Thursday, July 11, 2024

WAZIRI MAKAMBA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA 26 WA KAMATI YA MAWAZIRI WA ASASI YA SIASA, ULINZI NA USALAMA YA SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai, 2024.

 

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika kuanzia tarehe 08 hadi 09 Julai 2024, pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa ikiwemo Mapitio ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Mkutano wa 25 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC; Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Kanda; na Uimarishaji wa Demokrasia katika Kanda.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe amewakaribisha nchini Zambia wajumbe wa mkutano huo ambao agenda yake kuu ni kutathmini hali ya siasa, ulinzi na usalama katika nchi wanachama wa SADC na kuandaa mikakati ya pamoja ya kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana kwenye maeneo ya changamoto.

 

Aidha, akizungumzia hali ya amani na usalama kwenye maeneo yenye  changamoto hususan eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lesotho na eneo la Kaskazini mwa Msumbiji, Mhe. Haimbe amesema hali sasa inatia moyo na kutoa wito kwa nchi wanachama kuendelea kujitolea kwa hali na mali katika kuhakikisha amani, usalama na utulivu wa kudumu vinapatikana  kwenye maeneo hayo ili kuwa na maendeleo endelevu ya kiuchumi katika kanda.

 

Kadhalika amezipongeza misheni za ulinzi wa amani za SADC iliyopo DRC na ile iliyopo Kaskazini mwa Msumbiji kwa kujitoa kikamilifu katika kuhakikisha amani na usalama kwenye maeneo hayo vinarejea mbali na changamoto kadhaa wanazopitia.

 

Kuhusu misheni ya ulinzi wa amani ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) ambayo inamaliza muda wake wa operesheni mwezi Julai 2024, Mhe. Haimbe ameipongeza kwa kazi kubwa iliyofanyika ya kupambana na vitendo vya ugaidi na kurejesha hali ya amani kwa wananchi wa Jimbo la Cabo Delgado lililopo Kaskazini mwa Msumbiji.

 

“Napongeza misheni ya SAMIM kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanyika. Japo wanamaliza operesheni huko Kaskazini mwa Msumbiji, bado mapambano dhidi ya ugaidi na uhalifu wa kuvuka mipaka katika Nchi zote wanachama wa SADC yataendelea. Hivyo naziomba nchi zote wanachana kuendelea kushirikiana na kuandaa mikakati ya pamoja kukabiliana na vitisho hivi” alisisitiza Mhe. Haimbe.

 

Awali akizungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Mpedi Magosi amesema kuwa Sekretarieti ya SADC itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama hususan katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda zikiwemo za kiusalama, kijamii na kiuchumi ili hatimaye kuwa na Kanda tulivu kwa ajili ya maendeleo endelevu.

 

Pia aliongeza kusema bado jitihada za pamoja zinahitajika katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda ikiwemo ugaidi, vitendo vya uhalifu wa kuvuka mipaka na rushwa. Kadhalika, Mhe. Makosi alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri anayemaliza muda wake Mhe. Haimbe kwa kazi nzuri aliyofanya katika kipindi chote na kumkaribisha na kumwahidi ushirikiano Mwenyekiti mpya ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. January Makamba.

 

Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ilianzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kukuza na kulinda amani na usalama katika kanda ya SADC. Tanzania inachukua uenyekiti wa asasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Agosti 2024.

 

Mbali na Mhe. Makamba, ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Daniel Sillo, Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe,  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda,  Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jen. Mathew Mkingule, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Maafisa Waandamizi wa Wizara na Vyombo vya ulinzi na Usalama.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akiongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai 2024.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo (kulia) akiwa na  Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe wakishiriki  Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai 2024.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kushoto) kwa pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda (katikati) na Katibu Mkuu, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Mnyepe (kulia) wakishiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai 2024.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi  rasmi Mkutano huo iliyofanyika tarehe 11 Julai 2024  katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mulungushi uliopo jijini Lusaka, Zambia
Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya SADC, Bw. Elias Mpedi Magosi naye akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Shelukindo akiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri. Wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri
Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jenerali Mathew Mkingule akishiriki Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa SADC

Meza kuu

Mkutano ukiendelea

Mhe. Waziri Makamba akizungumza na viongozi mbalimbali kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC

Picha ya pamoja

 

Wednesday, July 10, 2024

WAZIRI MAKAMBA AZUNGUMZA NA WAZIRI MPYA ANAYESHUGHULIKIA USHIRIKIANO NA UHUSIANO WA KIMATAIFA WA AFRIKA KUSINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba leo tarehe 10 Julai 2024 akiwa jijini Lusaka, Zambia amezungumza kwa njia ya mtandao na Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Ronald Lamola.

 

Katika mazungumzo yao, Mhe. Makamba amempongeza Mhe. Lamola kwa kuteuliwa kwenye wadhifa huo hivi karibuni na kumuahidi ushirikiano kutoka kwake na Serikali ya Tanzania kwa ujumla ili kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kindugu uliopo baina ya nchi hizi mbili.

 

Vilevile viongozi hao wamejadili na kukubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ulinzi na usalama katika ukanda wa Kusini mwa Afrika pamoja na kuendelea kuwaunga mkono wagombea wa nafasi mbalimbali  wanaojitokeza kuwania nafasi kwenye mashirika ya  kikanda na kimataifa kutoka kwenye mataifa haya mawili.

 

Kupitia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ambayo wenyeviti wake ni Marais wa nchi hizi mbili, Mawaziri hao wamekubaliana  kuimarisha ushirikiano kwenye sekta za kimkakati ikiwemo biashara, uwekezaji na utalii ili kunufaika kiuchumi kupitia ushirikiano huo ambapo pia wamekubaliana kuandaa mkutano wa tume hiyo mapema mwaka 2025.

 

Katika kuimarisha sekta ya biashara na utalii, Mhe. Waziri Makamba pia alimjulisha Mhe. Lamola kwamba Shirika la Ndege la Tanzania  kuanzia mwezi Septemba 2024  litaanza kufanya safari zake mara nne kwa wiki nchini Afrika Kusini ikiwa ni ongezeko la safari tatu..

 

Kadhalika  viongozi hao wamezungumza na kukubaliana  kuendelea kushirikiana kwenye masuala yanayohusu ulinzi na usalama katika ukanda wa Kusini mwa Afrika na  katika masuala ya kikanda na kimataifa ikiwemo kuwaunga mkono wagombea wa nafasi mbalimbali  wanaojitokeza kuwania nafasi kwenye mashirika ya  kikanda na kimataifa kutoka kwenye mataifa haya mawili.

 

Aidha, Tanzania ikiwa mstari wa mbele wakati wa harakati za ukombozi kusini mwa Afrika, viongozi hao  wamekubaliana kushirikiana kwenye masuala ya utunzaji wa Historia na Urithi wa Ukombozi wa Afrika kwa vizazi vya sasa na vinavyokuja.

 

Mhe. Makamba pia alitumia nafasi hiyo kumkaribisha Mhe. Lamola kutembelea Tanzania na kumkubalia ombi lake la kumtafutia mwalimu wa kumfundisha Lugha adhimu ya Kiswahili.

 

Kwa upande wake, Mhe. Lamola alimshukuru Mhe. Makamba na Serikali ya Tanzania kwa ujumla kwa kuendeleza ushirikiano na nchi yake katika kipindi chote tangu enzi za harakati za ukombozi kusini mwa Afrika hadi sasa.

 

Katika hatua nyingine, Mhe. Lamola alimweleza Mhe. Makamba kuwa nchi yake inapongeza na kuunga mkono uamuzi wa Serikali ya Tanzania wa kuhamishia Makao makuu yake  jijini Dodoma na kwamba  nchi hiyo ipo katika hatua za upembuzi yakinifu ili kuitikia wito wa Serikali ya Tanzania wa kuzihimiza Balozi kuhamia katika jiji hilo.

