Thursday, June 9, 2022

MKUTANO WA 42 WA KAWAIDA WA BARAZA LA MAWAZIRI WAENDELEA KUFANYIKA JIJINI ARUSHA


Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama Balozi Stephen P. Mbundi, wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akichangia hoja kwenye Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaoendelea kufanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya, jijini Arusha

Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha kwa ngazi ya Maafisa Waandamizi. 

Mkutano huo ambao unafanyika kwa njia ya mseto (Video na ana kwa ana) pamoja na masuala mengine unatarajiwa kupitia ripoti mbalimbali kama vile; ripoti ya utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa na Mkutano wa 41 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya, ripoti ya ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ambayo itajumuisha taarifa za Ukaguzi wa Fedha, ripoti ya Mipango na Miundombinu na ripoti ya Sekta za Uzalishaji na Huduma za Jamii. 

Mkutano huo utakaofanyika kwa kipindi cha siku nne, umeanza katika ngazi ya Maafisa Waandamizi tarehe 8 na 9 Juni 2022, utafuatiwa na Makatibu Wakuu tarehe 10 Juni 2022 na hatimaye tarehe 11 Juni 2022 kuhitimishwa na Mawaziri.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo kwa ngazi ya Maafisa Waandamizi unaongozwa na Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama Balozi Stephen P. Mbundi, wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

Kila mwaka, Baraza la Mawaziri la Jumuiya hukutana mara mbili ambapo mkutano mmoja kati ya hiyo hufanyika kabla ya mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya. Miongoni mwa malengo ya Mikutano ya Baraza la Mawazi ni kuhusianisha maamuzi yanayofikiwa kwenye Mikutano ya Wakuu wa Nchi wa Jumuiya na majukumu ya utendaji wa kila siku ya Jumuiya. 
Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote akifungua Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaoendelea kufanyika jijini Arusha
Mkutano ukiendelea
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaoendelea jijini Arusha
Mkutano ukiendelea

Wednesday, June 8, 2022

BALOZI SOKOINE AMWAKILISHA BALOZI MULAMULA KATIKA MKUTANO WA 114 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA OACPS


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akiongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya OACPS unaofanyika jijini Brussels, Ubelgiji akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Rais wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) Mhe. Sylvie Baïpo Temon (katikati) akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo jijini Brussels nchini Ubelgiji. 


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akiwa katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya OACPS unaofanyika  jijini Brussels, Ubelgiji akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mulamula.Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga na kulia ni Bi Agness Kiama akimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.


Baadhi ya washiriki  kutoka nchi wanachama Jumuiya ya OACPS wakifuatilia ufunguzi wa mkutano Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa jumuiya hio unaofanyika jijini Brussels nchini Belgium

Baadhi ya washiriki  kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya OACPS wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika jijini Brussels nchini Belgium


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS) unaofanyika jijini Brussels, Ubelgiji.

Mkutano huo wa siku mbili unajadili masuala mbalimbali ukiwemo mustakakabali wa maendeleo ya Jumuiya hiyo na namna nchi wanachama zinavyoweza kuendelea kukuza ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo na Umoja wa Ulaya, ambaye ni mbia wa maendeleo wa muda mrefu.

Mkutano huo pia unajadili maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba, 2022 nchini Angola.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Sokoine amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya OACPS katika kuhakikisha vipaumbele vya nchi vinatekelezwa hususan katika sekta za kilimo, viwanda na biashara, uvuvi na madini ili nchi iweze kunufaika.

Mkutano huo unakutanisha nchi wanachama 79 wa Jumuiya hiyo ambao kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili wajumbe wake wanakutana ana kwa ana tangu dunia ilipokumbwa na janga la  UVIKO 19, wajumbe wengine  walioshindwa kuhudhuria wanashiriki kwa njia ya mtandao.

Baraza la Mawaziri la nchi wanachama wa OACPS ni chombo cha maamuzi cha Jumuiya hiyo ambacho kinahusika na utekelezaji wa maazimio yanayopitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.

Baraza hilo linaundwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka kwa Nchi wanachama na hukutana mara mbili kwa mwaka kujadili utekelezaji wa maazimio  yaliyofikiwa kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo.