Monday, November 29, 2021
HABARI PICHA: RAIS WA JAMHURI YA UGANDA AHITIMISHA ZAIRA YAKE YA KIKAZI YA SIKU TATU NCHINI
Sunday, November 28, 2021
TANZANIA KUSHIRIKI MKUTANO JUKWAA LA USHIRIKIANO KATI YA CHINA NA AFRIKA
Na mwandishi wetu, Dakar
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaoanza leo tarehe 28 hadi 30 Novemba 2021 jijini Dakar nchini Senegal.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ataongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo.
Katika Ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, Marais wa Nchi Wenyeviti Wenza wa Mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Senegal Mhe. Macky Sall na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping watahutubia Mkutano huo.
Mkutano huo wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika unatanguliwa na Mkutano wa Maafisa Waandamizi unaoanza leo tarehe 28 Novemba 2021 hapa Jijini Dakar, Senegal ambapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mpango Zanzibar Dkt. Juma Akil na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bibi Amina Shaaban watashiriki.
Mkutano huo utakaowashirikisha viongozi na wawakilishi kutoka nchi za Bara la Afrika na Jamhuri ya Watu wa China pamoja na mambo mengine utajikita katika majadiliano ya maeneo yafuatayo:- Ushirikiano wa Kisiasa, Ushirikiano wa Kiuchumi, Ushirikiano wa Maendeleo ya Kijamii, Utamaduni na Ushirikiano kati ya Watu na Watu, Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama, Mapinduzi ya Kijani, Ubadilishanaji Uzoefu katika masuala ya Uongozi Bora pamoja na Maendeleo ya Kitaasisi ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika.
RAIS SAMIA NA RAIS MUSEVENI WAFUNGA KONGAMANO LA WAFANYABIASHARA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
pamoja na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museven wameshiriki
katika kufunga Kongamano la Wafanyabiashara kati ya Tanzania na Uganda
lililofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam
Pamoja
na mambo mengine, Viongozi hao wameahidi kuendelea kushirikiana na sekta
binafsi katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika sekta ya nishati na
gesi ili kufungua fursa kwa wananchi wa pande zote mbili.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati
wa ufungaji wa Kongamano la Wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda
lililohudhuriwa na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika viwanja
vya Ikulu Jijini Dar es salaam
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati
wa ufungaji wa Kongamano la Wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda
lililohudhuriwa na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika viwanja
vya Ikulu Jijini Dar es salaam
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Rais
wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni mara baada ya kufunga Kongamano la
Wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda lililofanyika katika viwanja vya Ikulu
Jijini Dar es salaam
Baadhi
ya Mawaziri, Makatibu Wakuu pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali
wakifuatilia ufungaji wa Kongamano la Wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda
lililofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam
Sehemu ya Mawaziri na Wafanyabiashara wakifuatilia ufungaji wa Kongamano la Wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda
lililofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam
Saturday, November 27, 2021
TANZANIA NA UGANDA ZAKUBALINA KUIMARISHA USHIRIKIANO
Na Waandishi wetu, Dar
Tanzania na Uganda zimekubaliana kuimarisha
ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimkakati zikiwemo nishati, utalii,
usafirishaji, viwanda, kilimo na uvuvi kwa maslahi ya wananchi wa pande zote mbili.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo
rasmi kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
na Rais wa jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni yaliyofanyika leo
tarehe 27 Novemba 2021, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa ya mazungumzo baina yao kwa waandishi wa habari, Mhe. Rais Samia amesema
Tanzania na Uganda zimeendelea kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali ya uwekezaji
na biashara kwa miaka mingi ambapo hadi sasa Uganda ni nchi ya pili kwa
uwekezaji nchini Tanzania kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tumezungumza masuala mengi na Mhe. Rais Museveni
na tumekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kindugu uliopo kati yetu
hususan kwenye sekta za manufaa kwetu sote. Pia tumekubaliana kuimarisha
biashara na uwekezaji baina yetu na ninafurahi kuwajulisha kuwa hadi sasa Uganda
ni nchi ya pili kwa uwekezaji nchini Tanzania
kwa ukanda wa Afrika Mashariki ambapo ipo miradi 45 yenye thamani ya Dola
milioni 114 na imewezesha kutoa ajira kwa watanzania 2150”, amesema Mhe. Samia.
Kuhusu masuala ya biashara, Mhe. Rais Samia amesema
mwenendo wa biashara kati ya Tanzania na Uganda ni mzuri ambapo hadi kufikia
mwaka 2020 ujazo wa baishara kati ya nchi hizo umeongezeka hadi kufikia
Shilingi bilioni 607 kutoka shilingi bilioni 200 mwaka 20214.
Kadhalika, viongozii hao wamewaagiza Mawaziri
wanaoshughulikia masuala ya biashara wa Tanzania na Uganda kukutana mara kwa
mara ili kutatua changamoto mbalimbali za ufanyaji biashara na kuwataka
kukutana katika kipindi cha miezi miwili ijayo kujadili namna ya kuondoa
vikwazo visivyo vya kiforodha vilivyopo baina ya nchi hizo kwa lengo la
kurahisisha ufanyaji biashara.
