Friday, November 1, 2024

MISHENI ZA UANGALIZI UCHAGUZI MKUU BOTSWANA ZATOA TAARIFA ZA AWALI KUHUSU UCHAGUZI HUO ULIVYOENDESHWA


Wakuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi mkuu wa Botswana kutoka SADC -SEOM Mhe. Mizengo Pinda (katikati aliyekaa) akiwa na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi ya Umoja wa Afrika (AU-EOM) Mhe. Goodluck Jonathan (wa pili kushoto) na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi kutoka Jukwaa la Tume za Uchaguzi SADC(SADC -ECF) Jaji Jacob Mwambegele (wa pili kulia) wakiwa katika meza kuu

 

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi ya Umoja wa Afrika (AU-EOM) Mhe. Goodluck Jonathan (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi mkuu wa Botswana wa SADC -SEOM Mhe. Mizengo Pinda

Wakuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi mkuu wa Botswana kutoka SADC -SEOM Mhe. Mizengo Pinda (kulia) akiwa na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi ya Umoja wa Afrika (AU-EOM) Mhe. Goodluck Jonathan (katikati) na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi kutoka Jukwaa la Tume za Uchaguzi za SADC Jaji Jacob Mwambengele (kushoto) katika meza kuu wakati wa kuwsilisha tarifa za misheni zzao jijini Gaborone tarehe 01 November, 2024.

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi mkuu wa Botswana wa SADC -SEOM Mhe. Mizengo Pinda (kulia) akiwasilisha tarifa ya SEOM

 

wageni waalikwa wakisikiliza taarifa za awali kutoka kwa waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi mkuu wa Botswana zilizowasilishwa jijini Gaborone tarehe 01 Novemba 2024

Waangalizi wa SEOM  wakifuatilia tarifa ya wali iliyokuwa ikiwasilishwa na Mkuu wa misheni hiyo

wageni waalikwa wakisikiliza taarifa za awali kutoka kwa waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi mkuu wa Botswana zilizowasilishwa jijini Gaborone tarehe 01 Novemba 2024

 

Wakuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi mkuu wa Botswana kutoka SADC -SEOM Mhe. Mizengo Pinda (katikati aliyekaa) akiwa na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi ya Umoja wa Afrika (AU-EOM) Mhe. Goodluck Jonathan (wa pili kushoto) na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi kutoka Jukwaa la Tume za Uchaguzi SADC(SADC -ECF) Jaji Jacob Mwambegele (wa pili kulia) katika picha ya pamoja na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini Botswana baada ya misheni hizo kutoa taarifa za awali za mishenio zao jijini Gaborone tarehe 01 Novemba, 2024

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi mkuu wa Botswana wa SADC -SEOM Mhe. Mizengo Pinda (katikati) akiwa na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi ya Umoja wa Afrika (AU-EOM) Mhe. Goodluck Jonathan (wa pili kushoto) na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi kutoka Jukwaa la Tume za Uchaguzi SADC(SADC -ECF)Jaji Jacob Mwambegele (wa pili kulia) na Katibu Mtendaji wa SADC Mhe. Elias Magosi (kulia) na wajumbe wa SEOM waliosimama

Wakuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi mkuu wa Botswana kutoka SADC -SEOM Mhe. Mizengo Pinda (katikati aliyekaa) akiwa na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi kutoka Jukwaa la Tume za Uchaguzi SADC(SADC -ECF) Jaji Jacob Mwambegele (wa pili kushoto) katika picha ya pamoja na wajumbe wa SEOM na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Botswana Mhe. James Bwana (kulia)  jijini Gaborone tarehe 01 Novemba, 2024


Misheni za Uangalizi uchaguzi mkuu wa Botswana kutoka Jumumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC-SEOM), Umoja wa Afrika (AU_EOM) na Jukwaa la Tume za Uchaguzi la SADC (ECF) zimetoa taarifa za awali kuhusiana na uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika tarehe 30 Oktoba 2024.

Akıwasilisha taarifa hiyo jijini Gaborone, kwa upande wa misheni ya  SADC-SEOM  Mkuu wa Misheni hiyo Mhe.Mizengo Pinda amesema katika uchaguzi huo SEOM imeona kuwa mazingira ya kisiasa nchini humo yalikuwa ya utulivu na yenye amani kuanzia kipindi cha kampeni, siku ya kupiga kura na hata baada ya kupiga kura.

“SEOM iliona kuwa shughuli za kisiasa kuanzia hatua za awali kuelekea siku ya uchaguzi na siku ya kupiga katika Jamhuri ya Botswana zilifanyika kwa amani na kwa utulivu mkubwa na hivyo kuwawezesha wananchi wa Botswana kutumia haki yao ya kimsingi ya kidemokrasia ya kupiga kura, kwa utulivu na amani pia,” alisisitiza Mhe. Pinda.

Ameongeza kuwa SEOM ilishuhudia vyama vya siasa na wagombea binafsi nchini humo wakiendesha kampeni kwa uhuru na amani  ambazo zilifanyika kupitia mikutano, nyumba kwa nyumba, midahalo kwa wagombea wa urais , mahojiano na mijadala katika vyombo vya Habari na mabango katika sehemu mbalimbali nchini humo ambapo amesema katika shughuli zote hizo hakukuwa na vurugu wala fujo hali iliyoonesha uvumilivu wa hali ya juu wa kisiasa na ukomavu kwa watu wa Botswana.

Akiongelea zoezi la upigaji kura la awali lililofanyika tarehe 19 na 26 Oktoba 2024, Mhe.Pinda alisema kuwa zoezi hilo liliendeshwa kwa amani licha ya kuwepo kwa tukio la mpiga kura mmoja kuondoka na karatasi ya kupigia kura na baadhi ya vyama kulalamika kuondolewa kwa mabango yao na kuongeza kuwa askari polisi walikuwepo  katika mikutano ya kampeni katika maeneo yote na kuliendelea kuwa na amani hata pale ambapo hakukuwa na askari polisi.

Amesema SEOM  iliangalia masuala mbalimbali ya muhimu kabla na wakati wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na hali ya siasa na usalama chini humo, usimamizi wa uchaguzi, ripoti za vyombo vya habari kuhusu uchaguzi, na uwakilishi wa jinsia na Makundi maalum ambayo yote yametekelezwa kwa kiasi kikubwa.

Akiwasilisha taarifa ya misheni yake Mkuu wa Misheni ya AU_EOM na Rais wa zamani wa Nigeria Mhe. Goodluck Jonathan amesema AU pia inawapongeza wananchi wa Botswana  kwa kuonyesha ukomavu wa kisiasa na uvumilivu wa hali ya juu katika kipindi chote cha uchaguzi, na kuwasihi kuendelea hivyo kwakuwa siasa si uadui bali ni ushindani wa hoja na kupigiana kura zitakazoamua kupitia uchaguzi.

Naye Mkuu wa misheni ya SADC _ECF na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania Mhe. Jaji Jacob Mwambegele ametoa wito kwa wadau mbalimbali nchini humo kuendelea kuwa watulivu na wavumilivu wakati mamlaka za usimamizi wa uchaguzi zikikamilisha matokeo ya uchaguzi kabla ya kutangazwa rasmi, akiwaomba kuendelea kuhamasisha amani, uvumilivu, na utulivu kupitia majukwaa mbalimbali katika kipindi hiki cha baada ya uchaguzi.

Kulingana na Misingi na Miongozo ya SADC inayosimamia uchaguzi wa kidemokrasi iliyorekebishwa mwaka 2021, misheni hizo za SADC na AU zitatoa taarifa ya mwisho kuhusu uchaguzi siku 30 baada ya kutoa taarifa ya awali ambayo itawasilishwa kwa Serikali ya nchi hiyo ili kufanyia kazi mapendekezo ya taarifa hizo na hivyo kuboresha mazingira ya ufanyaji uchaguzi mkuu mwingine ujao nchini humo.

SEOM ilipeleka waangalizi 72 waliotoka katika nchi 10 wanachama wa SADC  ambao walikwenda katika wilaya 9 za kiutawala za nchini humo za Kati, Ghanzi; Kgalagadi; Kgatleng; Kweneng; Ngamiland; Kaskazini Mashariki; Kusini na Kusini Mashariki.

Siku ya Uchaguzi tarehe 30 Oktoba, 2024 Misheni hizo zilitembelea vituo vya uchaguzi kuangalia namna zoezi linavyoendeshwa na pia zilishuhudia awamu ya pili ya upigaji kura wa awali uliofanyika tarehe 26 Oktoba,2024.


SERIKALI KUENDELEA KUKUZA MATUMIZI YA LUGHA YA KISWAHILI KIKANDA NA KIMATAIFA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) ameliambia Bunge kuwa Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza na kutangaza Lugha ya Kiswahili duniani ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha matumizi ya Lugha hiyo katika Taasisi za Kikanda na Kimataifa na kuhakikisha inafundishwa kama taaluma ili kuzalisha wakalimani bora.

 

Mhe. Chumi ametoa kauli hiyo Bungeni, jijini Dodoma leo tarehe 01 Novemba 2024 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Hawa Subira Mwaifunga aliyetaka kujua kwa nini Lugha ya Kiswahili haitumiki kwenye Jukwaa la Wabunge la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF) kama inavyotumika kwenye Bunge la Afrika (PAP).

 

Mhe. Chumi ambaye alizungumza kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwenye nafasi hiyo, mwezi Julai 2024,  amesema kuwa Tanzania imeendelea  na jitihada mbalimbali za kukuza Lugha ya Kiswahili na kufanikisha Lugha hiyo kuridhiwa  na SADC kama lugha ya kazi katika Mikutano ya Wakuu wa Nchi na Serikali na Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo tangu mwaka 2019, huku ikiendelea na jitihada za kukiwezesha Kiswahili kutumika katika Mikutano ya ngazi ya Makatibu Wakuu na Taasisi nyingine za SADC ikiwemo Jukwaa la Wabunge la SADC.

 

Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Mwaifunga, kuhusu changamoto kwa Serikali katika kugharamia wakalimani ili kukitangaza Kiswahili, Mhe. Chumi amesema kwamba Serikali kupitia ushawishi wake, imefanikiwa kujenga hoja ya kushirikiana na SADC katika kugharamia wakalimali na hoja hiyo kukubalika ambapo sasa SADC inagharamia wakalimani  katika mikutano yote inayoendelea chini ya Jumuiaya hiyo.

 

“Kuhusu wakalimani, ni kweli kuna gharama kubwa za kugharamia suala zima la ukalimani. Hata hivyo, kwa ushawishi Serikali imefanikiwa kujenga hoja ili kusudi mzigo huo uweze kubebwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na SADC na kwa sasa SADC katika mikutano inayoendelea wamekubali kugharamia wakalimani,” alisema Mhe. Chumi.

 

Kadhalika ameongeza kusema, ili lugha iwe rasmi yapo mabadiliko ya kanuni na miongozo yanayotakiwa kufanyiwa kazi ndani ya SADC na kwamba Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kipengele hicho kinafanyiwa marekebisho ili kuifanya Lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne katika Jumuiya ya SADC.

 

Aidha, akijibu swali la nyongeza la Mhe. Anatropia Lwehikila kuhusu mikakati ya Serikali katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa wakalimani kutoka Tanzania, Mhe. Chumi amesema kuwa, ukalimani ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine na kutoa wito kwa wadau mbalimbali vikiwemo Vyuo chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwekeza katika kuhakikisha mafunzo ya ukalimani yanatolewa kama taaluma ili kuwawezesha wakalimani kutoka Tanzania kukidhi vigezo vinavyotakiwa na kutumiwa katika mikutano mbalimbali duniani.

 

‘Ukalimani ni taaluma, kujua Kiswahili na Kiingereza kama lugha haitoshi kukufanya kuwa mkalimani.  Hivyo, natoa wito kwa Vyuo vyetu nchini chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha wanatoa mafunzo ya ukalimani kama taaluma ili na sisi tunapokwenda katika mikutano mbalimbali duniani tukutane na wakalimani ambao ni watanzania’ alisisitiza Mhe. Chumi.

 

Kadhalika amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta ikiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya  Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Kiswahili Tanzania  (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) na Balozi za Tanzania imeendelea na jitihada za kutangaza Kiswahili kama bidhaa kupitia majukwaa mbalimbali ya kimataifa ikiwemo makongamano, mikutano pamoja na kuwa na madawati ya kiswahili kwenye Balozi za Tanzania na kuzishawishi Balozi zinazowakilisha nchi zao hapa Tanzania kuwa na madawati ya namna hiyo.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) akizungumza wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu Bungeni jijini Dodoma leo tarehe 1 Novemba 2024.
Mhe, Chumi akijibu swali Bungeni



 

Wagonjwa wa Moyo kutoka Malawi Kutibiwa JKCI

Serikali ya Jamhuri ya Malawi imeahidi kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili wagonjwa wa moyo waliopo nchini humo hasa watoto kwenda kutibiwa katika taasisi hiyo.

Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya wa nchi hiyo Mhe. Khumbize Kandodo Chiponda alipotembelea taasisi hiyo kwaajili ya kuona huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinazotolewa.

Mhe. waziri Chiponda ambaye pia kitaaluma ni mfamasia alisema ameridhika na huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa kwani ameona vifaa vya kisasa vya matibabu ya moyo, amekutana na wataalamu wabobezi ambao wanatibu moyo na kuipongeza JKCI kwa kuokoa maisha ya wagonjwa wenye matatizo ya moyo.

 “Nimefurahi sana kufika hapa nimeona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali yenu pamoja na huduma inayotolewa ni jambo la kufurahi na kushangaa kuona huduma hii inapatikana Afrika tena katika nchi jirani ya Tanzania, tukirudi nyumbani tutaona namna ya kuwa na makubaliano na taasisi hii ili wagonjwa wetu waje kutibiwa hapa hasa watoto”.

“Ninawashukuru wataalamu wa taasisi hii kwani mmekuwa mkiwahudumia wagonjwa kutoka nchini Malawi ninawaomba mzidi kuwahudumia kwani tunahitaji msaada wenu tunafurahi kuona baada ya kupata matibabu wagonjwa wanarudi nyumbani wakiwa na furaha. Pia ninawaomba mje nchini kwetu japo kwa wiki mbili kufanya kambi za matibabu ili kuwasaidia watu wenye matatizo ya moyo”, alisema waziri Chiponda.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge, Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo Dkt. Angela Muhozya alimshukuru waziri huyo kwa kutembelea JKCI na kusema kuwa watahakikisha wanatoa huduma ya matibabu ya moyo kwa wananchi wa Malawi wenye matatizo hayo.

Dkt. Angela alisema mwaka jana wataalamu wa taasisi hiyo walikwenda nchini Malawi katika hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo katika nchi hiyo kufanya kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo ambapo waliona watu 724 kati ya hao waliokuwa na matatizo ya moyo walikuwa 537.  

“Taasisi yetu imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika hasa zile tunazopakana nazo mipaka ikiwemo ya Malawi hadi sasa tumeona wagonjwa 33 kutoka nchini hiyo ambapo watu wazima walikuwa 22 na watoto 11”.

“Licha ya kutoa huduma ya matibabu ya moyo taasisi yetu pia inatoa mafunzo mbalimbali kwa wataalamu wa afya, ninawaomba muwatume madaktari na wauguzi na wataalamu wa vifaa tiba vya moyo waje kujifunza jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa moyo pamoja na kutumia vifaa hivyo”, alisema Dkt.Angela.

Kwa upande wake balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Agnes Kayola alisema wamekuwa wakitumia majukwaa mbalimbali kutangaza diplomasia ya uchumi inayojumuisha mipango ya kuinufaisha nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa. 

“Wenzetu kutoka nchini Malawi wamekuja Tanzania kuhudhuria mkutano wa MERCK Foundation nasi tukaona tutumie nafasi hii kuwaleta JKCI ili waone huduma za matibabu ya moyo tunazozitoa, wamefika hapa wameziona na kuzitambua hii itasaidia kuwashawishi wamalawi kuja kutibiwa moyo nchini kwetu”, alisema Mhe. Balozi Agnes.

Mhe. Balozi Agnes alisema Tanzania imepiga hatua katika sekta ya afya kwani wananchi wanapata kwa karibu huduma za kibingwa za matibabu wao kama ubalozi wataendelea kuwashawishi wamalawi kuja kutumia huduma za matibabu ya zilizopo nchini. 



AICC NI MUHIMILI WA SEKTA YA UTALII NCHINI


Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kimeelezwa kuwa ni moja ya muhimili muhimu katika kufanikisha agenda ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza sekta ya utalii nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 31, 2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo alipokutana na uongozi wa kituo hicho chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Christine Mwakatobe.

Mhe. Londo alisema kuwa Rais Samia amelipa umuhimu mkubwa suala la utalii ndiyo maana amecheza filamu ya Tanzania: The Royal Tour, na manufaa yake yameaanza kupatikana kwa kuongezeka kwa watalii na fedha za kigeni nchini.

 "Utalii una maeneo mengi na moja kati ya hayo maeneo ni utalii wa mikutano. Hivyo, kwa  Tanzania hakuna taasisi nyingine inayotegemewa na Serikali kulitekeleza kwa ufanisi eneo hili na kulitolea  miongozo isipokuwa AICC pekee", Waziri Londo alisema.

Mhe. Londo aliongeza kuwa AICC ndiyo sura na kioo cha nchi na ni moja ya kituvu cha diplomasia ya Tanzania, hivyo,  endapo watumishi wa kituo hicho watajituma kwa kutoa huduma zenye ubora wa kimataifa, basi watakuwa wamelitangaza vyema jina la Tanzania. 

"Mnapokea wageni wengi kutoka nje ya nchi, wanaokuja kushiriki mikutano. Wageni hawa, wengi wao huwa hawapati fursa ya kwenda sehemu yoyote zaidi ya AICC kutokana na ratiba za mikutano, maana yake wakiridhika na huduma zenu, mtakuwa mmelitangaza jina la Tanzania na kinyume chake mtakuwa mnalibomoa jina la Tanzania" Mhe. Londo alitahadharisha.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Bi. Mwakatobe ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo, amesema kuwa malengo yake ni kukifanya kituo hicho kuwa taasisi namba moja nchini, Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla. Hivyo ameomba ushirikiano kutoka kwa wadau ili aweze kufanikisha lengo hilo.

Amesema licha ya changamoto mbalimbali zinazokikabili kituo hicho kama vile uchakavu wa miundombinu, kwa kushirikiana na bodi ya wakurugenzi, ameanza kuchukua hatua ya kufanya maboresho ya majengo na ununuzi wa vifaa vya kisasa kama vile vifaa vya ukalimani, vyoo na vipoza joto.

Aidha, amesema  kwa kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao, Kituo kimeanza kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili shughuli zote ziweze kufanyika kidigitali kwa lengo la kuongeza mapato na kuleta ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wateja. 

Amemalizia kwa kusema kuwa mapato ya kituo hicho yameongezeka kwa kupata faida ghafi ya bilioni 6.5 mwaka 2023/2024 ukilinganisha na faida ya bilioni 1.7 mwaka 2022/2023.

Mhe. Naibu Waziri Londo kabla ya kufanya kikao na menejimenti ya AICC alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali yanayomilikiwa na kituo hicho. Maeneo hayo ni pamoja na Kijenge site D 1 lenye nyumba za makazi na ukubwa wa ekari 21, Kijenge site E lenye nyumba za makazi na ukubwa wa ekari 48 na Soweto ambapo pia kuna makazi na ukubwa wa ekari zaidi ya 50. 

Mhe. Naibu Waziri baada ya kuona maeneo hayo ambayo yote yapo katikati ya jiji la Arusha, amesema kuwa AICC ina uwezo wa kulibadilisha jiji hilo endapo rasilimali hizo zitatumiwa ipasavyo.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo akizungumza na Menejimenti ya Kituo  cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Aliyesimama ni Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Christine Mwakatobe akiwasilisha taarifa fupi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya AICC.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo akisisitiza jambo alipozuru eneo Kijenge lenye nyumba za makazi na ukubwa wa ekari 48. Eneo hilo inamilikiwa na linapatikana katikati ya jiji la Arusha.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Bi. Christine Mwakatobe kabla ya Mhe. Naibu Waziri hajaanza ziara ya kukagua miradi ya kituo hicho jijini Arusha.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo (kulia) akiwa katika eneo lingine la makazi linalomilikiwa na AICC ambalo pia lipo Kijnege. eneo hili lina ukubwa wa ekari 21 pia linapatikana katikati ya jiji la Arusha.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo (kulia) akiwa katika moja ya maeneo ya AICC. Anayetoa maelezo kwa Mhe. Naibu Waziri ni Afisa Mwandamizi wa Kituo hicho, Bw. Assah Mwambene. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo akisaini Kitabu cha Wageni baada ya kuwasili AICC kwa ajili ya kufahamu shgughuli za kituo hicho. Anayemwangalia ni Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Christine Mwakatobe

 

Thursday, October 31, 2024

SERIKALI IPO TAYARI KUPOKEA MAPENDEKEZO YA KUFANIKISHA MPANGO WA BIMA YA AFRYA KWA WOTE, WAZIRI MKUU


Serikali imewahakikishia wananchi kuwa ina dhamira ya dhati ya kutekeleza mpango wa bima ya afya kwa wote, na kutoa wito kwa washiriki wa kongamano la mpango wa bima ya afya kwa wote na mdahalo wa kitaifa kuhusu ufadhili wa sekta ya afya kuja na mapendekezo yatakayosaidia kutimiza dhamira hiyo.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) wakati anafungua matukio hayo mawili yanayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.

