Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Bernard Membe akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake kufuatia Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Madola uliofanyika Mjini Perth Australia. Katika mkutano na waandishi wa habari Waziri Membe pia alizungumzia msimamo wa Tanzania kuhusu kauli ya Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. David Cameron kuhusu utoaji wa misaada kwa nchi zinazoendelea kwa masharti. Kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Mahadhi Juma Mahadhi na Katibu Mkuu wa Wizara John Haule.
Maelezo ya Mhe. Bernard K. Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa baada ya kuwasili nchini kutoka kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Madola 1. Nimewaita ili kuwaeleza kwa kifupi kuhusu kikao kilichofanyika Perth Australia kuhusu Jumuiya ya Madola, lakini pia nitazungumzia suala la ‘ushoga’ ambalo limejitokeza hapa na ndio maana wengi wenu mmenyoosha vidole kutaka kuuliza maswali. 2. Kikao cha Viongozi wa Jumuiya ya Madola kilikwenda vizuri Mjini Perth, kilifanyika vizuri sana kati ya tarehe 28-30 mwezi Oktoba. 3. Katika kikao kile kulikuwa na masuala matatu makubwa yaliyojitokeza: a. La kwanza ni pendekezo la Jumuiya ya Madola kuwa na charter. Charter ni utaratibu wa kuwa na kanuni, taratibu na muongozo wa kufuatwa na wananchi wa Jumuiya ya Madola. Jumuiya hii ni kubwa kwa sababu ina watu bilioni mbili kutoka nchi 54. Kuna dini zote kubwa duniani Wahindu milioni mia saba, Waislamu milioni mia sita, Wakristu milioni mia nne. Hivyo ni Jumuiya kubwa inayostahili kuwa na charter (kanuni) kama ilivyo kwenye Umoja wa Mataifa. Hili lilizungumzwa na kukubaliwa kimsingi na kupitishwa kwenye vikao vya Mawaziri na baadaye kupitishwa na Wakuu wa nchi. b. Suala la pili kwenye kikao hicho lilikuwa ni kuimarisha demokrasia, utawala bora, na haki za binadamu.Hili nalo lilizungumzwa kwa pendekezo kwamba tuwe na kamishana, ambaye atashughulikia mambo hayo matatu. Baada ya mjadala mkali kwenye ngazi ya mawaziri na baadae kwa viongozi wan chi, suala hilo halikukubalika kwa sababu Jumuiya ya Madola ina vyombo viwili:- i. Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola ii. Kamati maalum ya Mawaziri wa Jumuiya ya Madola (CMAG) Vyombo vyote hivi vinahusika na uratibu wa demokrasia, utawala bora na haki za binadamu. Kwa hivyo kuunda chombo kipya cha Kamishna kuratibu mambo haya haya, itaonekana kama ni kupoteza fedha na muda (redundant). Kwa hiyo hilo lilikataliwa.
c. La tatu lilikuwa linahusu mabadiliko ya tabia nchi au hali ya hewa. Huko nyuma jumuiya ilijikita zaidi kwenye masuala ya haki za binadamu, utawala bora na masuala ya demokrasia. Safari hii viongozi wakasema pamoja ya kwamba mambo haya ni muhimu ni vizuri masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na masuala ya maendeleo ya nchi wanachama wa jumuiya yapate uzito kwani bado nchi nyingi za Jumuiya ya Madola ziko kwenye maendeleo sasa na zinakumbwa na zinakumbwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
4. Serikali na Tanzania imesikia tamko la Waziri Mkuu wa Uingereza kwenye Vyombo vya Habari, kuhusu suala la ushoga. Na katika matamko hayo, ushoga unaunganishwa na msaada wa maendeleo “development aid”. Kwamba ili upate msaada wa maendeleo basi ukubali sheria za ushoga zinazoruhusu watu wa jinsia moja kufunga ndoa, na kuishi pamoja.
