Thursday, December 19, 2024

WAZIRI KOMBO AWASILI NCHINI SOMALIA KWA ZIARA YA KIKAZI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili jijini Mogadishu, Shirikisho la Jamhuri ya Somalia kwa ziara ya kikazi atakayoifanya nchini humo kuanzia terehe 18 hadi 20 Disemba 2024. 

Akiwasili nchini humo tarehe 18 Disemba 2024, kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden Abdulle jijini Mogadishu, Waziri Kombo amepokelewa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo Nje Mhe. Balozi Ahmed Moalim Fiqi na viongozi wengine waandamizi wa ngazi mbalimbali Serikalini. 

Waziri Kombo akiwa nchini humo anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Jamhuri ya Somali yatakayofanyika jijini Mogandishu tarehe 19 Disemba 2024 

Mazungumzo hayo ambayo yataambatana na hafla ya kusaini hati kadhaa za makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali, vilevile yanalenga kuibua maeneo mapya ya ushirikiano, kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi. 

Aidha, mazungumzo hayo yanatarajiwa kufungua na kuongeza fursa mpya za uchumi na biashara kwa manufaa ya pande zote mbili, ikiwemo upatikanaji wa soko la bidhaa zinazozalishwa katika nchi hizo mbili kama vile mazao ya kilimo, bidhaa za viwandani na huduma mbalimbali ikiwemo usafiri wa anga, afya na elimu. 

Ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo hayo utajumuisha Watendaji na Viongozi mbalimbali wa Serikali ikiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Pindi Chana, Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel, Viongozi waandamizi wa Vyombo vya ulinzi na Usalama na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden Abdulle jijini Mogadishu tarehe 18 Disemba 2024

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akipokelewa na Waziri wa Mambo Nje wa Mhe. Balozi Ahmed Moalim Fiqi alipowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden Abdulle jijini Mogadishu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akiangalia ngoma ya asili alipowasili jijini Mogadishu, Somalia. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akisalimiana na Balozi wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia nchini Tanzania Mhe. Ilyas Ali Hassanalipowasili katika uwanja ndege wa kimataifa wa Aden Abdulle jijini Mogadishu.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.