Rais wa
Chama Cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA), Bw. Paul
Faraji Koyi, amefanya ziara ya kikazi
nchini Oman hivi karibuni. Akiwa nchini Oman amekutana na kufanya
mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Jumuiya
ya Wafanyabiashara na wenye Viwanda ya Oman, Mhandisi Redha Jumaa Al Saleh.
Katika mazungumzo yao, ambayo yalihudhuriwa pia na
Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Abasi Kilima, viongozi hao walijadili
masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo kukuza biashara na uwekezaji baina ya pande hizo mbili
ili kuzitumia kikamilifu fursa nyingi za kiuchumi zinazopatikana katika nchi
hizi mbili na hatimaye kukuza kiwango cha biashara kati ya nchi hizi ambacho kwa sasa
kinaonekana bado kipo chini.
Wakati wa mazungumzo hayo, Bw. Koyi aliueleza ujumbe wa Oman kuwa,
zipo fursa nyingi nchini Tanzania ambazo Oman inaweza kunufaika nazo zikiwemo za uwekezaji wa Viwanda vya
kuchakata mazao ya Kilimo, Utalii, Uzalishaji Umeme, Kilimo, Ujenzi wa nyumba
na sekta ya usafirishaji wa anga na baharini. Kadhalika aliwajulisha kuwa, Serikali ya Tanzania
inachukua hatua mbalimbali za kuboresha miundombinu ya umeme, barabara, reli na
viwanja vya ndege Ili kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara.
Kwa upande
wake, Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Oman, Mhandisi Al Saleh aliwaeleza
wajumbe kuwa, nchi hiyo imefungua milango ya uwekezaji katika Maeneo Huru ya
Uwekezaji (EPZ) ya Salala, Duqm na Sohar. Aidha, Serikali ya Oman imetoa fursa
kwa wawekezaji kutoka nje kutolazimika kuwa na ubia na mwekezaji mwenyeji.
Akizungumzia suluhisho la changamoto za ufanyaji
biashara kati ya Tanzania na Oman, Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdalah
Kilima amesema tayari Ubalozi huo umewasilisha pendekezo hapa nchini la
kuanzisha safari za ndege ya mizigo kwenda Oman kupitia Shirika la Ndege la
Tanzania (ATCL). Pia Ubalozi umezungumza na mashirika ya meli nchini Oman ili kuanzisha
safari za moja kwa moja kati ya nchi hizi mbili
Wakati
huohuo, Ujumbe wa Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na
Wakulima ya Tanzania walikutana na Viongozi wa Baraza la Biashara kati ya Oman na
Tanzania wa upande wa Oman ambapo walikubaliana kufufua mikakati ya ushirikiano
kupitia Kampuni ya Uwekezaji ya Oman na Tanzania (OTIC) iliyoanzishwa mwaka 2016.
Mbali na kushiriki mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Oman,
Ujumbe wa TCCIA ulifanya ziara katika Kiwanda cha Taifa cha Chai cha Oman,
wazalishaji wa chai ya MUMTAZ jijini Muscat na kupata maelezo ya utendaji wa
kiwanda hicho ambapo pamoja na mambo mengine, Kampuni hiyo imeahidi kufuatilia fursa
zilizopo nchini, ikiwemo upatikanaji wa chai.
Kwenye
ziara hiyo, Rais wa TCCIA nchini alifuatana na Bw. Abdul Mwilima, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara
Mkoa wa Kigoma; Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Nerbat Mwapele na Afisa Masoko
Mwandamizi, Bi. Fatma Khamis.
|
Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA), Bw. Paul Faraji Koyi (mwenye barakoa nyeupe) akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na wenye Viwanda ya Oman, Mhandisi Redha Jumaa Al Saleh (wa kwanza kulia). Bw. Koyi alikuwa nchini Oman kwa ziara ya kikazi ya kuimarisha ushirikiano kati ya TCCIA na Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Oman. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Abasi Kilima (mwenye suti nyeusi). |
|
Viongozi wa Jumuiya za Wafanyabiashara wa Tanzania na Oman wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Kilima ( wa nne kushoto) mara baada ya mazunungumzo ya kuimarisha ushirikiano wa Taasisi zao.
|
|
Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA) akiwa kwenye mazungumzo na Ujumbe wa Kampuni ya Uwekezaji ya Oman na Tanzania (OTIC). Bw. Koyi alikuwa nchini Oman kwa ziara ya kikazi ya kuimarisha ushirikiano kati ya TCCIA na Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Oman. |
|
Mhe. Balozi Kilima (wa pili kushoto) akiwa na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA), Bw. Paul Faraji Koyi (kushoto) walipotembelea kiwanda cha Chai cha Taifa cha Oman kinachozalisha chai ya MUMTAZ jijini Musact hivi karibuni. Bw. Koyi alikuwa nchini Oman kwa ziara ya kikazi. |