FAO YAISHAURI TANZANIA KUHUSU MAZAO YA KILIMO KATIKA SOKO LA KIMATAIFA
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeishauri Tanzania kuweka kipaumbele katika zao moja la kilimo litakaloitambulisha Tanzania Kimataifa ili kuweza kupenya kirahisi katika soko la Kimataifa la mazao ya kilimo.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Dkt. Qu Dongyu alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula(Mb) mazungumzo yaliyofanyika katika makao makuu ya Shirika hilo Roma,Italia.
Dkt. Qu Dongyu ameongeza kuwa Tanzania ina mazao muhimu na mengi ya kilimo ambayo yanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza pato la Taifa lakini changamoto kubwa ni namna ya kupenya katika soko la kimataifa kutokana na kukosa zao la utambulisho na kwamba Shirika hilo FAO iko tayari kusaidia ujuzi na kuijengea uwezo Tanzania kufikia lengo hilo .
Dkt. Qu Dongyu ameongeza kuwa kwa sasa FAO imeanzisha jukwaa maalum la kuwawezesha wanawake na vijana kunufaika na sekta ya kilimo kutokana na utafiti kuonesha kuwa wanawake wengi katika nchi zinazoendelea wanajihusisha na kilimo.
Katika mazungumzo hayo Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Libearata Mulamula amesema Tanzania imeupokea ushauri wa FAO na kwamba itaufanyia kazi ili kuiwezesha Tanzania kutambulika na kunufaika katika soko la Kimataifa la mazao ya kilimo ili kuwawezesha wakulima kujikomboa kiuchumi kwa kuongeza pato la kaya na hivyo kuinua uchumi wa Tanzania.
Ameongeza kuwa Tanzania imejipanga kikamilifu kunufaika na mpango wa Shirika la chakula na Kilimo la Umoja wa Matiafa (FAO) wa kuanzisha jukwaa maalum la kuwawezesha wanawake na vijana kunufaika na sekta ya kilimo kutokana na utafiti kuonesha kuwa wanawake wengi katika nchi zinazoendelea wanajihusisha na kilimo
Balozi Mulamula yuko Roma,Italia kushiriki Mkutano wa tatu wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi za Afrika na Italia pamoja na kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa amani.