 

Mhe. Makamba yupo nchini Zambia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unatarajiwa kufanyika tarehe 11 na 12 Julai 2024.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza kwa njia ya mtandao na Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Ronald Lamola ambapo pamoja na mambo mengine amempongeza kwa kuteuliwa katika wadhifa huo na kumwahidi ushirikiano. Mazugumzo hayo yamefanyika huku Mhe. Makamba akiwa jijini Lusaka, Zambia ambapo anatarajiwa kushiriki Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC utakaofanyika tarehe 11 na 12 Julai 2024. Mkutano huo pia umehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (aliyeketi kushoto kwa Mhe. Waziri Makamba), Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ali Sakila na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. James Bwana ambao walishiriki kwa njia ya mtandao.
Mhe. Waziri Makamba na ujumbe aliofuatana nao akiendelea na mazungumzo na Mhe. Lamola




 

WAZIRI BYABATO AIPONGEZA BURUNDI KWA KUDUMISHA AMANI NA USALAMA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Balozi wa Burundi nchini Tanzania Mhe. Leontine Nzeyimana katika picha ya pamoja alipowasili kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Jamhuri ya Burundi iliyofanyika jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato amepoingeza Jamhuri ya Burundi kwa kuendelea kulinda na kudumisha amani na usalama nchini humo.

Naibu Waziri Byabato amasema hayo alipokuwa akihutubia Jumuiya ya Wadiplomasia na wageni wengine waalikwa kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Jamhuri ya Burundi iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Vilevile alibainisha kuwa katika kipindi hicho cha miaka 62 dunia imeshuhudi Taifa hilo likipiga hatua muhimu ya maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo siasa na uchumi. 

“Hakika mtakubaliana nami kuwa katika kipindi cha miaka 62, Burundi imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika nyanja za kisiasa na kiuchumi. Mathalani, kisiasa tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Amani hapa jijini Dar es Salaam mwaka 2006, Burundi imeweza kudumisha amani na usalama nchini kote pamoja na kukuza demokrasia na utawala bora” Alieleza Naibu Waziri Byabato

Mbali na hayo Waziri Byabato aliongeza kuwa Tanzania na Burundi zimeendelea kuwa na ushirikiano wa karibu wakati wote, ukichagizwa na mkaba uliosaniwa mwaka 1975 wa uanzishaji wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ambao ulifungua ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimkakati ikiwemo elimu, afya, kilimo, biashara na uwekezaji, utalii,nishati, usafirishaji, ulinzi na usalama na masuala ya uhamiaji. 

Kwa upande wake Balozi wa Burundi nchini Tanzania Mhe. Leontine Nzeyimana alieleza kuwa katika kipindi cha miaka 62 ya uhuru, Taifa hilo linajivunia kuendelea kudumisha uhusiano mzuri wa kidiplomasia na Mataifa mbalimbali duniani na nchi jirani katika Kanda ya Afrika Mashariki.

Balozi Nzeyimana aliendelea kubainisha kuwa katika nyanja ya uchumi Burundi inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo Tanzania, ambapo mradi wa SGR unatarajiwa kuliunganisha Taifa hilo na Bandari ya Dar es Salaam hivyo kutoa mchango mkubwa katika kurahishisha na kuongeza biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Burundi. 

Takwimu zinaonyesha kuwa biashara kati ya Tanzania na Burundi inaendelea kukua ambapo ilifikia dola milioni 212.8 mwaka 2022/2023 kutoka dola 61.3 milioni mwaka 2017/2018. Huku takriban asilimia 95 ya mizigo ya Burundi ikipitia Bandari ya Dar es Salaam. 

Tanzania na Burundi zinashirikiana kwa karibu katika ngazi za kikanda na kimataifa ikiwemo EAC, ICGRL, AU, UN, Jumuiya ya Nchi zisizofungamana na Siasa za Upande wowote (NAM). 

