Friday, May 26, 2017

Wizara ya Mambo ya Nje yawazawadia watumishi walionyesha utendaji bora

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima (wa kwanza kulia), akimkabidhi zawadi Afisa Mambo ya Nje, Bi. Eva Ng'itu kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa. Bi. Ng'itu amekuwa Mfakazi Hodari wa wa Wizara ya Mambo ya Nje kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
Dkt. Mlima aliwapongeza na kuwasihi wafanyakazi waliofanya vizuri kuwa zawadi walizokabidhiwa iwe chachu ya kuongeza juhudi na ufanisi katika utumishi wao.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy akimpongeza  Bi. Ng'itu kwa kuwa mfanyakazi Hodari wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Bw. Mohammed Kheri kutoka Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar akipokea zawadi yake kwa kuwa mfanyakazi bora wa Idara hiyo.
 Bw.Joseph Mlingi akipokea zawadi kwa kuwa mfanyakazi bora kwa upande wa madereva wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Bw. Emannuel Luangisa akipokea zawadi yake ya kuwa mfanyakazi bora wa Idara ya Asia na Australasia.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora na Mratibu wa Mafunzo wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago naye akipokea zawadi ya ufanyakazi bora wa Idara ya Diaspora
Bi Eva Kaluwa kutoka Idara ya Sera na Mipango akipokea zawadi yake kutoka kwa Dkt. Mlima.
Bi. Kisa Mwaseba akipokea zawadi ya Mfanyakazi bora wa Idara ya Mashariki ya Kati.
Bi. Upendo Mwasha akipokea zawadi ya mfanyakazi bora wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda.
Bi. Nelusigwe kutoka Kitengo cha Ununuzi na Ugavi akipokea zawadi baada ya kuibuka mfanyajkazi bora wa Kitengo hicho.
Bw. Erick Ngilangwa kutoka Idara ya Afrika akipokea zawadi ya mfanyakazi bora wa Idara hiyo
Afisa Habari wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Rose Mbilinyi akipokea zawadi yake kutoka kwa Dkt. Mlima.
Katibu Mkuu Dkt. Mlima akizungumza katika kikao cha  baraza la wafanyakazi la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Mambo ya Nje, Zanzibar akichangia jambo katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi.
Sehemu ya wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakimsikiliza kwa makini Katibu mkuu alipo kuwa akizungumza nao
Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu, Dkt. Mlima na wafanyakazi bora kutoka kwenye Idara na Vitengo vya Wizara. Mwanamke pekee aliyeketi ni Bi. Eva Ng'itu ambaye ameibuka mfanyakazi hodari wa Wizara nzima kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Thursday, May 25, 2017

Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Mfalme Letsie wa III wa Lesotho


 Mkuu wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akisalimiana na Mfalme Letsie wa III wa Falme ya Lesotho, alipo kutana nae na kufanya mazungumzo.  


Waziri Mahiga akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazungumzo yake na Mfalme Letsie wa III, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Balozi Innocent Shiyo.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Mfalme Letsie wa III kuelekea Uchaguzi wa Mkuu wa Lesotho



Mkuu wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amemhakikishia Mfalme Letsie wa III wa Lesotho kuwa Asasi ya Ushirikiano ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama imethibitisha pasipo mashaka utayari wa wapiga kura wa nchi hiyo kupiga kura siku ya Jumamosi tarehe 3 Juni 2017.



Hayo yamesemwa kwenye mazungumzo ya viongozi hao ambapo Mhe. Dkt. Mahiga alimuelezea Mtukufu Mfalme Letsie wa III, hatua mbalimbali za uangalizi wa uchaguzi zilizochukuliwa na Jumuiya ya SADC tangu alipofika nchini Lesotho. Jumuiya hiyo mbali na kupeleka waangalizi 41 wa uchaguzi kutoka kwenye nchi tisa wanachama, pia ina wajumbe wawili wa Baraza la Ushauri wa Masuala ya Uchaguzi ambapo mmoja wa wajumbe hao ni Jaji Mstaafu John Tendwa wa Tanzania.



Mhe. Mahiga pia alisifu jitihada za Serikali na Tume Huru ya Uchaguzi ya Lesotho ambao kwa pamoja wamehakikisha kuwa mazingira mazuri yameandaliwa yatakayoruhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu kufanyika kama ilivyopangwa.



Kwenye mazungumzo yao, Mhe. Mahiga alitumia pia nafasi hiyo kumpelekea Mfalme Letsie salaam za heshima kutoka kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama ambayo inaundwa na nchi za Tanzania, Msumbiji na Angola kwa sasa.



