Tuesday, March 8, 2022

UBALOZI WA TANZANIA NCHINI ITALIA WAKUTANA NA WANADIASPORA

 Na Mwandishi wetu, Roma

Ubalozi wa Tanzania nchini Italia umekutana na kufanya Mkutano Mkuu na Jumuiya mbalimbali za Watanzania wanaoishi maeneo mbalimbali nchini Italia (Diaspora) kwaajili ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya pande mbili.

Akifungua mkutano huo mwishoni mwa wiki, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo alitoa wito kwa Watanzania hao kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuiletea Tanzania maendeleo.

“Nawashauri kujisajili katika daftari la Diaspora wa Italia ili kuwa na takwimu na kumbukumbu sahihi za Watanzania waliopo Italia. Takwimu na kumbukumbu hizi zitasaidia Ubalozi kuwaunganisha Wanadiaspora na wabia wa maendeleo ambao wana nia au tayari wanaendesha shughuli zao nchini Tanzania na wanahitaji kushirikiana na Diaspora,” Amesema Balozi Kombo.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulijadili masuala mbalimbali yanayowahusu wanadiaspora ikiwemo changamoto za kiutendaji na ushirikiano katika Jumuiya zao ambazo zilianishwa wazi kwenye taarifa za kiutendaji zilizowasilishwa na Viongozi wa Jumuiya.

Mkutano uliazimia kuendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya Wanadiaspora na Ubalozi kwa kuanisha mkakati thabiti wa kuboresha mawasiliano baina ya pande mbili.

Aidha, wanadiaspora hao wameahidi kuendelea kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia  katika kuiletea nchi yao maendeleo kwa kuwekeza nchini kwao. Kadhalika, Ubalozi umeahidi kutafuta suluhu ya kudumu dhidi ya changamoto zinazowakabili wanadiaspora waishio nchini Italia.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na wanadiaspora takriban 100 akiwemo Mhashamu Baba Askofu Mkuu Protase Rugambwa, Katibu Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu.

Nchini Italia zipo Jumuiya sita zinazotoka maeneo ya Roma, Napoli, Modena Central North, Genova, Modena na Umoja wa Watanzania Wakatoliki unaojumuisha Waklero, Watawa, Waseminari na walelewa wa Utawa wanaofanya kazi za kitume hapa Italia.

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akiongea na Wanadiaspora (hawapo pichani) wanaoishi nchini Italia wakati wa Mkutano 

Katibu wa Jumuiya ya Watanzania Roma akiwasilisha Bi. Anastacia Lubangila, taarifa ya Jumuiya hiyo wakati wa mkutano


Mhashamu Baba Askofu Mkuu, Protase Rugambwa akifuatalia majadiliano


Mwenyekiti Kamati Kuu ya Wanadiaspora Italia Bw. Maulid Kagutta, akiwasilisha taarifa ya Diaspora Italia 


Balozi Kombo akipokea picha ya nembo rasmi ya Jumuiya ya Watanzania Genova kutoka kwa Bi. Eva Nangela, Mwenyekiti wa Jumuiya (kushoto). Wanaoshuhudia (kulia) ni Bi. Zakia Kombo, Mwenza wa Mhe. Balozi; Baba Askofu Mkuu Rugambwa na Maafisa Ubalozi, Bw. Sigfried Nnembuka pamoja na Jacqueline Mbuya. 


Wanadiaspora wakifuatilia mkutano

Wanadiaspora wakifuatilia mkutano



Tanzania Yashiriki Maadhimisho ya Miaka 25 ya IORA

Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika  Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amewasilisha kwa njia ya mtandao salamu za pongezi ya Miaka 25 ya Jumuiya ya Nchi Wanachama wa Mwambao wa Bahari ya Hindi (Indian Ocean Rim Assocaition-IORA) yaliyofanyika jijini Mapou, Mauritius tarehe 7 Machi 2022.

Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki imewakilishwa na Balozi Agnes Richard Kayola, Mkurugenzi, Idara ya Ushirikiano wa Kikanda aliyeambatana na Dkt. Mnata Resani,  Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Katika Maadhimisho hayo, nchi wanachama zimepata fursa ya kutangaza Utamaduni wao kwa kupitia vyakula, nyimbo na ngoma za asili. Tanzania iliandaa chai na kahawa ya hapa nchini na Kikundi cha ngoma kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA) kilitumbwiza kwenye maadhimisho hayo.


