Friday, October 7, 2016

Rais Dkt. Magufuli akutana na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania Nje ya nchi Ikulu Dar es Saalam


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Eng. John Kijazi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt Hamisi Kigwangwalla katika picha ya kumbukumbu   na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi alipokutana nao Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 7, 2016.

Thursday, October 6, 2016

Naibu Waziri akutana na Naibu Waziri wa Jamhuri ya Czech

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (kulia) akimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe.Ivan Jancarek wakati wa mazungumzo waliyoyafanya Wizarani Jijini Dar es Salaam. Katika mazungumzo yao walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, elimu na utalii.
Naibu Waziri Mhe. Dkt. Susan Kolimba akifafanua jambo kwa  Mhe.Jancarek
Wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe waliofuatana na Mhe. Jancarek.

Wednesday, October 5, 2016

Rais wa Congo ahitimisha ziara yake nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mhe. Joseph Kabila (aneyepunga mkono) alipomsindikiza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tayari kwa kuondoka kurejea nchini kwake baada ya kumaliza ziara yake ya siku tatu nchini
Mhe. Kabila akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga katika hafla ya kumwaga baada ya kuhitimisha ziara yake nchini.
Mhe. Rais Kabila akimwaga  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan huku Mhe. Rais Magufuli akishuhudia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akiagana rasmi  na Rais Kabila wakati akielekea kupanda ndege kurejea nchini Congo baada ya kuhitimisha ziara yake nchini


Taarifa ya ufafanuzi kuhusu habari za Watanzania kuteswa katika nchi za Mashariki ya Kati

Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya kati wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijiji Dar es Salaam tarehe 05 Oktoba, 2016.
Katika Mkutano huo Balozi Kilima alitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu taarifa za mateso wanayofanyiwa Watanzania wanaofanya kazi nchini Oman na nchi nyingine za Mashariki ya Kati. Taarifa hizo husambazwa katika mitandao ya jamii pamoja na vyombo vingine vya habari likiwemo gazeti la Tanzania Mpya la tarehe 04 Oktoba, 2016 Toleo Na. 23.

Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia Mkutano, kutoka kulia ni Bw. Hangi Mgaka, Bw. Odilo Fidelis na Bw. Fred Maro.
Mkutano ukiendelea


=======================================================



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU TAARIFA ZA KUTESWA KWA WATANZANIA WANAOKWENDA KUFANYA KAZI OMAN NA NCHI NYINGINE ZA MASHARIKI YA KATI

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inachukua fursa hii leo kupeleka taarifa kwa Umma kupitia vyombo vya habari juu ya habari zilizochapishwa katika gazeti moja kuhusu mateso wanayopata Watanzania wanaofanya kazi za ndani nchini Oman ili  kuondoa utata uliojitokeza kutokana na habari hiyo. Aidha, Wizara inapenda kutoa uelewa na  ufafanuzi ili kupata ushirikiano kutoka kwa wananchi katika kukabiliana na changamoto wanazopata Watanzania nje ya nchi wakitafuta maslahi ya kiuchumi.

Ndugu Wanahabari,

Jana siku ya Jumanne tarehe 4 Oktoba 2016, Gazeti la Tanzania Mpya katika toleo lake Na.23 katika ukurasa wake wa mbele lilichapisha habari yenye kichwa cha maneno watanzania wateswa nchini Oman na kuwa wengine hunyofolewa figo zao na kupewa ndugu wa waajiri wenye mahitaji. Habari hii ambayo imeendelea ukurasa wa pili na watano imeambatana na picha ya Mheshimiwa Dr. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na hivyo kuwafanya wasomaji wengi kuamini kuwa taarifa ile imetolewa na Mheshimiwa Waziri.

Kitendo hiki cha kuchapisha habari hii na kutumia picha ya Mheshimiwa Waziri kimeleta usumbufu kwa mheshimiwa Waziri na pia kwa wasomaji kwani wengi wameamini kuwa taarifa ile imetolewa na Mhe. Waziri.

Wizara inapenda kuutangazia umma kwa ujumla kwamba Mheshimiwa Dr. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  hausiki na taarifa hiyo na wala hakuwahi kuzungumza na mwandishi wa habari wa makala husika na kuwa yaliyomo kwenye taarifa hiyo ni maoni binafsi ya mwandishi na gazeti husika na kwa vyovyote vile hayawakilishi msimamo wa Mheshimiwa Waziri na Wizara anayoiongoza na serikali kwa ujumla.

Habari hii ni mfululizo wa uchapishaji wa habari zenye maudhui kama haya kwenye baadhi ya magazeti na mitandao ya kijamii ambazo hazijafanyiwa utafiti wa kina na kuwa na taarifa sahihi kuhusu mada husika. Taarifa hizi zinaweza kuharibu uhusiano mzuri na wa kindugu uliopo baina ya Tanzania na Oman kati ya serikali na serikali na pia watu wake ambao wengi wana uhusiano wa damu


Ndugu Wanahabari,

Baada ya kusema hayo sasa naomba kutoa taarifa ya kina kuhusu suala zima la watanzania wanaokwenda kufanya kazi nchini Oman na nchi nyingine za mashariki ya kati na utaratibu ambao serikali imeweka katika kuratibu zoezi zima

Eneo la mashariki ya kati linaundwa na nchi za Oman , Saudi Arabia, Qatar, Bahrain, Kuwait, Umoja wa Falme za Kiarabu ( Abu Dhabi, Dubai, Ajman, Al Ain, Fujairah, Ras Al Khaimah na Sharjah), Lebanon, Syria, Iran, Iraq, Yemen.

Nchi hizi kwa kiasi kikubwa ni tegemezi ya nguvu kazi kutoka nje ya eneo hili na hivyo kuwa soko kubwa la ajira kwa nchi mbalimbali, ajira hizi ni kuanzia watendaji wakuu, watendaji wa ngazi mbalimbali hadi wahudumu na watumishi wa majumbani
Kati ya nchi za mashariki ya kati Oman imekuwa na uhusiano wa karibu sana ambao ni wa kihistoria na kidamu, ambapo nusu ya familia za Oman asili yake ni Tanzania na hivyo kufanya kuwa na muingiliano wa karibu.

Kwa kuzingatia uhusiano huu Oman imekuwa ikipokea wafanyakazi mbalimbali kutoka Tanzania katika kada za madaktari, walimu, wauguzi, wahadhiri, wapishi, wahudumu katika masaluni ( nywele na kuchora Heena), madereva, wahudumu wa mashamba na bustani na watumishi wa nyumbani.
Kuanzia miaka ya 2010 wimbi la watanzania kwenda kufanya kazi Oman lilishika kasi na hivyo kuongeza idadi ya watanzania wanaoingia Oman kwa ajili ya kufanyakazi mbalimbali hasa majumbani ( Housemaids) , kufuatia wimbi hili ubalozi ulianza kupokea watanzania wanaolalamikia mazingira magumu ya kufanyia kazi, malalamiko yao yalihusu kufanya kazi masaa mengi, mshahara mdogo, kukosa mapumziko, kutoruhusiwa kutoka nje ya nyumba, kufanya kazi zaidi ya nyumba moja , kunyanyaswa kijinsia , kufanyishwa kazi ziadi ya kazi za Housemaid.

Katika mazungumzo na watumishi husika, ubalozi ulibaini kutokuwepo kwa utaratibu maalum wa kuratibu ajira zao kuja Oman, hivyo basi Ubalozi kwa kushirikiana na wadau wengine hapa Tanzania ( Uhamiaji, Wizara ya Kazi, Wakala wa huduma za ajira Tanzania (TAESA) , Kamisheni ya kazi Zanzibar, Mamlaka ya viwanja vya ndege, Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa) vilianza utekelezaji wa utaratibu wa kufuatwa kwa wale wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi na hasa Oman.

Ndugu wanahabari

Chini ya utaratibu huu, Raia wa Oman mwenye nia ya kumwajiri mtanazania anapaswa kwenda Ubalozini na kujaza fomu ya kuomba kumwajiri mtanzania, baada ya fomu yake kuridhiwa na Ubalozi atapewa mkataba ambao atajaza na kuurudisha Ubalozi akiambatanisha nakala ya kitambulisho chake cha taifa, Uthibitisho wa makazi ( bili ya maji au umeme), nakala ya pasipoti ya mfanya kazi, hati ya kiapo na dhamana ya rial 100 .
Baada ya Ubalozi kuridhika na vielelezo vyake, ubalozi utapitisha mkataba na kumtaka mwajiri husika kuuwasilisha Tanzania kwa mtumishi husika ambae ataupokea na kuuwasilisha TAESA au kamisheni ya kazi ambao nao watamuhoji muhusika na kujiridhisha kuwa anaulewa wa kazi anayokwenda kufanya pamoja na masharti yake, wakijiridhisha watampa kibali ambacho ni barua ikimuomba kamishna wa uhamiaji amruhusu muhusika kusafiri nje ya nchi baada ya kutimiza utaratibu uliowekwa.

Ndugu wanahabari

Utekelezaji wa utaratibu huu umekuwa na mafanikio na pia changamoto, kwa kiasi kikubwa uratibu huu umeweza kupunguza matatizo waliyokuwa wanayapata ndugu zetu, kuongeza mshahara wao, kuwapatia haki ya kupumzika na mawasiliano na pia kuongeza uelewa wa watanzania juu ya haki zao na namna ya kuzipata pale zinapokiukwa.

Kufuatia kufanikiwa kwa utekelezaji wa utaratibu huu nchini Oman, serikali sasa imeanza kutumia utaratibu huu katika nchi yingine za mashariki ya kati

Pamoja na mafanikio kumekuwa na changamoto kama vile baadhi ya watu kukwepa kufuata utaratibu husika kwa kuwapitisha wahusika njia za panya, kughushi nyaraka husika, kuwepo kwa mawakala bubu na kuwa na tamaa ya kufanikiwa haraka, watanzania kutokuwa na ujuzi au uzoefu wa kazi wanayokwenda kuifanya, kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa maadili kama vile wizi, udanganyifu nk

Ndugu wanahabari

Ndugu wana habari, naomba nitumie nafasi hii pia kutoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya kunyang’anywa hati za kusafiria, huu ni utaratibu unaofuatwa na waajiri katika nchi zote za mashariki ya kati ambapo katika kipindi chote cha mkataba hati ya kusafiria huwekwa chini ya uangalizi wa mwajiri, utaratibu hufanyika kwa waajiri wa aina zote kwa maana ya taasisi ( Wizara, Idara, mashirika binafsi ) na watu binafsi, hivyo tunaomba ieleweke kuwa ni suala la utaratibu

Ndugu wanahabari

Katika kupambana na changamoto hizi serikali imejipanga kuimarisha udhibiti wa utekelezaji wa utaratibu huu kupitia vikao mbalimbali vya wadau. Vikao hivyo viliazimia Kuandaa mtaala wa kuongeza stadi na ujuzi kwa wanaokusudia kufanya kazi za Housemaid  

   Kuanza kutumia mawakala rasmi wa ajira walioandikishwa na mamlaka husika

   Kuwepo mkataba wa ajira unaotambuliwa na Mamlaka za Nchi unayotaka kwenda. Kwa hapa nyumbani mamlaka zinazoweza kusaidia ni pamoja na Ofisi za Ubalozi za Nchi husika, Wakala wa Ajira Tanzania - TAESA (Tanzania Bara) au Kamisheni ya Kazi (Zanzibar);  Mtanzania asikubali kuanza safari bila kupata mkataba na Kibali kutoka TAESA au Kamisheni ya Kazi.
kila Ubalozi  katika nchi za Mashariki ya Kati uandae   mikataba ya kazi kutokana na muongozo uliokubaliwa na wadau wote.

Vilevile, kupitia kwenu wanahabari, tunatoa wito kwa watanzania wote, tuwe makini pale tunapopata fursa za kazi nje ya nchi.  Kama nilivyosema hapo awali, ni muhimu kujiridhisha kwamba mambo yote ya msingi yanayohusiana na ajira hizo yamekaa sawa ikiwa ni pamoja na:

  
      Kuzingatia na kufuata utaratibu uliowekwa na serikali, na wala mtanzania asikubali kuambiwa kuwa mktaba  ataukuta huko anakokwenda au kusafiri kupitia nchi jirani kwenda kuanza kazi nje ya nchi,

  wito kwa Taasisi zote zinazoratibu safari za Nje katika viwanja vya ndege au vituo vya mipakani kuhakikisha hawamruhusu mtu kusafiri nje kwa nia ya kufanya kazi bila kuwa na vibali husika.
      Kutafuta msaada wa kupata uthibitisho kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki au Wizara ya Kazi kama kweli kazi uliyoahidiwa ipo- Wizara yetu itaweza kutumia Balozi zetu kuthibitisha;
      Na pale unapokwenda Nje, ni muhimu kuhakikisha kwamba unajisajili kweye ofisi za Ubalozi wa Tanzania uliopo katika nchi hizo au ubalozi wa Uingereza mahali ambapo hakuna Ubalozi wa Tanzania.
       Kutokubali kuweka hati yako ya kusaifiria kama rehani kwasababu yoyote ile;

Katika kupata suluhisho la kudumu ikiwa ni pamoja na kuwasaidia Watanzania kupata fursa za ajira nje ya nchi, Wizara kwa kushirikiana na wadau husika inaendelea na jitihada za kusaini Mikataba ya Ushirikiano katika Sekta ya Ajira na Kazi baina ya Serikali ya Tanzania na nchi hizo kama ule wa Tanzania na Qatar. Kusainiwa kwa mikataba hiyo sio tu kutasaidia kupata fursa za ajira katika nchi hizo bali kutailazimu Serikali ya nchi hizo kushirikiana na Wizara pindi raia wao watapokwenda kinyume na mikataba ya ajira iliyopo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 05 Oktoba 2016.