Kwa upande wake, Mtukufu Mfalme Letsie wa III wa Falme ya Lesotho alimshukuru Mhe. Rais Magufuli  kama kiongozi wa asasi hiyo muhimu ya Jumuiya ya SADC na kuongeza kuwa ni matarajio yake kuwa chini ya uongozi wake makini na mahiri, nchi wanachama wa Jumuiya watatekeleza kwa ufanisi majukumu yao muhimu ya kuendeleza jumuiya.



Mfalme huyo mrithi wa baba yake Mfalme Moshoeshoe wa II anayetawala Lesotho tangu mwaka 1996 kama Falme ya Kikatiba, alisema anaiheshimu sana Tanzania kwa mchango mkubwa kwa nchi hiyo hususan kwenye kuendeleza taaluma mbalimbali nchini humo. Alisema kwa miaka mingi sasa wataalamu wa masuala ya afya na elimu kutoka Tanzania wameendelea kufanya kazi Lesotho na kuongeza kuwa hata yeye binafsi alifundishwa Chuo Kikuu cha Lesotho na Mtanzania masomo ya Sheria na Sayansi ya Siasa.

Mtukufu Mfalme Letsie alimaliza kwa kuahidi kuendeleza ushirikiano wa karibu uliopo baina ya Lesotho na Tanzania ambapo chimbuko lake ni kuwa nchi zote mbili ni wanachama waanzilishi wa Jumuiya ya SADC. Aidha alionesha nia kubwa ya kuzuru Tanzania siku za usoni, na kumuomba Mhe. Dkt. Mahiga, kufikisha salamu za heshima na ushirikiano kwa Rais na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 



 -Mwisho-



Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Maseru, Lesotho 25 Mei, 2017


Wednesday, May 24, 2017

Waziri Mahiga Aongoza Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa SADC nchini Lesotho

Dr. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrioka Mashariki na Mkuu wa Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa SADC akizungumza na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Lesotho, Mhe. Jaji Mstaafu Lesao Lehohla   (wa pili kutoka kulia) alipotembelea tume hiyo mjini Maseru Lesotho kabla ya kuzindua rasmi Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya SADC.
Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Mkuu wa Umoja wa Makanisa wa Lesotho Archbishopp Gerald Tlali Lerotholi na ujumbe wake alipotembelea ujumbe huo kusikiliza maoni yao kuhusu uchaguzi mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika tarehe 3 Juni 2017.
Dkt. Mahiga na ujumbe wake wakikamilisha majumuisho ya mikutano mbalimbali waliyoifanyana na wadau .
5: Dkt Mahiga akiagana na wenyeji wake nje ya Tume Huru ya Uchaguzi.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri Mahiga Aongoza Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa SADC nchini Lesotho



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, amezihimiza taasisi za Serikali na za dini nchini Lesotho kudumisha amani na usalama kwenye kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi mkuu nchini hapa ili kuwezesha Serikali itakayoingia madarakani kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa ajili ya wananchi wa Lesotho.



Uchaguzi huo mkuu wa wabunge ambao ni wa tatu kufanyika ndani ya kipindi cha miaka mitano, unatarajiwa kufanyika tarehe 3 Juni 2017 ambapo vyama 26 kati ya 30 vilivyojiandikisha, vitashiriki kwenye kinyang’anyiro hicho cha kuchagua wawakilishi Bungeni.



Kwa mujibu wa Katiba ya Falme ya Lesotho, kiongozi wa chama kitakachoshinda viti vingi zaidi vya ubunge kwenye uchaguzi huo ndiye  atakayeapishwa kuwa Waziri Mkuu na Kiongozi wa Serikali, ambapo mkuu wa nchi na mtawala mkuu anaendelea kuwa Mfalme Letsie III.



“Wakati umefika sasa kwa Jumuiya yetu ya SADC kushiriki kwenye uangalizi wa uchaguzi huu tukiwa na habari njema ya kurejesha matumaini kwa wananchi kuhusu mustakabali wa uongozi. Lakini pia tuwe na ujumbe mzito kwa Serikali ijayo ili iweze kufanya mageuzi ya kweli kwenye nyanja mbalimbali kwa manufaa ya wananchi” Mhe. Mahiga amehimiza kwa wajumbe wa timu ya waangalizi wa uchaguzi.



Tangu alipowasili nchini hapa tarehe 22 Mei 2017, Dkt. Mahiga na ujumbe wake wamekutana na wadau mbalimbali wakiwemo Tume Huru ya Uchaguzi ya Lesotho na Umoja ya Makanisa wa Lesotho kwa lengo la kupata maoni ya kina kabla ya kuzindua Timu ya Uangalizi ya SADC (SADC Elections Observersion Mission - SEOM) tarehe 25 Mei 2017.



