Wednesday, May 29, 2019
Tuesday, May 28, 2019
Dkt. Ndumbaro aeleza mikakati ya Tanzania katika kunufaika na Programu ya ACP
Waandishi wa habari wakimsikiliza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb). |
TAARIFA
KUHUSU USHIRIKI WA TANZANIA KWENYE MKUTANO WA 109 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA NCHI
ZA AFRIKA, KARIBBEAN, NA PASIFIKI (ACP) NA MKUTANO WA 44 WA PAMOJA WA BARAZA LA
MAWAZIRI WA ACP NA UMOJA WA ULAYA, TAREHE 20 - 24 MEI 2019 BRUSSELS, UBELGIJI
Ndugu Waandishi wa
Habari,
1. Nilipata heshima
ya kuongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa 109 wa
Baraza la Mawaziri wa nchi za Afrika, Karibiani, na Pasifiki (ACP) uliofanyika
Brussels, Ubelgiji kuanzia tarahe 20 hadi 22 Mei 2019. Mkutano huu, ulifuatiwa
na Mkutano wa 44 wa pamoja wa Mawaziri wa nchi za ACP na wenzetu wa Umoja wa
Ulaya (EU) ambao ulifanyika mnamo tarehe 23 na 24 Mei 2019.
2. Katika mkutano
huu, upande wa Tanzania niliongozana na Watendaji Waandamizi kutoka Wizara ya
Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha na Mipango, na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Pia, Watalaam kutoka Ofisi ya Ubalozi wetu wa
Tanzania Brussels, walishiriki mikutano hii.
3. Aidha, katika
mikutano yote miwili, majadiliano yetu yalijikita katika maeneo makuu matatu.
Mosi, ni kupitia na kutathimini utekelezaji wa makubaliano na mipango mbalimbali
tuliyonayo ndani ya nchi za ACP na baina ya nchi za ACP na EU. Pili, kuainisha,
kujadili, na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika
ushirikiano ndani ya nchi za ACP na baina ya nchi za ACP na EU. Tatu, kutoa
muongozo juu ya mustakabali wa ushirikiano tunaotarajia uwepo ndani ya nchi za
ACP na baina ya nchi za ACP na EU katika kipindi kijacho.
4. Kwa upande wa agenda ya kwanza, tulipitia
utekelezaji wa makubaliano ya programu mbalimbali ndani ya nchi za ACP na baina
ya nchi za ACP na EU. Programu hizo ni pamoja na zile zinazohusu masuala ya
ubia wa kimaendeleo, biashara, masoko, kilimo, elimu, maendeleo ya sekta
binafsi, teknolojia, mifumo ya kodi, uhifadhi wa mazingira, hifadhi ya bahari,
na masuala mengine yanayofanana na hayo. Kwa ujumla tulikubaliana kuwa programu
hizi ni muhimu katika kuchochea kasi ya maendeleo ya nchi zetu na zikaendelea
kutekelezwa kwa kasi inayostahili, mgawanyo ulio sawa na kwa kuzingatia
mahitaji ya nchi husika.
5. Kwa mfano, katika
eneo la kilimo, Tanzania ilitoa hoja ambayo baada ya majadiliano ya kina
ilikubalika kuongeza mazao ya korosho, pamba, na kahawa katika orodha ya mazao
yaliyopo katika mpango wa mwaka 2019 wa utekelezaji wa programu ya ACP ya
kuendeleza mnyororo wa thamani katika mazao ya kilimo. Mpango huu unafadhiliwa
na EU na umetengewa kiasi cha Euro milioni 125. Katika zao la korosho, nchi
wanachama wa ACP iliisifu na kuipongeza Tanzania kwa uamuzi wa kishujaa
uliochukuliwa na Serikali chini ya uongozi thabiti wa Mhe. Rais Magufuli kwa kuzuia
mwendelezo wa mdororo wa bei ya korosho na hatua za makusudi zinazoendelea
katika kuongeza mnyororo wa thamani wa zao hilo.
6. Katika kuimarisha
sekta binafsi, ujumbe wa Tanzania uliuomba Umoja wa Ulaya kupitia mkakati wa
kusaidia sekta binafsi (ACP Private Sector Development Strategy), kuangalia
uwezekano wa kuja na mfumo rafiki kwa nchi za ACP, na Tanzania ikiwemo, ambao
utawezesha sekta binafsi ya nchi hizo kunufaika. Katika mkutadha huo, ujumbe wa
Tanzania uliiomba Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB),
inayosimamia mpango huo, kuanza majadiliano na serikali na kukubaliana namna ya
kusaidia sekta binafsi katika utoaji wa mikopo nafuu ya maendeleo (development
finance) kwa ajili ya kuchochea uzalishaji na 3 kuongeza thamani ya mazao ya
kilimo. Umoja wa Ulaya kupitia mpango wake wa kuwezesha ufanikishaji wa
utekelezaji miradi ya kibiashara na sekta binafsi imetenga kiasi cha Euro
bilioni 1.1 kwa kipindi cha mwaka 2014 hadi 2020.
7. Wakati wa mkutano
huu, ujumbe wa Tanzania ulieleza kwa kina hatua mbalimbali zinazochukuliwa na
Serikali ya awamu ya tano katika kujenga uchumi wa viwanda kwa lengo la kufikia
uchumi wa kati. Miongoni mwa hatua tulizozieleza ni pamoja na utekelezaji wa
miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), mradi wa
uzalishaji wa umeme wa mto Rufiji, ununuzi wa ndege na kufufuliwa kwa ATCL,
ujenzi wa barabara, kupanuliwa kwa bandari, viwanja vya ndege na miradi
mingine. Tulitumia nafasi hiyo kuzihakikishia nchi za ACP na Umoja wa Ulaya juu
ya uwepo wa mazingira rafiki ya uwekezaji na biashara nchini Tanzania na
kuwajulisha kuwa Serikali kupitia mwongozo wa BLUEPRINT inatekeleza mikakati ya
kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji na biashara. Hatimaye, tuliwaomba wadau
wetu wa maendeleo ndani ya ACP na Umoja wa Ulaya kuunga mkono juhudi hizi
madhubuti za Serikali na kuhimiza raia wa nchi zao kuja kuwekeza nchini.
8. Katika agenda ya
kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika ushirikiano wetu,
tulibainisha na kujadiliana na wenzetu wa Umoja wa Ulaya juu ya changamoto hizo
na umuhimu wa kupata ufumbuzi wake. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na
kasi ndogo ya utekelezaji wa baadhi ya programu za maendeleo, kiwango kidogo
cha biashara baina ya nchi za ACP, kuendelea kuibuka kwa vikwazo vipya vya
biashara visivyo vya kiforodha kwa bidhaa za ACP katika soko la Ulaya,
sintofahamu inayoendelea baina ya nchi za ACP na Umoja wa Ulaya katika
kusainiwa na kutekelezwa kwa Mikataba ya Ubia wa Kiuchumi (Economic Partnership
Agreements – EPAs), na kuwepo kwa vikwazo kwa baadhi ya nchi wanachamaa wa ACP
na kuwepo kwa maamuzi 4 yasiyozingatia misingi ya uhuru wa nchi (sovereignty),
usawa (equal partnership), na kuheshimiana. Nchi za ACP, ikiwemo Tanzania,
zilisisitiza changamoto hizi zipatiwe ufumbuzi haraka kwa kila upande
unaohusika na tulikubaliana kuwa katika ushirikiano wetu ni muhimu kila upande
ukaheshimu kanuni za ushirikiano, sheria na tamaduni za nchi husika. Kwenye
hili, Tanzania ikiungwa mkono na nchi nyingine za ACP haja na umuhimu wa kuzingatia
na kuheshimu matakwa ya Ibara ya 12 ya mkataba wa ubia wa sasa unaojulikana kama
Cotonou Partnership Agreement. Ibara hiyo inazuia upande wowote kuchukua uamuzi
wenye madhara kwa upande mwingine bila kuingia kwenye mashauriano ya kina na
upande huo.
9. Katika majadiliano
yetu, juu ya mstakabali wa ubia mpya baina ya nchi za ACP na Umoja wa Ulaya
baada ya ubia wa sasa kufikia ukomo wake ifikapo tarehe 29 Februari 2020,
tulipokea taarifa ya majadiliano yanayoendelea. Tulisisitiza mambo makuu
matatu. Kwanza, mkataba wa ubia mpya uzingatie zaidi kuziinua nchi za ACP
kiuchumi, maendeleo, na biashara. Pili, tulisisitiza umuhimu wa mkataba wa ubia
mpya kutohusianishwa moja kwa moja na mikataba mingine ambayo majadiliano yake
bado yanaendelea baina ya nchi za ACP na Umoja wa Ulaya ikiwemo mkataba wa EPA
na mikataba mingine. Tatu, kwa kuzingatia kuwa tunahitahi majadiliano ya kina
na yanayozingatia maslahi mapana ya nchi za ACP, ikiwemo Tanzania, tulitoa
fursa kwa majadiliano haya kuendelea hata ikibidi kwa muda wa nyongeza ili
kuwezesha zoezi hilo muhimu la majadiliano kwa mstakabali wa ushirikiano wetu
na EU kwa miaka mingine ijayo kukamilika kwa ufanisi unaostahiki.
10.Katika hatua ya
kuimarisha zaidi ushirikiano na nchi mbalimbali katika ngazi ya kitaifa, kikanda,
na kimataifa, hususan kwenye masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, tulipata
pia fursa ya kuonana na kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa nchi 5
zingine zilizoshiriki mkutano huo. Viongozi tulioonana nao na kufanya
mazungumzo ni pamoja na kiongozi wa ujumbe wa Ethiopia, Eswatini, Chadi,
Zambia, Equatorial Guinea, Commoro, na Namibia. Pia, tulipata nafasi ya kufanya
mazungumzo na viongozi wa nchi ya Romania na Umoja wa Ulaya. Mazungumzo haya
kwa ujumla yametupa uelewa wa pamoja baina ya nchi yetu na nchi hizo kwenye
agenda mbalimbali za kitaifa, kikanda, na kimataifa na pia kuimarisha zaidi
ushirikiano wenye maslahi baina ya Tanzania na nchi hizo.
11.Ndugu Waandishi wa
Habari, kwa ujumla ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano huu ulikuwa muhimu na
wenye manufaa. Ujumbe wa Tanzania ulitoa mchango mkubwa na kwa hakika hoja
nyingi za Tanzania zilikubaliwa na kuwa sehemu ya maamuzi na maazimio ya
mkutano. Tutaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maamuzi na maazimio
hayo.
Asanteni kwa kunisikiliza. NAIBU WAZIRI,
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI 28 MEI 2019, DODOMA
Rais Magufuli Afanya Ziara Rasmi Ya Kitaifa Nchini Namibia,Afungua Mtaa Mkubwa Uliopewa Jina La Mwl. Nyerere
Subscribe to:
Posts (Atom)