Thursday, December 19, 2024

TANZANIA, SOMALIA ZA ZASAINI HATI NNE ZA MKUBALIANO YA USHIRIKIANO


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Ulinzi wa Somali Mhe. Abdiqadir Mohamed Nur wakionesha hati ya makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya Ulinzi mara baada kusainiwa jijini Mogadishu, Somalia. Waziri Kombo amesaini hati hiyo kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi wa Tanzania Mhe. Dkt. Stergomena Tax.


· Waziri Kombo apongeza mageuzi ya uchumi na utulivu wa kisiasa unaoendelea nchini humo

· Wautaja umoja amani na usalama wa Tanzania kuwa ni mfano wa kuigwa Afrika 

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Shirikisho la Somalia zimesaini hati nne za makubaliano ya ushirikiano katika mkutano uliofanyika jijini Mogadishu leo tarehe 19 Disemba 2024 chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Balozi Ahmed Moalim Fiqi. 

Hati hizo nne zilizosainiwa zimehusisha Ushirikiano wa jumla, sekta ya Utalii, Ulinzi na Afya. Hatua hiyoinalenga kukuza ushirikiano wa kidiplomasia na uchumi sambamba na kuboresha utoaji huduma kwenye sekta hizo kwa manufaa ya raia wa mataifa yote mawili. 

Waziri Kombo akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini wa hati hizo Waziri Kombo ameeleza Tanzania imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za afya ambapo kupitia makubaliano hayo Somalia watapata fursa ya kunufaika na huduma mbalimbali zinazopatikana nchini kwenye sekta hiyo ikiwemo matibabu, kununua madawa na vifaa tiba na mafunzo. 

Aliendelea kueleza kuwa Serikali za pande zote mbili zinatambua kuwa ili wananchi waweze kunufaika na fursa hizo ni muhimu kuhakikisha huduma za mawasiliano na usafiri kati ya Tanzania na Somalia zinaimarishwa. Hivyo amehimiza kuharakishwa kwa mazungumzo yanayoendelea ili huduma ya usafiri wa moja kwa moja kwa njia ya anga kati ya Dar es Salaam na Mogadishu ianze kupatikana mapema iwezekanavyo. 

Aidha Waziri Kombo ameelekeza watendaji kuandaa utaratibu maalumu wa kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa mikataba mamkubaliano yaliyofikiwa huku akihimiza kuwa nataka kuona ikitekelezwa kwa vitendo. 

Ushirikiano huu utasaidia mataifa yetu kufikia malengo yake ya kiuchumi sambamba na kukidhi matarajio ya Wakuu wa Nchi zetu ambao dhamira yao nikuona ustawi wa uchumi wa wananchi kupitia fursa zainazotokana ushirikiano huu. Hivyo ni muhimu kwetu sote kuhakikisha makubaliano haya yanatekelezwa kwa vitendo. Alieleza Waziri Kombo. 

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Balozi Ahmed Moalim Fiqi licha ya Somalia kushirikiana na Tanzania kupitia majukwaa mbalimbali na Mtangamano wa Afrika Mashariki wanaona ni muhimu zaidi kuimarisha uhusiano wa uwili ili kujenga ukaribu zaidi na uwanja mpana wa ushirikiano.

Ameeleza kuwa, kufanya hivyo kunatoa fursa ya kushirikiana zaidi katika kutatua changamo mbalimbali zinatukabili katika ukanda ikiwemo suala la amani na usalama ambalo limekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Naye Naibu Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jumhuri ya Somalia Mhe. Saalax Axmed Jaamac akifunga hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo ameeleza kuwa ushirikiano huo umewadia wakati sahihi ambapo Taifa hilo linaendelea kufanya mageuzi ya kisiasa, hivyo wanayo mengi ya kujifunza na kuiga kutoka Tanzania ambayo kwa muda mrefu imekuwa na amani na umoja licha ya kuwa na tofauti nyingi za kijamii ikiwemo mila, dini na itikadi tofauti za kisiasa. 

Tukio hilo la kihistoria lililofanyika kwa mara ya kwanza katika kipindi miaka 40 ambalo lina ashiria zama mpya za uhusiano wa kidiplomasia na uchumi baina ya pande kutoka Tanzania viongozi mbalimbali ikiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Pindi Chana, Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel na watendaji wa ngazi mbalimbali Serikalini wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo. 

Makubaliano hayo yamefikiwa kufuatia mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan a Rais wa Shikisho la Jamhuri ya Somali Mhe. Dkt. Hassan Sheik Mohamud yaliyofanyika pembezoni mwa mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha tarehe 30 Novemba 2024. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akizungumza kwenye ufunguzi wa hafla ya kusaini hati za makubaliano ya ushirikiano iliyofanyika jijini Mogadishu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) na Waziri wa Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Somalia Mhe. Balozi Ahmed Moalim Fiqi wakitia saini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa jumla katika hafla iliyofanyika jijini Mogadishu, Somalia, Disemba 19, 2024. 
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Pindi Chana (Mb.) na Waziri wa Habari, Utamaduni na Utalii wa Somalia wakitia saini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya Utalii katika hafla iliyofanyika jijini Mogadishu, Somalia Disemba 19, 2024.

 Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Edwin Mollel (Mb.) na Waziri wa Afya wa Somalia Mhe. Dkt. Ali Hajiadam Abubakar wakitia saini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya Afya katika hafla iliyofanyika jijini Mogadishu, Somalia Disemba 19, 2024.

Wimbo wa Taifa ukipigwa 
Picha ya pamoja.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jumhuri ya Somalia Mhe. Saalax Axmed Jaamac kwenye hafla ya kusaini hati za makubaliano ya ushirikiano iliyofanyika jijini Mogadishu, Somalia.
Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Ellen Maduhu akiwasilisha tamko la pamoja kati ya Tanzania na Somalia wakati wa hafla ya kusaini hati za makubaliano ya ushirikiano iliyofanyika jijini Mogadishu.
Naibu Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jumhuri ya Somalia Mhe. Saalax Axmed Jaamac akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa hafla ya kusaini hati za makubaliano ya ushirikiano iliyofanyika jijini Mogadishu.
Waziri wa Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Somalia Mhe. Balozi Ahmed Moalim Fiqi akifungua hafla ya kusaini hati za makubaliano ya ushirikiano iliyofanyika jijini Mogadishu.

WAZIRI KOMBO AWASILI NCHINI SOMALIA KWA ZIARA YA KIKAZI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili jijini Mogadishu, Shirikisho la Jamhuri ya Somalia kwa ziara ya kikazi atakayoifanya nchini humo kuanzia terehe 18 hadi 20 Disemba 2024. 

Akiwasili nchini humo tarehe 18 Disemba 2024, kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden Abdulle jijini Mogadishu, Waziri Kombo amepokelewa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo Nje Mhe. Balozi Ahmed Moalim Fiqi na viongozi wengine waandamizi wa ngazi mbalimbali Serikalini. 

Waziri Kombo akiwa nchini humo anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Jamhuri ya Somali yatakayofanyika jijini Mogandishu tarehe 19 Disemba 2024 

Mazungumzo hayo ambayo yataambatana na hafla ya kusaini hati kadhaa za makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali, vilevile yanalenga kuibua maeneo mapya ya ushirikiano, kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi. 

Aidha, mazungumzo hayo yanatarajiwa kufungua na kuongeza fursa mpya za uchumi na biashara kwa manufaa ya pande zote mbili, ikiwemo upatikanaji wa soko la bidhaa zinazozalishwa katika nchi hizo mbili kama vile mazao ya kilimo, bidhaa za viwandani na huduma mbalimbali ikiwemo usafiri wa anga, afya na elimu. 

Ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo hayo utajumuisha Watendaji na Viongozi mbalimbali wa Serikali ikiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Pindi Chana, Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel, Viongozi waandamizi wa Vyombo vya ulinzi na Usalama na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden Abdulle jijini Mogadishu tarehe 18 Disemba 2024

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akipokelewa na Waziri wa Mambo Nje wa Mhe. Balozi Ahmed Moalim Fiqi alipowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden Abdulle jijini Mogadishu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akiangalia ngoma ya asili alipowasili jijini Mogadishu, Somalia. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akisalimiana na Balozi wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia nchini Tanzania Mhe. Ilyas Ali Hassanalipowasili katika uwanja ndege wa kimataifa wa Aden Abdulle jijini Mogadishu.

Wednesday, December 11, 2024

WAZIRI KOMBO AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA DHARURA WA MAWAZIRI WA SADC ORGAN







Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC- Organ), Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Organ Troika) uliofanyika katika Afisi ya Mambo ya Nje Zanzibar tarehe 11 Desemba, 2024.

Mkutano huo umewakutanisha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Nchi Wanachama wa SADC ambapo Tanzania ni Mwenyekiti wa Asasi hiyo, Malawi ni Mwenyekiti Ajaye na Zambia ni Mwenyekiti Anayemaliza Muda Wake.

Pamoja na masuala mengine Mawaziri hao wamejadili hali ya ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambayo ni pamoja na bajeti ya Misheni ya Ulinzi na usalama katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (SAMIDRC) kwa mwaka 2024 hadi 2025.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC- Organ), Balozi Dkt. Samweli Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Faraji Mnyepe, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Shaaban, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania Luteni Jenerali Salum Haji Othman, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Talha Waziri pamoja na maafisa waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkutano huo ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama Balozi, Dkt. Samwel Shelukindo.