Prof. Kabudi akizungumza na wanafunzi hao |
Wanafunzi hao wakimsikiliza Prof. Kabudi (hayupo pichani) |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe naye akiwaasa wanafunzi hao kuzingatia maadili na kuwa wazalendo wanapokuwa kwenye mafunzo nchini Israel |
Dkt. Mnyepe akizungumza |
Mhe. Prof. Kabudi akimkabidhi tiketi na hati ya kusafiri, Bi. Janeth Barnaba ambaye ni mmoja wa wanafunzi wanaokwenda kushiriki mafunzo ya kilimo nchini Israel |
Mwanafunzi mwingine akipokea tiketi na hati yake ya kusafiria tayari kuelekea nchini Israel tarehe 5 Septemba 2019 kwa ajili ya kuanza program ya mafunzo ya kilimo |
Prof. Kabudi akiendelea na zoezi la kuwakabidhi wanafunzi hao tiketi na hati zao za kusafiria kama inavyoonekana pichani |
Zoezi la kukabidha tiketi na hati za kusafiria likiandelea |
Wanafunzi wakishuhuda mwenzao akikabidhiwa hati yake ya kusafiria na tiketi ya ndege |
Prof. Kabudi akikabidhi hati za kusafiria na tiketi za ndege kwa wanafunzi wanaokwenda Israel kushiriki program ya mafunzo ya kilimo kwa vitendo |
mwanafunzi akifurahia kukabidhiwa hati ya kusafiria na tiketi ya ndege vitakavyomwezesha kwenda Israel kushiriki mafunzo ya kilimo |
Prof. Kabudi akimkabidhi hati ya kusafiria na tiketi ya ndege mwanafunzi atakayeshiriki program ya mafunzo ya kilimo nchini Israel |
Wanafunzi wakiwa wameshikilia hati zao za kusafiria na tiketi za ndege zitakazowawezesha kusafiri kwenda Israel kushiriki program ya mafunzo ya kilimo |
Mhe. Prof. Kabudi akiwaasa wanafunzi hao mara baada ya kuwakabidhi tiketi zao na hati za kusafiria zitakazowawezesha kwenda Isarel kuanza mafunzo ya kilimo kwa vitendo. Prof. Kabudi aliwataka wanafunzi hao kuwa waadilifu, wasikivu, wachapakazi, wazalendo na warejee nyumbani wakiwa na ujuzi na maarifa kwa manufaa ya Taifa. ===============================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Serikali ya Tanzania inaungana na Serikali ya Afrika
Kusini kulaani vikali vitendo vya ubaguzi na mashambulizi vinavyofanywa na raia
wachache wa nchi hiyo dhidi ya raia wa nchi zingine za Afrika na kuziasa nchi
zingine kutolipa kisasi kutokana na vitendo hivyo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati wa hafla
fupi ya kuwaaga wanafunzi 100 kutoka Tanzania wanaokwenda Israel kushiriki
mafunzo ya kilimo iliyofanyika leo tarehe 4 Septemba 2019 katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mhe. Prof. Kabudi amesema kuwa, vitendo vinavyofanywa
na raia wachache wa Afrika Kusini vya kuwashambulia raia kutoka nchi zingine za
Afrika na kuharibu mali zao vinasikitisha na kuivunjia heshima nchi hiyo. Hata
hivyo, alisema kuwa Serikali ya Tanzania inaunga mkono kauli ya Rais wa Afrika
Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa aliyoitoa hivi karibuni ya kukemea na kulaani
vikali vitendo vinavyofanywa na raia hao wachache.
Aidha, ameongeza kuwa, vitendo hivyo ambavyo vinatokana na raia hao wengi kukosa
ajira, ardhi na pia kutopenda kujishughulisha havihalalishi watu wengine
wakiwemo watanzania kulipa kisasi kwa namna yoyote ile.
