Friday, September 6, 2019

TANZANIA NA UGANDA ZAKUBALIANA KUIMARISHA BIASHARA ILI KUKUZA UCHUMI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 6 Septemba 2019. Ufunguzi huo ulihudhuriwa pia na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Mawaziri, Wafanyabiashara kutoka Tanzania na Uganda na wadau mbalimbali
Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni nae akihutubia Kongamano hilo litakalofanyika tarehe 6 na 7 Septemba 2019.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Uganda
Marais wakiwa meza kuu pamoja na Mawaziri kutoka Tanzania na Uganda akiwemo Waziri wa Elimu wa Uganda ambaye pia ni Mke wa Rais Museveni, Mhe. Mama Janeth Museveni (kushoto)
Mawaziri wa Tanzania wakiwa Ukumbini kabla ya ufunguzi rasmi kuanza 
Wadau mbalimbali wakiwemo Mabalozi walioshiriki ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uganda
Wadau wengine wakiwa ukumbini kabla ya ufunguzi wa kongamano la biashara kuanza
Marais pamoja na Mawaziri wakiwa wamesisimama kwa heshima wakati nyimbo za mataifa yao zikipigwa kabla ya kuanza ufunguzi rasmi wa kongamano la kwanza la biashara kati ya Tanzania na Uganda
Picha inayoonesha washiriki wa kongamano hilo
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akibadilishana  Hati ya Makubaliano  kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda kwenye masuala ya Kilimo na Waziri wa Uganda, Mhe. Vincent Mwahiche mara baada ya kusaini. Wanaoshuhudia ni Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Museveni pamoja na baadhi ya Mawaziri kutoka Tanzania na Uganda
Mhe. Prof. Kabudi kwa pamoja na waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa wakionesha Hati mbalimbali za Makubaliano mbalimbali walizosaini ikiwemo Hati ya Makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya Uhamiaji, Magereza na Tume ya Pamoja ya Ushirikiano

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe (katikati) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Trademark East Afrika, Bw. John Ulanga (kushoto) na mdau mwingine kabla ya kuanza kwa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uganda
Dkt. Mnyepe akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Uganda, Balozi Patrick Mugoya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bibi Caroline Chipeta wakimsikiliza Mratibu wa Program (MC) ya ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uganda
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kushoto) akimsikiliza mdau kutoka sekta binafsi, Bw. Mustapha Hassanal ambaye alishiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uganda.
=================================================================================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TANZANIA NA UGANDA ZAKUBALIANA KUIMARISHA SEKTA YA BIASHARA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema Serikali ya Tanzania na Uganda zimedhamiria kuimarisha sekta ya biashara kwa kushughulikia changamoto zote zilinazoikabili sekta hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Mhe. Rais Magufuli leo tarehe 6 Septemba 2019 wakati wa ufunguzi rasmi wa Kongamano la Kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Uganda lililofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli amesema kwamba wakati sasa umefika wa kutumia makongamano na mahusiano ya kihistoria, kidiplomasia na kindugu yaliyopo kati ya Tanzania na Uganda ili kusukuma mbele agenda ya maendeleo ya kiuchumi kwa maslahi ya nchi hizo mbili. Aliongeza kwamba nchi hizi mbili zina rasilimali za kutosha kujiletea maendeleo ikiwemo utalii, madini, mifugo, uvuvi, kilimo na gesi na mafuta.

Akionesha kusikitishwa na kiwango kidogo cha ufanyaji biashara kati ya Tanzanai na Uganda, Mhe. Rais Magufuli alieleza kuwa kwa miaka mingi kiwango hicho bado kipo chini sana ukilinganisha na nchi nyingine zinazoshirikiana kibiashara na Tanzania. Alisema hadi sasa ni Kampuni 22 pekee za Uganda zimewekeza nchini huku tani 167,000 pekee za mizigo zikipita Tanzania kwa mwaka 2017/2018 tofauti na tani milioni 7.1 za bidhaa zilizoingizwa nchini humo.


