Serikali
imewahakikishia wananchi kuwa ina dhamira ya dhati ya kutekeleza mpango wa bima
ya afya kwa wote, na kutoa wito kwa washiriki wa kongamano la mpango wa bima ya
afya kwa wote na mdahalo wa kitaifa kuhusu ufadhili wa sekta ya afya kuja na
mapendekezo yatakayosaidia kutimiza dhamira hiyo.
Hayo
yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim
Majaliwa Majaliwa (Mb) wakati anafungua matukio hayo mawili yanayofanyika
katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30,
2024.
Matukio
hayo yanayofanyika kwa siku nne hadi Novemba 1, 2024 yamekusanya wadau wa afya
kutoka ndani na nje ya nchi ili kwa pamoja kujadili mikakati na mbinu bora
zitakazoiwezesha Serikali kuwa na mipango endelevu ya kuhakikisha kuwa kila
mwananchi, anakuwa na bima ya afya itakayomwezesha kupata matibabu bila
kuangalia kipato chake.
Waziri
Mkuu ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali katika hafla hiyo ya ufunguzi,
wakiwemo Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika
Mashariki, Mhe. Denis Londo (Mb) na viongozi wa mkoa wa Arusha, amesema kuwa
Serikali imejiandaa vyema kutekeleza mpango wa bima ya afya kwa wote kwa
kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya.
Imeelezwa
kuwa tokea aingie madarakani, Rais Samia Suluhu Hassan, jumla ya trillion 6.2
zimeelekezwa katika sekta ya afya. Fedha hizo zimetumika kujenga miundombinu
kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa, ununuzi wa vifaa tiba na kuwapatia ujuzi na
elimu watumishi wa sekta ya afya. Umetolewa
mfano kuwa wakati Rais Samia anaingia madarakani, nchi ilikuwa na upungufu wa
madaktari bingwa 2989, lakini kwa kipindi cha miaka mitatu tu, kupitia Ufadhili
wa Mama Samia (Samia Scholarships), madaktari bingwa 1485 wamesomeshwa na
kupunguza upungufu huo kwa takribani nusu.
Mhe.
Waziri Mkuu amesema uwepo wa madaktari hao, ujenzi wa hospitali za ngazi
mbalimvali pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa umeiwezesha nchi kuwa na uwezo
wa kufanya tiba za kibingwa kama vile upandikizaji wa figo, uboho, mimba na
vifaa vya kusikia ambapo awali tiba hizo zilikuwa zinapatikana nje ya nchi. Eneo
lingine ambalo Serikali imeliimaalisha ni upatikanaji wa dawa katika ngazi zote
kuanzia zahanati hadi hospitali za rufaa. Imeelezwa kuwa upatikanaji huo
unatofautiana ambapo unaanzia asilimia 75 katika zahanati hadi 98 kwa hospitali
za rufaa. Bohari Kuu ya Dawa imejenga vituo kila kanda na baadhi ya halimashauri
ili kurahisisha usambazaji wa dawa katika maeneo husika. Waziri
Mkuu amesema kuwa uwekezaji katika sekta ya afya umepunguza vifo kwa asilimia 20
hadi 30 na matarajio ni kwamba mpango wa bima ya afya kwa wote utakapokamilika
utapunguza zaidi vifo nchini. Waziri
Mkuu alihitimisha hotuba yake kwa kutoa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na
Wizara ya Afrya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa
wote, ili itakapoanza kusiwe na mtu atakayeachwa nyuma. Awali,
Mhe. Naibu Waziri Londo alisema kuwa kufanyika kwa mdahalo wa kitaifa kuhusu
ufadhili wa sekta ya afya ni utekelezaji wa maagizo ya Baraza la Kisekta la Mawaziri
wa Afya la Jumuiya ya Afrika Mashariki, waliyoyatoa wakati wa mkutano wao
uliofanyika jijini Dar Es Salaam mwezi Mei 2024. Aidha, ameongeza kuwa mdahalo huo
ni mwendelezo wa vita vilivyoasisiwa na waasisi wa taifa hili dhidi ya maadui
wakubwa watatu ambao ni maradhi, umasikini na ujinga,
Matukio
hayo yamehudhuriwa na wadau wa maendeleo na nchi marafiki kama vile Shirika la Afya
Duniani, Mfuko wa Afya, Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA), Jamhuri ya
Korea, Indonesia, Rwanda ambao wameahidi kuwa watashirikiana na Serikali ya
Tanzania katika safari yake ya kufikia bima ya afya kwa kila mwananchi.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.