“Ni jambo la kusikitisha lakini Serikali ya Afrika
Kusini inalisimamia kikamilifu na sisi tupo tayari kushirikiana nao ili
kulitafutia ufumbuzi wa kudumu.Nawasihi Watanzania wenzangu tusilipize kisasi
na tutaendelea kuwalinda raia wa Afrika Kusini waliopo Tanzania kwani tunaamini
kuwa Afrika ni moja na waafrika ni ndugu zetu” alisema Prof. Kabudi.
Kadhalika, Prof. Kabudi alieleza kuwa hadi sasa hakuna
taarifa kuhusu Mtanzania kuuawa, kujeruhiwa au kuharibiwa mali kutokana na
vurugu hizo. Pia alisema kuwa Wizara itaendelea kutoa taarifa za uhakika kadri
zinavyopatikana kutoka kwenye vyanzo vya uhakika ukiwemo Ubalozi wa Tanzania
nchini Afrika Kusini.
Wakati huohuo, Mhe. Prof. Kabudi amewaaga wanafunzi 44 kati ya 100
waliochaguliwa kwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo kwa vitendo kwa
kipindi cha miezi tisa kuanzia mwezi Septemba 2019. Wanafunzi hao ambao wengi
wamehitimu katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Taasisi ya Kilimo ya
Uyole ya Mbeya na Ukiriguru ya Mwanza wanakwenda kushiriki mafunzo hayo ya
vitendo kwenye sekta mbalimbali za kilimo ikiwemo uzalishaji na teknolojia. Kati ya Wanafunzi hao, 16 wameondoka nchini tarehe 4 Septemba, 2019, kuelekea Israel, 44 wataondoka nchini tarehe 5 Septemba 2019 na idadi iliyosalia itaondoka tarehe 10 Septemba 2019.
Katika hotuba yake, Mhe. Prof. Kabudi amewataka
wanafunzi hao vijana kuzingatia mafunzo hayo ili kuja kutoa mchango wao kwenye
mapinduzi ya kilimo ambayo yatachochea mapinduzi ya viwanda nchini. Aidha
aliwaasa kuwa waadilifu, kufanyakazi kwa bidii, kushikamana na kujiepusha na
vitendo viovu.
“Mnaenda Israel kutafuta ujuzi, uzoefu na ubunifu katika
maeneo ya uzalishaji mazao. Hivyo tunaamini kuwa mna nafasi kubwa ya kuja
kuibadilisha Tanzania katika eneo la kilimo na mtaleta mapinduzi ya kilimo
kwani vijana mpo wengi nchini, mna ari na ni nguvu kazi ya Taifa” alisisitiza
Prof. Kabudi.
Akiielezea Israel, Mhe.Prof. Kabudi amesema kuwa nchi hiyo
ni nusu jangwa kama ilivyo baadhi ya mikoa hapa nchini. Hata hivyo Israel
inaongoza kwa kuuza mazao ya mbogamboga na matunda kwenye nchi za Ulaya
kutokana na watu wa nchi hiyo kutumia maarifa katika kugeuza ukame kuwa fursa.
Hivyo aliwataka wanafunzi hao kuhakikisha wanapata maarifa na kujifunza mbinu
bora na teknolojia za kisasa ili kuja kuendeleza kilimo kikiwemo kile cha
umwagiliaji kwenye mikoa kama Singida, Manyara, Shinyanga na Dodoma.
Wanafunzi hao mia moja (100) wamechaguliwa kati ya
wanafunzi 1,440 waliotuma maombi ya kwenda kushiriki program ya mafunzo ya
kilimo nchini Israel ambayo hufanyika kwa kipindi cha miezi tisa. Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliratibu zoezi la upatikanaji
wa wanafunzi hao kwa maelekezo ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa mwezi Novemba 2018 alipofanya mazungumzo
na Balozi wa Israel nchini, Mhe. Noah Gal Gendler.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar
es Salaam.
4 Septemba 2019
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.