Thursday, June 23, 2016

Katibu Mkuu wa AALCO, Prof. Gastorn afanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga )(Mb) kulia akifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mashauriano ya Masuala ya Kisheria katika Nchi za Asia na Afrika (Asian – African Legal Consultative Organization (AALCO), Prof. Kennedy Gastorn. Prof. Gastorn alichaguliwa kushika nafasi hiyo wakati wa Mkutano wa 55  uliofanyika mjini New Delhi, India mwezi Mei 2016. Prof. Gastorn alikuja kumuona Mhe. Waziri kwa lengo la kujitambulisha, kushukuru kwa kuungwa mkono na kubadilishana taarifa kuhusu Jumuiya hiyo.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mashauriano ya Masuala ya Kisheria katika Nchi za Asia na Afrika (Asian – African Legal Consultative Organization (AALCO), Prof. Kennedy Gastorn akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo hayo. Alibainisha kwamba nafasi hiyo ni heshima kubwa kwake na nchi kwa ujumla kwa kuwa jukwaa hilo ni jukwaa muhimu kwa maendeleo ya sheria za Kimataifa nchini na Barani Afrika. Aliiomba Serikali ya Tanzania kuendelea kumuunga mkono kwenye utekelezaji wa majukumu yake kwa kuzisihi nchi za Afrika zijiunge na AALCO.
Mhe. Waziri akiendelea na mazungumzo yake ambapo alitoa pongezi kwa Prof. Gastorn na kumtakia kila la kheri kwenye utekelezaji wa majukumu yake mapya na kumuahidi ushirikiano wa Serikali ya Tanzania. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Baraka Luvanda (tai nyekundu) na Afisa wa Kitengo hicho, Bw. Abdallah Mtibora.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atembelea watumishi katika ofisi zao

Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wameaswa kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kuongeza ufanisi kwenye maeneo yao ya kazi.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) alipokuwa anatembelea ofisi za watumishi hao jijini Dar es Salaam jana asubuhi.

”Nimekuja kuwatembelea katika maeneo yenu ya kazi ili nijionee mazingira mnayofanyia kazi pamoja na changamoto zinazowakabili ili kwa pamoja tutafute namna ya kuzitatua”. Mhe. Mahiga aliwaeleza watumishi hao kila ofisi aliyopita.

“Lengo la ziara yangu kwenu ni kuwatia morari ili mfanye kazi kwa bidii na kwa ubunifu wa hali ya juu ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017. Kutimia kwa Malengo ya taasisi moja moja kama yetu ndiyo itapelekea kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa awamu ya pili ambayo imejikita katika uwekezaji wa viwanda”.

Alisema watumishi hawana budi kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuwa Serikali yao chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imejipanga kuboresha maslahi yao. Alisema dhamira hiyo imedhihirishwa na kitendo cha Rais Magufuli kupunguza kodi ya mapato (payee) kutoka asilimia 11 hadi 09.

Aliwataka watumishi kuepuka vitendo vya ubadhirifu badala yake kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni za utumishi na kuonya kuwa, Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayebainika kwenda kinyume na maadili ya utumishi.

Waziri Mahiga aliendelea kuwaeleza watumishi wake kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ambayo inajukumu la kuratibu Sera ya Mambo ya Nje ya Nchi ina mchango mkubwa wa kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na jina zuri na kubwa ulimwenguni kote ili sifa hiyo itumike vizuri kuvutia uwekezaji wa viwanda nchini.

“Alisema kwa nafasi zenu nyie watumishi mlio hapa Makao Makuu na wale wa Balozini lazima  mshirikiane kwa pamoja kwa kutumia taaluma zenu na vipaji alivyowapa Mwenyezi Mungu kuzitangaza rasilimali za Tanzania ulimwenguni kote, kwa madhumuni ya kuvutia uwekezaji na utalii ili kuongeza mapato ya Serikali na ajira kwa Watanzania”.

Alihitimisha nasaha zake kwa kuwakumbusha watumishi kaulimbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya  “Hapa kazi tu” Alisema kauli hiyo lazima itafsiriwe kivitendo kwa kila mtumishi bila kusahau kuweka mbele uzalendo na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu.



Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 23 Juni 2016.