Rais Samia ameongeza kuwa pia wamekubaliana kufungua
Ofisi ya Bandari nchini Uganda ili kurahisisha na kukuza biashara kati ya
Tanzania na Uganda.
Akizungumzia kuhusu Ugonjwa wa UVIKO 19, Mhe. Rais Samia
amesema wamekubaliana kuanzisha kiwanda cha pamoja cha kuzalisha dawa na chanjo
kwa ajili ya binadamu na wanyama kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya
mlipuko ikiwemo UVIKO 19.
Aidha, Rais Samia ametumia fursa hiyo kumpongeza
Mhe. Rais Museveni kwa kufadhili ujenzi wa Shule ya Msingi huko Wilayani Chato,
Mkoani Geita na kusema kitendo hicho ni cha kuigwa kwani Mhe. Rais Museveni
anatambua umuhimu wa elimu kwa watoto wa Tanzania.
Rais Samia amesema pia katika mazungumzo yao
wamewaagiza Mawaziri wa Mambo ya Nje kufanya mkutano wa Tume ya Pamoja ya
Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda mwezi Disemba ili kuweka mikakati ya
kutekeleza makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa kwa nyakati tofauti na nchini
hizi mbili.
Kwa upande wake, Rais Museveni amemshukuru mwenyeji
wake kwa mwaliko na kusisitiza kwamba ushirikiano huo wa kindugu kati ya Tanzania na Uganda utaimarishwa na kuenziwa kwa maslahi mapana ya pande zote
mbili.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la
Afrika Mashariki, Rais Museveni amesema kuwa matayarisho ya msingi kuhusu kuanza
kwa ujenzi wa mradi wa bomba hilo yamekamilika.
Mhe. Rais Museveni yupo nchini kwa ziara ya kitaifa
ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine, atashiriki Kongamano la Biashara
kati ya Tanzania na Uganda, atatembelea Bandari ya Dar es Salaam na mradi wa Ujenzi
wa Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na kukabidhi shule ya msingi iliyojengwa
Wilayani Chato kwa ufadhili wake.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimtambulisha
mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni kwa wakuu wa vyombo
vya Ulinzi na Usalama mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam
Rais
wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni akisalimiana na viongozi mbalimbali
wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makala. Wengine ni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata
Mulamula (Mb), Balozi wa Tanzania Nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima pamoja na
Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Naimi Aziz
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na mgeni
wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni Ikulu Jijini Dar es Salaam
Rais
wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni akiteta jambo na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam
Rais
wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni akiongea na waandishi wa habari
(hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam
Baadhi ya Mawaziri, Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na viongozi waandamizi serikalini wakifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiongea na waandishi wa habari Ikulu Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akisoma tamko la pamoja kati ya Tanzania na Uganda, Ikulu Jijini Dar es Salaam |
Friday, November 26, 2021
Maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa EAC yakamilika
Na Mwandishi Maalum,
Arusha
Mawaziri
wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) watakutana jijini Arusha katika
Mkutano wao wa 41 wa Baraza la Mawairi uliopangwa kufanyika tarehe 29 Novemba
2021.
Makatibu
Wakuu wamekamilisha maandalizi yote yanayohitajika ya mkutano huo, zikiwemo
nyaraka za taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Jumuiya, vyombo na Taasisi
zake katika kikao kilichofayika tarehe 25 na 26 Novemba 2021.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Joseph Sokoine ameongoza Makatibu Wakuu wenzake katika kikao hicho, akiwemo Katibu
Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome; Katibu Mkuu wa Ofisi
ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro;
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Ikulu, Zanzibar, Bw Mussa Haji Ali na Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah.
Mkutano
wa Mawaziri ambao utakuwa chini ya uenyekiti wa Kenya unatarajiwa kufanya maamuzi
na kutoa maelekezo kuhusu utekeleaji wa masuala ya mtangamano katika maeneo mbalimbali
yakiwemo ya biashara, miundombinu, afya, ajira, fedha na uanzishwaji wa taasisi
mpya hususan taasisi za fedha zitakazosimamia Umoja wa Fedha.
Waheshimiwa
Mawaziri pia watapitia na kupitisha ratiba ya shughuli za EAC kwa kipindi cha
kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2022. Shughuli hizo zinajumuisha mikutano
ambapo kwa kanuni za EAC asilimia 50 ya mikutano inafanyika katika nchi
wanachama na asilimia 50 iliyosalia inafanyika makao makuu ya Jumuiya. Licha ya
makao makuu ya EAC kuwa Tanzania, bado nchi hiyo inapewa mgawo wa mikutano ya
asilimia 50 inayofanyika katika nchi wanachama.
Mkutano wa Mawaziri unatarajiwa kuhitimishwa kwa Mawaziri kushuhudia uwekaji saini wa mikataba ya utekelezaji wa majukumu (performance contracts) kati ya Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na Katibu Mkuu wa EAC na baina ya Katibu Mkuu wa EAC na Naibu Makatibu Wakuu na Wakurugenzi wa Idara mbalimbali za EAC.
