Saturday, September 21, 2019

MAKAMU WA RAIS KUFUNGUA RASMI TAMASHA LA UTAMADUNI LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI




Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa pamoja na viongozi wengine kutoka Tanzania na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa wamesimama kwa ajili ya kuyapokea maandamano ya vikundi mbalimbali vya sanaa na utamaduni vitakavyoshiriki Tamasha la Utamaduni na Sanaa la Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama JAMAFEST litakalofunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam tarehe 22 Septemba 2019.
Maandamano ya vikundi vya utamaduni kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yakipita mbele ya mgeni rasmi 
Umati wa wananchi uliojitokeza kujionea vikundi mbalimbali vya utamaduni kuelekea ufunguzi rasmi wa Tamasha la Nne la JAMAFEST hapo tarehe 22 Septemba 2019

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota (mwenye suti) akiwa na Maafisa kutoka Wizara na wadau wengine wakati wa maandalizi ya ufunguzi rasmi wa Tamasha la Nne la JAMAFEST utakaofanyika tarehe 22 Septemba 2019

Wadau mbalimbali
Kikundi kutoka Burundi

 

Kikundi kutoka Kenya
Kikundi kutoka Rwanda
Kikundi kutoka Tanzania
Kikundi kutoka Uganda
Wadau kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifurahia kukamilika kwa maandalizi kabla ya ufunguzi rasmi wa JAMAFEST tarehe 22 Septemba 2019
==============================================================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Makamu wa Rais kufungua Tamasha la Nne la Utamaduni la Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua rasmi Tamasha la Nne la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Jumuiya ya Afrika Mashariki Utamaduni Festival (JAMAFEST) litakalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 22 hadi 28 Septemba 2019.

Tamasha hilo ambalo limebeba kauli mbiu isemayo “Cultural diversity: A key Driver to Regional Intergration, Economic Growth and Promotion of Tourism” linalenga kuwa jukwaa la kuonesha utamaduni wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi hizo kutumia fursa hii kama njia mojawapo  ya kuwaleta pamoja viongozi na wananchi wa Afrika Mashariki pamoja ili kusherehekea utajiri wa utamaduni uliopo.

Aidha, kufanyika kwa JAMAFEST hapa Tananzania kutawezesha ushiriki mkubwa wa wananchi na hii ni fursa adhimu ya kutangaza mila, utamaduni na Sanaa za Tanzania kwa Wana Afrika Mashariki. Pia Tanzania itatumia nafasi hiyo kutangaza utalii wa kitamaduni uliopo pamoja na wananchi kunufaika kiuchumi kupitia biashara mbalimbali zitakazofanyika wakati wa Tamasha hilo.

Akizungumza wakati wa kutangaza kukamilika kwa maandalizi ya Tamasha hilo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe alitoa wito kwa wananchi wa Tanzania hususan wakazi wa Dar es Salaam kuchangamkia fursa ya uwepo wa Tamasha hili ili kunufaika nalo. 

Alisema kuwa, nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimetuma vikundi mbalimbali vya Sanaa na utamaduni kwa ajili ya kushiriki tamasha hilo la aina yake. Aidha, alisema kuwa fursa hii ni muhimu kwa Nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuuonesha ulimwengu urithi mkubwa wa utamaduni uliopo miongoni mwao.

Vilevile, alitoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaa kujitokeza kwa wingi, bila kukosa kwenye sherehe za ufunguzi wa Tamasha hilo zitakazofanyika kwenye Uwanja wa Taifa tarehe 22 Septemba 2019.

Tamasha la Nne la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na mambo mengine litaangazia shughuli mbalimbali za kitamaduni na sanaa zitakazofanyika Uwanjani hapo ikiwa ni pamoja na: Midahalo na Warsha; Maonesho ya Sanaa za uoni, Uoneshaji na Ushindanishaji wa Filamu, Masoko ya Sanaa na Ubunifu, Michezo ya Watoto, Michezo ya Jadi, Soko na Maonesho ya Vyakula vya asili, Maonesho ya Mavazi na Ulimbwende na Ziara, Tuzo na Utalii kwa washiriki.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni miongoni mwa waratibu wa Tamasha hilo ambalo linashirikisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania, Uganda na Sudan Kusini.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
21 Septemba 2019

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.