Thursday, September 5, 2019

MWAKILISHI MKAZI WA UNDP AKABIDHI NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipofika Wizarani kukabidhi nakala ya hati za utambulisho.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa katika mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam wakati Bi. Musisi alipofika Wizarani hapo kukabidhi nakala ya hati za utambulisho kwa Waziri.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi akifurahia jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi(hayupo pichani) wakati alipofika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam,kukabidhi nakala ya hati za utambulisho kwa Waziri.

 Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akimsikiliza Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi (hayupo pichani)
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa katika mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi. 

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akipokea nakala za hati za utambulisho kutoka kwa mwakilishi mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi.

Wednesday, September 4, 2019

WAZIRI WA MAMBO YA NJE PROF. PALAMAGAMBA JOHN KABUDI AWAAGA WANAFUNZI WANAOKWENDA ISRAEL KUSHIRIKI MAFUNZO YA KILIMO


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wanafunzi 44 kati ya 100 waliochaguliwa kwenda nchini Israel kushiriki program ya mafunzo ya kilimo kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia mwezi Septemba 2019. Hafla hiyo imefanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 4 Septemba 2019. Wengine katika picha kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Bw. Ayoub Mndeme na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bw. Emmanuel Buhohela.
Prof. Kabudi akizungumza na wanafunzi hao 
Wanafunzi hao wakimsikiliza Prof. Kabudi (hayupo pichani)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe naye akiwaasa wanafunzi hao kuzingatia maadili na kuwa wazalendo wanapokuwa kwenye mafunzo nchini Israel
Dkt. Mnyepe akizungumza
Mhe. Prof. Kabudi akimkabidhi tiketi na hati ya kusafiri, Bi. Janeth Barnaba ambaye ni mmoja wa wanafunzi wanaokwenda kushiriki mafunzo ya kilimo nchini Israel
Mwanafunzi mwingine akipokea tiketi na hati yake ya kusafiria tayari kuelekea nchini Israel tarehe 5 Septemba 2019 kwa ajili ya kuanza program ya mafunzo ya kilimo
Prof. Kabudi akiendelea na zoezi la kuwakabidhi wanafunzi hao tiketi na hati zao za kusafiria kama inavyoonekana pichani
Zoezi la kukabidha tiketi na hati za kusafiria likiandelea
Wanafunzi wakishuhuda mwenzao akikabidhiwa hati yake ya kusafiria na tiketi ya ndege
Prof. Kabudi akikabidhi hati za kusafiria na tiketi za ndege kwa wanafunzi wanaokwenda Israel kushiriki program ya mafunzo ya kilimo kwa vitendo
mwanafunzi akifurahia kukabidhiwa hati ya kusafiria na tiketi ya ndege vitakavyomwezesha kwenda Israel kushiriki mafunzo ya kilimo
Prof. Kabudi akimkabidhi hati ya kusafiria na tiketi ya ndege mwanafunzi atakayeshiriki program ya mafunzo ya kilimo nchini Israel
Wanafunzi wakiwa wameshikilia hati zao za kusafiria na tiketi za ndege zitakazowawezesha kusafiri kwenda Israel kushiriki program ya mafunzo ya kilimo
Mhe. Prof. Kabudi akiwaasa wanafunzi hao mara baada ya kuwakabidhi tiketi zao na hati za kusafiria zitakazowawezesha kwenda Isarel kuanza mafunzo ya kilimo kwa vitendo. Prof. Kabudi aliwataka wanafunzi hao kuwa waadilifu, wasikivu, wachapakazi, wazalendo na warejee nyumbani wakiwa na ujuzi na maarifa kwa manufaa ya Taifa.
===============================================================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali ya Tanzania inaungana na Serikali ya Afrika Kusini kulaani vikali vitendo vya ubaguzi na mashambulizi vinavyofanywa na raia wachache wa nchi hiyo dhidi ya raia wa nchi zingine za Afrika na kuziasa nchi zingine kutolipa kisasi kutokana na vitendo hivyo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wanafunzi 100 kutoka Tanzania wanaokwenda Israel kushiriki mafunzo ya kilimo iliyofanyika leo tarehe 4 Septemba 2019 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mhe. Prof. Kabudi amesema kuwa, vitendo vinavyofanywa na raia wachache wa Afrika Kusini vya kuwashambulia raia kutoka nchi zingine za Afrika na kuharibu mali zao vinasikitisha na kuivunjia heshima nchi hiyo. Hata hivyo, alisema kuwa Serikali ya Tanzania inaunga mkono kauli ya Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa aliyoitoa hivi karibuni ya kukemea na kulaani vikali vitendo vinavyofanywa na raia hao wachache.