Akielezea sababu zilizoshusha kiwango cha biashara kati ya nchi hizi mbili, Mhe. Rais Magufuli alisema kuwa ni pamoja na urasimu kutoka kwa watendaji wa Serikali hizi mbili, kuwepo kwa vikwazo vya kodi na visivyo vya kodi; miundombinu hafifu ya usafiri na usafirishaji na ufanisi mdogo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Hata hivyo, Mhe. Rais Magufuli alifafanua kuwa, Serikali ya Tanzania iliitambua changamoto hiyo mapema na kuanza kuchukua jitihada za makusudi za kukabiliana nayo ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kati ya Tanzania na Uganda. Alisema jitihada hizo ni pamoja na kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirshaji kwa kuanza ukarabati wa reli ya kati na ununuzi wa vichwa vya treni; upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa gharama ya takribani Shilingi Trilioni moja na ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli aliongeza kuwa, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Uganda zimefufua vivuko kwa ajili ya kusafirisha mizigo kutokea Bandari ya Mwanza kupitia Bandari ya Portbell nchini Uganda pamoja na kufufua shirika la ndege la Tanzania na Uganda ambapo Ndege za Shirika la Tanzania zilianza safari nchini Uganda mwezi Agosti 2018 huku ndege za Shirika la Uganda zikizindua safari zake nchini mwezi Agosti 2019.

Jitihada zingine ni kudhibitiwa kwa vitendo vya uhalifu kwenye Bandari pamoja na kuimarishwa kwa vituo vya kutoa huduma za pamoja mipakani na kuendelea kubuni mipango mahsusi ya kitaifa yenye lengo la kuboresha biashara na uwekezaji.

“Nawakaribisha sana Uganda tufanye biashara yenye tija kwani kimsingi tumechelewa. Hivyo ni imani yangu kuwa Mkutano huu utakuwa mwanzo wa biashara kubwa kwa watu wetu” alisisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa pande zote kuheshimu sharia na kanuni zilizowekwa na nchi husika na zile za Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kujenga uchumi wa nchi hizi mbili. Vilevile, alitoa wito kwa washiriki wa Kongamano hilo kuchangamkia fursa za kibiashara zilizopo kati ya nchi hizi mbili na kutumia kongamano hilo kuainisha changamoto zote za kibiashara na kutoa mapendekezo ya namna ya kuzitatua.

Akizungumzia Mradi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga ambao unarajiwa kutengeneza zaidi ya ajira 20,000, Mhe. Rais Magufuli alitoa rai kwa Serikali ya Uganda kuongeza kasi ya kukamilisha masuala yaliyosalia ili mradi huo uanze mapema.

Kwa upande wake, Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni aliwataka watendaji wa Serikali zote kutambua umuhimu wa sekta ya biashara na mchango wake katika maendeleo ya nchi zao badala ya kuendelea kuweka vikwazo na urasimu.

Aidha, Mhe. Rais Museveni alimshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuupa kipaumbele Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka nchini kwake hadi Tanzania na kuahidi kutekeleza yale yote waliyokubaliana ili mradi huo uanze kutekelezwa haraka iwezekanavyo.

Awali akizungumza kwenye Kongamano hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi alisema kuwa, Tanzania na Uganda zimefanya mkutano wa tatu wa Tume ya pamoja ya Ushirikiano ambapo masuala ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali yalijadiliwa. Alisema kuwa, Mkutano huo pamoja na mambo mengine pia  uliteua Maafisa kutoka pande hizo mbili kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, Bw. Salum Shamte ambaye alizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara na sekta binafsi nchini alisema kuwa, ana imani kubwa kuwa Kongamano hilo la biashara litakuwa mwanzo mzuri wa kukuza biashara kati ya Tanzania na Uganda, kwani litatoa nafasi kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Uganda na Tanzania kuelewa kwa undani fursa zilizopo kati ya nchi hizi mbili. Pia alisisitiza umuhimu wa kampuni za Uganda kufanya biashara kwa ubia na kampuni za Tanzania na vivyo hivyo kwa kwa Tanzania ili kurahisisha biashara miongoni mwao.

Wakati wa Kongamano hilo ambalo limewashirikisha zaidi ya wafanyabiashara na wawekezaji 1,000 kutoka Tanzania na Uganda, Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Museveni walishuhudia kusainiwa kwa Hati za Makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya Uhamiaji, Magerereza, Kilimo na Tume ya Pamoja ya Ushirikiano.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam.
6 Septemba 2019

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.