Matukio hayo yanayofanyika kwa siku nne hadi Novemba 1, 2024 yamekusanya wadau wa afya kutoka ndani na nje ya nchi ili kwa pamoja kujadili mikakati na mbinu bora zitakazoiwezesha Serikali kuwa na mipango endelevu ya kuhakikisha kuwa kila mwananchi, anakuwa na bima ya afya itakayomwezesha kupata matibabu bila kuangalia kipato chake.

Waziri Mkuu ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali katika hafla hiyo ya ufunguzi, wakiwemo Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo (Mb) na viongozi wa mkoa wa Arusha, amesema kuwa Serikali imejiandaa vyema kutekeleza mpango wa bima ya afya kwa wote kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya.

Imeelezwa kuwa tokea aingie madarakani, Rais Samia Suluhu Hassan, jumla ya trillion 6.2 zimeelekezwa katika sekta ya afya. Fedha hizo zimetumika kujenga miundombinu kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa, ununuzi wa vifaa tiba na kuwapatia ujuzi na elimu watumishi wa sekta ya afya.

Umetolewa mfano kuwa wakati Rais Samia anaingia madarakani, nchi ilikuwa na upungufu wa madaktari bingwa 2989, lakini kwa kipindi cha miaka mitatu tu, kupitia Ufadhili wa Mama Samia (Samia Scholarships), madaktari bingwa 1485 wamesomeshwa na kupunguza upungufu huo kwa takribani nusu.

Mhe. Waziri Mkuu amesema uwepo wa madaktari hao, ujenzi wa hospitali za ngazi mbalimvali pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa umeiwezesha nchi kuwa na uwezo wa kufanya tiba za kibingwa kama vile upandikizaji wa figo, uboho, mimba na vifaa vya kusikia ambapo awali tiba hizo zilikuwa zinapatikana nje ya nchi.

Eneo lingine ambalo Serikali imeliimaalisha ni upatikanaji wa dawa katika ngazi zote kuanzia zahanati hadi hospitali za rufaa. Imeelezwa kuwa upatikanaji huo unatofautiana ambapo unaanzia asilimia 75 katika zahanati hadi 98 kwa hospitali za rufaa. Bohari Kuu ya Dawa imejenga vituo kila kanda na baadhi ya halimashauri ili kurahisisha usambazaji wa dawa katika maeneo husika.

Waziri Mkuu amesema kuwa uwekezaji katika sekta ya afya umepunguza vifo kwa asilimia 20 hadi 30 na matarajio ni kwamba mpango wa bima ya afya kwa wote utakapokamilika utapunguza zaidi vifo nchini.

Waziri Mkuu alihitimisha hotuba yake kwa kutoa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara ya Afrya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa wote, ili itakapoanza kusiwe na mtu atakayeachwa nyuma.   

Awali, Mhe. Naibu Waziri Londo alisema kuwa kufanyika kwa mdahalo wa kitaifa kuhusu ufadhili wa sekta ya afya ni utekelezaji wa maagizo ya Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya la Jumuiya ya Afrika Mashariki, waliyoyatoa wakati wa mkutano wao uliofanyika jijini Dar Es Salaam mwezi Mei 2024. Aidha, ameongeza kuwa mdahalo huo ni mwendelezo wa vita vilivyoasisiwa na waasisi wa taifa hili dhidi ya maadui wakubwa watatu ambao ni maradhi, umasikini na ujinga,

Matukio hayo yamehudhuriwa na wadau wa maendeleo na nchi marafiki kama vile Shirika la Afya Duniani, Mfuko wa Afya, Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA), Jamhuri ya Korea, Indonesia, Rwanda ambao wameahidi kuwa watashirikiana na Serikali ya Tanzania katika safari yake ya kufikia bima ya afya kwa kila mwananchi.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) akiwasilisha hotuba kwa washiriki wa kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.
Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akitoa neno kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) kutoa hotuba ya ufunguzi katika kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo (Mb) akitoa neno katika kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo wakiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha, Bi. Christine Mwakatobe

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha, Bi. Christine Mwakatobe (wa pili kushoto) wakiwa na watumisha wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wanaoshiriki  kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya maandalizi ya kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.

Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka akifuatilia hotuba mbalimbali wakati wa ufunguzi wa kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.

Hadhira ikifuatilia

Washiriki mbalimbali wakifuatilia kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.