Aidha, ameongeza kuwa, vitendo hivyo  ambavyo vinatokana na raia hao wengi kukosa ajira, ardhi na pia kutopenda kujishughulisha havihalalishi watu wengine wakiwemo watanzania kulipa kisasi kwa namna yoyote ile.

“Ni jambo la kusikitisha lakini Serikali ya Afrika Kusini inalisimamia kikamilifu na sisi tupo tayari kushirikiana nao ili kulitafutia ufumbuzi wa kudumu.Nawasihi Watanzania wenzangu tusilipize kisasi na tutaendelea kuwalinda raia wa Afrika Kusini waliopo Tanzania kwani tunaamini kuwa Afrika ni moja na waafrika ni ndugu zetu” alisema Prof. Kabudi.

Kadhalika, Prof. Kabudi alieleza kuwa hadi sasa hakuna taarifa kuhusu Mtanzania kuuawa, kujeruhiwa au kuharibiwa mali kutokana na vurugu hizo. Pia alisema kuwa Wizara itaendelea kutoa taarifa za uhakika kadri zinavyopatikana kutoka kwenye vyanzo vya uhakika ukiwemo Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.

Wakati huohuo, Mhe. Prof. Kabudi amewaaga wanafunzi 44 kati ya 100 waliochaguliwa kwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo kwa vitendo kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia mwezi Septemba 2019. Wanafunzi hao ambao wengi wamehitimu katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Taasisi ya Kilimo ya Uyole ya Mbeya na Ukiriguru ya Mwanza wanakwenda kushiriki mafunzo hayo ya vitendo kwenye sekta mbalimbali za kilimo ikiwemo uzalishaji na teknolojia. Kati ya Wanafunzi hao, 16 wameondoka nchini tarehe 4 Septemba, 2019, kuelekea Israel, 44 wataondoka nchini tarehe 5 Septemba 2019 na idadi iliyosalia itaondoka tarehe 10 Septemba 2019.

Katika hotuba yake, Mhe. Prof. Kabudi amewataka wanafunzi hao vijana kuzingatia mafunzo hayo ili kuja kutoa mchango wao kwenye mapinduzi ya kilimo ambayo yatachochea mapinduzi ya viwanda nchini. Aidha aliwaasa kuwa waadilifu, kufanyakazi kwa bidii, kushikamana na kujiepusha na vitendo viovu.

“Mnaenda Israel kutafuta ujuzi, uzoefu na ubunifu katika maeneo ya uzalishaji mazao. Hivyo tunaamini kuwa mna nafasi kubwa ya kuja kuibadilisha Tanzania katika eneo la kilimo na mtaleta mapinduzi ya kilimo kwani vijana mpo wengi nchini, mna ari na ni nguvu kazi ya Taifa” alisisitiza Prof. Kabudi.

Akiielezea Israel, Mhe.Prof. Kabudi amesema kuwa nchi hiyo ni nusu jangwa kama ilivyo baadhi ya mikoa hapa nchini. Hata hivyo Israel inaongoza kwa kuuza mazao ya mbogamboga na matunda kwenye nchi za Ulaya kutokana na watu wa nchi hiyo kutumia maarifa katika kugeuza ukame kuwa fursa. Hivyo aliwataka wanafunzi hao kuhakikisha wanapata maarifa na kujifunza mbinu bora na teknolojia za kisasa ili kuja kuendeleza kilimo kikiwemo kile cha umwagiliaji kwenye mikoa kama Singida, Manyara, Shinyanga na Dodoma.

Wanafunzi hao mia moja (100) wamechaguliwa kati ya wanafunzi 1,440 waliotuma maombi ya kwenda kushiriki program ya mafunzo ya kilimo nchini Israel ambayo hufanyika kwa kipindi cha miezi tisa. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliratibu zoezi la upatikanaji wa wanafunzi hao kwa maelekezo ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa mwezi Novemba 2018 alipofanya mazungumzo na Balozi wa Israel nchini, Mhe. Noah Gal Gendler.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam.
4 Septemba 2019

Tuesday, September 3, 2019

MKUTANO WA TATU WA TUME YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA UGANDA KUFANYIKA DAR ES SALAAM


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Wilbroad Kayombo akizungumza wakati wa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika kwa ngazi ya wataalam jijini Dar es Salaam tarehe 3 Septemba 2019. Mkutano huo wa wataalam utafuatiwa na mkutano wa Makatibu Wakuu tarehe 4 Septemba 2019 na kuhitimishwa na Mkutano wa Mawaziri tarehe 5 Septemba 2019.  Kutoka kushoto walioketi ni Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Dkt. Azizi Mlima na Balozi wa Uganda nchini, Mhe. Richard Kabonero
Sehemu ya ujumbe wa Uganda wakiwa kwenye mkutano wa tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika kwa ngazi ya wataalam
Kiongozi wa ujumbe wa Uganda kwenye mkutano wa ngazi ya wataalam akizungumza wakati wa Mkutano huo 
Sehemu ya wataalam kutoka sekta mbalimbali za Tanzania ikiwemo Nishati, miundombinu, elimu, afya, biashara na uwekezaji
Mkutano ukiendelea
=====================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MKUTANO WA TUME YA PAMOJA YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA UGANDA

Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda umeanza leo tarehe 3 Septemba 2019 jijini Dar es Salaam kwa ngazi  ya wataalamu.

