|
Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea Wizarani ikiwemo maandalizi ya ziara ya kikazi ya Rais wa Sudan Kusini, Mhe. Salva Mayardit Kiir atakayoifanya nchini tarehe 15 Aprili, 2016. Mkutano huo ulifanyika Jijini Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) tarehe 14 Aprili, 2016. |
|
|
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Miundombinu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bw. Abdilah Mataka akiwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa iliyokuwa Wizara ya Afrika Mashariki, Bi. Robi Bwiru wakati wa mkutano wa Wizara na Waandishi wa Habari |
|
Wawakilishi kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara nao wakifuatilia mkutano kati ya Wizara na waandishi wa habari. Kulia ni Bi. Praxeda kutoka Taasisi ya Mpango wa Nchi za Afrika kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) na Bi. Beatha Hyera kutoka Taasisi ya Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC). |
|
Bw. Mataka naye akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya masuala wakati wa mkutano huo. |
|
Mwandishi wa Habari akiuliza swali. |
|
Mkutano ukiendelea. | |
|
=========================================
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Mhe. Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya ziara
ya kikazi nchini Rwanda tarehe 06 na 07 Aprili 2016. Ziara hiyo ilianzia
wilayani Ngara ambapo kwa kushirikiana na mwenyeji wake, Mhe. Paul Kagame, Rais
wa Rwanda walizindua Daraja la Rusumo na Kituo cha Pamoja cha kutoa Huduma
Mpakani (OSBP). Baada ya uzinduzi, Waheshimiwa Marais walielekea Kigali ambapo
walifanya mazungumzo ya pande mbili katika kijiji cha Muhanzi.
-Katika
mazungumzo hayo Wakuu hao wa Nchi walikubaliana mambo mbalimbali ikiwa ni
pamoja na:
· -
Kudumisha na Kuimarisha ushirikiano na
uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda;
·
Kuboresha miundombinu katika Ushoroba
wa Kati ikiwemo ujenzi wa reli kutoka Tanzania hadi Kigali;
·
Ushirikiano katika sekta ya usafiri wa
Anga kati ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na lile la Rwanda (Air
Rwanda);
· Kushirikiana katika usimamizi wa mradi
wa umeme wa Rusumo ili kuzalisha Mega Watts 80. Mradi huo utakapokamilika
utazifaidisha nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi; na
·
Kuagiza Mkutano wa Tume yaKudumu ya
Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda ufanyike Kigali tarehe 29 na
30 Aprili 2016.
Uzinduzi
wa Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja (One Stop
Border Post - OSBP) Tarehe 6 Aprili, 2016
Marais
wa Tanzania na Rwanda walizindua Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha
Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Rusumo. Tukio hili lilihudhuriwa na viongozi wa ngazi
za juu Serikalini kutoka Tanzania na Rwanda, Mabalozi, na Viongozi wa Taasisi
mbambali za Kitaifa na Kimataifa.
Ujenzi
wa Daraja na Kituo hiki cha Huduma kwa Pamoja Mpakani ni mradi uliotekelezwa
kwa msaada kutoka Serikali ya Japan kwa nchi za Tanzania na Rwanda kupitia
Shirika lake la Maendeleo (JICA). Mradi huu umegawanyika katika sehemu mbili:
i. Sehemu ya kwanza ni ujenzi wa Daraja
la Rusumo linalounganisha nchi za
Tanzania na Rwanda; na
ii.
Sehemu ya pili ni ujenzi wa majengo na
eneo la Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) kwa pande zote mbili za
Tanzania na Rwanda.
Kazi zilizotekelezwa katika Mradi huu
ni pamoja na:
·
Kujenga daraja lenye urefu wa Mita 80
la njia mbili zenye upana wa mita 3.75;
·
Kujenga sehemu ya wapita kwa miguu
yenye upana wa mita 1.5;
·
Kujenga maingilio ya barabara kwa
kiwango cha zege la lami lenye unene wa milimita 150 wa mita 7;
·
Kujenga barabara ya kilometa 2 na
mabega ya barabara yenye upana wa mita 1.5; na
·
Kujenga Kituo cha Kutoa Huduma kwa
Pamoja mpakani (OSBP).
Mradi huu kwa upande wa
Tanzania umegharimu jumla ya Shilingi 33,206,508,072.07
ambapo
kati ya fedha hizo Serikali ya Tanzania ilitoa Shilingi 542,385,122.07 kwa ajili ya fidia na uunganishaji wa
huduma ya maji na umeme.
