TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
DKT. SALIM ATUNUKIWA NISHANI YA JUU YA URAFIKI YA JAMHURI YA WATU
WA CHINA
Rais wa Jamhuri ya Watu wa
China, Mheshimiwa Xi Jinping, leo asubuhi tarehe 29 Septemba 2019 amemtunukia
Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa. Dk. Salim Ahmed Salim, Nishani ya Juu ya
Urafiki ya Jamhuri ya Watu wa China ikiwa ni sehemu ya matukio ya maadhimisho
ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China iliyofanyika jijini
Beijing. Mheshimiwa Dkt. Salim anakuwa
mwafrika wa kwanza kupewa heshima na tuzo hiyo ya juu katika historia ya China.
Nishani hiyo ilipokelewa na
Bi. Maryam Salim, Binti ya Dk. Salim Ahmed Salim ambaye pia ni Mwakilishi Mkazi
wa Benki ya Dunia nchini Albania kwa niaba ya Baba yake kutokana na kushindwa
kuhudhuria kwa sababu za kiafya. Katika tukio hilo, Serikali ya Tanzania
iliwakilisha na Balozi wa Tanzania nchini China Mheshimiwa Mbelwa Kairuki.
Hafla hiyo kubwa ya kitaifa ya
kukabidhi nishani ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Chama na Serikali ya
China akiwemo Makamu wa Rais Mheshimiwa Wang Qishan, Waziri Mkuu Mheshimiwa Li
Keqiang, Spika wa Bunge Mheshimiwa Li Zhanshu na Wajumbe wote wa Kamati Kuu ya
Chama cha Kikomunisti cha China na Baraza la Taifa.
Mbali na Dk.Salim, wengine waliotunukiwa Nishani ya Urafiki ni
pamoja na Kiongozi wa Chama cha Kikoministi cha Cuba Jenerali Raul Castro, Dada
wa Mfalme wa Thailand Maha Chakri Sirindhorn, Kiongozi wa Jumuiya ya Urafiki ya
China na Urusi Ndugu Galina Kulikova, Waziri Mkuu Mstaafu wa Ufaransa
Jean-Pierre Raffarin na Bi Isabel
Crook kutoka Canada.
Vilevile Rais Xi alitoa Nishani ya Jamhuri na Nishani ya Heshima ya Taifa kwa
raia 36 wa China kwa kutambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa la
China kupitia kazi zao katika fani mbalimbali.
Nishani ya Juu ya Urafiki ya
Taifa la China imetolewa kwa Dkt. Salim
kutokana na mchango wake wa kuiwezesha Jamhuri ya Watu wa China kuwa
Mwanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 1971 alipokuwa Mwakilishi wa Kudumu wa
Tanzania katika Umoja wa Mataifa. Aidha,
mchango wa Dk. Salim katika kuimarisha mahusiano kati ya China na Tanzania
wakati aliposhikilia nyadhifa mbalimbali umetajwa kama sababu ya kutunukiwa
Nishani hiyo. Vilevile, mchango wa Dk.Salim katika kujenga mahusiano kati ya
China na Afrika akiwa na nafasi ya Katibu Mkuu wa OAU umetajwa kuwa sababu nyingine
ya kutunukiwa Nishani.
Tukio la Kutoa Nishani
limetangazwa moja kwa moja na Televisheni zote za Jamhuri ya Watu wa China na
kushuhudiwa na watu zaidi ya Milioni 500.
Kwa mujibu wa maelezo ya
Balozi wa Tanzania nchini China Ndugu Mbelwa Kairuki Kupitia tukio la leo,
mamilioni ya Wachina hususan vijana wamepata fursa ya kufahamu nafasi na
mchango wa Tanzania na Bara la Afrika katika historia ya taifa lao. Aidha,
tukio la leo limeifanya Tanzania kufahamika kwa watu wengi zaidi nchini China
kupitia tukio mara moja. Hatua hiyo itaamsha udadisi na hamasa miongoni mwa
Wachina wengi wa kizazi kipya kutaka kuifahamu zaidi Tanzania. Hali hii yaweza
kujitafsiri katika fursa kubwa ya kukua kwa utalii, biashara na wawekezaji
ikizingatiwa kuwa wananchi wa China hutoa
mwitikio mkubwa kwa nchi ambazo husemwa vizuri na kuthaminiwa na Serikali yao.
Aidha Balozi Kairuki ameeleza
kwamba maadhimisho ya miaka 70 ya Jamhuri ya Watu wa China mwaka huu
yanaambatana na maadhimisho ya miaka 55 ya urafiki na udugu kati ya China na
Tanzania kufuatia kuanzishwa kwa mahusiano rasmi ya kidiplomasia mwaka 1964.
Uhusiano wa China na Tanzania uliotokana na uhusiano mzuri wa waasisi wa
mataifa haya mawili, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na
Hayati Mao Tsetung. Uhusiano huo umeendelezwa na viongozi wa pande zote mbili
ambao umekuwa ukiimarika siku hadi siku. Uhusiano huu umekwenda mbali zaidi ya
uhusiano kati ya Serikali na Serikali na kushamiri kwa uhusiano wa watu kwa
watu.
Ni kwasababu hiyo, katika
maadhimisho ya miaka 70 ya Taifa la China, Jumuiya ya Urafiki wa watu wa China
na Tanzania ni miongoni mwa Jumuiya za mataifa 17 yenye urafiki wa majira yote
na China walioalikwa kushiriki kwenye
maadhimisho hayo na tarehe 1 Oktoba 2019 watakuwa na gwaride lao maalum. Katika
jumuiya hizo 17, Kutoka Barani Afrika ni Tanzania na Zambia ndio watahudhuria.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki,
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.