Mkutano huo  ambao pamoja na mambo mengine utajadili masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, utafuatiwa na ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 4 Septemba 2019 na Mawaziri tarehe 5 Septemba 2019.

Lengo la Mkutano wa Tatu wa Tume ya Ushirikiano ni kujadili na kutathmini hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa masuala mbalimbali yaliyokubalika kwenye Mkutano wa Pili uliofanyika jijini Kampala, Uganda mwezi Agosti 2018 pamoja na kutathmini utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa Mawaziri kuhusu masuala ya Mipaka kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika mkoani Kagera mwezi Julai 2017.

Kadhalika, mkutano huu wa Tatu utatoa fursa kwa nchi hizi mbili kujadiliana na kukubaliana kuhusu agenda mbalimbali za ushirikiano. Miongoni mwa maeneo hayo ya ushirikiano ni pamoja na: Siasa na Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Maendeleo ya Miundombinu, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo na Uvuvi, Maji na Mazingira, Afya, Elimu na Mafunzo na Habari na Utamaduni.

Mkutano wa Tatu wa Tume ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda pia utashuhudia Kongamano la Kwanza la Biashara na Uwekezaji kati ya nchi hizi litakalofanyika tarehe 6 Septemba 2019. Kongamano hili litahusisha maonesho ya bidhaa na huduma mbalimbali kutoka Tanzania na Uganda.

Tangu kuanzishwa kwa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda tayari nchi hizi zimefanya vikao viwili vya pamoja. Kikao cha mwisho kilifanyika jijini Kampala, Uganda mwezi Agosti 2018. Vikao vya tume ya pamoja ya ushirikiano huwashirikisha viongozi na wataalam kutoka sekta mbalimbali za nchi hizi mbili.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam.
3 Septemba 2019

Friday, August 30, 2019

TANGAZO LA NAFASI ZA AJIRA



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kuujulisha Umma wa Watanzania kuwa, Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (United Nations Environment Programme-UNEP) imetangaza nafasi 5 za ajira zifuatazo:-
  1. Senior Administrative Officer;
  2. Senior Programme Management Officer;
  3. Chief of Section;
  4. Human Resource and Management;
  5. Deputy Chief Officer.


Wizara inawahimiza Watanzania wenye vigezo na sifa stahiki kuomba nafasi hizi. Kupata taarifa zaidi na taratibu za kuomba nafasi hizo tafadhali bofya HAPA


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika 

Mashariki

Dodoma, Tanzania.

30 Agosti 2019

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MKUTANO KUHUSU KUIMARISHA AMANI NA UTULIVU BARANI AFRIKA – TICAD7 YOKOHAMA JAPAN


Tanzania imetoa rai kwa Jumuiya ya Kimataifa na Japan kuendelea kutafuta suluhu ya kudumu kwenye changamoto mbalimbalii ambazo bado zinajitokeza kwenye baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo ugaidi wa kimataifa, uhalifu, mabadiliko ya tabianchi, ukame, njaa na magonjwa sambamba na kujitolea kuchangia na kuwekeza kwenye miradi iliyobuniwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuboresha mazingira yaliyoharibiwa kutokana na uwepo wa kambi za Wakimbizi kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Rai hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu kuimarisha amani na usalama barani Afrika uliofanyika wakati wa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) uliomalizika leo tarehe 30 Agosti 2019 jijiji Yokohama, Japan.

Mhe. Waziri Mkuu amesema kuwa, miradi hiyo ambayo ni pamoja na kubadilishana teknolojia hususan kwenye maeneo ya mipakani na mifumo ya kutoa taarifa mapema kwa ajili ya kujikinga na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza itasaidia kuboresha mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa yameharibiwa na wakimbizi na watu wanaotafuta makazi.

“Uwepo wa wakimbizi na watu wanaotafuta makazi kwa namna moja au nyingine huathiri mazingira, jamii usalama na uchumi wan chi inayowapokea. Hivyo ni ombi letu kwenu kushirikiana nasi kwenye miradi mbalimbali katika kuboresha mazingira” alisema Mhe. Waziri Mkuu.