Meza Kuu wakati wa Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu Wakuu ikiendesha kikao jijini Arusha. |
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kenya ukifuatilia kikao |
Ujumbe wa Tanzania kutoka Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali unaoshiriki mkutano huo. |
Wakurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mjadala wa mkutano wa Makatibu Wakuu. |
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Ellen Maduhu akifuatilia kwa makini mjadala wa mkutano. |
TANZANIA, USWISI KUIMARISHA USHIRIKIANO ZAIDI
Na Mwandishi Wetu, Dar
Tanzania na
Uswisi zimekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta za afya,
elimu na uchumi kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa pande zote mbili.
Ahadi hiyo
imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi
Liberata Mulamula (Mb) alipokuwa katika maadhimisho ya miaka 40 ya Ushirikiano
wa Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi jana jioni jijini Dar es Salaam.
Balozi
Mulamula amesema kuwa katika miaka 40 ya Ushirikiano wa maendeleo kati ya
Tanzania na Uswisi, ushirikiano umeimarika na nchi hizi zimekuwa zikiufurahia
kwa kipindi chote, na kuongeza kuwa “Uhusiano
kati ya Tanzania na Uswisi ni mzuri na imara na umekuwa na manufaa kwa pande
zote mbili,” amesema Balozi Mulamula
“Tunapozindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Uswisi na Tanzania 2021-2024,
ambao pamoja na mambo mengine, umejikita katika kuimarisha taasisi za serikali,
kulinda na kuboresha afya na maisha ya vijana. Napongeza juhudi zinazofanywa na
Uswisi katika maandalizi na ukamilishaji wa mpango wa maendeleo ambao sasa
unatupeleka katika hatua nyingine ya utekelezaji,” ameongeza Balozi Mulamula.
Waziri Mulamula ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa
ikichukua hatua madhubuti katika kupitia na kuboresha mazingira ya biashara na
uwekezaji hapa nchini ambapo Serikali na sekta binafsi wanafanya kazi kwa
kutunga na kuboresha sera zitakazolinda na kuwezesha sekta binafsi kukua.
Pia Balozi Mulamula amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za
kurekebisha Sera ya Uwekezaji ya mwaka 1996. Utaratibu huu unafanywa kwa njia
shirikishi ambayo inahusisha sekta ya umma na binafsi. Mipango hii itachangia
katika kuweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji na biashara kwa wawekezaji na
biashara kutoka mataifa makubwa duniani na washirika wengine wa kibiashara.
Kwa upande wake, Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot amesema
kuwa ushirikiano wa Uswisi na Tanzania umelenga zaidi uboreshaji wa barabara za
vijijini, maendeleo ya kilimo, sekta ya afya na uwezeshaji wa asasi za kiraia.
Aliongeza kusema kuwa, miradi ya maendeleo ya Uswisi nchini Tanzania imepanuka
na kujumuisha shughuli mbalimbali katika nyanja za utawala, uvumbuzi, kuongeza
ujuzi, mafunzo ya ufundi stadi na utamaduni.
“Ushirikiano wetu umekuwa na mafanikio mengi na katika kipindi cha miaka
40 iliyopita ambapo Uswisi imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa katika sekta za
afya, ujenzi wa taasisi na mafunzo ya wafanyakazi wa afya,” amesema Balozi
Chassot
Balozi Chassot ameongeza kuwa, Uswisi itaendelea kushirikiana na Tanzania
katika kuimarisha utawala wa kidemokrasia, kutoa msaada wa kuimarisha taasisi
za serikali ili kuongeza mapato ya umma na kutoa huduma bora za umma, zenye
usawa na zinazofaa zaidi kwa wananchi wote, kupunguza vikwazo vya kijamii na
kiuchumi pamoja na kuimarisha matarajio ya kiuchumi kwa vijana.
Tunatazamia kuimarisha zaidi ushirikiano wetu na washirika wetu
serikalini na mashirika ya kiraia katika kutekeleza agenda ya kimataifa ya
kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Dazi
amesema kuwa wameridhishwa na hatua za maendeleo ambazo Tanzania imepiga na
kuahidi kuendelea kushirikiana zaidi katika kuwainua wananchi kiuchumi.
“Uswisi imekuwa ikishirikiana na Tanzania kwa zaidi ya miaka 40 na tutaendelea kuudumisha ushirikiano huu kuwainua vijana kiuchumi ili kuwawezesha kufikia malengo yao kijamii na kisiasa,” amesema Bi. Dazi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Liberata Mulamula akihutubia katika maadhimisho ya miaka 40 ya
Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi jana jioni jijini Dar es
Salaam
Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot akihutubia
katika maadhimisho ya miaka 40 ya Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Tanzania na
Uswisi jana jioni jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Uswisi
Bi. Patricia Dazi akihutubia katika maadhimisho ya miaka 40 ya Ushirikiano wa
Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier
Chassot katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la
Uswisi Bi. Patricia Dazi
Sehemu ya wageni waalikwa walioshiriki katika maadhimisho
ya miaka 40 ya Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi jana jioni
jijini Dar es Salaam
|