5. Suala la ushoga halikuwa sehemu ya ajenda, na wala halikuzungumziwa kwenye kikao cha Viongozi wa Jumuiya ya Madola. Katika Mkutano wa ngazi ya Maafisa Waandamizi kulikuwa na jaribio la Serikali ya Uingereza kuwasilisha pendekezo la kuingizwa aya katika Charter (kanuni) ya Jumuiya ya Madola inayosisitiza kulinda na kuheshimu haki za binadamu kwa ujumla wake, ikiwemo haki za Mashoga. Pendekezo hilo lilipata upinzani mkali na kutupiliwa mbali kwenye ngazi ya Mawaziri na pia halikujitokeza kabisa kwenye ngazi ya Wakuu wa Nchi.
6. Tamko hili ni la Chama Tawala cha Conservative, na ndiyo sera yao ambapo sasa kwa tamko hili inashinikiza mataifa wanayowapa misaada kuafikiana na suala hili.
7. Hapa Tanzania, dini zetu na tamaduni za makabila yetu haziruhusu ndoa za jinsia moja. Sheria yetu ya Ndoa ya Mwaka 1971 na sheria ya makosa ya jinai ambazo kwa kiasi kikubwa tulizirithi kutoka kwa Waingereza, zinatambua tu mahusiano kati ya mume na mke, yaani jinsia mbili tofauti. Na Watanzania tunajua kama msingi wa Taifa ni familia, ambayo kwa kanuni na sheria za asili ni muungano wa mwanaume na mwanamke. Matokeo ya muungano huu ni vizazi, ambavyo ndio nguvu kazi na uhai wa taifa. Hivyo basi sheria zetu zinachukulia ndoa za jinsia moja kama kinyume cha maumbile na kosa la jinai ambalo mwenye hatia anaweza kuhukumiwa hadi miaka 30 jela.
8. Tanzania inafuata utamaduni wa familia ya mume na mke, na kamwe hatutapokea amri wala ushauri wa mtu yoyote nje ya nchi yetu kuja kuingilia masuala ya nchi yetu.
9. Huu utamaduni mpya wa kuunganisha misaada ya maendeleo na ushoga, kwamba ili upate hiki, fanya hili, inavunja uhusiano wa kimataifa. Ni tamko hatarishi linaloweza kuvunja uhusiano kati ya nchi na nchi. Muhimu zaidi ni kwamba tamko hili linatoka Uingereza ambao ndio walezi wa Jumuiya ya Madola na tumetoka nalo kwenye Mkutano, likitaka kupenyezwa. Tamko hili ni hatari kwa Jumuiya ya Madola na Jumuiya inaweza kuvunjika kwa matamko ya aina hii. Na ikivunjika, Waziri Mkuu wa Uingereza atawajibika na usambaratishaji au kuvunjika kwa Jumuiya ya Madola.
10. Suala la Mashoga halikubaliwi kwenye Jumuiya ya Madola na iwapo Waziri Mkuu wa Uingereza akililazimisha ndani ya Jumuiya, atahatarisha uhai wa Jumuiya yenyewe. Jumuiya ya Madola ina nchi 54 na ni nchi 13 tu ndio zinaabudu suala hili. Nchi 41 haziabudu suala hili, na hawa ndio wengi. Hili si suala la Uingereza kulishabikia, wala si suala la Uingereza kulitamka wazi leo. Wanaweza kujuta.
11. Tanzania hatuwezi kuyumbishwa wala kupindisha utaifa wetu kwa maagizo wala masharti ya aina hii, tuko tayari kwa lolote lile, bora tuitunze heshima yetu. Tanzania ni nchi maskini sana, na tuna tofauti zetu nyingi za ndani (ya nchi) lakini kamwe hatutaruhusu mtu, au kundi la watu wa nchi yoyote iwe kubwa tajiri itakayokuja kutupa masharti ya kubadilisha utaifa wetu eti kwa sababu tuwe na tumbo lililoshiba, tunakataa. Natamka sasa, tutakataa. Kama wanadhani kuwa misaada kwa nchi zinazoendelea na nchi ya Tanzania itatolewa kwa masharti kwamba sisi tuanze sasa kukubaliana na masuala nje ya sheria na kanuni zetu kama suala hili la mashoga, wakae na hela zao.
Mwisho. |