Mhe. Dkt. Mahiga anaongoza timu hii ya waangalizi wa uchaguzi ya SADC kwasababu kwa sasa Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC Organ).



Akiongoza mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Lesotho Mhe. Mampono Khaketla, Mhe. Mahiga alipongeza jitihada za Serikali kuhakikisha kuwa usalama wa raia  na amani vinatawala nchini humo wakati wa uchaguzi. Hata hivyo aliongeza kuwa yeye na ujumbe mzima wa asasi hiyo muhimu ya maamuzi ya SADC ipo Lesotho kwa mara ya tatu, kama waangalizi wa uchaguzi ambapo mara ya kwanza na ya pili ilikuwa uchaguzi wa mwaka 2012 na 2015.



Alisema ni matarajio yake na ujumbe mzima kuwa uchaguzi wa mwaka huu utazaa matunda yatakayoleta matumaini kwa wananchi ya kuwa na Serikali imara itakoyoongoza na kusimamia mageuzi ya kweli. “Haya ni matumaini ya wananchi wa nchi hii, na mimi kama  kiongozi wa SEOM nimekuja kuwahakikishia ndugu zangu, tutasimama pamoja nanyi, tutawasindikiza kwenye uchaguzi huu, kama misingi ya Jumuiya yetu inavyoelekeza lakini pia wananchi wanatarajia hayo”



Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya SADC imewasili nchini Lesotho tarehe 18 Mei, 2017 na inaundwa na nchi tisa ambazo ni wananchama wa Jumuiya hiyo. Wajumbe wapatao 41 watasambaa kwenye majimbo yote ya uchaguzi kama waangalizi na kutoa taarifa ya kina siku chache baada ya uchaguzi huo, kuhusu mwelekeo na mwenendo wa uchaguzi huo.



 -Mwisho-



Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Maseru, Lesotho 23 Mei, 2017

Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar yazinduliwa rasmi.



 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar yazinduliwa rasmi.

Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar zilizinduliwa rams tarehe 19 Mei 2017. Shughuli za ufunguzi ziliongozwa na Mhe. Fatma Mohammed Rajab, Balozi wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Qatar ambaye alisaini kitabu cha wageni kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Ubalozi.
Wawakilishi wa makundi mbalimbali ya Watanzaia wanaoishi nchi Qatar walishiriki katika hafla hiyo.

Mhe. Balozi alitumia fursa hiyo kuzungumza machache na Watanzania walioshiriki. Aliwaeleza kwamba kufunguliwa kwa Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar ni sehemu ya kutekeleza malengo ya Serikali ya Tanzania ya kusogeza huduma zake kwenda kuwekeza Tanzania hususan katika sekta ya viwanda. Aliwahakikishia kwamba Ubalozi utawapatia ushirikiano watakaouhitaji katika kufanikisha azma hiyo.

Balozi aliwapongeza Watanzania hao kwa kuendelea kuwa na sifa nzuri nchini Qatar na kudumisha mshikamano miongoni mwao. Aliwahimiza waendelee kuwa raia wema na kulinda haiba na jina la Tanzania kwa kufuata sheria za nchi wanapoishi. Alisema milango ya Ubalozi itakuwa wazi kupokea ushauri wao katika mambo ambayo yatalenga kuleta tija na mafanikio kwa taifa.

Naye Bw. Said Ahmed, Mwenyekiti wa Watanzania wanaoishi Qatar aliishukuru Serikali kwa kusikia kilio chao na hatimaye kufungua Ubalozi na kuwa na Balozi Mkazi nchini Qatar. Alimueleza Balozi kwamba jamii ya Watanzania wanaoishi Qatar itashirikiana na Ofisi za Ubalozi na kufanya kazi bega kwa bega katika kuitafutia maslahi Tanzania. Wawakilishi hao waliomba Ubalozi uandae mkutano mkubwa utakaowawezesha Watanzania wengi zaidi kushiriki ili kusikia maoni yao na changamoto zinazowakabili. Balozi aliahidi kufanya mkutano huo mapema iwezekanavyo.


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Doha, Qatar 24 Mei, 2017 
Mhe. Fatma Mohammed Rajab, Balozi wa Tanzania nchini Qatar akiongea na Watanzania waliohudhuria sherehe za uzinduzi wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar
Mhe. Balozi Fatma Mohammed Rajab akiwa katika picha ya pamoja na Watanzania waliohudhuria sherehe za uzinduzi wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar