Thursday, December 8, 2016

Afrika ijifunze kutoka Korea, Mawaziri





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Afrika ijifunze kutoka Korea, Mawaziri.


Nchi za Afrika zimehimizana kutumia sera , mbinu na mfumo wa maendeleo uliotumiwa na Jamhuri ya Korea kufanya mapinduzi makubwa ya uchumi, viwanda na teknolojia katika kipindi cha miongo michache iliyopita.

Hayo yamejiri kwenye Mkutano wa  Mawaziri wa  nchi za Afrika na Korea uliohitimishwa leo jijini Addis Ababa, Ethiopia.

"Katika miaka ya 1960 hali ya uchumi na mazingira ya Korea yalikuwa yanalingana na bara la Afrika, hivyo, mfumo ulioifanya Korea kufanya mapinduzi ya uchumi unafaa kutumiwa na bara la Afrika kwa kuwa mazingira yetu yanafanana".

Katika mkutano huo ambaoTanzania iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga, Mawaziri walielezea kuridhishwa na ushirikiano huo tokea ulipoanzishwa mwaka 2006, kwa kuwa unazingatia maslahi ya pande zote na haufungamani na masharti ya aina yoyote.

Walisema kuwa Bara la Afrika lina fursa lukuki zikiwemo maliasiri kama madini, mafuta na ardhi nzuri kwa kilimo.

 Rasilimali hizo miaka yote zimekuwa zikiuzwa nje bila kuendelezwa kutokana na ukosefu wa viwanda na teknolojia, hali iliyochangia  kwa kiasi kikubwa kulifanya bara hilo kubaki nyuma kimaendeleo.
Hivyo, kupitia jukwaa hilo la ushirikiano na Korea, bara la Afrika litapokea misaada ya fedha za maendeleo na teknolojia  itakayotumiwa kujenga viwanda vya kusindika rasilimali ili kuziongezea thamani.

Kwa kuwa maendeleo na amani na usalama ni vitu vinavyotegemeana, Mawaziri walisisitiza umuhimu wa kutunza amani barani Afrika kwa kushirikiana na Korea.

 Walibainisha masuala mbalimbali yanayotishia amani ya  dunia likiwemo tatizo la ugaidi wa kimataifa. Walikubaliana kuwa ugaidi ni changamoto ya ulimwengu mzima na ili ufumbuzi wake upatikane lazima wadau duniani kote washirikiane.

Ushirikiano wa nchi za Afrika na Korea unatimiza miaka 10 mwaka huu tokea ulipoanzishwa mwaka 2006. Kwa muktadha huo, ulisisitizwa umuhimu wa kufanya tathmini na ufuatiliaji wa miradi ya utekelezaji ili kubaini mafanikio mapungufu na changamoto.  Hiyo itasaidia kuchukua hatua stahiki katika kufikia malengo yaliyowekwa na umoja huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea, Mhe. Yun Byung-se alieleza mafanikio ya ushirikiano huo tokea kunzishwa kwake. Alisema katika eneo la ushirikiano wa kiuchumi na Afrika, Korea ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa tano wa Mawaziri wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Korea na Afrika mwezi Oktoba 2016.

 Katika mkutano huo, Korea iliahidi kutoa Dola za Marekani bilioni 5 kwa ajili ya kusaidia masuala ya kiuchumi barani Afrika. Fedha hizo zinatarajiwa kuongezeka  mara dufu katika kipindi kijacho. Aidha, Korea inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la ushirikiano wa viwanda kati ya Korea na Afrika katika wiki mbili zijazo.

Vile vile, Korea imeongeza mara dufu misaada ya maendeleo kwa bara la Afrika na ile misaada ya maendeleo inayohusisha nchi mbili (bilateral)  itaongezeka kutoka asilimia 24 hadi kufikia asilimia 35 itakapofika mwaka 2020.

Waheshimiwa Mawaziri walihitimisha mkutano wao kwa kuridhia nyaraka mbili ambazo ni Tamko la Addis Ababa na Mwongozo wa Ushirikiano kati ya Korea na Afrika. Mwongozo huo umeainisha miradi mbali mbali itakayotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano 2017 - 2021. Maeneo hayo ni pamoja na: biashara, kuendeleza viwanda na uwekezaji; uzalishaji katika kilimo na kiwango cha mavuno; uchumi wa bahari, uendeshaji wa bandari na usafiri wa majini; kuwaendeleza vijana na kuwajengea uwezo wanawake.

Wajumbe walikubaliana kuwa mkutano ujao utafanyika Seoul, Korea mwaka 2021.


Imetolewa na: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZASRA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI.
TAREHE 08 DESEMBA 2016

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisoma hotuba ya Tanzania kwenye Mkutano wa Nne wa Ushirikiano wa nchi za Afrika na Jamhuri ya Korea uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 06 na 07 Desemba 2016.
Mhe. Waziri Mahiga akipitia makabrasha ya mkutano. Nyuma ya Mhe. Waziri ni Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na kwenye Umoja wa Afrika, Mhe. Naimi Aziz na Afisa wa Ubalozi huo, Bi Suma Mwakyusa.

Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje nao wakifuatilia mkutano huo. Kutoka kushoto ni Bw. Gerlad Mbwafu, Katibu wa Waziri, Bi. Berther Makilagi, Afisa Dawati la Korea na Bw. Benedict Msuya anayemwakilishsa Mkurugenzi wa Asia na Australasia.

Picha ya pamoja

Wednesday, December 7, 2016

Waziri Mahiga akutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri Mahiga akutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea jijini Addis Ababa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Yun Byung-se ametangaza kuwa Tanzania itapokea msaada mkubwa zaidi wa maendeleo kuliko nchi yeyote barani Afrika inayotolewa na Serikali ya Korea kwa ajili ya bara hilo.
Hayo aliyabainisha leo alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya  Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga kando ya Mkutano wa Ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Korea ulioanza jana  jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Mahiga aliipongeza Korea kwa hatua ya maendeleo iliyofikia ambapo katika kipindi kifupi imeweza kuendelea kiviwanda na teknolojia ili hali wakati nchi za Afrika zinapata uhuru katika miaka ya 60 Korea ilikuwa ni moja ya nchi masikini duniani.

Waziri Mahiga aliishukuru Jamhuri ya Korea kwa misaada inayoipatia Tanzania. Alisema misaada hiyo ni kwa ajili ya watu masikini kwa kuwa inaelekezwa maeneo yanayogusa watu wa chini kama vile afya, maji, elimu na miundombinu ya mawasiliano.

Waziri Mahiga aliweka wazi kuwa Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Korea kwa dhamira ya kujifunza namna nchi hiyo ilivyopiga hatua ya maendeleo ya viwanda na teknolojia ili nayo iweze kufikia azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

"Tunahitaji kushirikiana na Korea katika maeneo ya viwanda, nishati jadilifu, miundombinu, madini, tehama na gesi na mafuta.  Kutokana na  hatua ya maendeleo iliyofikiwa na Korea,  Tanzania ina matumaini makubwa kuwa nchi hiyo itatoa msukumo mkubwa katika kuendeleza maeneo hayo".

Aliongeza kuwa Tanzania inahitaji sio ilimradi viwanda bali viwanda vitakavyotumia malighafi za kilimo na madini ambavyo licha ya kutoa soko kwa wakulima bali pia vitaongeza ajira kwa wananchi.

Aidha, Dkt. Mahiga aliishauri Korea kuangalia namna itakavyoshirikiana na bara zima la Afrika, hususan kusaidia miradi ambayo itakuwa alama ya kudumu ya  ushirikiano kati ya nchi hiyo na bara la Afrika. Alitolea mfano wa mradi wenye sifa hiyo ni Korea kufadhili ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu yenye makao yake jijini Arusha, Tanzania. Mahakama hiyo ni muhimu katika uimarishaji wa utawala wa sheria na demokrasia barani Afrika.

Halikadhalika, Waziri Mahiga alipendekeza Chuo cha Diplomasia cha Tanzania na kile cha Korea vianzishe ushirikiano wa kindugu ili vibadilishane uzoefu na kutatua changamoto zinazovikabili vyuo hivyo kwa pamoja.

Vile vile. Mhe. Waziri alimfahamisha Waziri mwenzake kuwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alishateua Balozi kwa ajili ya kuiwakilisha Tanzania nchini Korea kwenye Ofisi ya Ubalozi itakayofunguliwa hapo baadaye katika mwaka wa fedha 2016/2017.

Kwa upande wake, Mhe. Yun alieleza kuwa Tanzania ni mshirika mkubwa wa Korea na kusisitiza umuhimu wa Serikali kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji ili makampuni ya Korea yaje kwa wingi kuwekeza Tanzania. Alisisitiza umuhimu wa kukamilisha Mkataba wa Kulinda Vitega Uchumi na ule wa Kuepuka Tozo ya Kodi mara mbili kama moja ya njia ya kuvutia wawekezaji kutoka Korea.

