Na Waandishi wetu, Dar
Umoja wa Ulaya umeoneshwa kuridhishwa na mazingira ya uwekezaji na ufanyaji wa biashara nchini Tanzania na kuahidi kuhamasisha wawekezaji kutoka katika umoja huo kuja kuwekeza na kufanya biashara zaidi.
Akizungumza katika ufunguzi wa majadiliano kuhusu masuala mtambuka na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti mwenza wa Kikao hicho ambaye pia ni Mkurugenzi Mwendeshaji anayeshughulikia masuala ya Afrika kutoka Umoja wa Ulaya Balozi Rita Liranjinha amesema Umoja wa Ulaya Umeridhishwa na mazingira ya biashara na uwekezaji hapa Tanzania na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika Sekta ya biashara na uwekezaji.
Balozi Rita pia amepongeza kitendo cha Tanzania kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali katika harakati za kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini na hivyo kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji wengi nchini.
Kadhalika, Balozi Rita ameipongeza Tanzania kwa kufanya kazi na watanzania wote hasa sekta binafsi kwani huchangia kutoa ajira kwa watu wengi na kuichangia kuinua maendeleo.
“Naipongeza Serikali kwa kusikiliza sauti za wananchi na kuchukua hatua kukabiliana na changammoto zinazowakabili wananchi kwa wakati ambacho amekielezea kuwa ni sawa na kupanda mbegu ya matumaini kwa wanachi,” amesema Balozi Rita.
Ameongeza kuwa Umoja wa Ulaya unaiona Tanzania ni mdau mkubwa wa Tanzania na kwamba umoja huo utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha maendeleo ya kweli yanapatikana kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na Tanzania kuboresha mazingira bora ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kama Uviko 19, mabadiliko ya tabia nchi na kuondoa umasikini,” amesema Balozi Rita.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti mwenza wa majadiliano hayo, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameupongeza Umoja wa Ulaya kwa utayari wake wa kuisaida Tanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili dunia kwa sasa.
Balozi Mulamula amesema Uhusiano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya umedumu kwa muda mrefu na kwamba Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya katika kukuza na kuendeleza ushirikiano huo kwa maslahi ya pande zote mbili hasa katika kukuza na kuendeleza biashara, uwekezaji, haki za binadamu na mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO19.
Balozi Mulamula ameihakikisha Jumuiya hiyo kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya katika harakati zake za kupambana na umasikini nchini hata kwa nchi nyingine zinazoizunguka.
Ameongeza kuwa pamoja na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza kama vile ugonjwa wa Uviko 19, Tanzania itaendelea kuchukua tahadhari na kuimarisha sekta ya afya ili kuendelea kupambana na janga hilo.
Waziri Mulamula ameuhakikishia Umoja wa Ulaya kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili kukuza uchumi na hivyo kuleta maendeleo.
Majadiliano hayo yamehudhuriwa na mabalozi mbalimbali kutoka Umoja wa Ulaya ambao ni Balozi wa Umoja wa Ulaya, Ubelgiji, Finland, Sweden, Denmark, Italia, Czech, Ufaransa, Ujerumani, Hispania, Canada, Poland, Ireland na Uholanzi.