Friday, March 18, 2022

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA DKT. STERGOMENA L. TAX AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA KAWAIDA WA SADC UNAOFANYIKA LILOLONGWE, MALAWI

   Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) akiongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa kawaida wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika Lilongwe Malawi (Machi 18 – 19,2022). Kushoto kwa Dkt. Tax ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor (Mb) Mbarouk,akifuatiwa na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) na Mipango na Naibu Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb)


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) pamoja na ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alioongozana nao wakifuatilia Mkutano wa kawaida wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaoendelea Lilongwe,Malawi

    Sehemu ya Mawaziri wa Mawaziri wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakiwa katika mkutano.


Mawaziri wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC )wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa kawaida wa Mawaziri wa SADC uofanyika Lilongwe Malawi Machi 18 – 19,2022

 

Balozi Possi Afanya Ziara ya Kikazi Jamhuri ya Czech

Balozi Possi Afanya Ziara ya Kikazi Jamhuri Czech

Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Czech mwenye makazi yake Berlin, Ujerumani, Dkt. Abdallah Possi amefanya ziara ya kikazi katika nchi ya Jamhuri ya Czech na kufanya mazungumzo na Naibu Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Miloslav Stašek; Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Jakub Dvořáček na Naibu Waziri wa Elimu, Mhe. Prof. Jaroslav Miller tarehe 17 Machi 2022.

Wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dkt. Possi aliwasilisha ombi ili Watanzania waweze kunufaika na Mpango wa Nafasi za Ufadhili wa Masomo unaoratibiwa na Wizara hiyo. Kwa sasa, nchi za Africa zinazonufaika na mpango huo ni Zambia na Ethiopia. Mhe, Naibu Waziri aliahidi kulifanyia kazi ombi hilo. Aidha, Mhe. Stašek aliwasilisha mualiko wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufanya ziara ya kikazi Jamhuri ya Czech.

Katika mazungumzo yake na Naibu Waziri wa Afya, Balozi Possi aliomba Serikali ya nchi hiyo kuangalia uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta ya Afya, hususan katika magonjwa ya moyo na figo. Serikali ya Jamhuri ya Czech imeahidi kulifanyia kazi ombi hilo na kuahidi pia kuwa ipo tayari kuisaidia Tanzania dozi za chanjo ya UVIKO-19.

Kwa upande wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Elimu, wawili hao walijadili kuhusu ushirikiano wa Vyuo Vikuu, na namna ambavyo wanafunzi wa Tanzania waliokatiza masomo nchini Ukraine wanaweza kurahisishiwa mchakato wa kuhamisha alama na kumalizia masomo yao katika vyuo vikuu vya Czech.  Prof. Miller alimweleza Balozi Dkt. Possi wataanza na utaratibu wa awali wa kuvitaarifu vyuo vikuu vya Czech na kutoa kipaumbele kwa wanafunzi wa Tanzania, huku taratibu nyingine za kiufundi zikifuata.

Mhe. Miller aliahidi pia kuwa mamlaka husika zitaweka tangazo katika tovuti ya “Study in Czech Republic” ili  kuwahamasisha wanafunzi wa Tanzania waliokuwa Ukraine kuomba kujiunga na vyuo vikuu Jamhuri ya Czech.

 

Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Czech mwenye makazi yake Berlin, Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe.Miloslav Stašek walipokutana kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi zao.

Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Czech mwenye makazi yake Berlin, Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi akisalimiana na Naibu Waziri wa Elimu wa Jamhuri ya Czech,Mhe. Prof. Jaroslav Miller walipokutana kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano baina ya sekta za afya za nchi zao.

Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Czech mwenye makazi yake Berlin, Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi akisalimiana na Naibu Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Jakub Dvořáček walipokutana kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano baina ya sekta za elimu za nchi zao.

 


 

WFP YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUBORESHA SEKTA YA KILIMO NCHINI

Na Mwandishi wetu, Dar 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeahidi kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha kilimo nchini na kukifanya kuwa cha kisasa zaidi.

Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini mwa Afrika wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Dkt. Menghestab Haile alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Haile amesema WFP inajivunia uhusiano mzuri na Tanzania na itaendelea kudumisha uhusiano na ushirikiano huo kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Leo tumejadili na kuona ni namna gani tunaweza kuwaunga mkono wakulima wa Tanzania ili waweze kupata faida zaidi kupitia kilimo ambapo faida hiyo itawasaidia kuyaboresha zaidi maisha yao,” amesema Dkt. Haile

“………… kwa kuwa kilimo ndiyo sekta pekee inayotoa fursa ya ajira kwa wingi duniani, tuna mkakati wa kuwawezesha vijana kujikita zaidi kwenye kilimo ili kupunguza tatizo la ajira,” amesema Dkt. Haile na kuongeza kuwa WFP itahakikisha Tanzania inakuwa kituo cha uzalishaji katika ukanda wa Kusini mwa Afrika kwa kuwa ina rasilimali za kutosha kuwekeza katika sekta ya Kilimo. 

Nae Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amemuahidi Mkurugenzi huyo wa WFP kuwa Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha sekta ya kilimo nchini inaboreshwa zaidi.

“Nimewahakikishia WFP kuwa Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano katika kuhakikisha maboresho katika sekta ya kilimo yanafanyika na kuboresha maisha ya wakulima na kuwafanya vijana kujikita zaidi kwenye sekta hiyo muhimu,” amesema Balozi Mulamula.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na WFP katika kuboresha zaidi sekta ya kilimo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiongea na Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini mwa Afrika wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Dkt. Menghestab Haile katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini mwa Afrika wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Dkt. Menghestab Haile akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini mwa Afrika wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Dkt. Menghestab Haile kikiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini mwa Afrika wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Dkt. Menghestab Haile katika picha ya Pamoja Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bibi. Sarah Gordon-Gibson wa kwanza kushoto, kulia mwa Balozi Mulamula ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Makocha Tembele anayefuatia ni Bw. Hlalanathi Fundzo kutoka WFP.