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI




Rais Kagame kufungua Maonesho ya 40 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba)

Mhe. Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Rwanda anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini tarehe 01 Julai 2016 kufuatia mwaliko kutoka kwa Mhe. Dkt, John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiwa nchini Mheshimiwa Rais Kagame atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli na baadaye kwa pamoja viongozi hao watashuhudia uwekaji saini wa Makubaliano ya Pamoja (MoUs) baina ya Tanzania na Rwanda katika sekta mbalimbali za ushirikiano. 

Aidha, Mheshimiwa Kagame atashiriki dhifa rasmi ya kitaifa itakayoandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Magufuli .

Mchana wa tarehe 1 Julai, 2016 Mheshimiwa Rais Kagame akiambatana na mwenyeji wake atahudhuria maonesho ya 40 ya Kimataifa ya Biashara  (Sabasaba)  kama Mgeni Rasmi kwa ajili ya kuyafungua

Ziara hiyo ya Mheshimiwa Kagame inafuatia ziara yenye mafanikio aliyofanya Mhe. Dkt. John Pombe Jospeh Magufuli nchini Rwanda mwezi Aprili 2016. Ziara hiyo ni ishara nyingine ya kuimarika kwa mahusiano baina ya nchi hizi  mbili.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 23 Juni 2016.


Ubalozi wa Kuwait watoa msaada wa madawati 300

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye Hafla ya kukabidhi Madawati 300 kutoka Ubalozi wa Kuwait hapa nchini. Balozi Jasem Al Najem ndio aliyokabidhi msaada huo wa madawati.
 Juu na Chini ni sehemu ya Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakimsikiliza kwa Makini Waziri Mahiga alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani)

Balozi wa Kuwait nchini, Jasem Al Najem akizungumza katika hafla hiyo.
Sehemu nyingine ya Wakuu Idara na Vitengo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Balozi Najem akiendelea kuzungumza
Waziri Mahiga (kulia), Balozi Najem na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Abdallah Kilima, kwa pamoja wakiwa wamekaa kwenye madawati yaliyotolewa na Ubalozi wa Kuwait hapa nchini.
Waziri Mahiga na Balozi Najem wakiwa katika picha ya pamoja na wakuu wa Idara na Vitego mara baada ya kumaliza mkutano na waandishi wa habari

 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga ameupongeza Ubalozi wa Kuwait kwa kuwa wa  kwanza kuitikia maombi yake ya kuchangia madawati kwa ajili ya shule za msingi na sekondari hapa nchini. 

Pongezi hizo alizitoa jana wakati wa hafla ya kupokea madawati 300 ambayo Ubalozi huo uliahidi kuipa Serikali. Hafla ilifanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Tumeanza kupokea madawati kutoka kwa rafiki zetu, huu ni mwanzo tu, na wengine watafuatia na taarifa ya kila dawati litakalokuwa linapatikana nitaiwasilisha kwa Mhe. Waziri Mkuu. Dkt. Mahiga alieleza.

Mhe. Waziri aliwaambia wahudhuriaji wa hafla hiyo kuwa katika utekelezaji wa malengo ya milennia, Tanzania ilifanya vizuri katika baadhi ya maeneo hususan, elimu na afya ya mama na mtoto. Licha ya idadi ya watoto kuandikishwa mashuleni iliongezeka, bado kulikuwa na changamoto ya kuboresha ubora wa elimu na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia kama vile vitabu na majengo ya maabara na vifaa vyake.

Aliendelea kueleza kuwa baada ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kutangaza elimu bure, udahili mashuleni umeongezeka maradufu na hivyo kusababisha changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba mkubwa wa madawati. 

“Kufuatia hali hiyo, Serikali imejipanga kutumia mbinu mbalimbali kutatua changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuwaomba marafiki zetu watusaidie. Hivyo, Kuwait imejitokeza kutusaidia na imeahidi kusaidia sio madawati tu bali, hata maeneo mengine yenye changamoto kwenye elimu”.

Kwa upande wake, Balozi wa Kuwait,  Mhe. Jasem Al Najem alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya jitihada za Serikali yake kuunga mkono mkakati wa Rais Magufuli wa kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari.  

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 23 Juni 2016.