Watu mbalimbali wakichukua vyakula vya Kitanzania vilivyoandaliwa kwa ajili ya kuadhimisha miaka 25 ya Jumuiya ya Nchi Wanachama wa Mwambao wa Bahari ya Hindi (Indian Ocean Rim Assocaition-IORA) yaliyofanyika jijini Mapou, Mauritius tarehe 7 Machi 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritius, Mhe. Alan Ganoo
 akitoa neno wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 25 ya umuiya ya Nchi Wanachama wa Mwambao wa Bahari ya Hindi (Indian Ocean Rim Assocaition-IORA) yaliyofanyika jijini Mapou, Mauritius tarehe 7 Machi 2022.

Mkurugenzi wa Idara ya Ushrikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola akiwa na wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma Mauritius.

Monday, March 7, 2022

WAZIRI MULAMULA AZINDUA BODI YA WAKURUGENZI YA AICC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) leo tarehe 7 Machi 2022 amezindua Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) katika hafla fupi iliyofanyika jijini Arusha. 

Akizungumza katika uzinduzi huo wa Bodi ya Wakurugezi, Waziri Mulamula ameeleza Wizara na Serikali kwa ujumla inaimani kubwa kuwa kutokana na taalamu, uzoefu na uadilifu wa wajumbe wa bodi hiyo wataiongezea AICC ufanisi na tija. “Wote tunafahamu vyema katika kipindi cha miaka miwili ya hivi karibuni Dunia imepitia changamoto ya janga la UVIKO-19 ambalo limeathiri biashara nyingi  duniani ikiwemo  Sekta ya Mikutano ya Kimataifa, hivyo kutokana na weledi wa wajumbe wa bodi hii kwa kushirikiana na Wafanyakazi bila shaka mtaenda kubuni njia mbadala za kuongeza mapato” amaeeleza Waziri Mulamula.

Kwa upande wake Balozi Begum Karim Taj ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo sambamba na kuzishukuru mamlaka za uteuzi kwa kuwaamini kuingoza AICC, ameelezea utayari wa Bodi ya Wakurugenzi hiyo katika kutimiza matarajio ya Serikali ya kuhakikisha AICC inaongeza ufanisi na kuleta tija nchini. “Tupo tayari kuifanya kazi iliyoko mbele yetu ya kuhakikisha AICC inaendelea kufanya kazi kwa weledi na ubunifu, kuitangaza nchi na wakati huo huo kuhakikisha mapato yake yanaongezeka. Hii ni pamoja na kuongeza msukumo katika kudai madeni ambayo Kituo kinadai kwa wateja wake na kuhakisha yanalipwa kwa wakati ili kuendelea kutoa fursa kwa AICC kufanya kazi kwa ufanisi zaidi”. Balozi Begum Taj

Aidha, Waziri Mulamula amewahakikishia ushirikiano Wajumbe wa Bodi hiyo katika kutimiza malengo waliyojiwekea.

Wakati huohuo Waziri wa Mambo ya Nje wa ushirikiano w Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula, leo Tarehe 7 Machi 2022 amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa UN Women wa Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika Dkt. Maxime Houinato jijini Arusha.

Mazungumzo yao yalilenga kukuza ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Tanzania na UN Women. Katika Mazungumzo hayo, Dkt. Houinato ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza jitihada zake za kumkomboa mwanamke katika nyanja zote za maendeleo.

Dkt. Houinato amemuhakikishia Mhe. Balozi Mulamula kuwa UN Women inathamini mchango wa Tanzania katika kuleta usawa wa kijinsia barani Afrika na itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha mipango yake ya kumkomboa mwanamke nchini inatekelezwa kwa ufanisi.

Kwa upande wake Mhe. Balozi Mulamula ameishukuru UN Women kwa kuendelea kuwa mdau mkubwa wa masuala ya wanawake Nchini. Aliishukuru UN Women kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake yanayolenga kuleta usawa wa kijinsia, kuwainua wanawake kiuchumi na kupambana na ukatili wa kijinsia.

Balozi Mulamula ameihakikishia UN Women utayari wa Serikali kuendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha kuwa Wanawake wanapiga hatua za kimaendeleo. 

