Tuesday, September 3, 2019

MKUTANO WA TATU WA TUME YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA UGANDA KUFANYIKA DAR ES SALAAM


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Wilbroad Kayombo akizungumza wakati wa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika kwa ngazi ya wataalam jijini Dar es Salaam tarehe 3 Septemba 2019. Mkutano huo wa wataalam utafuatiwa na mkutano wa Makatibu Wakuu tarehe 4 Septemba 2019 na kuhitimishwa na Mkutano wa Mawaziri tarehe 5 Septemba 2019.  Kutoka kushoto walioketi ni Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Dkt. Azizi Mlima na Balozi wa Uganda nchini, Mhe. Richard Kabonero
Sehemu ya ujumbe wa Uganda wakiwa kwenye mkutano wa tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika kwa ngazi ya wataalam
Kiongozi wa ujumbe wa Uganda kwenye mkutano wa ngazi ya wataalam akizungumza wakati wa Mkutano huo 
Sehemu ya wataalam kutoka sekta mbalimbali za Tanzania ikiwemo Nishati, miundombinu, elimu, afya, biashara na uwekezaji
Mkutano ukiendelea
=====================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MKUTANO WA TUME YA PAMOJA YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA UGANDA

Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda umeanza leo tarehe 3 Septemba 2019 jijini Dar es Salaam kwa ngazi  ya wataalamu.

Mkutano huo  ambao pamoja na mambo mengine utajadili masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, utafuatiwa na ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 4 Septemba 2019 na Mawaziri tarehe 5 Septemba 2019.

Lengo la Mkutano wa Tatu wa Tume ya Ushirikiano ni kujadili na kutathmini hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa masuala mbalimbali yaliyokubalika kwenye Mkutano wa Pili uliofanyika jijini Kampala, Uganda mwezi Agosti 2018 pamoja na kutathmini utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa Mawaziri kuhusu masuala ya Mipaka kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika mkoani Kagera mwezi Julai 2017.

Kadhalika, mkutano huu wa Tatu utatoa fursa kwa nchi hizi mbili kujadiliana na kukubaliana kuhusu agenda mbalimbali za ushirikiano. Miongoni mwa maeneo hayo ya ushirikiano ni pamoja na: Siasa na Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Maendeleo ya Miundombinu, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo na Uvuvi, Maji na Mazingira, Afya, Elimu na Mafunzo na Habari na Utamaduni.

Mkutano wa Tatu wa Tume ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda pia utashuhudia Kongamano la Kwanza la Biashara na Uwekezaji kati ya nchi hizi litakalofanyika tarehe 6 Septemba 2019. Kongamano hili litahusisha maonesho ya bidhaa na huduma mbalimbali kutoka Tanzania na Uganda.

Tangu kuanzishwa kwa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda tayari nchi hizi zimefanya vikao viwili vya pamoja. Kikao cha mwisho kilifanyika jijini Kampala, Uganda mwezi Agosti 2018. Vikao vya tume ya pamoja ya ushirikiano huwashirikisha viongozi na wataalam kutoka sekta mbalimbali za nchi hizi mbili.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam.
3 Septemba 2019

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.