Aidha, alikumbusha kuwa  mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Korea yanatimiza miaka 25 mwaka 2017 tokea yalipoanzishwa mwaka 1992, hivyo alihimiza umuhimu wa nchi hizi mbili kuangalia namna zitakavyoadhimisha miaka 25 ya ushirikiano huo.



Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
06 Desemba, 2016.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (kulia) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Yun Byung-se.  Mazungumzo hayo yalifanyika jijini Addis Ababa kando ya Mkutano wa Ushirikiano wa nchi za Afrika na Korea
 
Bw. Benedict Msuya na Bi. Berther Makilagi ambao ni maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje wakinukuu masuala muhimu ya mazungumzo ya Waheshimiwa Mawaziri wa Korea na Tanzania.
Maafisa walioambatana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea nao wakinukuu taarifa za mazungumzo.

Mhe. Mahiga na Mhe. Yun wakishikana mikono ya kuombeana kheri baada ya kukamilisha mazungumzo yao.

Tuesday, December 6, 2016

Afrika na Korea zajadili maendeleo jijini Addis Ababa

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na katika Umoja wa Afrika, Mhe. Naimi Aziz akipitia makabrasha ya Mkutano wa nne wa Ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Jamhuri ya Korea unaofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia. Nyuma ya Mhe. Balozi ni Afisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Bi. Suma Mwakyusa.


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI 


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Afrika na Korea zajadili maendeleo jijini Addis Ababa

Mkutano wa nne wa siku mbili wa Ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Jamhuri ya Korea kwa ngazi ya Mawaziri ambao kwa mara ya kwanza unafanyika barani Afrika umeanza leo jijini Addis Ababa, Ethiopia kwa kikao cha Maafisa Waandamizi. Katika kikao hicho ambapo Tanzania inawakilishwa na Balozi wake nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz ni kwa ajili ya kuandaa mkutano wa Mawaziri utakaofanyika kesho tarehe 07 Desemba 2016, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga tayari alishawasili Ethiopia kuiwakilisha Tanzania.

Maafisa Waandamizi pamoja na mambo mengine, walipata fursa ya kupokea taarifa mbalimbali ikiwemo kupitia Azimio la Addis Ababa litakaloidhinishwa na Mkutano wa Mawaziri pamoja na utekelezaji wa mpango kazi (Kati Ya mwaka 2013-2015) katika maeneo yaliyoafikiwa katika Mkutano wa tatu wa Korea-Afrika uliofanyika mwaka 2012, Seoul, Jamhuri ya Korea. Mkutano wa kwanza na wa pili ilifanyika mwaka 2006 Na 2009, Seoul, Korea.

Maeneo ambayo Nchi za Afrika zilikubaliana kushirikiana na Korea ni pamoja na maendeleo endelevu, elimu, afya, kilimo, mabadiliko ya tabianchi, biashara, uwekezaji na uchumi, amanina usalama na masuala ya mtambuka kama vile masuala ya jinsia, wanawake na watoto, masuala Ya TEHAMA n.k.

Wajumbe walielezwa kuwa katika maeneo yote hayo Korea ilitekeleza wajibu wake ipasavyo kwa kuongeza fedha takriban katika kila eneo kuanzia mwaka 2012 hadi 2015.

Kwa upande wa kilimo Korea imekuwa ikishirikiana na nchi za Afrika kwenye ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji na masuala mengine ya kiufundi ambapo kiasi cha msaada katika eneo hilo kimeongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 16 mwaka 2012 na kufikia Dola bilioni 40 mwaka 2015. Kwa upande wa Tanzania; Zanzibar imefaidika na fedha hizo ambapo imepokea Dola milioni 50 kwa ajili ya uendelezaji wa kilimo cha mwani.

Eneo lingine ambalo Korea iliwekeza fedha za kutosha ni lile la afya ambapo kiasi kilichotolewa kimefikia Dola milioni 27 mwaka 2015 ukilinganisha na kiasi cha Dola milioni 16 kilichotolewa mwaka 2012. Jiji la Dar es Salaam limefaidika na fedha hizo kwa kujengewa hospitali ya uchunguzi ya afya ya mama kwenye eneo la Chanika wilayani Ilala ambayo inatarajiwa kukamilika mwaka 2017.

