Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Rwanda umeanza kufanyika leo tarehe 25 Oktoba 2021 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Tanzania. Mkutano huu utakaofanyika kwa kipindi cha siku nne kuanzia tarehe 25 hadi 28 Oktoba, 2021 unalenga kujadili mambo mbalimbali muhimu ya ushirikiano ikiwemo Mahusiano ya Kidiplomasia, miundombinu na usafirishaji, Sekta ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo, nishati, utalii na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano sambamba na kuibua maeneo mapya ya ushikiano kwa lengo la kuchagiza maendeleo baina ya Mataifa haya mawali (Tanzania na Rwanda).
Mkutano huu muhimu kwa ustawi wa ushirikiano na maendeleo baina ya mataifa haya mawili, unafanyika kwa lengo la kufanya ufuatiliaji na tathimini ya utelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Paul Kagame Rais wa Jamhuri ya Rwanda, wakati wa ziara yake aliyoifanya Nchini Rwanda Agosti 2, 2021.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo katika ngazi ya Wataalamu, Balozi Naimi S.H. Azizi, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amebainisha kuwa mkutano huo umetoa fursa hadhimu kwa pande zote mbili kukutana ili kutathmini utekelezaji pia kuweka mipango na mikakati ya pamoja itakayoimarisha ushirikiano kwenye utekelezaji wa vipaumbele vya shughuli za maendeleo katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili. “Natambua dhahiri kuwa Mkutano huu wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano utatuwezesha kufanya tathimini na kubaini hatua tuliyoifikia katika utekezaji wa maagizo yaliyotolewa na Wakuu wetu wa Nchi hizi mbili (Tanzania na Rwanda). Nimatumaini yangu pia, kuwa Mkutano huu utatuwezesha kuweka mikakati na mipango ya pamoja itakayotuwezesha kuongeza kasi ya kutekelezaji katika maeneo ambayo bado hatujafanya vizuri.”Alisema Balozi Naimi S.H. Azizi.
Balozi Naimi S.H. Azizi aliongeza kusema kuwa ni muhimu wajumbe wa mkutano wajikite katika kujadili masuala muhimu yenye maslahi kwa pande zote mbili ili kukidhi matarajio ya Wakuu wa Nchi hizi mbili, ya kuona Wataalamu katika Serikali wanazoziongoza wanaendelea kuwajibika ipasavyo katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Mkutano huu umejumuisha Viongozi, Watendaji na Maafisa mbalimbali wa Serikali kutoka Tanzania na Rwanda.