Saturday, October 5, 2024

WAZIRI KOMBO AWATAKA WATAFITI WA AFRIKA KIZANGATI UZALENDO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akichangia mada kwenye Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika (APSD) ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaondelea jijini Johannesburg, nchini Afrika Kusini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewataka Wanazuoni, Asasi za Kiraia na Taasisi zinazofanya tafiti kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Bara la Afrika kutanguliza uzalendo na maslahi ya Afrika ili matokeo ya tafiti hizo yaweze kuwa na tija kwa Afrika.

Waziri Kombo ameyaeleza hayo alipokuwa akichangia mada kwenye ufunguzi wa Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika (APSD) ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaoendelea jijini Johannesburg, nchini Afrika Kusini. Mada hiyo ilihitaji ufafanuzi kuhusu, namna Serikali za Afrika zinatumia na kuzingatia matokeo ya tafiti katika kufanya maamuzi ya masuala mbalimbali ikiwemo utatuzi wa migogoro. 

Akizungumza kuhusu mada hiyo Waziri Kombo licha ya kueleza kuhusu umuhimu wa utafiti na mchango wake kwa Serikali katika kufanya maamuzi yenye tija kwa wanchini, alisema kuwa Watafiti wengi wa Waafrika wamekuwa wakitanguliza maslahi ya wanaowafadhili na hivyo kupotosha uhalisia wa masuala husika ambapo huondoa uhalali na ushawishi wa kutumiwa na Serikali za Afrika katika kufanya maamuzi mbalimbali.

“Sote tunatambua kuwa, kufanya tafiti kunahitaji rasilimali, fedha nyingi na muda wakutosha, hivyo Serikali nyingi za Afrika zimekosa uwezo wa kutafati masuala mengi kwa wakati. Nitoe wito kwa wanazuoni na taasisi mbalimbali inapotokea fursa za kufanya tafiti lazima kutanguliza uzalendo na maslahi ya Afrika kwanza ili matokeo ya tafiti husika yawe na mchango kwa Serikali na watu wake”. Alieleza Waziri Kombo 

Waziri Kombo katika mchango wake ambao uliwavutia wengi katika mdahalo huo, aliongeza kusema kuwa yapo masuala mengi muhimu yanayohusu Waafrika ambayo tulipaswa kuyafahamu, mathalani kiwango na aina za rasilimali tulizonazo katika mataifa yetu, lakini tafiti nyingi hazijielekezi katika kutafuta majawabu ya masuala kama hayo badala yake yanajielekeza kutafiti masuala yenye maslahi kwa wafadhili wao. 

Mbali na kusisitiza suala la uzalendo Waziri Kombo aliwataka Watafiti kuzingatia ubora na weledi wa tafiti zao. Alieleza kuwa wakati mwingine watafiti wamekuwa wakitoa matokeo yenye taarifa zisizokuwa na uhalisia hasa takwimu hivyo kuadhiri utekelezaji wa mipango na mikakati inayotegemea taarifa za tafiti hizo.

Katika mdahalo huo uliohudhuriwa na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Mhe. Thabo Mbeki, Waziri Kombo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbambwe Mhe. Federick Shava walishirikiana katika kujadili na kuchangia mada hiyo wakiongozwa na Prof. Antoni van Nieuwkerk kutoka Chuo Kikuu cha Wits cha jijini Johannesburg.

Mdahalo huo wa siku tatu unalenga kujadili masuala ya Amani na Ulinzi pamoja na kutafuta namna bora ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa migogoro inayoendelea Barani Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akifuatilia jambo kwenye Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaondelea jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akifafanua jambo kwenye Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaondelea jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbambwe Mhe. Federick Shava na Prof. Antoni van Nieuwkerk (katikati) akiongoza mdahalo huo
 Mdahalo ukiendelea
 Mdahalo ukiendelea
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Bertha Makilagi akifuatilia Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaondelea jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Afisa Mambo ya Nje Mwandamizi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Emmanuel Shayo akifuatilia Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaondelea jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Mhe. Thabo Mbeki akifuatilia Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaondelea jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Rais wa zamani wa Zibwabwe Mhe. Johaquim Chissano akihutubia kwenye ufunguzi wa Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika uliofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini kwa njia ya mtandao.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.