Friday, October 11, 2024

MISHENI YA SADC YATOA TAARIFA YA AWALI KUHUSU UCHAGUZI MKUU NCHINI MSUMBIJI


Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume, leo tarehe 11 Oktoba 2024 ametangaza Taarifa ya Awali kuhusu Uchaguzi wa Rais na Wabunge kufuatia uchaguzi uliofanyika nchini humo tarehe 9 Oktoba 2024.

 

Katika hotuba yake, Mhe. Dkt. Karume amesema kuwa uchaguzi nchini Msumbiji kwa kiasi kikubwa umezingatia kanuni na miongozo ya uchaguzi wa kidemokrasia ya SADC, inayosisitiza katika haki, uhuru, usawa, na uwazi.

 

Amesema katika kutekeleza jukumu lake, misheni hiyo iliangalia masuala mbalimbali muhimu kabla na wakati wa uchaguzi, ikiwemo hali ya siasa na usalama nchini humo, usimamizi wa uchaguzi, ripoti za vyombo vya habari kuhusu uchaguzi, na uwakilishi wa jinsia, ambayo yote yametekelezwa kwa kiasi kikubwa.

 

Aidha, Misheni hiyo imeshuhudia nchi hiyo ikiwa katika hali ya amani na utulivu katika kipindi chote cha kabla na wakati wa uchaguzi, ambapo kampeni, mikutano ya hadhara  na mchakato wa upigaji kura vilifanyika kwa amani, licha ya changamoto za kiusalama katika baadhi ya maeneo, hususan katika jimbo la Cabo Delgado.

 

Pia Mhe. Dkt. Karume ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi wa Msumbiji kwa kuonyesha ukomavu wa kisiasa na uvumilivu katika kipindi chote cha uchaguzi, akiwataka washindani wa kisiasa kufuata taratibu za kisheria endapo kutatokea migogoro yoyote kuhusu uchaguzi.

 

Pia ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuwa watulivu na wavumilivu wakati mamlaka za usimamizi wa uchaguzi zikikamilisha matokeo ya uchaguzi kabla ya kutangazwa rasmi, akiwaomba kuendelea kuhamasisha amani, uvumilivu, na utulivu kupitia majukwaa mbalimbali katika kipindi cha baada ya uchaguzi.

 

Kulingana na Misingi na Miongozo ya SADC inayosimamia uchaguzi wa kidemokrasia iliyorekebishwa mwaka 2021, misheni hiyo itatoa taarifa ya mwisho kuhusu uchaguzi siku 30 baada ya kutolewa kwa taarifa ya awali.

 

Misheni ya SADC, iliyozinduliwa rasmi tarehe 3 Oktoba 2024, ilipeleka waangalizi 52 katika majimbo yote 11 ya Msumbiji ili kuangalia uchaguzi.

 

Mhe. Dkt. Karume aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi, na Usalama, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuongoza misheni hiyo.


Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume, akitangaza Taarifa ya Awali ya Misheni hiyo kuhusu Uchaguzi wa Rais na Wabunge kufuatia uchaguzi uliofanyika nchini Msumbiji tarehe 9 Oktoba 2024
Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Magosi akishiriki Mkutano wakati Mkuu wa Misheni na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Karume akitangaza kwa waandishi wa habari Taarifa ya Awali ya Uangalizi kuhusu uchaguzi Mkuu wa Msumbiji uliofanyika tarehe 09 Oktoba 2024
Wajumbe wa Troika kutoka Tanzania ambao ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa (kulia) na Mshauri wa Rais masuala ya Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Sofia Mjema (kushoto) wakifuatilia taarifa ya awali ya SADC kuhusu uangalizi wa uchaguzi nchini Msumbiji
Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mhe. Phaustine Kasike akishiriki mkutano wa uwasilishwaji wa Taarifa ya Awali ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu nchini Msumbiji
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri akishiriki mkutano wa uwasilishwaji wa Taarifa ya Awali ya Misheni ya Uangalizi ya SADC kuhusu uchaguzi mkuu nchini Msumbiji
Sehemu ya wadau mbalimbali walioshiriki mkutano
Sehemu nyingine ya wadau
Mkutano ukiendelea
Mkutano ukiendelea
Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya SADC ya  Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mtendaji wa SADC na Wakuu wa Misheni za Kimataifa za Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji mara baada ya kukamilisha mkutano wa pamoja wa kutoa taarifa zao za awali za uangalizi wa uchaguzi nchini humo. Kutoka kulia ni Mhe. Elias Magosi, Katibu Mtendaji wa SADC, Mkuu wa Misheni ya Uangalizi kutoka Umoja wa Afrika (AU-EOM) na Makamu wa Rais Mstaafu wa  Angola, Mhe. Bornito de Sousa Baltazar Diogo, ,  Mkuu wa Misheni ya Uangaliz ya Jumuiya ya Madola na Waziri Mkuu Mstaafu wa Saint Lucia, Mhe. Kenny Anthony, Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Jumuiya ya Nchi zinazozungumza Kireno na Waziri wa Mambo ya Nje mstaafu wa Ureno, Mhe. João Gomes Cravinho na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi ya Jukwaa la Uchaguzi la SADC, Jaji Dkt. Manuel Pereira da Silva 











































 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.