Aidha Naibu Waziri Byabato alisisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Burundi ili kuimarisha zaidi uhusiano kwa manufaa ya pande zote mbili na watu wake. Vile vile, kuendelea kuwa mshirika wa wakati wote na wa kuaminika wa Burundi kwenye masuala ya kikanda na kimataifa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akihutubia wageni waalikwa kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Jamhuri ya Burundi iliyofanyika jijini Dar es Salaam
Picha ya pamoja
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akifurahia jambo na baadhi ya wageni waalikwa kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Jamhuri ya Burundi iliyofanyika jijini Dar es Salaam
Balozi wa Burundi nchini Tanzania Mhe. Leontine Nzeyimana akihutubia kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Jamhuri ya Burundi iliyofanyika jijini Dar es Salaam
Sehemu ya wageni waalikwa wakifuatilia matukio kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Jamhuri ya Burundi iliyofanyika jijini Dar es Salaam

Tuesday, July 9, 2024

WAZIRI MAKAMBA AMUAGA BALOZI WA DENMARK

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Balozi wa Denmark aliyemaliza muda wake wa kuhudumu nchini Mhe. Mette Norgaard Dissing – Spandet walipokuwa katika mazungumzo yaliyofanyika kwenye ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba amemuaga Balozi wa Denmark nchini Tanzania Mhe. Mette Norgaard Dissing – Spandet baada ya kumaliza muda wake wa kuhudumu hapa nchini katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Waziri Makamba amempongeza Balozi Mette kwa kazi nzuri aliyoifanya nchini katika kipindi cha uwakili wake, sio tu kwa kukuza na kudumisha uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na Denmark vilevile kwa mchango wake hadhimu kwenye utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ambayo imechangia katika ukuaji wa maendeleo nchini. 

Aidha Waziri Makamba amempongeza Balozi Mette kwa mchango wake alioutoa katika kutafuta suluhu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia ikiwemo kukabiliana na mabadiliko ya TabiaNchi na masuala ya amani na usalama. 

Kwa upande wake Balozi Mette ameeleza kuwa licha kuendelea kukua kwa uhusiano wa kidiplomasia bado juhudi zaidi zinahitajika katika kukuza kiwango cha biashara na uwekezaji katika ya Tanzania na Denmark. Aidha, Balozi Mette ameishukuru Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi mahiri wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa ushirikiano mzuri alioupata wakati wote akitimza majukumu yake hapa nchini.

"Natambua kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, licha kumaliza kipindi changu cha kuhudumu kama Balozi, nitaendelea kutoa mchango wangu kwa namna mbalimbali ili kuhakikisha kiwango cha biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na Denmark kinaongezeka" Alieleza Balozi Mette

Tanzania na Denmark zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya, elimu na biashara na uwekezaji. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Balozi wa Denmark nchini Tanzania Mhe. Mette Norgaard Dissing – Spandet anayemaliza muda wake wa kuhudumu nchini katika katika picha ya pamoja
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Denmark nchini Tanzania Mhe. Mette Norgaard Dissing – Spandet aliyemaliza muda wake wa kuhudumu nchini yaliyofanyika katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akimsikiliza Balozi wa Denmark aliyemaliza muda wake wa kuhudumu nchini Mhe. Mette Norgaard Dissing – Spandet walipokuwa katika mazungumzo yaliyofanyika kwenye ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaa

Monday, July 8, 2024

MKUTANO WA MAWAZIRI WA EAC WAMALIZIKA ZANZIBAR

 














 

 


 

Mkutano wa faragha wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wanashughulikia masuala ya Afrika Mashariki ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Zanzibar tarehe 6-8 Julai,2024 wamalizika.

Mkutano huo ulikuwa chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba ulihudhuriwa na Mawaziri kutoka nchi za Burundi, DRC, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Uganda na mwenyeji Tanzania