo yake na Waziri wa Jamhuri wa Czech Mhe. Staŝek yamejikita zaidi katika kukuza uhusiano wa uchumi hasa masuala ya biashara na uwekezaji.

Leo Mhe. Waziri ameambata na ujumbe wa wafanyabiashara waliokuja kujione fursa mbalimbali hapa nchini ili kuinua sekta ya biashara na uwekezaji…………..”leo pia watakuwa na mkutano ambao utawakutanisha na wafanyabiashara wa Tanzania ili kuona fursa za ushirikiano baina ya Tanzania na Czech,” Amesema Balozi Mbarouk.

“Tumeongelea suala la kuongeza uhusiano katika sekta ya elimu kwa kutoa fursa za masomo kwa wanafunzi wa Tanzania kwenda kusoma Czech ambapo wamekubali na kuahidi kuongeza nafasi za masomo kwa wanafunzi wa Tanzania ili kutoa fursa ya watanzania wengi kunufaika na elimu,” Ameongeza Balozi Mbarouk.

Pia viongozi hao wamejadili suala la kukuza sekta ya utalii hapa nchini ambapo Czech ipo katika mchakato wa kuanzisha safari ya ndege ya kuja Tanzania moja kwa moja ili kukuza na kutangaza Utalii lakini pia kukuza biashara kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Kadhalika, Balozi Mbarouk amemuahidi Mhe. Staŝek kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuhakikisha inalinda na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina yake na Jamhuri ya Czech kwa kuwa uhusiano wa mataifa hayo mawili ni wa muda mrefu na wenye maslahi ya mataifa yote mawili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek akiongea na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) wakati walipokutana leo kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek wakati walipokutana leo kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Majadiliano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek akiongea na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) yakiendelea wakati wa mazungumzo leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Majadiliano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek akiongea na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) yakiendelea wakati wa mazungumzo leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek akiongea akipokea zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro kutoka kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) leo Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) leo Jijini Dar es Salaam



Thursday, October 7, 2021

JAMHURI YA CZECH YAKABIDHI VITANDA VIWILI VYA KISASA VYA WAGONJWA OCEAN ROAD

Na Mwandishi wetu, Dar  

Jamhuri ya Czech kwa kushirikiana na kampuni ya Linet Group pamoja na Gama Pharmaceuticals (T) Limited imefanikiwa kuchangia vitanda viwili vya kisasa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road vyenye thamani ya shilingi milioni 16 za kitanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek amekabidhi vitanda hivyo kwa taasisi hiyo na kupokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dr. Julius Mwaiselage pamoja na viongozi wengine wa taasisi mbalimbali za Serikali.

Mhe. Staŝek amesema Serikali ya Czech itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa karibu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina ya mataifa hayo mawili.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi ameishukuru Czech kwa ushirikiano ambao imekuwa ikiutoa kwa Tanzania na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kudumisha ushirikiano wake na Czech kwa maslahi ya pande zote mbili.

Awali akitoa salamu za shukrani, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dr. Julius Mwaiselage ameishukuru Jamhuri ya Czech kwa msaada huo na kuongeza kuwa pamoja na msaada huo, bado taasisi hiyo ina kabiliwa na changamoto ya uhitaji wa vitanda vya kisasa 25 ambapo hadi sasa wanavyo vitanda nane (8) tu hivyo kuwa na uhitaji wa vitanda vingine 17.

Meza kuu wakifuatilia hafla fupi ya makabidhiano ya vitanda viwili vya kisasa vilivyotolewa na Jamhuri ya Czech kwa kushirikiana na kampuni ya Linet Group pamoja na Gama Pharmaceuticals (T) Limited 

Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi akitoa shukrani kwa Jamhuri ya Czech kwa kushirikiana na kampuni ya Linet Group pamoja na Gama Pharmaceuticals (T) Limited kwa msaada wa vitanda vya kisasa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road


Balozi wa Jamhuri ya Czech Mhe. Martin Klepetko, mwenye makazi nchini Kenya akiongea na watumishi pamoja na waandishi wa habari waliohudhuria hafla fupi ya makabidhiano ya vitanda viwili vya kisasa vya Ocean Road

