=====================================================
Tanzania imeendelea kuunga mkono jitihada za kitaifa na kimataifa katika kuhakikisha usalama wa chakula pamoja na lishe bora yenye virutubisho muhimu hususan kwa watoto wadogo, kina mama wajawazito na wanaonyonyesha inapatikana kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda alipozungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Kilele wa Dunia kuhusu masuala ya Chakula na Lishe uliofanyika kwenye Hoteli ya Mount Meru, Jijini Arusha hivi karibuni.
Mhe. Pinda alisema kuwa jitihada hizo ambazo kwa kiasi kikubwa zimeelekezwa katika kuhamasisha unyonyeshaji wa watoto wachanga na kutumia vyakula vyenye virutubisho kwa watoto wa kuanzia miezi sita hadi mwaka mmoja umesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza vifo vitokananvyo na ukosefu wa chakula bora na utapiamlo.
Aliongeza kuwa Tanzania imekuwa na program mbalimbali kwa vipindi tofauti katika kupambana na magonjwa yatokanayo na ukosefu wa vyakula vyenye virutubisho na madini muhimu ikiwemo program ya kuongeza madini joto kwenye chumvi iliyozinduliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mhe. Ali Hassan Mwinyi mapema mwaka 1990 ili kupambana na magonjwa yanayosababishwa na upungufu wa madini hayo mwilini ikiwemo ugonjwa wa goiter ambao ulienea nchini miaka ya 1980.
Aidha, mwaka 2013 Serikali ilizindua Program ya Kitaifa ya Uboreshaji wa Chakula ambapo virutubisho muhimu viliongezwa kwenye vyakula vinavyoliwa zaidi katika jamiii ya Watanzania ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 25 ya watu wanatumia unga wa ngano na mahindi pamoja na mafuta ya kupikia yaliyoongezwa virutubisho vyenye madini na vitamin muhimu kama chuma, zinki na Vitamini A na B12.
“Kwa upande wa Tanzania jitihada nyingi za kuhakikisha suala zima la upatikanaji wa chakula bora ili kuwawezesha wananchi kuwa na afya bora ili kuchangia katika maendeleo ya taifa lao zimefanyika. Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kuhamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa watoto wachanga, kuzinduliwa kwa Mkakati wa Taifa wa Lishe wa miaka mitano hapo mwaka 2011 ambao lengo lake kubwa ni kuhamasisha matumizi ya vyakula vyenye virutubisho” alisema Mhe. Pinda.
Aidha, alieleza kuwa kwa sasa Serikali kupitia Mamlaka za Serikali za mitaa imeweka mkazo kuhakikisha huduma ya uboreshaji vyakula kwa kuongeza virutubisho muhimu inapelekwa katika maeneo ya vivijini ambapo zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanaishi huko. “Mifumo inaandaliwa ili kuhakikisha mamalaka hizi zinafanikisha uboreshaji wa vyakula ikiwemo unga wa nafaka unaozalishwa katika mashine za kawaida na mafuta ya kula yanayotengenezwa na wananchi vijijini yanaboreshwa” alisisitiza Mhe. Pinda.
Katika hatua nyingine Mhe. Pinda alisifu na kuwashukuru waandaaji wa mkutano huo kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji kwani ni wakati muafaka ambapo kampeni hii ya dunia itasaidia kuhamasisha pia wananchi na wawekezaji katika sekta ya chakula hapa nchini na hatimaye kuleta matokeo endelevu katika lishe na usalama wa afya ya jamii kwa ujumla.
Pia alisema kuwa kwa vile mkutano huo umewashirikisha watu kutoka Serikalini, wafanyabiashara, taasisi za kiraia, mashirika ya kimataifa, wanazuoni na washirika wa maendeleo ana imani kubwa kuwa utaainisha mafanikio, changamoto na kuweka mikakati ya baadaye kuhusu uboreshaji wa afya ya jamii zetu kwa maendeleo endelevu.
Mkutano huo ambao ulihudhuriwa pia na Mfalme Letsie III kutoka Lesotho ambaye pia ni Kiongozi wa kuhamashisha matumizi ya chakula bora na lishe wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, alisema kwamba lishe bora ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi kwa kila taifa. Kwamba kuwekeza kwenye lishe ni muhimu ili kupunguza umaskini kwa kuhakikisha kila mwanajamii anachangia kwa taifa lake.
Alieleza kuwa Mkakati wa Lishe wa Kanda ya Afrika kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015-2025 uliozinduliwa mwezi Julai mwaka huu kuwa unasisitiza ushirikishwaji wa sekta mbalimbali katika kuboresha lishe ikiwemo sekta binafsi ambapo alitoa tahadhari kwa wafanyabiashara kutotumia fursa hii kujitengenezea faida kubwa kwa bidhaa watakazozalisha badala ya kuangalia afya za watu kwanza. Pia mapendekezo kuhusu njia bora za uchangiaji mpango wa lishe Afrika yalijadiliwa.
“Natoa tahadhari kwa wenzetu wa sekta binafsi kuhakikisha afya ya mtu inapewa kipaumbele na kuhakikisha ari ya kujipatia faida haihatarishi afya ya mtu yeyote”alisisitiza Mfalme Letsie III.
Pia aliongeza kuwa, Kamisheni ya Umoja wa Afrika na nchi wanachama zinatambua kwamba Serikali pekee haziwezi kutatua changamoto ya lishe duni inayolikabili Bara la Afrika bali jitihada za wadau wote muhimu zinahitajika ikiwemo sekta binafsi hususan kampuni zinazozalisha na kutengeneza vyakula, Mashirika ya Kimataifa, taasisi za kiraia na wanazuoni wanatakiwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya lishe bora kwa kila mtu.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mhe. Dkt. Kebwe Steven Kebwe alisma kuwa amefarijika mkutano wa kwanza kuhusu masuala ya chakula na lishe umefanyika nchini na kwamba mada zitakazojadiliwa wakati wa mkutano huo zitaziwezesha nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kuangalia namna bora ya kuboresha lishe kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Mkutano wa Kilele wa Dunia kuhusu uboreshaji wa Chakula na Lishe uliowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo mashirika ya kimataifa, serikali, wanazuoni, washirika wa maendeleo na sekta binafsi umefanyika Jijini Arusha kuanzia tarehe 09 Septemba, 2015.
=mwisho=