Dkt. Houinato yuko Nchini kushiriki katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika Tarehe 8 Machi ya Kila mwaka.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb), Mkurugenzi wa UN Women wa Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika Dkt. Maxime Houinato (kushoto) muwakilishi wa UN Women nchini Bi Hodan Addou (kulia) walipokutana kwa mazungumzo jijini Arusha.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akipokelewa alipowasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kwa zoezi la uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akisaini kitabu cha Wageni alipowasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kwa zoezi la uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya AICC (walioketi) na Baadhi ya Watendaji wa AICC (waliosimama) baada ya hafla uzinduzi wa bodi hiyo Machi 7, 2022

Friday, March 4, 2022

WAZIRI MULAMULA AAGANA NA BALOZI WA KENYA NCHINI

 

Balozi wa Kenya hapa nchini ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi Mhe.  Dan Kazungu akizungumza  na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula alipofika katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam  kwa ajili ya kumuaga. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula  akimsikiliza Balozi wa Kenya ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini Mhe. Dan Kazungu katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula  akizungumza alipokutana na Balozi wa Kenya ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini Mhe. Dan Kazungu katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Kenya ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini Mhe. Dan Kazungu akizungumza alipofika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuagana na Mhe Waziri.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi zawadi Balozi wa Kenya hapa nchini Mhe.  Dan Kazungu ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini alipofika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuaga.

 

 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameagana na Balozi wa Kenya hapa nchini Mhe.  Dan Kazungu ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na balozi Kazungu Waziri Mulamula ameelezea kuridhishwa kwake na utendaji kazi uliotukuka wa Balozi Kazungu ambao umewezesha Tanzania na Kenya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kindugu, kijirani na kijamii ambao umekuwepo siku zote.

Amesema uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Kenya ni jambo lililochochewa na kazi nzuri iliyofanywa balozi Kazungu nchini na kuchochea ukuaji wa biashara, uwekezaji na ustawi wa jamii katika nchi hizo na amemuomba Balozi huyo kuwa balozi mzuri wa Tanzania pindi atakaporejea nyumbani kwao Kenya.

“Katika kipindi chako cha uwakilishi umeiwakilisha vyema Kenya hapa nchini na kuonesha mafanikio makubwa ambayo Tanzania na Kenya tumeyapata kwa pamoja, kazi yako imechochea ukuaji wa biashara uwekezaji na hata ustawi wa jamii katika nchi zetu, nikuombe ukawe balozi mzuri wa Tanzania nchini Kenya’, alisema Mhe. Waziri.

Naye Balozi wa Kenya hapa nchini Mhe. Dany Kazungu amesema anajivunia uwepo wake hapa nchini, amejifunza mengi ikiwemo kuthamini utu na ukarimu wa Watanzania, na amewashukuru Watanzania kwa upendo mkubwa waliomuonesha katika kipindi cha miaka minne aliyokuwepo nchini.

"shukurani nyingi kwa upendo wenu Watanzania, mhe. Waziri niwaombee heri na baraka zote katika harakati za kuijenga Tanzania, ni wakati mgumu kusema kwaheri lakini hakuna budi, tuendeee kushirikiana  na tufanye kazi pamoja ili kuleta maendeleo ya watu wetu, siku zote nitakumbuka utu na ukarimu wa Watanzania, mnathamini utu hakuna kukwezana, nimejifunza hili toka kwenu," alisema Mhe. balozi Kazungu

Amesema daima atakumbuka tabia ya Watanzania kutokutweza utu wa mtu na ukarimu wao na kuahidi kuwa atakuwa balozi mwema wa Tanzania nchini Kenya na kuwaombea heri na baraka katika hatau mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi, kijamii  na kisiasa ambazo Tanzania imekuwa ikizichukua chini ya Uongozi imara wa Rais Samia Suluhu Hassan.

 

WIZARA YAKABIDHI OFISI KWA CHAMA CHA MABALOZI WASTAAFU NCHINI



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mmbo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (kushoto) akizungumza wakati wa kukabidhi Ofisi kwa Chama cha Mabalozi Wastaafu nchni.
Mwenyekiti wa Chama cha Mabalozi Wastaafu nchini Balozi Celestine Christopher Liundi (kulia) akishukuru wakati wa hafla ya kukabiddhiwa Ofisi kwa Chma hicho huku Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mmbo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (kushoto) wakimsikiliza 
Mwenyekiti wa Chama cha Mabalozi Wastaafu nchini Balozi Celestine Christopher Liundi (kulia) akizungumza wakati wa hafla ya kukabiddhiwa Ofisi kwa Chma hicho huku Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mmbo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (kushoto) wakimsikiliza
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mmbo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (kushoto) wakimsikiliza katika picha ya pamoja na viongozi wa Chama cha Mabalozi Wastaafu nchini wakati wa hafla ya kukabiddhiwa Ofisi kwa Chama hicho zilizofanyika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na viongozi wa Chama cha Mabalozi Wastaafu nchni na baadhi ya viongozi wa Wizara wakati wa hafla ya kukabiddhiwa Ofisi kwa Chama hicho zilizofanyika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam. 