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek akitoa salamu za Serikali yake wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya vitanda viwili vya kisasa vya Ocean Road

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dr. Julius Mwaiselage wakikata utepe wakati wa makabidhiano ya vitanda viwili vya kisasa vitakavyotumika kuhudumia wagonjwa Ocean Road

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dr. Julius Mwaiselage wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi na wawakilishi wa Taasisi mbalimbali mara baada ya kukabidhi vitanda viwili vya kisasa Ocean Road 



 

WAFANYABIASHARA, WAWEKEZAJI KUTOKA CZECH WAONYESHA UTAYARI KUWEKEZA TANZANIA

 Na Mwandishi wetu, Dar

Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Jamhuri ya Czech wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya kilimo hasa Pamba pamoja na viwanda vya nguo hapa nchini.

Akibainisha kuhusu utayari wa Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Czech, kuwekeza hapa nchini, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek amesema wamefurahishwa sana na mazingira ya biashara hapa Tanzania na wapo tayari kuwekeza katika sekta kilimo na viwanda.

Mhe. Staŝek ameyasema hayo wakati alipokutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi leo jijini Dar es Salaam.

Katika ziara yake ya kikazi hapa nchini, Mhe. Staŝek ameambatana na viongozi mbalimbali wa Jamhuri ya Czech akiwemo Naibu Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Czech, mhe. Karel Tyll pamoja na Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka nchini humo.  

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Meh. Miloslav Staŝek amesema yeye pamoja na wajumbe alioongozana nao wamejadiliana na uongozi wa TIC na kupata fursa ya kutambua masuala mbalimbali ya kuongeza ushirikiano ili kuimarisha sekta ya uwekezaji kati ya Czech na Tanzania kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Mimi na Timu yangu tumejadili mambo mbalimbali ya kuwekeza hapa Tanzania ikiwa ni pamoja na utengezaji wa ndege, kilimo, teknolojia pamoja na viwanda.

“Moja ya kampuni niliyoambatana nayo inauzoefu mkubwa katika uzalisha dawa na vifaa tiba, hivyo kampuni hii itakapo pata fursa ya kuwekeza hapa Tanzania itasaidia kuimarisha mahusiano yetu pamoja na kuboresha sekta ya afya,” Amesema mhe. Staŝek.

Mhe. Staŝek ameongeza kuwa wamekubaliana na uongozi wa TIC pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara kutafuta namna bora ya kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wale wa Czech ili kutoa fursa kwa kampuni mbalimbali za Czech kuja kuwekeza kwa wingi hapa Tanzania na wafanyabiashara wa Tanzania kuwekeza nchini Czech kwa maslahi ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi amesema kuwa mara baada ya mazungumzo ya awali, wawekezaji hao wameonsha nia kubwa sana ya kuwekeza katika Pamba na viwanda vya nguo hapa nchini.

“Wameonesha uwezo mkubwa katika biashara na uwekezaji kwenye maeneo ya ufundi wa ndege ambapo baadae kutakuwa na mafunzo mbalimbali ya kubadilishana ujuzi na fursa za uwekezaji……...lakini pia wamevutiwa na sekta ya kilimo hasa katika viwanda vya kutengeneza mafuta ya kula,” Amesema Dkt. Kazi

Nae Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa tunatangaza fursa za biashara na uwekezaji.

“Fursa za kupata wafanyabiashara kutoka Zchec zinazidi kuongezeka hapa nchini, hivyo nitoe rai kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji,” Amesema Dkt. Posi  

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali yaliyolenga kukuza na kuimarisha sekta ya uwekezaji baina ya Tanzania na Czech hapa nchini. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek akiongea na uongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Maduhu Kazi leo jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek wakati Waziri Staŝek alipotembelea taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam


Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi (wa kwanza kulia) akieleza jambo wakati wa mkutano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek na uongozi wa TIC


Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek akimueleza jambo Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam 


Mkutano ukiendelea