Faida
Daraja
la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani ni kiungo muhimu
katika barabara za Ushoroba wa Kati (Central Corridor). Ushoroba wa Kati una
mtandao wa barabara unaounganisha barabara kuu ya Dar es Salaam - Chalinze – Morogoro – Dodoma – Singida –
Nzega – Tinde – Isaka – Lusahunga - Rusumo hadi Kigali Nchini Rwanda.
Barabara
hii inaunganisha barabara kuu ya kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC)
na kuifanya kuwa kiungo muhimu cha usafiri na usafirishaji wa mazao mbalimbali
ya chakula na biashara kuelekea nchi za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Kongo (DRC). Aidha, barabara hii ni sehemu ya mtandao wa barabara mbalimbali za
ukanda wa Afrika Mashariki zinazoendelea kujengwa.
Kukamilika
kwa ujenzi wa Daraja na Kituo hiki cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP)
Rusumo kutafungua fursa nyingi, ikiwa ni pamoja na:
i.
Kurahisisha usafiri wa watu na
usafirishaji wa bidhaa kati ya Jamhuri
ya Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na nchi yetu pamoja na
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC na COMESA;
ii.
Kukuza na kuchochea uzalishaji katika
sekta za kilimo, viwanda na utalii;
iii.
Kuimarisha ushirikiano na kuhamasisha
biashara ndani ya nchi na baina ya nchi jirani; na
iv.
Kuwezesha urahisi wa mawasiliano ya
kijamii kati ya watu wa Tanzania na Rwanda na Wanaafrika Mashariki kwa ujumla.
Dhana
ya Vituo vya Pamoja vya Utoaji Huduma Mipakani
Dhana ya Vituo vya Pamoja vya Utoaji
Huduma Mipakani inahusu Nchi zinazopakana kushughulikia huduma na shughuli za
udhibiti kama forodha, uhamiaji, usalama na afya kwa kushirikiana. Hivyo,
abiria au msafirishaji bidhaa hulazimika kusimama na kukaguliwa au kukamilisha
taratibu za udhibiti sehemu moja wakati wa kutoka kwenye nchi moja na kuingia
nchi nyingine. Hatua hii inawezesha Idara, Taasisi na Wakala zinazotoa huduma
na udhibiti mpakani kufanya kazi kwa pamoja na hivyo kupunguza muda wa kukaa
mpakani na kuondoa vikwazo visivyo vya
kiforodha.
Ziara
ya Mhe. Salva Kiir, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Tarehe 15 Aprili 2016
Katika hatua nyingine, Mhe. Salva Kiir, Rais wa Jamhuri
ya Sudan Kusini atafanya ziara ya siku moja nchini Tanzania tarehe 15 Aprili
2016. Rais Kiir anakuja nchini kusaini Mkataba wa kuwezesha Jamhuri ya Sudan
Kusini kuwa Mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo tangazo
la kukubaliwa kuwa Mwanachama wa EAC lilitangazwa na Mwenyekiti wa Jumuiya
hiyo, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika jijini Arusha mwezi
Machi 2016.
Sudan Kusini ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinaweza
kuzifaidisha Nchi Wanachama wa EAC ikiwemo Tanzania endapo mipango madhubuti
itawekwa kuzichangamkia. Fursa hizo ni pamoja na kibiashara kwa kuwa karibu
kila bidhaa inayotumia Sudan Kusini inaagizwa kutoka Nje ya nchi. Sudan Kusini
inakabiliwa na uhaba wa chakula, huduma za kibenki, bima na wataalamu
mbalimbali. Hivyo, jamii ya wafanyabiashara wa Tanzania wanahimizwa
kuchangamkia fursa zinazopatikana nchini humo.
Wakati huo huo,
Serikali imepokea viongozi wa ngazi za juu kutoka nchi mbalimbali
duniani. Viongozi hao ni :
i.
Mhe. Dkt. Mario Giro, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia alifanya ziara
nchini tarehe 5 – 7 Aprili, 2016. Mhe. Giro aliambatana na Dr. Raffaele De
Lutio, Mkurugenzi wa Masuala ya Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia.
Madhumuni ya ziara hiyo ilikuwa ni kukutana na wadau mbalimbali wa maendeleo,
kuomba kuungwa mkono na Serikali ya Tanzania katika uchaguzi wa nafasi isiyo ya
kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) na kuomba Waziri wa Mambo ya Nje kushiriki katika Mkutano wa
Kwanza kati ya Afrika na Italia (First
Africa – Italy Conference) utakaofanyika tarehe 18 Mei, 2016;
ii.
Mhe. Gerd Müller,
Waziri wa Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo wa Ujerumani alifanya ziara ya
kikazi nchini, kuanzia tarehe 30 Machi hadi 1 Aprili,
2016. Katika ziara hiyo, Mhe. Müller aliambatana na viongozi mbalimbali wa
Wizara, Wabunge na wawakilishi wa asasi za kiraia. Mhe. Gerd Müller ni Waziri
mwenye dhamana ya fedha za misaada na ana ushawishi mkubwa katika kufanya
maamuzi kwenye Serikali ya Ujerumani. Serikali ya Ujerumani imekuwa mstari wa
mbele katika kuhakikisha Tanzania inapata fedha kila mwaka kwa ajili ya sekta
za kipaumbele ambazo ni maji, afya, viumbe hai (biodiversity) na kukabiliana na
ujangili;
iii.
Ujumbe wa
Wabunge nane (8) wa Kamati ya Fedha ya Bunge la Finland ulifanya ziara ya
kikazi hapa nchini, kuanzia tarehe 9 hadi 13 Aprili, 2016. Lengo la ziara hiyo
lilikuwa kuwajengea ufahamu zaidi
Wabunge hao kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya
Finland hapa nchini. Wabunge hao walianza ziara yao kwa kutembelea Mbuga ya
wanyama ya Mikumi. Baada ya hapo walielekea mkoani Iringa na kutembelea Chuo
Kikuu cha Iringa ambacho ni moja ya vyuo vinavyofaidika na ufadhili wa Serikali
ya Finland kupitia mradi wa TANZICT unaolenga kukuza masuala ya ubunifu na
ugunduzi kwa kutumia TEHAMA. Kabla ya kuondoka Iringa, Ujumbe huo ulikutana kwa
mazungumzo pia na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza.
iv.
Mhe. Marián Jurečka, Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Czech amefanya
ziara nchini tarehe 12 hadi 13 Aprili, 2014. Katika ziara hiyo Mhe. Jurečka
aliambatana na Manaibu Waziri wafuatao:-
· Mhe. Vladimír Bärtl, Naibu Waziri wa Biashara na
Viwanda wa Czech;
· Mhe.
Jiří JIRSA, Naibu Waziri wa Kilimo (Utawala);
· Mhe.
Zdeněk Adamec, Naibu Waziri Kilimo
(Uchumi na Teknolojia ya Habari);
· Mhe.
Pavel Sekáč, Naibu Waziri wa Kilimo (Jumuiya ya Ulaya, Sera za Uvuvi) na
· Mhe.
Jiří Šir, Naibu Waziri wa Kilimo (Bidhaa, Utafiti na Ushauri)
Mawaziri
hao waliambatana pia na maofisa mbalimbali wa Serikali ya Czech pamoja na
wafanyabiashara wamiliki wa makampuni mbalimbali takribani 15.
Madhumuni ya ziara hii yalikuwa ni kujadiliana
masuala mbalimbali ya kukuza na kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi
hizi mbili hususan katika masuala ya kilimo, nishati, uwekezaji, biashara na
maendeleo ya viwanda.
Mhe. Marián Jurečka, Waziri
wa Kilimo wa Czech alionana na Mhe.
Mwigulu Nchemba, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na viongozi wengine
wa Wizara hiyo. Katika mkutano wake aliambatana na Manaibu Waziri wake watatu.
Mhe. Vladimír Bärtl, Naibu
Waziri wa Biashara na Viwanda wa Czech alionana na
Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Katika
mazungumzo hayo ilikubalika kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na ushirikiano kati ya Tanzania na Czech
(Economic Cooperation and Bilateral Agreement) rasimu ya Mkataba wa Double Taxation na Investment Protection.
v.Aidha, Mhe. Dkt. Ali Masoud Al Sunaidy, Waziri
wa Biashara na Viwanda wa Oman aliwasili nchini tarehe 12 Aprili 2016
akiongozana na ujumbe wa wafanyabiashara zaidi ya 100 kwa ajili ya kutafuta
fursa za biashara na uwekezaji hapa nchini.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Dar es
Salaam
14
Aprili, 2016