Tuesday, August 27, 2013

TAARIFA KWA UMMA


Mhe. Waziri Membe akielezea kuhusu suala la uraia wa nchi mbili. 



TAARIFA KWA UMMA

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kuujulisha Umma kuwa jana tarehe 26 Agosti, 2013, Mheshimiwa Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alikutana na Uongozi wa Tume ya Marekebisho ya Katiba.  Lengo la kukutana na Tume ilikuwa ni kuwasilisha pendekezo la haki ya Uraia wa nchi mbili kutamkwa na kutambuliwa kwenye Katiba mpya.

Mheshimiwa Waziri alikutana na Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Augustino Ramadhani, Makamu Mwenyekiti wa  Tume pamoja na Katibu wa Tume na Naibu Katibu wa Tume.

Akiwasilisha hoja yake mbele ya Tume ya Marekebisho ya Katiba, Mheshimiwa Waziri alisema yafuatayo:-

1.    Suala la Uraia wa Nchi mbili haliko kwenye rasimu ya sasa iliyotolewa.  Lengo la kufika Tume ni ni kuomba suala hilo liingizwe kwenye rasimu.

2.    Amependekeza Katiba itamke kwamba, Raia wa Tanzania aliyeko nje hatafutiwa uraia wake na mtu yeyote, chombo chochote sheria au Katiba, eti tu kwa sababu raia huyo amechukua uraia nje ya nchi.

3.    Katiba ikitamka hivyo, itungwe Sheria itakayofafanua haki, wajibu na masharti ya Mtanzania mwenye uraia wa nchi mbili.

4.    Katika kujenga hoja hizo tatu, Tume ilielezwa faida zitakazopatikana kwa kuitambua na kuishirikisha jamii ya Watanzania waliopo ughaibuni (Diaspora).  Tume pia iliondolewa wasiwasi juu ya madai kuwa uraia wa nchi mbili unahatarisha usalama wa taifa au utawafanya baadhi ya watu kupiga kura wakiwa nje. Tume iliambiwa kuwa Sheria za Uchaguzi hutawala upigaji kura kwa raia walio ndani  na nje na hauwi  holela.  Kuhusu suala la usalama, Waziri alisisitiza kama ni mashaka, basi mashaka hayo yawe kwa wageni wanaoomba uraia  nchini kuliko watanzania walioko nje.


Katika kumalizia, Mheshimiwa Waziri alisisitiza, “bado naamini watanzania walioko nje sio wasaliti, They are just as smart citizen”.



IMETOLEWA NA:


 WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA 

KIMATAIFA


27 Agosti, 2013





Monday, August 26, 2013

Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa lazinduliwa rasmi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), akizungumza na Mgeni Rasmi ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim kabla ya ufunguzi rasmi wa Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba. Ufunguzi huo uliowahusisha Mabalozi Wastaafu, Watumishi wa Wizara na Taasisi na wadau wengine ulifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Agosti, 2013. Wengine katika picha ni Bw. John Haule, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Balozi Mstaafu, Mhe. David Kapya.

Mhe. Membe akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo  ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim kufungua rasmi Baraza hilo.

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza hilo ambao ni Mabalozi Wastaafu wakimsikiliza Mhe. Membe wakati wa ufunguzi wa Baraza hilo.
Mgeni Rasmi na Mjumbe wa Tume ya Mambadiliko ya Katiba, Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim akifungua rasmi Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Baadhi ya Wajumbe wakimsikiliza Mhe. Dkt. Salim (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Baraza la Katiba la Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajabu Gamaha.

Bw. Haule, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mmbo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwakaribisha Wajumbe kwenye ufunguzi huo.

Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Simba Yahya (wa pili kushoto) akiwa na baadhi ya Mabalozi Wastaafu wakati wa ufunguzi huo.

Wajumbe zaidi wakati wa ufunguzi huo.

Wajumbe wakiwemo Mabalozi Wastaafu na Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje wakati wa ufunguzi.


Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Bertha Semu-Somi akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Wilson Masilingi wakati wa ufunguzi wa Baraza la Katiba la Wizara.

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza ambao pia ni Wakuu wa Idara na Vitengo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano  wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Baraza hilo.

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza ambao pia ni Maafisa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa walioshiriki ufunguzi wa Baraza la Katiba la Wizara.


Baadhi ya Wajumbe kutoka Chuo cha Diplomasia (CFR) walioshiriki ufunguzi wa Baraza la Katiba la Wizara.
Mgeni Rasmi, Mhe. Dkt. Salim na Mhe. Membe wakiwa katika Picha ya Pamoja na Mabalozi Wastaafu.

Mgeni Rasmi, Mhe. Dkt. Salim na Mhe. Membe wakiwa katika Picha ya Pamoja na Mabalozi Wastaafu na Wakurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Taasisi zake.

Mgeni Rasmi, Mhe. Dkt. Salim na Mhe. Membe wakiwa katika Picha ya Pamoja na Wajumbe wote wa Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.


Picha na Reginald Philip.

Membe alonga na Warioba kuhusu Uraia wa Nchi Mbili


Mhe. Waziri Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiingia rasmi katika Ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo mjini Dar es Salaam.   Kulia ni Mhe. Balozi Rajabu Gamaha, Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. 

Mhe. Waziri Membe akiwa katika mazungumzo na Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Mhe. Jaji Warioba akimkaribisha Mhe Waziri Membe wakati wa mazungumzo yao kuhusu uraia wa nchi mbili. 

Mhe. Waziri Membe akielezea kuhusu suala la uraia wa nchi mbili. 

Mhe. Jaji Warioba akiwa na Dkt. Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Tume ya Katiba, Katibu wa Tume ya Katiba na Naibu Katibu Mkuu wa Tume ya Katiba. 

Balozi Bertha Semu-Somi (kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora, Bw. James Lugaganya, Mkurugenzi Idara ya Sera na Mipango na Bi. Naomi Zegezege, Afisa wa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakisikiliza kwa makini mazungumzo yanayoendelea. 

Mhe. Jaji Warioba akielezea maoni ya Watanzania kuhusu uraia wa nchi mbili.

Kikao kikiendelea.

Balozi Bertha Semu-Somi, Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akielezea changamoto mbalimbali za wanadiaspora na uraia wa nchi mbili. 

Dkt. Salim Ahmed Salim (kushoto), pamoja na Katibu wa Tume ya Katiba (katikati) na Naibu Katibu wa Tume ya Katiba wakimsikiliza Balozi Semu-Somi. 

Mkutano ukiendelea. 

Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba na Dkt. Salim Ahmed Salim wakisiliza kwa makini maoni ya Waziri Membe (hayupo pichani).

Jaji Mkuu Mstaafu Agostino Ramadhani, Makamu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (katikati) akielezea jambo wakati Mhe. Jaji Warioba na Mhe Waziri Membe wakimsikiliza.  

Mhe Waziri Membe akitoka katika Ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba mara baada ya kumaliza mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Jaji Joseph Warioba. 



Membe alonga na Warioba kuhusu Uraia wa Nchi Mbili


Na Tagie Daisy Mwakawago na Fatma Salum

“Uwepo wa Diaspora ni lazima utambulike Kikatiba,” asema Waziri Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Waziri Membe aliyasema hayo alipokutana na Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo katika Ofisi za Tume hiyo zilizopo mjini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao, viongozi hao walijadili suala la uraia wa nchi mbili (dual citizenship) ambalo linapiganiwa kwa kiasi kikubwa na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora)

“Tumekuja kuwasilisha masuala muhimu mawili:  moja, uwepo wa uraia wa nchi mbili katika Rasimu ya Katiba na pili, Katiba mpya iruhusu raia yoyote wa Tanzania aweze kuwa na uraia wa nchi nyingine pasipo kuukana uraia wa Tanzania,” alieleza Waziri Membe.

Alisema kuwa Wizara yake inatambua suala la uraia wa nchi mbili kuwa ni la msingi, ambalo halikugusiwa katika Rasimu ya Katiba iliyopo.

“Chimbuko la uraia wa nchi mbili lilitokana na wingi wa Watanzania walioko nje ya nchi ambao wanatafuta fursa ya kuwekeza na kuinua maendeleo ya nchi yao,” alisema Waziri Membe. 

Aliongeza pia, “Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 inawatambua Watanzania hao na kutaka wapewe fursa ya kuwa na uraia wa nchi mbili katika kuinua maendeleo ya nchi.”

Watanzania hao wamekuwa wakikabiliana na matatizo kadhaa ambayo yanawanyima haki za msingi, kama vile afya, elimu na masuala ya ajira.  “Kilio chao kimekuwa kero kubwa kwa vile wakati mwingine wanatibiwa kwa gharama kubwa sana ambazo hazilingani na kipato chao,” alisema Waziri Membe.

Aidha, changamoto hizo zimekuwa ni chanzo kikubwa cha kuwashawishi Watanzania hao kuchukua uraia wa nchi za kigeni ili kuwawezesha kupata huduma muhimu za kijamii kama vile elimu na afya.

“Hivi sasa sheria yetu haimruhusu Mtanzania kuchukua uraia wa nchi mbili pasipo kuukana uraia wa nchi yake,” alisema Membe, na kufafanua kuwa “Ilani ya CCM inamuhamasisha Mtanzania huyo achangie maendeleo ya nchi yake kupitia uraia wa nchi mbili.”

Waziri Membe alisema kuwa Watanzania wakiwa nje wanakosa fursa za kazi zenye kipato kikubwa wasipokuwa na uraia wa nchi hiyo, jambo linalopelekea maisha magumu na kushindwa kujikimu na kuchangia kipato chochote kwa ndugu zao walioko nchini. 

“Badala yake, unakuta Watanzania wananaswa na tamaa ya ‘kujilipua’ kwa kubadili uraia wa nchi nyingine zinazokubali uraia wa nchi mbili na kuachana na uraia wa Tanzania,” alieleza Waziri Membe.

Kwa upande wake, Mhe. Warioba alisema kuwa maoni hayo ya uraia wa nchi mbili yamekuwa yakijitokeza katika ukusanyaji wa maoni sehemu mbalimbali.  Na kuongeza kuwa, hofu kubwa ya wananchi ni usalama wa nchi yao endapo uraia wa nchi mbili utaruhusiwa.

Mhe. Waziri Membe alikuwa ameambatana na Balozi Gamaha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Balozi Bertha Semu-Somi, Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora na Bw. James Lugaganya, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.   Kwa upande wa Mhe. Warioba, alikuwepo Jaji Mkuu Mstaafu Agostino Ramadhani, Makamu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Salim Ahmed Salim, Mjumbe wa Tume, pamoja na Katibu na Naibu Katibu wa Tume ya Mabadiliko.


Mwisho.  





Baraza la Katiba la Wizara kukutana leo



220px-Coat of arms of Tanzania.svg f1f71


Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje linatarajiwa kukutana leo kuanzia saa 4 asubuhi hii kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, mjini Dar es Salaam.  

Wajumbe wapatao 100 wanatarajiwa kuhudhuria Mkutano huo wakiwemo viongozi wa Wizara, Wakurugenzi na Maafisa kutoka Wizarani,wawakilishi kutoka Taasisi ya Chuo cha Diplomasia -Kurasini (CFR), wawakilishi kutoka Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa - Arusha (AICC) na Waheshimiwa Mabalozi Wastaafu wapatao 43 na Waziri wa Mambo ya Nje mstaafu Mzee Ibrahim Kaduma. 

Mgeni rasmi atakuwa Mjumbe wa Tume ya Katiba na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe Dk. Salim Ahmed Salim.

Aidha, ripoti ya mwisho ya maoni hayo itawasilishwa rasmi kwenye Tume ya Katiba.