Thursday, October 7, 2021

WAFANYABIASHARA, WAWEKEZAJI KUTOKA CZECH WAONYESHA UTAYARI KUWEKEZA TANZANIA

 Na Mwandishi wetu, Dar

Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Jamhuri ya Czech wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya kilimo hasa Pamba pamoja na viwanda vya nguo hapa nchini.

Akibainisha kuhusu utayari wa Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Czech, kuwekeza hapa nchini, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek amesema wamefurahishwa sana na mazingira ya biashara hapa Tanzania na wapo tayari kuwekeza katika sekta kilimo na viwanda.

Mhe. Staŝek ameyasema hayo wakati alipokutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi leo jijini Dar es Salaam.

Katika ziara yake ya kikazi hapa nchini, Mhe. Staŝek ameambatana na viongozi mbalimbali wa Jamhuri ya Czech akiwemo Naibu Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Czech, mhe. Karel Tyll pamoja na Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka nchini humo.  

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Meh. Miloslav Staŝek amesema yeye pamoja na wajumbe alioongozana nao wamejadiliana na uongozi wa TIC na kupata fursa ya kutambua masuala mbalimbali ya kuongeza ushirikiano ili kuimarisha sekta ya uwekezaji kati ya Czech na Tanzania kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Mimi na Timu yangu tumejadili mambo mbalimbali ya kuwekeza hapa Tanzania ikiwa ni pamoja na utengezaji wa ndege, kilimo, teknolojia pamoja na viwanda.

“Moja ya kampuni niliyoambatana nayo inauzoefu mkubwa katika uzalisha dawa na vifaa tiba, hivyo kampuni hii itakapo pata fursa ya kuwekeza hapa Tanzania itasaidia kuimarisha mahusiano yetu pamoja na kuboresha sekta ya afya,” Amesema mhe. Staŝek.

Mhe. Staŝek ameongeza kuwa wamekubaliana na uongozi wa TIC pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara kutafuta namna bora ya kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wale wa Czech ili kutoa fursa kwa kampuni mbalimbali za Czech kuja kuwekeza kwa wingi hapa Tanzania na wafanyabiashara wa Tanzania kuwekeza nchini Czech kwa maslahi ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi amesema kuwa mara baada ya mazungumzo ya awali, wawekezaji hao wameonsha nia kubwa sana ya kuwekeza katika Pamba na viwanda vya nguo hapa nchini.

“Wameonesha uwezo mkubwa katika biashara na uwekezaji kwenye maeneo ya ufundi wa ndege ambapo baadae kutakuwa na mafunzo mbalimbali ya kubadilishana ujuzi na fursa za uwekezaji……...lakini pia wamevutiwa na sekta ya kilimo hasa katika viwanda vya kutengeneza mafuta ya kula,” Amesema Dkt. Kazi

Nae Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa tunatangaza fursa za biashara na uwekezaji.

“Fursa za kupata wafanyabiashara kutoka Zchec zinazidi kuongezeka hapa nchini, hivyo nitoe rai kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji,” Amesema Dkt. Posi  

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali yaliyolenga kukuza na kuimarisha sekta ya uwekezaji baina ya Tanzania na Czech hapa nchini. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek akiongea na uongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Maduhu Kazi leo jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek wakati Waziri Staŝek alipotembelea taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam


Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi (wa kwanza kulia) akieleza jambo wakati wa mkutano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek na uongozi wa TIC


Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek akimueleza jambo Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam 


Mkutano ukiendelea



Wednesday, October 6, 2021

BALOZI MULAMULA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI MKUU WA FAO, ROMA - ITALIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Dkt. Qu Dongyu. Mazungumzo hayoyamefanyika Makao Makuu ya Shirika hilo yaliyopo Roma,Italia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Dkt. Qu Dongyu. Wengine katika picha ni ujumbe wa Balozi Mulamula na Dkt. Qu wakifuatilia mazungumzo hayo

Balozi wa Tanzania Nchini Italia Balozi Mahmoud Kombo (kulia) akiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ulaya na Amerika Bw. Gerald Mbwafu (katikati) pamoja na Katibu wa Waziri Bw. Charles Mmbando wakifuatilia mazungumzo ya Balozi Mulamula (Mb) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa FAO (hawako pichani)

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa amesimama katika nembo ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) iliyopo katika makao makuu ya Shirika hilo yaliyopo Roma Italia,kabla ya kukutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo  Dkt. Qu Dongyu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia Balozi Mahmoud Kombo wakiwa katika picha ya pamoja Katika nembo ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) iliyopo katika makao makuu ya Shirika hilo yaliyopo Roma Italia,kabla ya kukutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo  Dkt. Qu Dongyu


FAO YAISHAURI TANZANIA KUHUSU MAZAO YA KILIMO KATIKA SOKO LA KIMATAIFA

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeishauri Tanzania kuweka kipaumbele katika zao moja la kilimo litakaloitambulisha Tanzania Kimataifa ili kuweza kupenya kirahisi katika soko la Kimataifa la mazao ya kilimo.

 

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Dkt. Qu Dongyu alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula(Mb) mazungumzo yaliyofanyika katika makao makuu ya Shirika hilo Roma,Italia.

 

Dkt. Qu Dongyu ameongeza kuwa Tanzania ina mazao muhimu na mengi ya kilimo ambayo yanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza pato la Taifa lakini changamoto kubwa ni namna ya kupenya katika soko la kimataifa kutokana na kukosa zao la utambulisho na kwamba Shirika hilo FAO iko tayari kusaidia ujuzi na kuijengea uwezo Tanzania kufikia lengo hilo .

 

Dkt. Qu Dongyu ameongeza kuwa kwa sasa FAO imeanzisha jukwaa maalum la kuwawezesha wanawake na vijana kunufaika na sekta ya kilimo kutokana na utafiti kuonesha kuwa wanawake wengi katika nchi zinazoendelea wanajihusisha na kilimo.

 

Katika mazungumzo hayo Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Libearata Mulamula amesema Tanzania imeupokea ushauri wa FAO na kwamba itaufanyia kazi ili kuiwezesha Tanzania kutambulika na kunufaika katika soko la Kimataifa la mazao ya kilimo ili kuwawezesha wakulima kujikomboa kiuchumi kwa kuongeza pato la kaya na hivyo kuinua uchumi wa Tanzania.

 

Ameongeza kuwa Tanzania imejipanga kikamilifu kunufaika na mpango wa Shirika la chakula na Kilimo la Umoja wa Matiafa (FAO) wa kuanzisha jukwaa maalum la kuwawezesha wanawake na vijana kunufaika na sekta ya kilimo kutokana na utafiti kuonesha kuwa wanawake wengi katika nchi zinazoendelea wanajihusisha na kilimo

 

Balozi Mulamula yuko Roma,Italia kushiriki Mkutano wa tatu wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi za Afrika na Italia pamoja na kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa amani.

 

 

Tuesday, October 5, 2021

UBALOZI WA TANZANIA NCHINI NAMIBIA WAANDAA MAONYESHO YA BIASHARA

Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia umeandaa maonyesho ya biashara yanayofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 8 Oktoba, 2021 katika Kituo cha Biashara cha Wernhil (Wernhil Shopping Mall) kilichopo mjini Windhoek. Maonesho haya muhimu katika utelezaji wa Diplomasia ya Uchumi yanalenga kutangaza bidhaa za Tanzania na Utalii nchini humo ili kukuza biashara na kuvutia wawekezaji nchini. 

Katika maonesho hayo Ubalozi umewashirikisha Watanzania wajisiriamali na wafanyabiashara waishio nchini humo (diaspora) ambao wamejitokeza kuonesha bidhaa mbalimbali ikiwemo mchele, korosho, kahawa, asali, majani ya chai, maharagwe, vitenge, batiki na nguo za kufuma.

Sambamba na kunesha bidhaa maonyesho haya yamejumuisha uuzaji wa vyakula mbalimbali vya kitanzania ambavyo vimekuwa vivutio kwa wateja wengi.

Maonesho hayo yalifunguliwa na Balozi wa Tanzania nchini Namibia Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba tarehe 4 Oktoba 202.
Balozi wa Tanzania nchini Namibia Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba akiwasili katika Kituo cha Biashara cha Wernhil (Wernhil Shopping Mall) kilichopo mjini Windhoek, Namibia kwa ajili ya ufunguzi wa maonesho ya biashara.
Balozi wa Tanzania nchini Namibia Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba akitazama sehemu ya bidhaa za Kitanzania kwenye maonesho yanayoendelea katika Kituo cha Biashara cha Wernhil Shopping Mall mjini Windhoek, Nambia.
Balozi wa Tanzania nchini Namibia Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wafanyabiashara wa Kitanzania waliojitokeza kuonesha bidhaa zao kwenye maonesho yanayoendelea katika Kituo cha Biashara cha Wernhil Shopping Mall mjini Windhoek, Namibia. 
Sehemu ya wafanyabiashara wa Kitanzania wakionesha bidhaa zao kwenye maonesho yanayoendelea katika Kituo cha Biashara cha Wernhil Shopping Mall mjini Windhoek, Namibia.
Balozi wa Tanzania nchini Namibia Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa Ubalozi huo walipotembele maonesho ya Biashara yanayoendelea katika Kituo cha Biashara cha Wernhil Shopping Mall mjini Windhoek, Namibia.

Monday, October 4, 2021

Mwenyekiti Mtendaji wa Shell ateta na Balozi wa Tanzania

Makamu wa Rais na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Shell ya Uholanzi mwenye makazi yake Tanzania, Bw. Jared Kuehl alitembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Uholanzi na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Irene Kasyanju hivi karibuni. 

Katika mazungumzo hayo, Pamoja na mambo mengine, Bw. Kuehl alimhakikishia Balozi Kasyanju utayari na dhamira ya dhati ya Kampuni yake kuendelea kuwekeza Tanzania kwa kutekeleza Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (Liquified Natural Gas - LNG) kwa kushirikiana na Kampuni ya Equinor ya Norway. 

Bw. Kuehl alisema anafurahishwa na ushirikiano ambao Ofisi yake (Shell Exploration & Production Tanzania Ltd) imekuwa inapata nchini Tanzania na kwamba hatua zinazochukuliwa na Serikali hivi sasa ni za kuridhisha wakati kampuni hiyo inapojiandaa kufanya majadiliano ya pamoja yanayolenga kufanikisha utekelezaji wa Mradi wa LNG.

“Kimsingi Kampuni ya Shell imefurahishwa na uamuzi wa Serikali kukubali Kampuni hizi mbili ziungane na zifanye kazi pamoja na namna inavyoandaa taratibu zinazohusu masuala ya kisheria na kiufundi, udhibiti wa Mradi pamoja na masuala ya kikodi yanayohusu Mradi huo wa NLG nchini”, Bw. Kuehl alisema.

Kwa upande wake, Balozi Kasyanju alifurahishwa na ujio wa Kiongozi huyo na kutumia fursa hiyo kumshukuru kwa kufika Ubalozini, kuishukuru Shell na Equinor kuwekeza Tanzania, na kuelezea matarajio yake kwamba uwekezaji huo utakuwa ni wa manufaa kwa pande zote mbili. Alimhakikishia Makamu wa Rais na Mwenyekiti Mtendaji huyo ushirikiano endelevu wa Ubalozi wake na wa Serikali nzima kwa ujumla.

Saturday, October 2, 2021

WAZIRI MULAMULA ASHIRIKI MAADHIMISHO YA MIAKA 61 YA UHURU WA NIGERIA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameshiriki sherehe ya Maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Taifa hilo iliyoandaliwa na Ubalozi wa Nigeria hapa nchini. 

Sherehe za Maadhimisho hayo ambazo zimefanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam zimehudhuriwa na wawakilishi kutoka makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo, Wafanyabiashara, Wanadiplomasia, Watendaji na Viongozi kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali. 

Akizungumza katika sherehe za maadhimisho hayo Waziri Mulamula licha ya kuipongeza Serikali ya Shirikisho la Nigeria kwa kuendelea kulinda Uhuru wake na kudumisha amani na usalama pia, amepongeza hatua ya maendeleo ya kiuchumi iliyofikiwa na Taifa hilo chini ya uongozi mahiri wa Rais Mhe. Muhammadu Buhari. Aliongeza kusema kwa kutambua hilo Tanzania itaendelea kudumisha na kukuza mahusiano ya kidiplomasia na kibiashara na Nigeria ili kwa pamoja kuweza kunufaika kiuchumi kutokana na fursa zilizopo. 

Kwa upande wake Balozi wa Nigeria hapa nchini Mhe. Hamisu Takalmawa amesema Serikali ya Shirikisho la Nigeria itaendelea kutumia matunda ya Uhuru wake kwa kuchukua hatua stahiki za kuboresha na kukuza mahusiano mazuri ya Kidiplomasia yaliyopo baina yake na Mataifa mengine ulimwenguni. 

Nigeria ilipata Uhuru wake Oktoba 1, 1960
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akifurahia jambo kwenye sherehe za Maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Nigeria zilizofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akihutubia katika sherehe za Maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Nigeria zilizofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Nigeria nchini Tanzania Mhe. Hamisu Takalmawa akihutubia kwenye sherehe za Maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Nigeria zilizofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Balozi wa Nigeria nchini Tanzania Mhe. Hamisu Takalmawa (kulia) na Balozi wa Comoro hapa nchini Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih (kushoto) wakikata keki kwenye sherehe za Maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Nigeria
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akihutubia katika sherehe za Maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Nigeria zilizofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja Wanadiplomasia walioshiriki katika sherehe za Maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Nigeria
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Balozi wa Nigeria nchini Tanzania Mhe. Hamisu Takalmawa (kulia) na Balozi wa Comoro hapa nchini Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih (kushoto) wakifuatilia matukio yaliyokuwa yakiendelea kwenye sherehe za Maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Nigeria

Friday, October 1, 2021

WAZIRI MULAMULA AWAAGA MABALOZI WALIOMALIZA MUDA WA UWAKILISHI NCHINI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) kwa nyakati tofauti amewaaga Balozi wa Indonesia Mhe. Prof. Ratlan Pardede na wa Ethiopia Mhe.Yonas Yosef Sanbe ambao wamemaliza muda wao wa uwakilishi hapa nchini.

Waziri Mulamula akiongea katika hafla ya kuwaaga Mabalozi hao iliyofanyika kwa nyakati tofauti katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, amewapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kudumisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi wanazoziwakilisha (Indonesia na Ethiopia).

Akizungumza na Balozi wa Indonesia Waziri Mulamula amemuahidi Mhe.Balozi Prof. Pardede kuwa licha ya mahusiano mazuri ya Kidiplomasia yaliyopo, Tanzania itaendelea kushirikiana na Indonesia katika sekta za elimu, kilimo na tehama kwa maslahi ya Nchi zote mbili. 

“Kwa niaba ya Serikali, naishuru Indonesia kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania za kuendeleza kilimo kwa kutoa fursa za masomo kwa vijana wetu, kusomea musuala mbalimbali katika Kilimo na Teknolojia, jambo ambalo litachangia kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya Kilimo hapa nchini” Waziri Mulamula. 

Kwa upande wake Balozi wa Indonesia Mhe. Prof. Pardede licha ya kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa ushirikiano wa kutosha wakati akitekeleza majukumu yake katika kipindi chote alichokuwepo hapa nchini. Vilevile ameelezea kufurahishwa kwake na mahusiano mzuri yaliyopo baina ya Indonesia na Tanzania.

Wakati huohuo Balozi wa Ethiopia hapa nchini Mhe. Sanbe amepongeza hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Tanzania imeendelea kuzichukua katika kutekeleza diplomasia ya uchumi sambamba na kutoa msukumo wa matumizi ya lugha ya Kiswahili barani Afrika. Aidha ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kudumisha na kukuza mahusiano ya Kidiplomasia na Ethiopia.

Tanzania na Ethiopia zimeendelea kuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri wa muda mrefu. Nchi hizi mbili zimeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo kukuza lugha ya Kishwahili, utalii, ulinzi na usalama, na usafiri wa anga.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Indonesia hapa nchini Mhe. Prof. Ratlan Pardede yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimsikiliza Balozi wa Indonesia Mhe. Prof. Ratlan Pardede ambaye anamaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini. Wa kwanza kulia ni Balozi Caesar Waitara Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia akifuatilia mazungumzo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Indonesia hapa nchini Mhe. Prof. Ratlan Pardede yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
Mazungumzo yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Ethiopia anayemaliza kipindi cha uwakilishi wake hapa nchini Mhe.Yonas Yosef yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza Balozi wa Ethiopia anayemaliza kipindi cha uwakilishi wake hapa nchini Mhe. Yonas Yosef wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza Balozi wa Ethiopia anayemaliza kipindi cha uwakilishi wake hapa nchini Mhe.Yonas. Wa kwanza kulia ni Balozi Naimi Azizi Mkurugenzi wa Idara ya Afrika akifuatilia mazungumzo
Mazungumzo yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Indonesia Mhe. Prof. Ratlan Pardede wakiwa katika mazungumzo.