Aidha, kwa kutambua umuhimu wa amani na usalama katika maendeleo ya Bara la Afrika, Korea imekuwa ikifadhili programu mbalimbali ndani ya Umoja wa Afrika zinazolenga kutatua migogoro na kuleta amani ya kudumu barani humo. 

Katika kikao hicho wajumbe walisisitiza umuhimu wa kufikia malengo yaliyowekwa na ushirikiano huo kwa kutekeleza kikamilifu miradi ya maendeleo iliyoainishwa na Umoja wa Afrika ili kuweza kupiga hatua za kiuchumi kwa faida ya Afrika kwa ujumla.

Mkutano huo unatarajiwa kukamilika kwa kutolewa Tamko ambalo pamoja na mambo mengine litainisha maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Korea na nchi za Afrika kwa kipindi cha miaka mitano ijayo 2017 - 2021.

Imetolewa na: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI.

06 DESEMBA, 2016

Friday, December 2, 2016

Waziri Mahiga ashiriki maadhimisho ya siku ya Kitaifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini Mhe.Abdulla Ibrahim Ghanim Alsuwaidi alipowasili katika ofisi za ubalozi huo kushiriki sherehe ya madhimisho ya miaka 45 ya muungano.Tanzania na UAE zimepiga hatua kubwa za ushirikiano hususan ya kiuchumi ambapo kwa takwimu za Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) hadi Juni, 2015 makampuni 67 ya uwekezaji kutoka UAE yamewekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali wenye thamani ya USD 497.12 Millioni na kuajiri Watanzania 9,044. Taifa la Umoja wa Falme za Kiarabu unaundwa na falme saba ambazo ni Abu Dhabi, Dubai, Sharjah, Ras Al Khaimah, Fujairah, Ajman na Umm al-Quwain
                                           
Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Taifa la Umoja wa Falme za Kiarabu Mhe.Abdulla Ibrahim Ghanim Alsuwaidi wakati wa sherehe ya maadhimisho ya miaka 45 ya muungano wa falme hizo

Mhe.Waziri Balozi Dkt.Mahiga akivalishwa skafu maalum

Mhe.Waziri Balozi Dkt. Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mhe.Abdulla Ibrahim Ghanim Alsuwaidi


Wageni waalikwa wakifuatilia jambo

Balozi wa Taifa la Umoja wa Falme za Kiarabu Mhe.Abdulla Ibrahim Ghanim Alsuwaidi akizungumza wakati wa maadhimisho 

Mhe. Waziri Balozi Dkt. Mahiga akitoa hutuba fupi wakati wa maadhimisho ya sherehe hizo


Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati Balozi Abdalla Kilima akisalimiana na Mhe. Balozi wakati wa sherehe za maadhimisho
         ------------------------------------------------------------------------------------------------------                                                                  

Tanzania na Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE) zimepiga hatua kubwa za ushirikiano hususan wa kiuchumi ambapo kwa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) hadi Juni, 2015 Makampuni 67 kutoka UAE yamewekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali kwa mtaji wa thamani ya Dola za Marekani  milioni  497.12  na kuajiri Watanzania zaidi ya 9,044. 
 
Hayo yalibainishwa jana katika sherehe za kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya UAE zilizofanyika jijini Dar Es Salaam ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga alikuwa Mgeni Rasmi. 

Tanzania na UAE  zinatarajiwa kufanya Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) ambao utakuwa chachu ya kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizi mbili hususan ya kiuchumi. 

Akiongea katika hafla hiyo, Mhe. Waziri alilipongeza taifa hilo kwa kuadhimisha siku yake ya Kitaifa ikiwa imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo ya kichumi, kijamii na kisiasa. Mhe.  Waziri alisema kuwa siku hiyo ni inatoa fursa pia ya kutathmini mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na UAE.

Kwa upande wake, Balozi wa UAE hapa nchini, Mhe. Abdulla Ibrahim Ghanim Alsuwaidi aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa inayotoa kwa Ubalozi huo ambao unamwezesha kutekeleza majukumu yake kwa wepesi ikiwa ni pamoja na kuimarisha mahusiano ya nchi hizi mbili. Mhe. Balozi aliahidi kuendeleza ushirikiano huo hususan katika kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda. 

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) unajumusha falme saba ambazo ni Abu Dhabi, Dubai, Sharjah, Ras Al Khaimah, Fujairah, Ajman na Umm al-Quwain huadhimisha siku yake ya Kitaifa tarehe 02 Disemba ya kila mwaka tokea mwaka 1971.