Friday, October 29, 2021

TANZANIA NA RWANDA ZASAINI HATI YA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA ULINZI

Tanzania na Rwanda zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Ulinzi (Memorandum of Understanding between United Republic of Tanzania and Republic of Rwanda on Defence Cooperation). Hati hiyo imesainiwa tarehe 28 Oktoba, 2021 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda Mhe. Dkt. Vincent Biruta kwenye Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ya Kudumu uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza kwenye Mkutano huo, Waziri Mulamula ameeleza kuwa miongoni mwa faida za mkutano huo ni kusainiwa kwa Hati hiyo ya Makubaliano ambayo itasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa watu,mali na mipaka baina ya Mataifa haya mawili.

“kusainiwa kwa Hati hii ni hatua muhimu kwenye mahusiano kati ya nchi zetu hizi mbili, vilevile nina imani kubwa yale yote yaliyokubalika yatatekelezwa kwa ufanisi ili kufikia malengo tarajiwa ya nchi hizi mbili na Serikali kwa ujumla” amesema Balozi Mulamula.

Sambamba na kusaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Ulinzi, Tanzania na Rwanda zilijadili na kukubaliana kuhusu maeneo mengine mapya ya ushirikiano ikiwemo Manunuzi ya Umeme kutoka Mradi wa Rusumo, Ushirikiano katika Uchimbaji wa Petroli na Gesi na kubadilishana wanafunzi kati ya Chuo cha Diplomasia cha Tanzania na Chuo cha Diplomasia cha Rwanda kinachorajiwa kuanzishwa mwaka 2022.

Kwa upande wake, Dkt. Birtua aliipongeza na kuishukuru Tanzania kwa kuandaa, kushiriki kikamilifu na kuupa uzito wa hali ya juu Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda ambapo alisema kuwa hiyo ni dalili njema inayoonesha nia iliyopo ya kudumisha na kukuza ushirikiano wa kihistoria na kindugu uliopo kati ya kati Nchi hizi mbili.

Vilevile Balozi Mulamula alitoa wito kwa Sekta zinazohusika na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano huo, kuhakikisha zinatekeleza kikamilifu maagizo yaliyotolewa na kuwasilisha ripoti zake katika Mkutano wa Kamati ya Pamoja ya Utekelezaji uliopangwa kufanyika mwezi Machi, 2022 nchini Rwanda. 

Mkutano huu wa Kumi na Tano (15) wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ya Kudumu ulitanguliwa na Kikao cha Wataalamu wa Tanzania na Rwanda kilichofanyika tarehe 25 na 26 Oktoba, 2021 na kufuatiwa na Kikao cha Makatibu Wakuu wa nchi hizi mbili kilichofanyika tarehe 27 Oktoba, 2021.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiongoza Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda katika ngazi ya Mawaziri uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda katika ngazi ya Mawaziri uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Meza kuu wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Taifa wa Tanzania na Rwanda unaimbwa kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika ngazi ya Mawaziri
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda Mhe. Dkt. Vincent Biruta akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwandakatika ngazi ya Mawaziri uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa Mkutano kutoka Tanzania na Rwanda wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Mataifa hayo mawili unaimbwa kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika ngazi ya Mawaziri
Mkutano ukiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda Mhe. Dkt. Vincent Biruta wakisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Ulinzi.
Picha ya pamoja ya Viongozi walioshiriki Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda
Picha ya pamoja ya washiriki wa Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.