Friday, September 13, 2019

MAADHIMISHO YA SIKU YA MARA YAFUNGULIWA RASMI

     

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MAADHIMISHO YA SIKU  YA MARA YAFUNGULIWA RASMI

Maadhimisho ya Siku ya Mara maarufu "Mara Day" yamefunguliwa rasmi tarehe 12 Septemba, 2019 na Mhe. Adam Malima Mkuu wa Mkoa wa Mara, katika uwanja wa Sokoine uliopo Mugumu, wilayani Serengeti. 

Maadhimisho haya yanayo adhimishwa kwa mzunguko kati ya nchi mbili za Tanzania na Kenya hufanyika kila mwaka, ambapo mwaka huu yanafanyika Tanzania katika Mji wa Mugumu wilayani Serengeti kuanzia tarehe 12 hadi 15 Septemba, 2019 yakiongozwa na kauli mbiu "Mimi ni Mto Mara, Nitunze Nikutunze".

 Madhimisho ya Siku ya Mara yanayolenga kuhimiza na kuhamasisha wananchi wanaozunguka bonde la mto Mara kuhifadhi mazingira ya mto, ili kulinda ikolojia ya bonde hilo ambalo ni muhimu kwa utastawi wa mazingira na uchumi wa jamii ya Tanzania na Kenya. Akizungumza katika sherehe za ufunguzi wa maadhimisho Mhe. Malima ambaye pia ni mgeni wa heshima katika sherehe hizo amesema, "ni jukumu la jamii na kizazi cha sasa kuhakikisha kuwa mazingira ya bonde la mto Mara yanaendelea kubaki salama na kustawi kwa mafuaa ya kizazi kilichopo na kijacho". 

Aidha, amewahamasisha  wananchi wa Mkoa wa Mara kuchangamkia fursa zinazotoka na maadhimisho hayo ikiwemo uuzaji wa bidhaa mbalimbali kwenye maonesho yanayoendelea  katika kipindi cha maadhimisho.

Maadhimisho ya Siku ya Mara yanafanyika ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afrika Mashariki la Bonde la Ziwa Victoria, uliofanyika terehe 4 Mei, 2012 jijini Kigali, Rwanda. Kilele cha maadhimisho haya hufanyika tarehe 15 Septemba kila mwaka ambayo pia inawiana na tukio la uhamaji wa wanyama pori kutoka Tanzania kwenda Kenya.

Bw. Eliabi Chodota Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, akizungumza na wanahabari amesisiza kuwa Serikali ya Tanzania na Kenya zimejidhatiti katika kuhifadhi bonde la mto Mara na kuwaasa wananchi wanaozunguka mazingira ya bonde hilo kuunga mkono jitihada za Serikali.
     
Maadhimisho haya yatakayofanyika kwa siku 4 yanahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo zoezi la upandaji miti ambapo, zaidi ya miti 500 itapandwa katika maeneo yanayozunguka bonde hilo. Vilevile yatahusisha uwekwaji wa alama za kuonesha mipaka ya ukomo wa shughuli za binadamu katika bonde hilo, mita kadhaa kutoka ukingo wa mto Mara.

Kwa mara ya kwanza maadhimisho haya yalifanyika tarehe 15 Septemba, 2012 mjini Mulot, Kenya yakiongozwa na kauli mbiu "Mara - Uhai wetu".


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam.
12 Septemba 2019
Mhe. Adam Malima Mkuu wa Mkoa wa Mara, akihutubia hadhira iliyojitokeza (hawapo pichani) kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Mara..
Moja ya banda linaloonesha na kuuza bidhaa za wajasiliamali katika maadhimisho ya siku ya Mara lililopo uwanja wa Sokoine - Mugumu, Serengeti.
Watendaji mbalimbali wa Serikali, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, na viongozi wa dini wakiwa tayari kumlaki mgeni wa heshima katika sherehe za ufunguzi Mhe. Adam Malima Mkuu wa Mkoa wa Mara .
Meza kuu wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Taifa ukipigwa kabla ya kuanza kwa sherehe za ufunguzi

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.