 

Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki umekabidhi ofisi kwa chama cha mabalozi Wastaafu nchini (ARTA).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekabidhi ofisi hizo zilizopo katika jengo la Wizara jijini Dar es salaam kwa niaba ya Wizara na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa wizara na watumishi .

Akikabidhi ofisi hizo Balozi Mulamula amesema ofisi hiyo iliyoko katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam itatatumiwa na mabalozi wastaafu hapa nchini ili kuwawezesha mabalozi hao kuendelea kutoa mchango wao katika ujenzi wa Taifa hususani katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

Akizungumza kwa niaba ya chama cha mabalozi wastaafu Mwenyekiti wa chama hicho Balozi Celestine Liundi amesema chama hicho kwa sasa kina wanachama hai 57 ambao bado wanaweza kuisaidia nchi katika nyanja ya uhusiano wa kimataifa. 

Balozi Liundi ameushukuru uongozi wa Wizara kwa kitendo cha kuwapatia ofisi ndani ya jengo la Wizara na kuongeza kuwa kitendo hicho kimewatia moyo wa kuendelea kutoa ushauri,mapendekezo na michango ya mawazo katika kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Mataifa mengine.

Thursday, March 3, 2022

WAZIRI MULAMULA AZINDUA BARAZA LA UONGOZI LA CHUO CHA DIPLOMASIA

 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza kuzindua Baraza la Uongozi la Chuo cha Diplomasia (CFR) cha jijini Dar es Salaam katika hafla iliyofanyika chuoni hapo jijini Dar es Salaam.

 Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Diplomasia (CFR) wakimsikiliza Waziri Mulamula wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza hilo jijini Dar es Salaam.

 

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Diplomasia (CFR) wakimsikiliza Waziri Mulamula wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza hilo jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha CFR Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi akizungumza neno la shukurani kwa Mhe. Waziri Mulamula baada ya uzinduzi wa Baraza la Chuo hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mulamula akimkabidhi kitendea kazi Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha CFR Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi katika hafla ya uzinduzi wa Baraza hilo iliyofanyika chuoni  hapo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Diplomasia (CFR) baada ya kuzindua baraza hilo jijini Dar es Salaam.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amezindua Baraza la Uongozi la Chuo cha Diplomasia (CFR) na kuwataka wajumbe wa Baraza hilo kufanya mabadiliko katika uendeshji wa Chuo hicho huku wakizangatia muktadha wa uanzishwaji wake

Balozi Mulamula amewataka wajumbe wa baraza hilo kuwasiliana na mamlaka husika ili CFR ibaki katika muundo wake wa asili yakiwemo maudhui ya kuanzishwa kwa chuo hicho ili kutojitenga kabisa na kuktadha huo huku kikiangalia namna bora ya kujiendesha.

“leo hii tuko hapa kuzindua Baraza la Chuo, Mwenyekiti na wajumbe wa Baraza hili, naomba muwasiliane na Mamlaka husika ili kuona namna Chuo kitakavyoweza  kuendelea kufuata  na kutekeleza nia na madhumuni ya kuanzishwa kwake na huku mkiangalia namna ya kujiendesha,”alisema Balozi Mulamula.

Amesema pamoja na kuwa Chuo kinaangalia namna mbalimbali za kujiendesha lakini hakiondoi jukumu lake la asili ambalo lililenga kuanzishwa kwake.

Amelitaka Baraza hilo kuangalia upya na kuandaa kozi mbalimbali ambazo walikuwa wakipatiwa maafisa mambo ya nje  ili kuwawezesha maafisa hao kwenda na wakati na kuongeza ujuzi.

Akizungumza katia uzinduzi huo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amesema Uteuzi wa wajumbe wa Baraza hilo la Chuo utasaidia Chuo katika utekelezaji wa majukumu yake hasa ikizingatiwa sifa za wajumbe wa baraza hilo.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi amemuhakikishia Mhe. Waziri  utayari wa wajumbe wa baraza hilo katika kutekeleza majukumu yake ili kukifanya chuo hicho kutimiza malengo yake.