Friday, March 18, 2022

WFP YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUBORESHA SEKTA YA KILIMO NCHINI

Na Mwandishi wetu, Dar 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeahidi kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha kilimo nchini na kukifanya kuwa cha kisasa zaidi.

Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini mwa Afrika wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Dkt. Menghestab Haile alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Haile amesema WFP inajivunia uhusiano mzuri na Tanzania na itaendelea kudumisha uhusiano na ushirikiano huo kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Leo tumejadili na kuona ni namna gani tunaweza kuwaunga mkono wakulima wa Tanzania ili waweze kupata faida zaidi kupitia kilimo ambapo faida hiyo itawasaidia kuyaboresha zaidi maisha yao,” amesema Dkt. Haile

“………… kwa kuwa kilimo ndiyo sekta pekee inayotoa fursa ya ajira kwa wingi duniani, tuna mkakati wa kuwawezesha vijana kujikita zaidi kwenye kilimo ili kupunguza tatizo la ajira,” amesema Dkt. Haile na kuongeza kuwa WFP itahakikisha Tanzania inakuwa kituo cha uzalishaji katika ukanda wa Kusini mwa Afrika kwa kuwa ina rasilimali za kutosha kuwekeza katika sekta ya Kilimo. 

Nae Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amemuahidi Mkurugenzi huyo wa WFP kuwa Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha sekta ya kilimo nchini inaboreshwa zaidi.

“Nimewahakikishia WFP kuwa Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano katika kuhakikisha maboresho katika sekta ya kilimo yanafanyika na kuboresha maisha ya wakulima na kuwafanya vijana kujikita zaidi kwenye sekta hiyo muhimu,” amesema Balozi Mulamula.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na WFP katika kuboresha zaidi sekta ya kilimo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiongea na Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini mwa Afrika wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Dkt. Menghestab Haile katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini mwa Afrika wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Dkt. Menghestab Haile akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini mwa Afrika wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Dkt. Menghestab Haile kikiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini mwa Afrika wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Dkt. Menghestab Haile katika picha ya Pamoja Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bibi. Sarah Gordon-Gibson wa kwanza kushoto, kulia mwa Balozi Mulamula ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Makocha Tembele anayefuatia ni Bw. Hlalanathi Fundzo kutoka WFP.  





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.