Friday, March 18, 2022

Balozi Possi Afanya Ziara ya Kikazi Jamhuri ya Czech

Balozi Possi Afanya Ziara ya Kikazi Jamhuri Czech

Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Czech mwenye makazi yake Berlin, Ujerumani, Dkt. Abdallah Possi amefanya ziara ya kikazi katika nchi ya Jamhuri ya Czech na kufanya mazungumzo na Naibu Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Miloslav Stašek; Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Jakub Dvořáček na Naibu Waziri wa Elimu, Mhe. Prof. Jaroslav Miller tarehe 17 Machi 2022.

Wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dkt. Possi aliwasilisha ombi ili Watanzania waweze kunufaika na Mpango wa Nafasi za Ufadhili wa Masomo unaoratibiwa na Wizara hiyo. Kwa sasa, nchi za Africa zinazonufaika na mpango huo ni Zambia na Ethiopia. Mhe, Naibu Waziri aliahidi kulifanyia kazi ombi hilo. Aidha, Mhe. Stašek aliwasilisha mualiko wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufanya ziara ya kikazi Jamhuri ya Czech.

Katika mazungumzo yake na Naibu Waziri wa Afya, Balozi Possi aliomba Serikali ya nchi hiyo kuangalia uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta ya Afya, hususan katika magonjwa ya moyo na figo. Serikali ya Jamhuri ya Czech imeahidi kulifanyia kazi ombi hilo na kuahidi pia kuwa ipo tayari kuisaidia Tanzania dozi za chanjo ya UVIKO-19.

Kwa upande wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Elimu, wawili hao walijadili kuhusu ushirikiano wa Vyuo Vikuu, na namna ambavyo wanafunzi wa Tanzania waliokatiza masomo nchini Ukraine wanaweza kurahisishiwa mchakato wa kuhamisha alama na kumalizia masomo yao katika vyuo vikuu vya Czech.  Prof. Miller alimweleza Balozi Dkt. Possi wataanza na utaratibu wa awali wa kuvitaarifu vyuo vikuu vya Czech na kutoa kipaumbele kwa wanafunzi wa Tanzania, huku taratibu nyingine za kiufundi zikifuata.

Mhe. Miller aliahidi pia kuwa mamlaka husika zitaweka tangazo katika tovuti ya “Study in Czech Republic” ili  kuwahamasisha wanafunzi wa Tanzania waliokuwa Ukraine kuomba kujiunga na vyuo vikuu Jamhuri ya Czech.

 

Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Czech mwenye makazi yake Berlin, Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe.Miloslav Stašek walipokutana kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi zao.

Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Czech mwenye makazi yake Berlin, Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi akisalimiana na Naibu Waziri wa Elimu wa Jamhuri ya Czech,Mhe. Prof. Jaroslav Miller walipokutana kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano baina ya sekta za afya za nchi zao.

Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Czech mwenye makazi yake Berlin, Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi akisalimiana na Naibu Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Jakub Dvořáček walipokutana kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano baina ya sekta za elimu za nchi zao.

 


 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.