Thursday, November 25, 2021

SERIKALI YAZIHAKIKISHIA KAMPUNI ZA USWISI MAZINGIRA SALAMA YA BIASHARA, UWEKEZAJI

 Na Waandishi wetu, Dar

Serikali ya Tanzania imezihakikishia kampuni za Uswisi mazingira salama ya biashara na uwekezaji nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi Mulamula amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita imetilia mkazo katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kupitia sheria na kuondoa baadhi ya kodi zilizokuwa ni kikwazo kwa wawekezaji.

“Serikali imepitia sheria zetu na kuweza kuondoa kodi zilizokuwa kero............na kupitia pia sheria ya uwekezaji kwa lengo la kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini,” amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi pamoja na ujumbe wake wameoneshwa kuridhishwa na juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na kuahidi kuendelea kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uswisi kuja kuwekeza Tanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi amesema pamoja na mambo mengine, wamejadiliana mazingira ya biashara na uwekezaji na vitu ambavyo kampuni za Uswisi zinahitaji ili kuwekeza zaidi Tanzania.

“Tumeridhishwa na juhudi za Serikali ya Tanzania za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na tumemhakikishia Waziri Mulamula kuwa tutaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara kutoka Uswisi kuja kuwekeza Tanzania,” amesema Bi. Daanzi

Bi. Daanzi ameongeza kuwa mbali na kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji pia kuna maeneo ya ushirikiano ambayo Serikali ya Uswisi itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha maisha ya watanzania.

Katika tukio jingine, Balozi Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China Nchini Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao pamoja na mambo mengine, wamejadili kuhusu Mkutano wa nane (8) wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 - 30 Jijini Dakar nchini Senegal.

Katika Mkutano huo Rais wa China Mhe.  Xi Jinpign anatarajiwa kuhutubia kwa njia ya Mtandao ambapo Tanzania itawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.

Mkutano huo utawajumuisha viongozi na wawakilishi kutoka Bara la Afrika na China ambapo utatoa fursa ya viongozi hao kujadili na kuangalia jinsi ambavyo China ilivyotekeleza hatua za ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitatu 2018 - 2021 kwenye  maeneo ya ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda barani Afrika, ujenzi wa miundombinu ya nishati, usafirishaji, habari na mawasiliano, kukuza wigo wa biashara kati ya China na mataifa ya Afrika.

Maeneo mengine ni kampeni ya mapinduzi ya kijani, mpango maalum wa mafunzo ya ufundi, kuboresha sekta ya Afya, ulinzi na usalama na ushirikiano katika masuala ya habari, utamaduni sanaa na michezo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi zaadi ya picha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi, Balozi wa Uswisi Nchini Mhe. Didier Chassot, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Swahiba Mndeme. Wengine ni ujumbe ulioambatana na Bi. Daanzi. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akimkaribisha Balozi wa China Nchini Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Balozi wa China Nchini Mhe. Chen Mingjian akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Wednesday, November 24, 2021

MAWIZIRI WA EAC KUKUTANA ARUSHA

Na. Mwandishi Maalum, Arusha

Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaendelea jijini Arusha katika ngazi ya maafisa waandamizi. Mkutano huo ulioanza  tarehe 22 Novemba 2021 utahitimishwa na Kikao cha Mawaziri wa Nchi za Jumuiya kitakachofanyika tarehe 29 Novemba 2021.

Tanzania ambayo ni mwanachama muasisi wa Jumuiya hiyo inashiriki kikamilifu katika mkutano huo ambapo Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen P. Mbundi anaongoza ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya maafisa waandamizi.

Maafisa waandamizi wanaandaa taarifa mbalimbali za utekelezaji wa shughuli za Mtangamano wa Afrika Mashariki ambazo zitawasilishwa kwenye ngazi ya Makatibu Wakuu na hatimaye ngazi ya Mawaziri kwa ajili ya kutolea maamuzi na maelekezo.

Waheshimiwa Mawaziri pia watapokea na kupitia taarifa za utekelezaji wa vyombo na Taasisi za EAC, zikiwemo Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kamisheni ya Kiswahili ambayo Makao Makuu yake yapo Zanzibar na Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Katika jitihada za Tanzania za kukuza lugha ya Kiswahili duniani, Waheshimiwa Mawaziri watapokea taarifa ya maendeleo ya mchakato wa kubadilisha sheria na taratibu za EAC ili kuwezesha kuanza rasmi matumizi ya  lugha ya Kiswahili pamoja na Kifaransa kama ilivyoelekezwa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki mwezi Februari 2021. Aidha, Waheshimiwa Mawaziri watapokea taarifa kuhusu mchakato wa uhakiki wa maombi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa mwanachama mpya wa EAC.

Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania katika kikao cha ngazi ya maafisa waandamizi, Balozi Stephen P. Mbundi akifuatilia kwa makini majadiliano ya mkutano wa EAC.  
Mwenyekiti wa kikao kutoka Kenya akiendesha kikao cha maafisa waandamizi.

Baadhi ya ujumbe wa Tanzania ambao ni Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika kikao cha ngazi ya maafisa waandamizi, Balozi Stephen P. Mbundi,  Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombimu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Bw. Eliabi Chodota (mwenye peni) na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, Bw. Benjamini Mwesiga (aliyesimama) wakijadili jambo wakati wa kikao cha maafisa waandamizi cha EAC.  

Ujumbe a Tanzania ukifuatilia majadiliano kuhusu agenda mbalimbali za kikao cha maafisa waandamizi wa EAC.

Wajumbe mbalimbali wakifuatilia majadiliano ya kikao cha EAC

Ujumbe kutoka Uganda ukifuatilia kikao cha EAC

 

BALOZI MULAMULA : WEKENI UTARATIBU WA KUSHUGHULIKIA DIASPORA

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (kushoto) akizungumza wakati wa kikao kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) na Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi, katikati ni Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk. Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia)  akizungumza wakati wa kikao na  Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi kilichofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao.


Kiongozi wa mabalozi wa Tanzania nje ya nchi ambaye pia ni Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi Mhe. Irene Kasianju (katikati) akizungumza katika kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao, kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab na kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Naimi Aziz.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Diaspora Bi Tagie Mwakawago (kushoto) akizungumza juu ya mfumo wa kielektroniki wa kuwasajili Diaspora katika kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi kilichofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao.
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara walioshiriki katika kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi kilichofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao wakifuatilia kikao hicho.



 


 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amewataka Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania Nje ya Nchi kuweka utaratibu wa kushughulikia masuala ya Diaspora katika meneo yao ya uwakilishi.

Balozi Mulamula ametoa agizo hilo Jijini Dar es Salaam alipozungumza na mabalozi hao kwa njia ya mtandao kwa lengo la kuwakumbusha na kuwapa tarifa juu ya utendaji kazi wa Wizara na mambo mengine yanayojiri nchini.

 ‘‘Anzisheni utaratibu wa kushughulikia masuala ya Diapora katika maeneo yenu ya uwakilishi, ikiwemo kuratibu mikutano ya mara kwa mara hata kama ni kwa njia ya mtandao’’ amesema Balozi Mulamula.

Waziri Mulamula pia amewataka mabalozi  kuratibu mikutano ya mara kwa mara na diaspora hata kama ni kwa njia ya mtandao ikiwa ni harakati za kuwaweka pamoja na kuwajumuisha katika mipango na harakati za kuiletea nchi maendeleo kupitia Watanzania hao wanaoishi nje ya nchi.

Amewaelekeza mabalozi pia kuhakikisha kuwa wanawatambua Diaspora wa Tanzania duniani kote na kuwawekea mazingira mazuri ya kuwawezesha kuchangia katika maendeleo na uchumi wa taifa.

 

Waziri Mulamula ameongeza kuwa, Wizara inatambua umuhimu wa Diaspora na kuthamini mchango wao katika maendeleo ya Taifa ndiyo maana  imeamua kuingiza masuala ya Diapora katika  Sera mpya ya Mambo ya Nje.

“Wizara tumehakikisha kuwa masuala ya Diapora yanakuwa sehemu ya Sera ya Mambo ya Nje hii ni kutokana na mchango wa Diapora kwa maendeleo ya Taifa,” amesema Waziri Mulamula.

 

Balozi mulamula ameongeza kuwa Serikali inalifanyia kazi ombi la Diaspora la kupatiwa hadhi maalum na kuutaka uongozi wa Wizara kuongeza jitihada za kuleta mfumo wa kielektroniki wa kuwasajili Diaspora wote duniani ili kuweza kupata tarifa muhimu na takwimu sahihi.

 

Katika kikao hicho Waziri Mulamula aliwaelezea mabalozi hao juu ya maandalizi ya Serikali katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, utengenezaji wa Sera mpya ya Mambo ya Nje, uanzishwaji wa Idara mpya ya Diplomacia ya uchumi ambayo itakuwa kiungo katika ya wizara, Balozi za Tanzania Nje na Idara na Balozi zetu taasisi nyingine za Umma na Sekta binafsi ili kufanikisha azma ya Serikali katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi na hivyo kujiletea maendeleo.

 

Aidha, amesema kuwa Serikali imekamilisha ufunguzi wa Konseli Kuu katika Mji wa Lubumbashi - Jamhuri ya Kimemokrasia ya Congo (DRC) na Guangzhou - Jamhuri ya Watu wa China pamoja na kuonesha nia ya kufungua Konseli Kuu katika Mji wa Shanghai na katika Jamhuri ya watu wa China.