Aliongeza kusema kuwa, kwa miaka mingi Tanzania imekuwa kimbilio kwa wakimbizi kutoka nchi jirani wanaokimbia nchi zao kutokana na migogoro ya kisisasa, kikabila na kuibuka kwa vikundi vya uasi. Alieleza kuwa hadi kufikia tarehe 1 Agosti 2019, Tanzania inahifadhi wakimbizi wapatao 305,983.

Vilevile, Mhe. Waziri Mkuu aliongeza kuwa, katika kuhakikisha amani inapatikana pote dunaiani, Tanzania ina mchango mkubwa katika amani, utulivu na utatuzi wa migogoro barani Afrika na kwamba ni miongoni mwa nchi zinazochangia misheni za ulinzi wa amani katika nchini mbalimbali Afrika na duniani. 


Wakati huo huo, Mhe. Waziri Mkuu amefanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Bw. Fillipo Grandi walipokutana pembezoni mwa Mkutano wa Saba wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika.

Wakati wa mazungumzo hayo, Mhe. Waziri Mkuu na Bw. Grandi wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika kuhakikisha usalama kwenye makambi ya wakimbizi, kuimarisha mipaka pamoja na kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira unaofanywa na Wakimbizi.

Akizungumzia Mkutano wa Saba wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) uliofanyika kwa siku tatu jijini Yokohama, Japan. Mhe. Waziri Mkuu amesema Mkutano huo umemalizika kwa mafanikio huku Wakuu wa Nchi a Serikali wakikubaliana kuteleleza Azimio la Yokohama linalolenga kuleta mapinduzi barani Afrika kwa kuimarisha  masuala ya usalama, elimu, sayansi na teknolojia na kukuza sekta binafsi.

Amesema kuwa, Tanzania itajipanga kikamilifu kutekeleza maazimio yaliyofikiwa kwenye mkutano huo ambayo ni ya manufaa makubwa kwa nchi za Afrika.
Mhe. Waziri Mkuu alieleza kuwa, maazimio hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yamegusa sekta zote muhimu zikiwemo afya, elimu, maendeleo ya miundombinu, sayansi na teknolojia na amani na usalama yanalenga kuzikwamua kiuchumi nchi za Afrika kupitia ushirikiano  na Serikali ya Japan.

“Tumemaliza kikao cha TICAD leo ambacho kimejadili mambo mengi yakiwemo ya usalama, maendeleo ya elimu, sayansi na teknolojia na namna nzuri ya kuendesha nchi zetu kupitia miradi ya maendeleo kama ujenzi wa miundombinu. Kikao hiki kwetu Tanzania ni chachu ya kuendeleza jitihada zetu za kufikia uchumi wa kati na mapinduzi ya viwanda ifikapo mwaka 2025”  alifafanua Waziri Mkuu. 

Mhe. Waziri Mkuu aliongeza kuwa, Japan imetenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kuzisaidia nchi za Afrika kupitia fursa ya mikopo na ufadhili. Aliongeza kuwa, Tanzania itajipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kuandaa maandiko mazuri ya miradi ya kipaumbele ili kupata fedha hizo.

Amesema kuwa, nchi za Afrika ambazo kwa kiasi kikubwa zimejaliwa kuwa na maliasili na malighafi za kutosha kwa ajili ya kujenga uchumi, zimesisitizwa kuimarisha mahusiano na sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa nchi hizo. 


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Yokohama, Japan
30 Agosti 2019

WAZIRI MKUU MHE MAJALIWA AKUTANA NA KAMISHNA MKUU WA UNHCR

  Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  (Mb) Mhe. Kassim M. Majaliwa akiwa katika mzungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi. Mazungumzo hayo yamefanyika kando na mkutano wa TICAD7 Yokohoma,Japan.

  Mazungumzo kati ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mb) Mhe. Kassim M. Majaliwa na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi kuhusu wakimbizi waliopo Tanzania yakiendelea. Yokohama, Japan.

   Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  (Mb) Prof. Palamagamba John Kabudiakifuatilia mazungumzo kati ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mb) Mhe. Kassim M. Majaliwa na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi(hayupo pichani) Yokohama, Japan.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mb) Mhe. Kassim M. Majaliwa akiagana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina yao kuhusu wakimbizi waliopo Tanzania. Mazungumzo hayo yamefanyika Yokohama, Japan

  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  (Mb) Prof. Palamagamba John Kabudia kisalimiana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandimara baada ya kumaliza kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu mhe. Kassim M. Majaliwa. Yokohama, Japan.

   Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  (Mb) Prof. Palamagamba John Kabudi akiteta jambo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi mara baada ya kumalizika mazungumzo ya Waziri Mkuu mhe. Kassim M. Majaliwa. Yokohama, Japan.